Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza naunga mkono hoja, lakini pili napenda nijikite kwenye hii hotuba ukurasa wa 46 ambao unazungumzia masuala ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pongezi kwa Serikali, hasa Wizara ya Maliasili, Waziri na wasaidizi wake kwa kuongeza idadi ya wageni kutoka 2015 mpaka sasa hivi 2021 idadi ambayo imetajwa pale sambamba na mapato yameongezeka kama ambavyo imetajwa kwenye hotuba kwa wale waliopitia, lakini pamoja na hayo niseme tu kwamba, hii dira ya Rais, maono yake ya kutaka kuongeza idadi ya wageni kutoka milioni moja na kitu mpaka milioni tano mwaka 2025 itafikiwa tu kama Wizara na wataalam wake wakitoa ushirikiano wa kutosha, lakini hasa kubadilisha mind set kwa maana ya kwamba, lazima tukubaliane utalii ni biashara. Kwa uzoefu tu wa kawaida kumekuwa na hali ya kwamba, uhifadhi umekuwa unashindana na utalii ndani ya Wizara na taasisi zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yangu ni kwamba, kunapokuwa na changamoto ya bajeti kwenye Wizara pamoja mashirika, lakini bajeti ya kwanza kuonewa ni ya utalii, lakini hasa ya masoko, kwa maana ya tourism promotion. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri na wasaidizi wake na wengine kwenye mashirika waanze kubadilika kwa maana ya kuona utalii ni biashara, lakini pia utalii ndio unamlea uhifadhi. Shughuli zote za doria za magari, za mafuta, uniform za wapiganaji, posho na vitu vingine vinanunuliwa au vinalipwa kutokana na makusanyo yanayotokana na utalii. Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu waweze kutoa kipaumbele kwenye bajeti za utalii kuliko vinginevyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata Bodi yetu ya Utalii ambayo sasa ndio inayofanya masoko imekutana na changamoto ya bajeti kwa miaka mingi. Tumekuwa tunajitahidi inawekwa fedha nyingi, lakini fedha ambayo inatoka kwa utekelezaji inakuwa ni ndogo sana, hali ambayo inafanya tusiweze kushindana kama ambavyo inapaswa. Ukiangalia wenzetu nchi jirani ya Kenya, wengine wa Afrika Kusini na Wamoroko wanafanya vizuri zaidi kitakwimu, wanaingiza wageni wengi, lakini hawana vivutio vingi kama ambavyo sisi tunavyo Watanzania. Kwa hiyo, utalii ni biashara, lazima tukubali kwamba, utalii ndio unalea uhifadhi, ili uhifadhi ufanyike kwa kiwango tunachokipenda, basi tupate fedha kwanza kutoka kwenye utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niwashukuru wafanyabiashara kwa maana ya wakala wa utalii. Wao ndio wamekuwa wakileta wageni kwa zaidi ya asilimia 80 hapa nchini. Kwa hiyo, niombe tu Wizara iendelee kushirikiananao kwa ukaribu kujifunza kuona wenzetu wanachokifanya, ili wageni waweze kuja kwa wingi kufikia hili lengo la Rais la kufikisha wageni milioni tano mwaka 2025.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, kumekuwa na changamoto ya migogoro ya mipaka ya ardhi. Sisi kwetu Bonde la Kilombero tuna changamoto nzuri kidogo niseme kwa sababu, kuna hili suala la mradi wetu wa umeme wa Nyerere, Stiegler’s George. Ni mradi mkubwa wa kitaifa ambao sote tunaupenda na tunautakia heri, hatuko tayari kumuona mtu yeyote ambaye anaharibu, lakini sisi watu wa Bonde la Kilombero imeonekana tunatoa sehemu kubwa ya maji ya mradi ule, kwa hiyo, kwa maana yake ni kwamba, baadhi ya maeneo ambao tulikuwa tunalima muda mrefu na kufuga kwa sasa yanakwenda