Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa muda nizungumze.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kabla sijazungumza kwa sababu na mimi ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili la Kumi na Mbili, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uzima na kunijaalia kila kitu mpaka hapa nilipofika. Pia niwashukuru wazazi wangu na familia yangu na watu wangu wote ambao wako karibu na wananifahamu wanajua nini kinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijachangia hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kuzindua Bunge la Kumi na Mbili iliyotolewa Novemba 2020, niseme kabisa nimesikilizia hotuba hiyo nikitokea gereza la Isanga ambako nilikuwa mahabusu pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia katika maeneo mawili, eneo la kwanza nitachangia katika ukurasa 13 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais ya mwaka 2020 ambako amezungumza na nitaanzia na hilo kwa sababu amezungumza kwenye hotuba yake kwamba ndiyo jambo la kwanza na la umuhimu ambalo anafikiri katika Serikali yake kwa muda wa miaka mitano atashughulika nalo ambalo ni kulinda na kudumisha amani ya nchi umoja, uhuru na mshikamano pamoja na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kwa uzito wa hoja hiyo na mimi naomba nichangie kwenye hoja hiyo kwa yafuatayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nia ya dhati ya kulinda amani ya nchi, kwa sababu wote tunafahamu kwamba amani ni tunda la haki, kwa hiyo, kimsingi unapozungumza kwamba Serikali imejipanga kulinda amani ya nchi lakini pia kulinda mshikamano wa nchi huwezi ku-ignore vitu vidogo vidogo ambavyo vinaonekana kama tunazungumza vitu vingine na tunatenda vitu vingine. Ninasema hivi kwa sababu naona hapa kama vile hawa wanazungumza hawa wanajibu lakini kimsingi kuna mambo ya msingi ambayo wote tunakumbuka, mimi nitasema deep down kila mtu anajua kwamba there was something very wrong kwenye uchaguzi wa 2020.

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Kuhusu Utaratibu.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anajua moyoni kwake kulikuwa kuna mambo ambayo si ya kawaida mpaka watu ambao si wanasiasa walikuwa wanajua, watu wanaofuatilia demokrasia ya nchi yetu, watu wanaofuatilia taratibu za uchaguzi kwenye nchi yetu walikuwa wanajua kuna shida kubwa imetokea kwenye uchaguzi wa 2020. That is the fact kwa sababu fact hazibishaniwi. Kwa hiyo, sitaenda into details nini kilitokea kwa sababu kila mtu anafahamu nini kilitokea Zanzibar, watu waliwekwa ndani, kesi zaidi ya 20 na kimsingi mpaka sasa kuna kesi mbili tu na sitaenda kwenye details kwa sababu najua kuna kanuni zinanizuia kuzungumza masuala ya kimahakama.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat, naomba ukae.

Mheshimiwa Ali King, kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 70 (1) mpaka 9 inaeleza kuhusu kusema ukweli au kuhusu kusema uongo. Mheshimiwa aliyekaa kitako, Mheshimiwa Nusrat Hanje anazungumza kwamba vyombo vyote ambavyo vilikuwa vinashughulikia uchaguzi huu vimethibitisha kwamba uchaguzi haukuwa mzuri au haukuwa huru na haki kwa mujibu wa maneno ambayo ameyatumia.

Mimi namthibitishia kwamba vyombo hivyo vyote vilivyoruhusiwa na kujihusisha na uchaguzi ikiwemo Tume ya Uchaguzi na observers wote walithibitisha kwamba uchaguzi ulikuwa uko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tume ya Uchaguzi ndiyo iliyotoa matokeo ya uchaguzi kwa sababu uchaguzi ulikuwa huru. Ma-observers wa Umoja wa Afrika, EISA ya South Africa, Umoja wa Ulaya na East Africa wote hawa walisema uchaguzi ulikuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa afute kauli yake au athibitishe chombo gani ambacho kilikuwa kina authority ambacho kimethibitisha uchaguzi haukuwa sawa. Nashukuru. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, alikuwa anachangia Mheshimiwa Nusrat Hanje, kwa mchango wake akasimama Mheshimiwa Ali King kuonesha kwamba anachokizungumza au anachochangia Mheshimiwa Nusrat kinavunja Kanuni ya 70 ambayo inakataza Waheshimiwa Wabunge wanapotoa michango yao kusema uongo Bungeni.

Mheshimiwa Ali King ameeleza yeye kwa kuvitaja ama kwa kuzitaja taasisi alizoona kwamba zilionesha kwamba uchaguzi huo ni huru. Wakati wote tukimsikiliza Mheshimiwa Nusrat nilikuwa najaribu kusikiliza hoja yake ni ipi kwa sababu ameeleza mambo ambayo yako jumla hajasema mahsusi, kwa hiyo nilikuwa nasikiliza hoja yake nijue inaelekea wapi.

