Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nami niungane na mchangiaji aliyetoka kuchangia, kwanza kukushukuru wewe binafsi kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge hili na ni mara yangu ya kwanza wananchi wamenipa ridhaa ya kuongoza ndani ya Jimbo la Rorya, Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru wewe binafsi kwa namna ambavyo, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza nimeona namna unavyoliongoza Bunge, lakini imetupa faraja hasa Wabunge wengi wapya; kwa namna ambavyo tulikuwa tunakuona nje na hakika wewe ni kiongozi bora sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kabla sijasahau Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja hotuba zote mbili za Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli; hotuba ya kwanza ilikuwa ya kufunga Bunge na ile aliyoitoa Novemba ya kufungua Bunge. Naunga mkono hoja hotuba hii.

Mheshimiwa Spika, nami niseme tu kwamba hotuba ya Rais wetu, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ilikuwa na mwelekeo chanya, ni hotuba ambayo ina matumaini mazuri kuanzia ngazi zote na sekta zote za kibiashara na kiuchumi na shughuli nyingi za ukuaji na ustawi wa jamii kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaenda kuchangia kwenye baadhi ya maeneo ambayo nimeona angalau niweze kuchangia katika kuboresha na katika utekelezaji wake utakavyokuwa.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais wetu katika hotuba yake ukurasa wa 34 na 35 amezungumzia namna ambavyo Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano chini ya Chama chetu Cha Mapinduzi, ilifanya kazi kubwa sana katika uboreshaji na uinuaji wa sekta ya maji. Nichukue nafasi hii kwa moyo wa dhati sana kumshukuru Waziri mhusika wa Wizara hii. Naweza kusema, kwa muda mfupi wa miezi hii mitatu, mimi nimepata ridhaa ya kutembelewa na Waziri wa Maji. Kwa kweli nichukue nafasi hii kumpongeza kwa kazi kubwa aliyoifanya. Ni imani yangu alikuwa anatekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais amemwagiza na ndiyo haya ambayo wananchi wetu wanatarajia kuyaona.

Mheshimiwa Spika, jimbo langu kwa asilimia 77 limezungukwa na maji; asilimia 23 peke yake ndiyo eneo la nchi kavu ambalo wananchi wanalima na kufanya shughuli nyingine za kiuchumi. Kwa miaka yetu mitano kwa chama chetu na Mheshimiwa Rais wetu, alituletea zaidi ya shilingi bilioni saba kwa ajili ya uboreshaji wa huduma ya maji. Nilikuwa naiona hapa kwenye hotuba yake hapa ameisema, hizi shilingi trilioni 2.2 ambazo zimeletwa kuinua na kuboresha sekta ya maji, sisi katika Jimbo letu ni miongoni mwa Majimbo ambayo yamepokea fedha hizi, lakini niseme tu kwamba haikutumika vizuri.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alipokuja kufanya ziara yake, ndiyo maana nimesema nianze kumpongeza, kuna maelekezo aliyatoa kutokana na namna fedha hizi zilivyotumika. Niendelee tu kumwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kukazia hapo, kwa sababu ndani ya Jimbo langu, nina changamoto kubwa sana ya maji. Unaweza kuona hiyo asilima 77 ambayo inazungukwa na maji, lakini hatuna mradi mkubwa unaotokana na Ziwa Victoria, asilimia iliyobaki 23 ndiyo maeneo ya nchi kavu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais alitupa fedha ili angalau fedha hizi ziweze kuinua na kuwasaidia wananchi wanyonge hasa akina mama lakini haijatumika sawasawa. Nachukua nafasi hii kumwomba Mheshimiwa Waziri aendelee kukazia wakandarasi wote ambao walichukua hizi fedha za umma ili angalau waweze kurudi sasa kuweza kutimiza na kumalizia hii miradi.

Mheshimiwa Spika, unaweza ukakuta mkandarasi ametekeleza mradi kwa asilimia sitini lakini amelipwa asilimia mia moja na ameuacha ule mradi hauna maji. Amelipwa zaidi ya shilingi bilioni moja na ushee. Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kukazia ili tuweze kulipata hili.

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake amezungumza namna tulivyofanya kwa miaka yetu mitano na matarajio yake ya miaka mitano kwenye sekta ya afya. Mimi nishauri kidogo kwenye Wizara yetu hii ya Afya, ndani ya jimbo langu mimi nina vituo vinne tu vya afya lakini kiukweli kwa population na wingi wa watu ulivyo, vituo vya afya hivi havitoshi na unaweza ukakuta kituo kimoja cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27. Kwa malengo mazuri ya Mheshimiwa Rais na naamini namna Waziri wa Afya anavyofanya kazi kwa muda toka amechaguliwa namwomba aitazame Rorya katika kipengele hiki cha upande wa sekta ya afya.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu unaweza ukakuta kituo kimoja cha afya kinahudumia zaidi ya vijiji 27, kina kata zaidi ya nane lakini ndani ya hicho kituo cha afya unakuta bado hakijapata huduma ya ambulance, wakati mwingine kuna changamoto kubwa sana kunapokuwa na wagonjwa kumtoa kwenye kata moja kumpeleka kwenye hospitali ya wilaya au kumsafirisha kwenda kwenye hospitali ya mkoa. Kwa hiyo, naomba na lenyewe hili ili kuendana na yale mazuri ambayo Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameyazungumza kwenye hotuba yake tuyaboreshe sasa tuendane na kasi hiyo katika sekta hii ya afya.

