Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Latifa Khamis Juwakali

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. LATIFA KHAMISI JUAKALI: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kwa kunipa nafasi hii kuweza kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naomba niungane na wenzangu kwa kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa hai, lakini pia kutujalia sote kuwa wazima.

Mheshimiwa Spika, kwa upekee sana naomba nikishukuru Chama changu cha Mapinduzi ambacho kinaongozwa na jemedari wetu, jembe, mpambanaji, mtu mahiri sana, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, kwa imani kubwa ambayo wamenionesha mimi kijana wao wa Chama Cha Mapinduzi kurejeshwa jina langu na kuja kuwawakilisha vijana wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana vijana wenzangu wote wa Tanzania nzima, tukianza na vijana wa Mkoa wangu wa Kusini Unguja na vijana wenzangu wote kwa imani ambayo wamenionesha, naomba niwaahidi kupitia kwenye Bunge lako hili tukufu kwamba sitawaangusha, nipo kwa niaba yao na nitafanya kazi kwa niaba yao. (Makofi)

Mwisho naomba niwashukuru wazazi wangu walezi kwa kunilea, kunitunza na kunifanya mpaka leo niko hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dakika zenyewe ni chache, naomba na mimi niunge mkono hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo iliwasilishwa hapa katika Bunge lililopita. Sote ni mashahidi, kazi ambayo imefanywa na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kubwa na sote tunaijua na Watanzania wote waijua, mwenye macho tunasema haambiwi tazama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi nimetembea katika Tanzania nzima, nimeona miradi mbalimbali iliyofanywa chini ya usimamizi wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vituo vya afya, miradi ya maji, miundombinu, barabara, hakuna asiyejua kazi kubwa ambayo imefanyika chini ya usimamizi wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka nichangie katika suala hili la elimu. Wachangiaji waliopita wamesema sana; elimu yetu ya Tanzania haimuandai kijana kuweza kujiajiri mwenyewe ama kuajirika. Naomba sana niishauri Wizara yetu ya Elimu sasa tuweze kubadilisha mitaala ambayo itaweza kumsaidia kijana wetu aweze kuajirika, lakini hiyo mitaala atakayoweza kumsaidia kijana huyu yeye anapomaliza elimu yake ikiwa elimu ya sekondari lakini hata katika elimu ya chuo kikuu aweze kuajirika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia naomba sana Wizara yetu ya Elimu tuandae mitaala ambayo itakuwa inaendana na wakati. Sisi vijana tuna msemo wetu tunasema lazima tuwe up to dated. Kwa mfano sasa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tupo katika uchumi wa kati, kwa hiyo je, sisi Wizara tunajipangaje kuendana na kasi ya uchumi huu wa kati. Kwa hiyo, lazima tuandae mitaala ambayo inaendana na uchumi.

Mheshimiwa Spika, nataka nishauri katika suala hili la mikopo, wenzetu wengi waliopita wamechangia kuwa lengo la mkopo ni kuwasaidia vijana wetu na kama lengo la mkopo ni kuwasaidia vijana wetu sasa ni vyema Bodi yetu ya Mikopo ikapunguza hii asilimia 15. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sote tunafahamu asilimia kubwa ya wanaopata mikopo ni vijana maskini wenzetu. Kwa hiyo, kama ni vijana maskini, leo kijana huyu amekopa mkopo let’s say milioni 10 ama milioni 15, lakini kijana huyu pengine anakaa miaka mitatu hajaajiriwa, baada ya kuajiriwa pengine mshahara wake ni mdogo, pengine analipwa shilingi 300,000, hiyo hiyo shilingi 300,000 Bodi ya Mikopo kuna asilimia 15 ambayo inaihitaji. Je, pengine analipwa shilingi 300,000 maana yake ukiwa unalipwa shilingi 300,000 Bodi ya Mikopo wanakata shilingi 45,000 kwa hiyo shilingi 300,000 toa shilingi 45,000 kuna kiasi kidogo ambacho kinabakia, bado hapa hujakatwa tax na vitu vingine; je hapa bado tutakuwa tumeendelea kuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. LATIFA KHAMISI JUAKALI: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, nakushukuru sana. (Makofi)