kuathirika. Suala la uhifadhi limekuwa serious sana na Serikali kwa hiyo, baadhi ya vitongoji vyetu vya Jimbo la Malinyi, Ulanga na Mlimba vitaenda kupotea kwa maana ya vinafutika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji kimoja cha Ngombo ambacho kipo Malinyi nacho kwa msimamo wa Serikali lazima kifutwe kwa sababu, inasemekana ndio chanzo cha maji mengi ambayo yanakwenda Stiegler’s. Pengine sisi hatuna pingamizi sana, niiombe Serikali, Waziri Mkuu yupo hapa na ndugu yangu Dkt. Ndumbaro, Waziri, yuko hapa tutatoa ushirikiano kadiri inavyotakiwa, lakini naomba tu tusaidike kwa maana ya Kijiji cha Ngombo kibaki, lakini kwa masharti ili tusiharibu uhifadhi. Kwa hiyo, tuko radhi kupunguza idadi ya mifugo. Serikali tutashirikiana nayo kupunguza hata matrekta na masuala mengine ambayo tunaona yanachangia kuharibu uhifadhi, ili mradi wetu huu mkubwa usikwame, lakini naomba Serikali itufikirie wananchi waweze kubaki kwa masharti ambayo watayatoa au ambayo tutaafikiana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, maeneo ya ziada ya kulima kwa Jimbo zima la Malinyi imekuwa ikitusumbua. Kuna mpaka wa mwaka 2012 uliwekwa, badaye kuna mpaka mwingine mpya 2017, yote hayo inasemekana hayapo kwenye GN, lakini niombe Serikali, hatubishani nao, lakini naomba tufikiriwe angalau mita 700 tu kutoka kwenye mpaka ule wa 2017 tuweze kupatiwa ili tuweze kuendeleza shughuli zetu za uchumi. Sasa hivi Malinyi imesimama, watu hawalimi, tunasubiri hatma ya mwisho ya Serikali kutuambia mustakabali wetu ukoje.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliambiwa kuna Mawaziri wanane wale watakuja kutoa hatima, lakini muda unazidi kwenda watu hawana cha kufanya, majibu yanatakiwa na mimi kama Mbunge majibu sina. Kwa hiyo, niwaombe Serikali basi itoe official statement tuweze kujua nini ni nini na nini kinachofuata, maana sasa hatujui hatima yetu. Kwa hiyo, nashukuru sana, naamini Wizara na Waziri Mkuu watashirikiana kuweza kutufikiria sisi watu wa Malinyi, Ulanga na Kilombero.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni suala la changamoto ya miundombinu ya barabara. Kwetu Malinyi kuna barabara kubwa ambayo tunaisubiria, maarufu kama Barabara ya Songea, lakini Kiserikali inaitwa Lupilo – Malinyi – Londo – Namtumbo, kilometa 296 ambayo itaunganisha Mkoa wa Morogoro na Mkoa wa Ruvuma kupitia Wilaya ya Malinyi na Namtumbo.

Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu na Serikali kiujumla kutufikiria hili jambo liweze kuanza kwa uharaka ili tuweze kutokea Songea na mikoa mingine. Jambo hili likifanyika itakuwa imetusaidia kukuza uchumi wa Malinyi na Ulanga Kilombero kama mbadala wa kilimo ambacho sasa inaelekea tunaenda kuacha kutokana na changamoto ya mpaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, nitoe shukrani kwa Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, hasa kunisaidia wakati nimeumwa Novemba, Disemba. Nilipata huduma nzuri Ofisi ya Bunge ilinisaidia, lakini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali ya Sokoine Morogoro, walinisaidia nilipata huduma nzuri kwa hiyo, nimesema nichukue wasaa huu kuwashukuru. Mwisho wazazi wangu Mzee Zeno Mgungusi na mke wake Theopista Nghwale na mke wangu Mariam Ali Mangara aka mama Moringe nawashukuru wote kwa kunipa ushirkiano.. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)