Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa huu ni mchango wangu wa mwisho kwa Wizara hii ya TAMISEMI, hususan kwa Bunge hili la Kumi na Moja, ninaomba nisajili mchango wangu wa ushawishi wa leo, ushawishi wa kesho mwezi Oktoba na kwa matumizi ya vijana wa karne hii na karne inayokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya ujenzi wa Tanzania mpya imefanywa na Mawaziri wengi. Lakini kipekee kabisa Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetimiza ndoto za ujenzi wa taifa jipya kifkra na kimtazamo. Wizara hii imefanikisha ujenzi wa Tanzania katika Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya, Sekta ya Miundombinu na katika maeneo mbalimbali. Wizara hii haikuijenga tu Tanzania, haikujenga tu Taifa, bali imejenga na imeimarisha mitazamo chanya ya kifikra na kimantiki ya wazalendo wapya hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuona Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kuwa ni kiongozi wa pili wa Taifa letu hili ambaye amefanikisha na anafanikiwa sasa kuzalisha wazalendo wapya hapa nchini. Na hii inajidhihirisha kwa mitazamo yake ya kielimu kama mwalimu, mitazamo yake ya kifkra kama mwanafalsafa wa Hapa Kazi Tu, na anatendea haki mitazamo yake hii ya Hapa Kazi Tu kwa kuwataka Watanzania wote kuchapa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wetu ni kiongozi mwenye misimamo isiyoyumba katika kufanya maamuzi. Na katika wazalendo ambao ninawaona Mheshimiwa Rais amefanikiwa kuwatengeneza, si mwingine bali ni wengi isipokuwa kipekee nimtaje Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Selemani Jafo. Amekuwa mkweli, hodari na mchapakazi mwenye kufika kila eneo, hasubiri Mheshimiwa Rais anapokwenda, yeye anatangulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunampongeza sana na kumtakia kila la heri katika wajibu wake. Na tunaamini wananchi wa Kisarawe watamchagua kwa wingi sana na pia hakutakuwa na ushindani katika jimbo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI, pamoja na mapambano tunayoendelea nayo ya Ugonjwa huu wa Corona, niombe sasa Ofisi hii ya Rais, TAMISEMI kutoa maelekezo ya makini kabisa kwa watendaji wote wa kata na vitongoji kutoa maelekezo kwa wenyeviti wote wa vijiji na vitongoji pamoja na wenyeviti wa mitaa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 9 ya Katiba yetu ambayo inatambua misingi ya uendeshaji wa nchi yetu kwamba ni misingi ya kijamaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, kwa viongozi wote hawa ofisi ya Rais TAMISEMI sasa itoe maelekezo kwa kuwataka viongozi hawa kufanya kazi kama mchwa ili kuweza kutambua katika maeneo yao wale wageni wanaoingia, wenyeji waliopo, wagonjwa waliopo, lakini pia kutambua wale wahalifu katika maeneo yao. Hii ni misingi ambayo tunaitambua nchi yetu inafuata iliyopo katika Ibara ya 9 ya Katiba yetu, misingi ya ujamaa na kujitegemea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe pongezi na shukrani sana kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, kwa namna ya kipekee kabisa Waziri wa TAMISEMI ametambua kwamba Rufiji ilizaliwa miaka 600 iliyopita, na kwa kutambua hilo amegundua kwamba wafanyakazi wa Halmashauri ya Rufiji wanafanya kazi katika jengo lililojengwa mwaka 1889, akaona ni bora wafanyakazi hawa awafikirie na kukubali kutoa fedha za ujenzi wa jengo jipya la Halmashari ya Wilaya ya Rufiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakupongeza sana na tukuombe Mheshimiwa Waziri sasa wataalam wako wanaoandaa michoro na BOQ kutuharakishia sana kwa sababu wananchi wa Rufiji wana kiu kubwa ya kupata jengo jipya kutokana na jengo lao hili kudumu zaidi ya miaka 100 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hiyo, niombe sasa Ofisi ya Rais TAMISEMI kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya ya Rufiji kwa kuwa hospitali iliyopo ilijengwa mwaka 1960 ikihudumia Wilaya za Kilwa na Rufiji pamoja na wilaya ziliopo karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na athari za mafuriko ambayo Rufiji imepata nimuombe Mheshimiwa Waziri Jafo, miaka kadhaa iliyopita niliomba fedha za ununuzi wa boti, mafuriko yametuletea shida kiasi kwamba hatukuwa na boti katika maeneo yetu. Kwa hiyo, kuna fedha Mheshimiwa Waziri alishatoa shilingi milioni 200, kwa bahati mbaya sana fedha hizi zilirudishwa tena TAMISEMI. Nikuombe Mheshimiwa Waziri utakapokuja kufunga hapa watangazie wananchi wa Rufiji kwamba sasa ile milioni 200 umeirudisha Rufiji ili tuweze kununua boti kuwasaidia wananchi wetu ambao watapata maafa ya mafuriko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, athari za mafuriko zimekumba baadhi ya vituo vyetu vya afya ikiwa ni pamoja na Kituo cha Afya cha Muhoro. Muhoro kuna watu takribani 25,000 lakini sasa hivi wanakosa huduma za afya kutokana na athari kubwa ya mafuriko ambayo tumeipata. Nikuombe Mheshimiwa Waziri ukiwa unafunga hapa sasa utuambie zile fedha za dharura zilizopo katika Wizara yako muweze kuzitenga kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Muhoro pamoja na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Ngorongo ambao leo hii hawawezi kwenda Kata ya Kipugira kwa ajili ya kupata huduma za afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo barabara ya TARURA, barabara ya kutoka Utete kwenda Ngarambe. Nimuombe Mheshimiwa Waziri aangalie uwezekano wa kukarabati barabara hii. Barabara hii iwapo itakarabatiwa basi itawezesha mizigo inayotoka kule Dangote inayokwenda kwenye mradi wa Rufiji kwa kuwa mradi huu ni kipaumbele cha Mheshimiwa Rais namba mbili kabisa baada ya Mradi wa SGR, kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwa kutambua kazi kubwa Mheshimiwa Waziri anayofanya, tunatambua leo hii anajenga Daraja la Mbuchi kule Muhoro. Lakini anapojenga Daraja la Mbuchi pale Muhoro mafuriko yamekomba Daraja la Muhoro kwa hiyo nimuombe kwa fedha zile anazoanza kule Mbuchi aanze sasa kujenga Daraja la Muhoro ili wananchi waweze kupita Muhoro waweze kwenda Mbuchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunatambua kiasi cha fedha nyingi ambacho Wizara yake imetoa katika eneo la elimu, eneo la afya, zaidi ya shilingi bilioni tano imeingia katika eneo la elimu na eneo la afya. Kwa Mtanzania asiyetambua mchango huu atakuwa na matatizo kichwani mwake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)