Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kuniona na kuweza kuniweka kwenye orodha hii. Kwa hakika ni bahati ya pekee kwa sababu ya muda, lakini nichukue nafasi hii kwa sababu ni mara ya kwanza, kumshukuru Mwenyezi Mungu kuweza kunijalia afya na uzima na kuweza kusimama mbele ya Bunge lako tukufu.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Singida Mashariki pamoja na chama changu, Chama Cha Mapinduzi chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniteuwa na kugombea ubunge na hatimaye wananchi wa Singida Mashariki walinichagua kwa kura nyingi za kishindo. Niwahakikishie uongozi uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze tu na maneno machache kwa maana ya kwamba, kiongozi wetu, Rais wetu ametoa hotuba nzuri ambayo imetoa muelekeo wa miaka mitano ijayo Tanzania tunayoitaka na hii imeanza toka mwaka 2016 alivyoingia hapa alionesha dira na kwa miaka mitano tumeona mambo makubwa yaliyofanywa katika nchi hii na kwa hakika ni historia ambayo haitafutika. Lazima sisi kama Watanzania tujivunie viongozi wa aina hii na tuendelee kuwapa moyo na kuwaunga mkono kwa sababu Tanzania yetu imepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kama ambavyo unajua miundombinu ipo ili iweze kuwezesha Watanzania au wananchi kuweza kuleta maendeleo. Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa, ni vizuri kama Watanzania tuendelee kuunga mkono juhudi hizi na kwa hakika kwa miaka mitano ijayo tumeona dira yake kwa hiyo, ombi langu tu nilikuwa nataka nieleze maneno machache kwenye eneo la elimu.

Mheshimiwa Spika, bado tuna changamoto kwenye maeneo ya miundombinu ya elimu. Niiombe sana Serikali kupitia Rais alivyoeleza tuendelee kuongeza nguvu ya kuleta fedha kwa ajili ya kuimarisha vyumba vya madarasa, kuimarisha mambo ya maabara, kuimarisha suala la mabweni kwa ajili ya watoto, hasa watoto wa kike. Watoto wa kike wengi wanapoteza ndoto zao za kusoma kwa sababu mazingira ni magumu katika shule zetu za kata ambazo wanatembea karibu kilometa zaidi ya tisa kufuata shule hizo. Kwa hiyo, niombe sana Wizara ya Elimu kuhakikisha kwamba tunaboresha miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini nieleze hili suala ambalo wenzangu wote wamesema, suala la miundombinu ya barabara. Ninaamini kabisa TANROADS inafanya kazi nzuri kwa sababu imewezeshwa, lakini tulivyoamua kuanzisha Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), lengo lilikuwa ni kuondoa urasimu uliokuwepo wa kuleta fedha kupitia Mfuko wa Barabara. Leo hii tunavyoleta mgawanyo wa asilimia 70 kwa TANROADS na asilimia 30 kwa barabara za TARURA ni kama vile tunaifanya taasisi isifanye kazi yake, inakuwa haina maana ya kuianzisha TARURA kama hatuipi fedha.

Mheshimiwa Spika, leo hii tuna barabara nyingi sana kwenye vijiji vyetu ambazo zinaenda kuboresha kilimo. Niombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi aeleze mipango ya kuiongezea TARURA fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba barabara za vijijini ambazo zinaleta huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya, zahanati nyingi ziko vijijini. Tusipokuwa na barabara nzuri maana yake hatuwezi kuwahudumia wananchi ambao wako maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nieleze maneno machache sana. Mheshimiwa Rais alikiri mbele ya Bunge kwamba ataboresha demokrasia, lakini utawala bora. Kwa miaka mitano tumeona kazi nzuri iliyofanyika ikiwemo kusimamia watumishi wa umma ambao walikuwa hawafanyi vizuri sana katika maeneo yetu. Watumishi wa umma wengi walikuwa wengine hawawatendei haki Watanzania na tumekuwa wengi tunalalamika hapa.

Mheshimiwa Spika, leo hii Mheshimiwa Rais amesimama amesema, lakini sisi wote ni mashahidi, leo hii kuna baadhi wanasimama hapa wanasema hakuna demokrasia, lakini utawala bora hakuna. Niwaulize wao wenyewe hivi leo wanataka turudi tulikotoka ambapo Watanzania wengi walikuwa wanalalamika baadhi ya watumishi ambao hawafanyi vizuri katika maeneo fulani?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe sana kama chama cha siasa wajibu wako wewe ni kuhakikisha unahudumia wananchi, lazima utatue kero zao. Wenzetu hawa wanaongea…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Miraji Mtaturu.

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa sababu ya muda naunga mkono hoja iliyoko mbele yetu. (Makofi)