Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi kuweza kuchangia katika hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza mimi kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama katika hadhira hii ningeanza kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhana Wataalah, lakini pia nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ali Mohammed Shein ambaye kwa kweli amenilea na kunikuza na kuniamini kunipa Idara ya Misitu kuweza kuiendesha kwa miaka karibu minne ambayo ndiyo imenijenga na kuwa mtu wa namna hii hapa nilipo.

Mheshimiwa Spika, pia ningependa kumshukuru mama yangu Bi. Jira binti Machano na mke wangu Shufaa binti Suleiman Hamad pamoja na wanangu bila kusahau wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi wa Jimbo la Donge ambao wamenipa imani kubwa ambayo imenisababisha mimi leo kusimama hapa nikiwawakilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja niende kwenye hotuba ya Mheshimwa Rais na nianzie ukurasa namba tisa ambapo Mheshimiwa Rais ameipongeza Tume ya Uchaguzi kwa kuendesha uchaguzi katika hali nzuri, lakini pia kutoa matokeo haraka na kuipongeza kwa kuweza kubana matumizi kwenye bajeti ambayo walikuwa wametengewa ya shilingi bilioni 331 na kutumia shilingi za Kitanzania bilioni 262.

Mheshimiwa Spika, hapa nilikuwa napenda kutoa angalizo maalum kwamba aliyepaswa kushukuriwa zaidi hapa ni Mheshimiwa Rais mwenyewe pamoja na Rais Dkt. Ali Mohamed Shein kwa sababu viongozi hawa wameweka alama katika uchaguzi wa mara hii kwa sababu ni mara ya kwanza Tanzania imeweza kuendesha uchaguzi kwa kutegemea fedha za ndani tofauti na miaka yote iliyopita. Kwa kweli tunawashukuru sana viongozi wawili hawa kwa sababu wameweka alama.

Mheshimiwa Spika, halikadhalika ningependa kwenda kwenye page number 13 ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kuelezea kwamba, atazienzi tunu za Taifa letu ambazo zinajumuisha amani, uhuru, mshikamano, umoja, Muungano pamoja na Mapinduzi ya Zanzibar. Pia ameendelea kwa kusema kwamba, atashirikiana na na Rais Dkt. Mwinyi kuweza kuhakikisha kwamba tunu hizi zinalindwa kwa gharama zozote zile.

Mheshimiwa Spika, hapa ningetoa pia angalizo kwa sababu kuna watu wanapenda kuchezea Muungano wetu na halikadhalika nafikiri juzi mnakumbuka kwamba kuna kiongozi mmoja wa kisiasa amejaribu kuzungumza kumzungumzia kiongozi mkuu wa Serikali kwamba, ana maradhi na lengo lake sote tulikuwa tunalifahamu kwamba ilikuwa ni kuleta mshtuko miongoni mwa jamii ambayo hivi sasa kama tunavyofahamu uchumi wetu umeanza kuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kule tulikotoka ndege zilikuwa hazionekani, watalii walikuwa hawaonekani, lakini hivi sasa tumeanza kuimarika, kwa hiyo, nafikiri bado ambao hawapendi mshikamano na umoja wa nchi yetu, Muungano una dumu, basi wanatafuta kila aina ya visingizio kuweza kutumia fursa kuweza kuleta chokochoko. Kwa hiyo, tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa angalizo hili kwamba atashirikiana na Dkt. Mwinyi kuweza kuhakikisha kwamba analinda tunu hizi za Taifa kwa gharama yoyote.

Mheshimiwa Spika, lakini ningependa kumalizia kwa kuhusu maliasili na utalii.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia.