Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nami nianze kuwashukuru wananchi waJimbo la Ngara kwa kunichagua kwa kishindo kikubwa na siku ya leo nipo hapa Bungeni kama Mbunge miongoni mwa Wabunge wa Bunge la Kumi na Mbili. Vilevile naomba nishukuru Chama changu Cha Mapinduzikwa kuniteua, bila Chama Cha Mapinduzi kuniteua leo hii nisingekuwepo hapa.

Nimesoma sana kwa umakini mkubwa hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiondoa vitabu vya dini kwa maana ya Biblia, hii hotuba ya Mheshimiwa Rais ni Biblia yangu ya pili. Ukiangalia namna hotuba hii ilivyopangiliwa maudhui yaliyomo utagundua kabisa ndiyo maana Taifa letu linasonga mbele kwa sababu Jemedari wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yuko vizuri na mipango ipo vizuri.

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie hotuba ya Rais kwenye maeneo matatu: Eneo la kwanza ni kuwezesha wananchi kiuchumi; eneo la pili, ni ufugaji; na eneo la tatu, ni upande wa sekta za maji, umeme pamoja na barabara.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na sehemu ya kwanza ya uwezeshaji wananchi kiuchumi. Ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Rais ukurasa wa11 imeelezea kwamba kuna mifuko ya kukopesha wananchi zaidi ya 18 na mifuko hiyo inaonekana haileti tija kwa sababu ya gharama za kuendesha mifuko hiyo, suala la uratibu, lakini ukiangalia na namna ya kupima matokeo inaleta changamoto kunapokuwepo na mifuko mingi.

Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba hiyo ukurasa huo wa11 utaona kuna ombi ambalo linamwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu kuangalia uwezekano wa kuunganisha mifuko hii ili iweze kuleta tija kwa Watanzania. Mimi mwenyewe nilisikia baadhi ya mifuko kwa mara ya kwanza alipokuwa anaisoma Mheshimiwa Rais. Nataka nikueleze Watanzania hawajui hii mifuko tena ukiangalia, Mheshimiwa Rais amesema kwenye hotuba yake hapa kwamba mikopo hii ni ile isiyokuwa na riba na ile yenye riba nafuu.

Mheshimiwa Spika, hata sisi Wabunge tungependa kwenda kukopa kwenye mifuko hii tukaachana na kukopa hadi kwenye gratuity za kwetu, naomba niiombe Serikali hasa Ofisi ya Waziri Mkuu iweke utaratibu mzuri kwanza wa utoaji taarifa kwa Watanzania juu yahii mifuko. Vile vile iweke utaratibu mzuri hii mifuko iweze kusaidia wananchi na wananchi wote nchi nzima waweze kupata taarifa sahihi za mifuko hii na utaratibu wa kuweza kupata fedha kutoka kwenye mifuko hii ya kuwezesha wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye upande wa ufugaji na hapa najikita kwenye kitu kinaitwa uhimilishaji, huduma ya uhimilishaji ni huduma inayomfanya mfugaji ahamuwe muda na siku ambapo na siku ambapo mfuko wake utapata mimba, huduma ya uhimilishaji inamwezesha mwananchi kupanga akitaka ng’ombe wake apate mimba kesho yake anamwita Daktari wa Mifugo, anaweka homoni pale anaweka mbegu na ng’ombe wake anapata mimba.

Mheshimiwa Spika, huduma hii inaweza kumfanya mfugaji kuamua idadi ya mifugo anayoitaka kila mwaka na hivyo tunaweza kuzalisha mifugo mingi na hivyo kukuza uchumi wa kaya moja moja na Taifa kwa ujumla. Naiomba Serikali kwenye eneo hili la uhimilishaji iweze kutenga fedha za kutosha kununua zana za uhimilishaji na kupeleka Madaktari wa Mifugo kwenye chuo kilichopo Arusha kinachofundisha masuala ya uhimilishaji ili kuweza kuleta tija kwenye eneo hili la ufugaji.

Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye upande wa miundombinu hasa specifically kwenye sekta za maji, umeme pamoja na barabara. Jimboni kwangu na maeneo mengine nimesikia Watanzania wengi sana wanalalamika hasa vibarua pamoja na kampuni za Kitanzania zinazofanya kandarasi kama sub-contractors na makampuni ya nje. Mimi mwenyewe nimewahi kuwa sub kwenye tenda ambayo walipewa Wajerumani. Nataka nieleze wazi kwamba tunapigwa sana kwenye eneo hili, mzungu anasaini mkataba wa dola milioni tatu anakupatia kazi kama sub tunafanya kazi yote asilimia 98, inapokuja kwenye malipo kipindi kingine anatuzungusha, kipindi kingine bargaining power inakuwa ni ndogo na hata kipindi kingine Watanzania tunadhulumiwa.

Mheshimiwa Spika, achilia mbali sisi ambao niConsultants, njoo upande wa vibarua takribani maeneo mengi sana nchi nzima, wananchi vibarua wanalia. Hapa ninaombi kwa Serikali hasa kwenye idara zote hizi upande wa sekta ya maji, umeme na barabara, naomba Wizara ziweke utaratibu mzuri wa wananchi hawa wa Tanzania kulipwa moja kwa moja kutoka kwenye Wizara husika. Tukifanya hivyo, Watanzania watalipwa moja kwa moja na ile dhuluma ambayo tunadhulumiwa haitakuwepo, ni suala la Serikali kuweka utaratibu mzuri, mkandarasi mkubwa anatoa taarifa kwa aliyetoa kazi za vibarua ama aliyefanya naye sub-contractors, then Serikali inalipa moja kwa moja, tunadhulumiwa sana kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa,naomba nieleze changamoto iliyopo kwenye upande wa barabara. Barabara nyingi hasa za mjini ni chafu kwa maana ya kwamba zimejaa mchanga. Utaratibu uliopo wa kusafisha barabara nimeshindwa kuelewa vizuri, nilikuwa najiuliza, barabara inajengwa nzuri ya lami lakini baada ya muda mfupi unakuta michanga imejaa na kaeneo ka kupita ni kadogo katikati ya barabara na ile michanga inamomonyoa barabara. Naomba Serikali iangalie utaratibu mzuri iuandae wa kusafisha hizo barabara kutoa michanga kwenye lami. Najiuliza jukumu la kusafisha barabara wakipewa TAMISEMI, akapewa Mheshimiwa Jafo, mtaa husika ukahusika kusafisha zile barabara ile michanga itaondoka maeneo yale na barabara zitakuwa safi.

Mheshimiwa Spika, zile barabara za mijini zilizotengenezwa kwa gharama kubwa hata ukipita wewe jaribu kuchungulia kwenye kioo cha gari yako utakuta michanga imesogea kabisa mpaka inataka kumaliza barabara.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana.(Makofi)