Kwa hiyo, pengine atakuwa pia na mifano kama ambavyo ziko taasisi, ama viko vyombo ambavyo vimesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Kwa hiyo, pengine viko vyombo vya habari, ama taarifa, ama taasisi zilizosema haukuwa! Kwa hiyo, mnipe fursa nisikilize mchango wake halafu nijue hoja yake inaishia wapi kwa sababu kwa sasa inanipa vigumu kidogo kutoa mwongozo mahususi. (Makofi)

Mheshimiwa Nusrat, ushauri wa jumla umesikiliza Waheshimiwa Wabunge wakichangia pande zote, hata wa huku umewasikiliza wakichangia hoja ambazo hauna uthibitisho mahususi zinatakiwa kusemwa kwa namna ambayo hutaambiwa ulete ushahidi, kwa hiyo, huo ni ushauri wa jumla, malizia ushauri wako.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi nilizungumza nikasema deep down ndani ya moyo wako kila mtu anajua kulikuwa kuna shida mahali kwenye uchaguzi wa 2020, kila mtu atajitafakari yeye na Mungu wake anajua hicho ndio nilichokizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia labda nishauri jambo moja ambalo ndio hoja ilikuwa hiyo, kama ni kweli umeshinda kihalali na umeshinda, kimsingi sitaki kwenda kwenye uchaguzi kwa sababu Taifa linasonga mbele na kimsingi Watanzania wana matumaini makubwa na pengine namba ndogo ambayo imepatikana na watu ambao wataleta chachu fulani kwenye Bunge hili. Kwa hiyo, wacha tu mwiba utokee ulipoingilia.

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, wacha tu mwiba utokee ulipoingilia. Kwa hiyo, kimsingi, nashauri kama kuna kesi ambazo zilitokana na uchaguzi…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri, Mheshimiwa Rais kwa sababu ya hotuba yake…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge mniruhusu hapa mbele nina majina mengi kwa hiyo hapana! Mheshimiwa Halima tafadhali! Kuhusu taarifa sitaziruhusu ili majina yaweze kuisha hapa, isipokuwa kama mtu anavunja kanuni hilo halivumiliki na Bunge kwa sababu muda tulionao ni mfupi na majina ni mengi. Mheshimiwa Nusrat. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa ushauri kwa Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri ambao wanahusika na masuala ya kisheria na kimahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi uchaguzi umeisha tujenge Taifa si ndio hivyo tunazungumza hivyo, sasa twende ili tusonge mbele. Kuna watu mpaka leo bado wanasumbuliwa mahakamani na kesi za uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kama kuna watu wanahusika na hayo mambo waachieni watu wakafanye maisha yao, kwa nini bado wanaenda mahakamani mpaka Mheshimiwa Salome Makamba bado ana kesi ya uchaguzi, tuna kesi zipatazo 20 Mainland na Visiwani. Sasa watu wa ACT kule kuna vitu walifanya huko na nini kesi zimepunguzwa mpaka zimebaki mbili ya Nassoro Mazrui na mwenzake yule Ally Omar Shekha. Kwa hiyo, kimsingi nashauri hivyo hatuna haja waache basi watu waendelee na mambo yao unawashikilia watu kwenye kesi za uchaguzi ambao unajua uchaguzi wenyewe yaani mtu unamchukulia mkewe halafu unataka kumuua, come on! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo la pili ambalo nataka kumalizia ni kuhusiana na masuala ya mahakama. Kwenye hotuba ya mwaka 2015 ya kufungua Bunge kwa maana ya Bunge la Kumi na Moja na Bunge la Kumi na Mbili, Mheshimiwa Rais alizungumzia suala zima la mahakama na ni miongoni mwa watu ambao nimeishi kwa vitendo na ninashuhudia vitu ambavyo vinafanyika kwenye mahakama zetu na kwenye magereza zetu. Kimsingi kuna tatizo kubwa sana na yeye alizungumza na akashauri kwamba wajaribu kurekebisha mifumo ya uendeshaji kesi ili kusiwe na mrundikano wa watu wengi sana kwenye magereza zetu. Kimsingi huwezi kutenganisha magereza, wafungwa, mahabusu na mahakama. Kwa hiyo, tukizungumza mahakama maana yake haya mambo yote yanahusika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka tunapozungumza tishio la COVID na mrundikano wa watu ambao wana kesi za upelelezi za miaka zaidi ya kumi kwenye magereza ni jambo la hatari kiafya. Mheshimiwa Waziri wa Afya yupo anasikia, kule kuna changamoto kubwa na niseme, Bunge likiwa hapa watu wale wadada zetu wale wengine wanafanya shughuli zao nyingine wanakuja, wakija hapa kila siku wanakamatwa wanapelekwa hapo, mimi nimekaa hapo Isanga, wanakuja pale tunaitaga kontena jipya mpaka wanatenga cell maalum ya watu wanaoletwa ambao wanaondoka na kuja ambayo unajua huyu wiki ijayo atakuja tena kwa sababu atakamatwa tena uzururaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, labda nishauri kuna vitu vya kurekebisha, Mheshimiwa Rais sijui kama wale wanaomshauri au pia Waziri kuna jambo moja la digital platform ya kuendesha kesi, siyo lazima watu wahudhurie mahakamani, lakini pia itasaidia kupunguza mlolongo wa kesi, kwa sababu kulikuwa kuna malalamiko kwenye kipindi cha corona watu walikuwa hawaendi kabisa mahakamani kwa sababu kila mtu alikuwa anajua mikusanyiko ilikuwa haitakiwi. Walijaribu kidogo kuendesha kesi kwa kupitia digital platform zoom, Jaji huko aliko kesi zinaamuliwa, nafikiri waongezewe uwezo wafanye kazi ili tupunguze milolongo na mrundikano wa kesi kwenye magereza zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimalizie…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa, huwezi kuanza na jambo jipya.

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. (Makofi)