Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi na mimi nichangie hotuba ya Rais. Kabla sijaendelea naomba nimshukuru Mungu kwamba amenipa maisha na amenisaidia kuwa mzima mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeangalia katika hotuba ya Rais ukurasa wa 10, alijikita kuzungumzia mambo ya viwanda. Viwanda ndivyo vinavyotoa ajira kwa vijana na ndivyo vinavyoongeza pato kwa Taifa. Ni kweli kwamba kuna kipindi tulibinafsisha viwanda na kwenye ukurasa huo Mheshimiwa Rais alizungumzia kusuasua kwa viwanda vilivyobinafsishwa.

Mheshimiwa Spika, viwanda vingi vilinunuliwa na watu wakabadilisha matumizi, siyo kama vile kusudio lilivyokuwa. Sisi katika Mkoa wetu wa Mbeya, Kiwanda cha Zana za Kilimo (ZZK) leo hii ukienda unakuta mtu amekodisha ghala za kuhifadhia pombe kwa ajili ya kuuza kwa bei ya jumla. Nafikiri ni wakati sasa Serikali ifuatilie kwa wale watu ambao walibinafsishwa na wakasema wataendeleza kile kilichokuwa kikiendelea wakabadilisha matumizi, ninaomba Serikali isimamie hiyo.

Mheshimiwa Spika, katika viwanda watu wengi wanataka kuwekeza, lakini unapotaka kuanzisha viwanda, kodi zinakuwa nyingi, lakini pia ufuatiliaji wa kodi hizo, unaenda madirisha mengi; unaenda TRA, unaenda sijui kwa watu wa viwango na vitu kama hivyo. Nashauri Serikali iweke dirisha moja ili watu waende kwa wakati mmoja, wafanye vitu vyote mahali pamoja.

Mheshimiwa Spika, viwanda vingi sana hapa nchini vingeendelezwa vingeweza kusaidia ajira ya vijana. Kwa mfano, hapa Tanzania tuna zao la ngozi. Kwa bajeti ya mwaka jana wauzaji wa ngozi nje ya nchi wamepoteza takribani milioni 200 kwa kukosesha kwenda kuuza ngozi kwa sababu ziliharibika. Ninaomba urasimu katika kusaidia wafanyabiashara ya ngozi nje ya nchi, upunguzwe ili tuweze kuona vijana wetu wakipata ajira katika viwanda hivi. Maana ni zaidi ya vijana 400 ambao walikosa ajira mwaka 2020 baada ya ngozi hizi kushindwa kusafirishwa.

Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Rungwe kuna Kiwira Coal Mining ambayo ilibinafsishwa. Iliajiri wanawake wengi na vijana wengi, lakini mpaka leo imekuwa gofu. Hata hilo wazo la kwanza la Baba wa Taifa kuona inafaa kwa Taifa letu la Tanzania, ndoto za Wanakiwira pamoja na Wanambeya zimeishia hapo baada ya kufunga migodi kama ile.

Mheshimiwa Spika, nasema viwanda bila kilimo haiwezekani. Watu zaidi ya asilimia 75 ni wakulima. Ili uweze kupata malighafi ni lazima uwekeze kwenye kilimo. Leo hii tunalalamika habari ya pembejeo. Mheshimiwa mmoja amesema hapa, tunategemea mvua. Ni wakati sasa wa kubadilisha kilimo chetu, ni wakati wa kuona kilimo ni uti wa mgongo kama mbiu ya zamani ilivyokuwa inasema. Tuanzishe umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, bajeti ya mwaka 2019/2020 tulipitisha hapa Bungeni takribani shilingi bilioni 37 kwa ajili ya umwagiliaji. Hata hivyo, ni shilingi bilioni nne tu zilitoka kwenye Wizara ya Kilimo. Ninashauri, Bunge linapopitisha bajeti, ni vyema Serikali ikajikita kusaidia ili iweze kupeleka maendeleo kwa watu wetu na hasa wakulima.

Mheshimiwa Spika, kilimo bila utafiti haiwezekani. Ili uwe na kilimo bora, lazima uwekeze kwenye asasi au taasisi za utafiti. Tuna Uyole pale Mbeya, ni Kituo cha Utafiti. Huu ni mwaka wa tatu sasa hawajapata fedha kwa ajili ya utafiti. Pana mitamba pale, ili uweze kujua mbegu bora ni lazima wasomi wetu SUA na sehemu nyingine wafanye utafiti. Naiomba Serikali iwekeze kwenye utafiti ili tuweze kupata mbegu bora.

Mheshimiwa Spika, TARURA, watu wengi wamezungumzia habari ya TARURA, zamani ilikuwa kwenye Halmashauri. Labda kwa kusema leo, jana nilimsikia Mheshimiwa Jafo akizungumza, vitu vingi vimerudi kwenye Halmashauri.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)