Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JOSEPH A. TADAYO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kuwa sehemu ya Bunge lako hili la Kumi na Mbili kwa mara ya kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, nikishukuru sana chama changu Cha Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini niweze kupeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita. Niwashukuru sana wananchi wa Mwanga kwa ushindi mkubwa walionipa wa kura za kishindo.

Mheshimiwa Spika, namwomba sana Mwenyezi Mungu anijaalie mimi lakini atujalize sisi sote tuweze kuwatumikia wananchi ipasavyo kwa kuwa utendaji wa Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kipindi cha miaka mitano ya kwanza pamoja na ushindi huu wa kishindo umeamsha shauku kubwa sana ya wananchi na matarajio makubwa ambayo wanayo. Kwa hiyo Mungu atujaalie tuweze kuyatimiza.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii ya hotuba ya Mheshimiwa Rais na sababu kubwa ni kwamba hotuba hii ni mwendelezo wa hotuba ya 2015 ambayo ilitekelezwa ikatutoa na kutupeleka kwenye uchumi wa kati. Ni dhahiri kwamba tukitekeleza hotuba hii mafanikio yatakayopatikana ni makubwa mno na yatatupeleka mbele sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeitazama hotuba hii nikaona pamoja na mambo mengine lakini kwakweli inatusababishia kwenye kushusha chini yale mafanikio makubwa ambayo yalipatikana kwenye miradi mikubwa ya kitaifa yaende yawaguse wananchi na kugusa uchumi wa mtu mmoja mmoja, jambo ambalo ndilo hasa wananchi wanalolitamani na kulitarajia. Naipongeza sana Serikali kwa sababu imeshaanza kutekeleza. Kwenye Jimbo langu la Mwanga tulikuwa na tatizo sugu la maji ambalo matumaini ya kuliondoa yalikuwa yanafifishwa na utendaji ambao ulikuwa hauridhishi wa mkandarasi ambaye kimsingi alikimbia site kwenye ule mradi mkubwa wa maji. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Maji kwa maana alisikia kilio chetu akachukua hatua za haraka za kuweza kusaidia na ule mradi sasahivi unaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali ni kwamba iwajali wale wafanyakazi waliokuwa chini ya mradi ule kwa sababu baada ya mkandarasi yule kuususa au ku- repudiateule mkataba na kuondoka wako wafanyakazi ambao stahiki zao hazijalipwa. Naamini kabisa kwamba kwa sababu mkandarasi amekimbia basi endapo kuna chochote anachodai Serikali inayo mamlaka ya kumkata na kuwalipa wale wafanyakazi nahata kama hakuna anachodai bado Serikali inaweza ikawalipa wafanyakazi pamoja na watu wengine waliokuwa wana mikataba na mkandarasi yule na ziko taratibu za kisheria za Serikali ku-recover fedha hizo.

Mheshimiwa Spika, naomba sana kwamba kwa kasi hiyo hiyo ambayo imeonekana kwenye miradi hii, basi miradi mingine ambayo iliahidiwa wakati wa kampeni ambayo wananchi wa Mwanga wameiomba sana itekelezwe. Kwa mfano, liko suala la mradi wa hospitali ya wilaya ambayo Mheshimiwa Rais alituahidi, kiwanja kipo tayari hekari 54, kwa hiyo tunaiomba Wizara husika basi iweze kulitekeleza jambo hilo kwa sababu litakidhi kiu na matamanio makubwa sana ya wananchi wa Mwanga. Pili, iko miradi ya umaliziaji wa vituo vya afya hasa Kituo cha Afya cha Kigonigoni ambacho kwa kweli kiko kwenye mkwamo. Tunaomba Wizara husika ilitazame suala hili.

Mheshimiwa Spika, tunashukuru Wizara ya Ujenzi kwa niaba ya Serikali kwamba kasi ya ujenzi wa barabara katika Jimbo la Mwanga inaendelea vizuri lakini bado ziko barabara, iko barabara ya Lembeni – Kilomeni mpaka Lomwe kilometa 31 ambayo tayari iko chini ya TANROADS tunaomba sasa barabara hiyo nayo itazamwe. Iko barabara ya Kisangara – Ngujini – Shingatini kilometa 25.9 na barabara ya Mgagao – Pangaro – Toroha kilometa 35 ambazo katika ngazi ya road board na RCC zimeshaombewa kuingia TANROADS. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri husika basi atusaidie barabara hizi ziingie TANROADS ili pia ziweze kupata matengenezo kama barabara zingine.

