Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Awali ya yote nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hotuba zake mbili nzuri ambazo zilinigusa mimi sana kama Mbunge wa Sikonge. Hotuba hizo mbili zimefanya mapitio ya nchi yetu, tulikotoka, tulipo na tunakoelekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili sisi Watanzania tuweze kujua tumetoka wapi na tunakoelekea ni wapi, jambo la kwanza kabisa ni kuangalia kwamba nchi yetu hii ilitawaliwa na wakoloni kwa muda wa miaka 74 na sisi tangu tujitawale kwa Tanzania Bara huu ni mwaka wa 60 na kwa Zanzibar ni mwaka wa 58. Utaona kwamba kipindi ambacho walikaa wakoloni katika nchi hii ni kirefu kuliko kipindi ambacho sisi tumekuwa huru. Katika kipindi ambacho tumekuwa huru, mambo ya maendeleo yaliyofanyika ni makubwa zaidi kuliko kipindi cha wakoloni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tangu tupate uhuru pia tumekuwa na vipindi vikuu vitano vya kiuchumi. Kipindi cha kwanza ni kipindi cha soko huria (1961 – 1967), kipindi cha pili cha uchumi hodhi miaka 18 kuanzia mwaka 1967 – 1985, kipindi cha tatu ni kipindi cha mpito cha marekebisho ya kufufua uchumi cha mwaka 1985 – 1995, kipindi cha nne ni cha mwaka 1995 – 2015 ambacho hicho ndiyo kiliweka prudent economic reforms ikiwemo ubinafsishaji, kurejesha baadhi ya njia ya kiuchumi kwenye sekta binafsi ikiwemo masuala ya ubi ana programs mbalimbali za maendeleo ikiwemo uandaaji wa dira na kuanza utekelezaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukirejea dira ina maeneo gani, maeneo makuu manne ya dira ambayo iliandaliwa na kuanza kutekelezwa mwaka 2000, eneo la kwanza ni huduma za jamii; eneo la pili ni amani, usalama na umoja wa Taifa; eneo la tatu utawala bora; na eneo la nne kukuza uchumi. Katika maeneo yote hayo manne hadi sasa tunavyozunguzma tumefanya vizuri zaidi na hasa kipindi hiki cha tano cha 2015 – 2025 tunakoelekea kumekuwa na uwekezaji kwenye maeneo karibu yote muhimu ya miundombinu na huduma za jamii, elimu, afya, maji, barabara, madaraja, viwanja vya ndege, bandari, reli na umeme mambo makubwa sana yanafanyika katika nchi hii hata watu wengine wanatuonea wivu. Juzi alikuja Mkongo mmoja akasema hebu tuazimeni Magufuli Congo angalau kwa muda mfupi aje kutawala huku. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais na kwa hotuba zake mbili muhimu sana. (Makofi)

Naomba sasa kupitia Bunge lako Tukufu niwasilishe changamoto kuu ambazo bado zinatukabili. Ya kwanza ni masoko ya mazao, bado wakulima katika maeneo mengi wana manung’uniko dhidi ya bei. Kwa Sikonge, tumbaku bado tuna manung’uniko makubwa lakini tunashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri Bashe alivyokuwa Tabora juzi alitoa hotuba nzuri ambayo imetuletea matumaini, tunachoomba vision yake iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya pili ni barabara vijijini. Ufinyu wa bajeti ya TARURA inatakiwa Serikali itafute chanzo chochote kile ili kuiongezea TARURA uwezo wake iweze kusaidia barabara vijijini. Hatuwezi kupata maendeleo ya kilimo kama TARURA hawezeshwi kutengeneza barabara za vijijini. Wanatengeneza barabara nyingi kwa udongo, ikija mvua kidogo tu inaosha na tunarudi kwenye matatizo yale yale. Changamoto kubwa ya tatu vijijini ni huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nina maombi maalum kutokana na hotuba ya Mheshimiwa Rais. Katika ukurasa wa 33 amesema: “Tunakusudia kujenga shule moja ya sekondari kila mkoa itakayofundisha masomo ya sayansi kwa wasichana”. Sikonge tunacho kituo cha vijana cha TULU ambacho kiliwekwa jiwe la msingi na Mheshimiwa Waziri Mkuu Pinda mwaka 2012 na kikazinduliwa na Mheshimiwa Rais Kikwete mwaka 2014. Hadi sasa waliofaidika pale hawazidi 100. Sasa kwa kuwa zilitumika shilingi bilioni 2.5 na zaidi za Serikali na kuna majengo pale Serikali iwekeze fedha kidogo tu ili tupate shule hii katika mkoa wa Tabora ambayo itakuwa Sikonge.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa naomba Serikali ijenge barabara ya Ipole – Rungwe ili kuunganisha Tabora na Mbeya. Vilevile ijenge na ikamilishe barabara ya kutoka Chunya - Itigi - Mkiwa ili kuunganisha Mkoa wa Mbeya na Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)