Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uzima na afya njema. Si kwa ujanja wetu bali ni kwa huruma na rehema yake. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana wananchi wa Mkoa wa Singida kwa kumchagua Mheshimiwa Rais kwa kura nyingi za kishindo, Madiwani na Wabunge wa CCM. Nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwashukuru sana wapiga kura wangu wanawake wa Mkoa wa Singida ambao wamenipa fursa ya kuwawakilisha katika Bunge letu tukufu. Ninawashukuru sana ninakiri kwamba ninalo deni kubwa kwao la kuwawakilisha na pia kamwe sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikupongeze wewe kwa kuwa Spika wa viwango, mwenye kujali maslahi ya Wabunge wake na ambaye umeleta mapinduzi makubwa sana ya kidijitali katika Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiaw Spika, ninaipongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo imetoa dira na mwelekeo wapi Tanzania mpya tunatakiwa kuwa katika miaka mitano ijayo. Ni hotuba iliyogusa sekta zote muhimu katika kukuza uchumi, ni hotuba iliyogusa maslahi mapana ya wanyonge. Ni hotuba inayokwenda kutofautisha Tanzania na nchi nyingine za Afrika katika suala zima la kukuza uchumi. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiisoma hotuba hii ya Mheshimiwa Rais utatambua kwamba Mheshimiwa Rais anayo dhamira ya dhati ya kujenga Tanzania mpya ya kuifikisha uchumi wa juu kabisa. Ukurasa wa 10 wa kitabu cha Mheshimiwa Rais ameahidi kuongeza juhudi za kuwapa mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu. Pia ameagiza mifuko na programu mbalimbali ambazo zitasaidia uwezeshwaji wa wananchi kiuchumi kuunganishwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili limewafurahisha sana wananchi na vijana wa Mkoa wa Singida na wameniagiza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi huo na kwa kuwa asilimia 10 zinazotolewa katika Halmashauri zetu hazikidhi mahitaji ya wananchi wetu. Niiombe sana Serikali iharakishe mchakato wa kuunganisha mifuko hiyo ili wale bodaboda wangu, mama na baba lishe na wajasiriamali wadogo wadogo waweze kunufaika na mifuko hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia makundi haya utaona kwamba ni makundi ambayo hayana dhamana ya kukopa kwenye benki zetu, hivyo uwepo wa mfuko huo utawasaidia sana wananchi wale wa kipato cha chini kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali ya Awa,u ya Tano kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maji lakini nikiri kwamba bado kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa maji safi na salama hususan maeneo ya vijijini. Mfano, katika mkoa wangu wa Singida upo mradi mkubwa wa Kitinku - Lusulile. Mradi huu umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu bila ya kukamilika. Niiombe sana Serikali katika bajeti ya mwaka ujao itenge fedha za kutosha ili miradi ile ambayo haijakamilika ikiwemo huu Mradi wa Kitinku – Lusilile uweze kukamilika na wannachi waweze kupata maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu katika suala zima la kilimo ambapo katika hotuba ya Mheshimiwa Rais...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Aysharose.

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja kwa asilimia 100. Nakushukuru sana. (Makofi)