Mheshimiwa Spika, ukienda ukurasa wa 15 wa hotuba ya Mheshimiwa Rais amezungumzia mkazo juu ya uwekezaji katika sekta ya nyama. Jimbo la Mwanga ni wadau wakubwa pia wa sekta hii ya nyama kwa sababu tunayo mifugo mingi na pia eneo letu location yetu iko mahali pazuri kwa ajili ya viwanda vya nyama kwa sababu kuna Bandari ya Tanga iko karibu, kuna Uwanja wa Ndege wa KIA na pia tuko mpakani. Nafahamu kabisa kwamba nyama ya Tanzania hasa nyama ya mbuzi ina soko kubwa sana middle east huko na nafahamu kabisa kwamba ziko nchi za jirani ambazo huwa zinachukua mbuzi wetu na kuwachinjia kwao na kutoa certificate of origin wale mbuzi waonekane wanatoka kwao, lakini ukweli wa mambo wale mbuzi wanatoka Tanzania na wanapata soko zuri nje kwa sababu ya ladha yake. Kwa hiyo, tunaomba Waziri anayehusika kutukumbuka katika uwekezaji kwenye sekta hii ya nyama hasa katika eneo la Kata ya Mgagao ambapo tayari kuna mnada mkubwa unaovuta watu kutoka hata nchi za jirani.

Mheshimiwa Spika, pamoja na ombi hili, ningependa pia niseme kwamba wafugaji katika Jimbo langu kwa sababu wako wanapakana na Mbuga ya Mkomazi wanakabiliwa na changamoto zinazokabili wafugaji wengi wanaopakana na maeneo ya hifadhi. Ni vizuri Serikali ikahakikisha kwamba mipaka kati ya maeneo ya wafugaji na hizi mbuga inaeleweka na wafugaji wapewe elimu inayotosheleza na kwa kweli ni vizuri wakaongezewa maeneo ya kulisha mifugo yao. Ziko faini ambazo wanatozwa pale ambapo mifugo yao imekosea ikaingia kwenye maeneo ya hifadhi. Zile faini ni kubwa mno na kwa kweli zinakuwa ni kama zinawakomoa hawa wafugaji. Wafugaji wanaishi maisha ya mashaka sana katika mipaka na hifadhi ikiwa ni pamoja na wafugaji wa Jimbo langu la Mwanga.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa niaba ya Serikali kwa jinsi ambavyo imeweza kudhibiti suala la…

Mheshimiwa Spika, nasikia kengele imelia. Nakushukuru kwa nafasi hii.

SPIKA: Hapana ni kengele ya kwanza.

MHE. JOSEPH A. TADAYO:Ni kengele ya kwanza, ahsante.

Mheshimiwa Spika, basi kwa haraka nizungumze tu kwamba suala la kudhibiti uwindaji haramu limefanikiwa katika kipindi cha miaka mitano. Hii imesaidia wanyamapori kuongezeka, lakini baraka hii ya wanyamapori kwa baadhi ya maeneo imesumbua sana.

Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo kubwa sana la tembo ambalo limefanya maeneo ya karibu kata tano za jimbo langu yawe magumu sana au yasifae kabisa kwa masuala ya kilimo. Nilimsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu akizungumzia juu ya kuweka kambi za hawa Askari wa Wanyamapori katika maeneo ya changamoto kama hizo. Naomba hilo liharakishwe kwa sababu ziko kata tano za jimbo langu ambazo kwa sasa hivi maisha ni magumu na wako watu kadhaa ambao wameshapoteza maisha kwa ajili ya wanyama hawa tembo.

Mheshimiwa Spika, naomba kurudia kwamba naunga mkono hoja kwa dhati kabisa na tuko pamoja katika kutekeleza haya yaliyomo humuna kuisukuma mbele nchi yetu kwenda kwenye uchumi wa kati wa juu sasa. Ahsante sana. (Makofi)