Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais na wananchi wa Madaba kwa kupata fursa ya kutumikia jimbo la Madaba kwa awamu ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja katika mambo makubwa ambayo yamejitokeza kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais, ni hoja na haja ya kuwa na uwekezaji jumuishi katika kilimo. Hili Mheshimiwa Rais alilipa kipaumbele kwenye hotuba yake kwa sababu kubwa tatu.

Mheshimiwa Spika, sababu ya kwanza sekta hii imeajiri zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania, lakini sababu ya pili ni kwamba asilimia kumi au zaidi ya Watanzania ambao hawajishughulishi moja kwa moja na kilimo wamejiajiri kupitia sehemu ya mnyonyoro wa thamani wa shughuli za kilimo. Wapo waliojiajiri kwenye biashara ya mazao ya kilimo, wapo waliojiajiri kwenye usindikaji kwa maana ya agro-process, wapo ambao wamejiajiri kwenye kutoa huduma za kifedha yakiwemo mabenki, SACCOS, wapo waliojiajiri kwenye usambazaji wa pembejeo, lakini pia wapo wengi waliojiajiri kwenye huduma za ugani.

Mheshimiwa Spika, sababu ya tatu ni kwamba sekta hii ndiyo inayochangia asilimia mia moja ya chakula cha Watanzania wote. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais alitoa kipaumbele kikubwa sana katika kueleza namna gani sekta hii ipewe kipaumbele na ipewe msukumo katika safari hii ya miaka mitano sehemu ya pili ya kipindi chake cha miaka kumi.

Mheshimiwa Spika, leo naomba nitoe ushauri wa namna nzuri sasa ya kutekeleza maelekezo haya, ndoto na matamanio ya Mheshimiwa Rais kwenye sekta hii ya kilimo. Vitu ambavyo au jambo pekee ambalo linamfanya Mtanzania, mkulima aende shambani akawekeze kwenye kilimo, kivutio au incentive ya mtu kwenda kulima ni upatikanaji wa soko la uhakika na tija kwenye kilimo. Mambo makubwa yanayomfanya Mwanamadaba, Mwanasongwe na Mtanzania mwingine aache shughuli zingine akalime ni soko na tija kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitoa kipaumbele miaka mitano iliyopita na kumekuwa na mafanikio, mipaka ilifunguliwa, masoko walau yalikuwa na unafuu. Hata hivyo, bado changamoto ni kubwa kwenye sekta hii upande wa tija kwenye kilimo.

Mheshimiwa Spika, nina mambo mawili ya kushauri na kabla sijashauri nimpongeze Profesa Mkenda na Naibu Waziri Mheshimiwa Bashe wameanza vizuri sana katika kukabiliana na changamoto za sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza ambalo napenda Serikali iendelee kuweka msisitizo ni kuwa na mkakati madhubuti wa masoko ya kilimo, bado hatujafaulu. Wakulima wa Madaba na maeneo mengine hata msimu huu wamepata shida ya soko la mahindi. Kwa hiyo ipo kazi kubwa ya kufanya. Namshauri Mheshimiwa Waziri aangalie sana mkakati endelevu wa kuimarisha vyama vya ushirika ili vitumike kama sehemu ya kupambana na changamoto ya soko lakini mkakati wa uwekezaji kwenye usindikaji wa mazao, sekta hii ni sekta mama ambayo itatutoa.

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ambalo nitatumia muda mrefu kulifafanua ni hili la kuwekeza kwenye kupunguza gharama za kilimo. Jitihada zilizofanyika miaka hii mitano zimeonekana za kuhakikisha kwamba wakulima wanapata masoko ya mazao lakini hata pamoja na masoko kupatikana faida ambayo mkulima anaipata kutokana na shughuli zake bado ni ndogo kwa sababu gharama za uwekezaji kwenye kilimo ni kubwa.

Mheshimiwa Spika, miongoni mwa mambo mengi yanayochangia mambo matatu nataka niyaseme. Jambo la kwanza linalochangia gharama ya uzalishaji ni upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu. Jambo la pili ni gharama za usafirishaji wa mazao maeneo ya vijijini na jambo la tatu ni upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo mkulima yupo Madaba na maeneo mengine ya vijijini, huko ndiko alikojaa Watanzania, huko ndiko wanakokaa asilimia 80 ya Watanzania na wanajishughulisha na kilimo. Moja ya vikwazo ambavyo nimevisema ni upatikanaji wa pembejeo kwa gharama nafuu. Hili la upatikanaji wa pembejeo lina mawanda mapanda, lakini moja katika maeneo ambayo nataka nisaidie na kuishauri Serikali ni uwekezaji kwenye maduka madogo madogo ya kusambaza pembejeo vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pembejeo nyingi zinapatikana mijini na huko vijijini ambapo wakulima wapo hakuna maduka ya kusambaza pembejeo. Mkulima ili azalishe anasafiri kilometa nyingi kufuata pembejeo mijini. Suala hili nililisema katika Bunge lililopita. Sasa kinachokwaza upatikanaji wa maduka ya pembejeo vijijini ni gharama za uanzishaji wa maduka. Hapa ningeweza kwenda kwa details, lakini TPRI, TFRA na TOSCI peke yao ili upate kibali cha kuwekeza kwenye duka la usambazaji pembejeo kijijini lazima uwe na laki nane ambayo haihusishi kununua mali ghafi. Sasa hatuwezi kupata mapinduzi ya kilimo kama hatutaki kutoa hizi tozo. Hatuwezi kumsaidia mwananchi wa kijijini kupata pembejeo kwa gharama nafuu kama hatutaki kupunguza hizi tozo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hili tutaenda nalo lakini naomba tulizingatie. Tuondoe hizi tozo ili tusaidie wajasiliamali wawekeze kwenye maduka madogo madogo ya pembejeo vijijini ili mkulima apunguziwe gharama za uzalishaji kilimo ili hata kama atakosa soko nzuri bado atauza kwa faida kwa sababu atakuwa amezalisha kwa gharama ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili ni gharama za usafirishaji wa mazao vijijini. Nashukuru Mheshimiwa mama Kilango amesema Watanzania wengi wamejaa vijijini, huko ndiko kwenye changamoto kubwa za miundombinu ya barabara na madaraja. Bajeti ya TARURA ni ndogo sana kuweza kukidhi mahitaji yaliyoko vijijini. Leo mkulima amelima mazao yake ili kusafirisha sehemu ambayo angesafirisha kwa shilingi laki moja anasafirisha kwa laki tano, hiyo inaongeza gharama za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa mama Kilango amesema ipo haya ya kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti TARURA ili barabara za vijijini zijengwe katika ubora, zipunguze gharama za uzalishaji kwa mkulima mdogo. Ndiyo maana nasema ni mkakati jumuishi wa sekta ya kilimo, sekta ya kilimo haiwezi kukua kama barabara za vijijini hazijaboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tatu nililotaka kuliongelea na kuishauri Serikali ni kwamba Serikali iangalie namna gani itapunguza upotevu na uharibifu wa mazao baada ya mavuno. Tafiti zinaonyesha asilimia 30 ya mazao ya mkulima yanaharibika baada ya mavuno. Sasa hii asilimia 30 kama ingeweza kufika sokoni ingempa faida huyu mkulima mdogo. Leo mkulima mdogo pamoja na gharama kubwa za uzalishaji inazotokana na kutopatikana pembejeo kwa wakati na karibu pamoja na gharama kubwa za usafirishaji bado…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana, hoja yako ni ya msingi sana lakini muda hauko upande wako.

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)