Mheshimiwa Spika, la tatu, Mheshimiwa Rais amegusia vizuri sana upande wa barabara na sisi wote ni mashahidi kwa kazi kubwa iliyofanyika miaka mitano iliyopita. Tuna barabara ambayo imezungumzwa kwenye Ilani toka mwaka 2010, 2015, 2020, barabara ya kutoka Mika - Shirati, lakini inanyooka mpaka Kilongo kule mpakani. Barabara hii ina umuhimu wa aina mbili, moja ni barabara ambayo inainua uchumi ndani ya Jimbo letu la Rorya, lakini ni barabara ambayo kiusalama kwa sababu sisi tuko mpakani inaweza ikarahisisha shughuli za kiusalama ndani ya Jimbo kwa sababu ni sehemu ambayo tunapatikana kwenye mpaka wetu wa Kenya, Uganda pamoja na Tanzania.

Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumuomba Mheshimiwa Waziri husika, hii barabara kwa kipindi hiki ambacho imetajwa kwenye Ilani iingizwe kwenye utekelezaji angalau wa kupatiwa lami ili wananchi wa maeneo yale tuweze kuinua uchumi wao. Pili kama nilivyosema itakuwa ni sehemu nzuri sasa pia ya kuboresha upande wa ulinzi na usalama ndani ya jimbo.

Mheshimiwa Spika, nne, nizungumzie kidogo kuhusiana na TARURA. Pamoja na mambo mazuri na makubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais, ndani ya Jimbo langu mimi la Rorya kuna shida kubwa sana ya barabara, hizi barabara za kuunganisha kata na kata na tarafa na tarafa ambapo ziko chini ya TARURA. Hivi navyozungumza kuna baadhi ya maeneo hayapitiki. Bado naamini kwa sababu ni mwanzo mzuri ambapo Serikali yetu ndiyo imeanza kufanya kazi chini ya Waziri Jafo, aone namna anavyoweza kutusaidia kwenye hii sekta hii ili angalau sasa tuendane na yale mazuri yaliyotajwa kwenye Ilani yetu hii na kwenye hotuba yetu ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumzie kuhusiana na wavuvi. Kwenye ukurasa wa 19, Mheshimiwa Rais amezungumza vizuri sana juu ya maboresho ya kodi na tozo mbalimbali zinazotolewa upande wa wenzetu wavuvi. Wabunge wote ambao wanatoka Kanda ya Ziwa watakuwa mashahidi, ilikuwa ni kazi kubwa sana kwa mwaka jana 2020 kupata kura kutoka kwa wananchi wanaofanya shughuli za uvuvi.

Mheshimiwa Spika, naomba kwa sababu Mheshimiwa Rais ametoa mwongozo mzuri sana kuhusiana na kupitia tozo zote ambazo zinawagusa wavuvi, Wizara kwanza ikae na hawa wavuvi wawape elimu na ipitie tozo hizo. Mimi nadhani si busara nzuri sana unapomkuta mvuvi anafanya biashara haramu ukamchomea mtumbwi wake kwa sababu wakati mwingine unakuta ule mtumbwi yeye mwenyewe siyo wa kwake, ameazima au amekodisha kutoka kwa mtu mwingine. Kwa hiyo, si tu kumrudisha yule mvuvi nyuma bali unamuathiri hata yule mmiliki halali wa ule mtumbwi.

Mheshimiwa Spika, wale wavuvi ndani ya jimbo na Kanda ya Ziwa wamekuwa wanalalamika kwa muda mrefu sana. Naiomba Wizara kipindi hiki turudi sasa tuone namna gani tunaweza tukapitia tozo lakini hata maboresho ya sheria ili angalau wale wenzetu wanaofanya shughuli za uvuvi wasiendelee kila siku kulalamika kwamba wanaonewa.

Mheshimiwa Spika, nikiri kwamba inawezekana wapo kweli wanaofanya biashara haramu na hawa sina maana kwamba tunatakiwa tuwatetee lakini wako ambao wananunua na wanapewa risiti halali kutoka kwenye maduka halali na wanakwenda kufanya biashara ile ya uvuvi. Mvuvi anakutwa ziwani ana risiti zote, ana mtego au ana nyenzo ile ile aliyonunua lakini wale watu wanamwambia kwamba wewe mtumbwi wako hauna uhalali wowote.

Mheshimiwa Spika, natamani sana Mheshimiwa Waziri kwenye kipengele hiki, maeneo yote ya Kanda ya Ziwa wakae wazungumze na hawa wavuvi na cha kwanza kabisa tutoe elimu. Kabla ya kumkamata uvuvi na kumpa kesi ya uhujumu uchumi, ningetamani sana tukae nao tuwaelimishe kwa sababu naamini mlinzi na mtetezi wa kwanza wa hizo maliasili ni mvuvi mwenyewe. Sisi Wabunge ambao tunatoka maeneo ya uvuvi, tuko tayari kutoa ushirikiano, wapewe elimu ili tuone namna gani tunanusuru hayo maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho nizungumze kidogo kuhusiana na rasilimali zetu. Moja kati ya kazi ya Mbunge ni pamoja na kutetea na kulinda maslahi ya wananchi na Serikali yetu kwa ujumla wake. Nilisema hili kwa sababu naamini Mheshimiwa Jafo ni mtendaji mzuri na anafanya kazi na anafuatilia sana utendaji na kulinda rasilimali za nchi.

Mheshimiwa Spika, kuna gari letu sisi ndani ya Halmashauri ya Rorya. Tulipewa gari hili na Serikali yetu kwa upendo kabisa toka mwaka 2009 lakini leo limekuwa na mkanganyiko mkubwa sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Jafari, Mbunge wa Rorya.

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)