Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Awali ya yote naomba niwashukuru wananchi wa Wanging‟ombe kwa kunipa kura nyingi sana nikawa Mbunge wa Bunge hili. Pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuniteua kuwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Naomba niwaahidi Watanzania pamoja na Mheshimiwa Rais kwamba nitaifanya kazi hii kwa bidii zote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi kila aliyesimama hapa amezungumza tatizo la maji kwenye eneo lake. Sitaweza kuyajibu yote, lakini nitatoa bango kitita cha kuelezea utekelezaji wa awamu ya kwanza ya programu ya maji ambayo imegusa kila Halmashauri, kila Wilaya, kila Mkoa, mji Mkuu wa Mkoa, Mji wa Wilaya; ni miradi mingi sana.
Katika awamu ya kwanza tumekuwa na miradi 1,888 na miradi 1,200 imekamilika, bado miradi 700 na kitu inaendelea na iko kwenye hatua mbali mbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru Wabunge. Bunge lililopita mliidhinisha tuanzishe Mfuko wa Maji ambapo tuliamua kabisa kwamba tuanze kwa shilingi 50 ya lita ya mafuta, tukapata shilingi bilioni 90. Sasa naomba sana, tutakapoingia kwenye Phase II ya programu ambapo tumeainisha miradi mingi yenye thamani ya bilioni 3.3 US Dollar ambayo ni sawa sawa na trilioni sita, ndani ya miaka mitano, tutatimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoiongelea kwenye hotuba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo pia ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, ambapo tunasema kwamba sasa imefika mahali tufikishe upatikanaji wa maji vijijini asilimia 85 na mijini asilimia 95. Katika miaka kumi ijayo tunataka tuseme asilimia 100 kwa vijijini na mjini lazima wapate maji, kulingana na programu ambayo tumeiandaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapofika kwenye bajeti tunaomba sana Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono ili fedha za ndani ziweze kutekeleza jambo hili. Wafadhili wameshaahidi zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kwamba watachangia kwenye hiyo shilingi bilioni 3.3 Us Dollar. Nusu tayari wameshaahidi. Kwa hiyo, ina maana kwamba Serikali lazima tutafute nusu nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ili kila mtu apate huo mradi wake, tunahitaji tupate mapato mengi ya ndani ili tuweze kutekeleza miradi hii. Kwa hiyo, naomba sana tutakapofikia mahali hapo, Waheshimiwa Wabunge, mtuunge mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme machache katika miradi ambayo inaendelea hivi sasa. Kwanza kulikuwa na mradi wa kutoa maji katika bomba la Kashwasa kupeleka Tabora - Igunga na Nzega pamoja na vijiji 89 vitakavyonufaika. Tumeshapata fedha kutoka Serikali ya India, sasa hivi tunatafuta mkandarasi, tunafanya kitu kinaitwa pre-qualification. Wataanza kuleta tender zao. Tunategemea ikifika Julai, Mkandarasi atakuwa ameanza kazi ya kujenga mradi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na kilio cha wananchi wengi wanaoishi kando kando ya Ziwa ya Victoria kwamba maji yale yaweze kupatikana. Tayari tumeshaanza miradi mingi ya kutoa maji ndani ya Ziwa Victoria kupeleka kwenye miji yote inayozunguka Ziwa Victoria. Kwa hiyo, mradi unaendelea na kazi nyingi zitaanza kuanzia mwezi wa saba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mradi pia wa kutoa maji kutoka Mto Ruvuma kupeleka Manispaa ya Mtwara na Mikindani. Tumeshakamilisha usanifu, bomba kubwa litajengwa kilometa 60 na vijiji karibu zaidi ya 29 ambavyo viko kando ya bomba lile vitapatiwa maji. Tunakamilisha mazungumzo na Serikali ya China kwa ajili ya kuweza kupata ufadhili pamoja na Serikali ili tuweze kukamilisha mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna mradi mwingine ambao utaongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Dar es Salaam. Tumekuwa na kilio na ahadi kwa muda mrefu. Sasa tumefika mahali kwamba mradi ule wa upanuzi wa Ruvu Chini utakamilika mwezi wa pili; na upanuzi wa mradi wa Ruvu Juu utakamilika mwezi wa tatu. Kwa hiyo, tukifika mwezi wa tatu matanki yote ya maji ambayo tuliyajenga kwa muda mrefu, yatakuwa yameshajaa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi tunayoendeleanayo sasa ni kusambaza maji yawafikie wananchi, kwa sababu kwenye sera ya maji tunasema upatikanaji wa maji uwe mita 400 hasa kwa wananchi walioko vijijini. Kwa wale wanaokaa mijini, tunataka tuwaunganishie maji kwenye nyumba zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kazi hii inaendelea na kwenye programu hii nina hakika kabisa tutaanza na maeneo kama ya Kimara, Kibamba, Kiluvya, kwenda mpaka Mlandizi, maeneo yale yote tutayasambazia maji baada ya kupatika wingi wa maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa eneo hili la Temeke na maeneo mengine ya upande huu pili kama Mkuranga, tuna uchimbaji wa visima Kimbiji na Mpera. Tumeshakamilisha visima nane na sasa hivi tutaingia kwenye awamu ya pili ya kujenga miundombinu ili tuhakikishe kwamba tunapata maji ya kutosha kwa wananchi wa Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda; na kwa sababu nimesema nitaleta bango kitita kwa utekelezaji wa mambo yote haya, naomba tukubaliane kwa leo kwamba mtapata report na mtatusaidia katika kujenga hoja katika kufanya miradi maeneo mengine ambayo yamebaki. Naomba kuwasilisha. (Makofi)