Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Wabunge wenzangu kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kazi nzuri anayowafanyia Watanzania kwa miradi mbalimbali ambayo imefanywa katika nchi yetu. Kazi zilizofanywa na Serikali hususani katika nchi yetu ni nyingi na ndiyo maana baadhi ya Wabunge wamesema na mimi naungana nao Mheshimiwa Rais huyu kwa kazi alizozifanya ndani ya miaka minne na zaidi, nadhani kwa sababu tuna ugonjwa huu wa Corona, tuna tatizo pia ambalo limeingia katika nchi yetu hasa miundombinu kuharibiwa na mvua ambazo zimenyesha nyingi sana, imevuruga mipango ya Rais ambayo alikuwa ameipanga katika miaka mitano na katika miaka mitano tena iwe kumi, kwa sababu mipango itakuwa imeharibika kutokana na haya mawili niliyoyataja, nadhani Bunge linalokuja iletwe Katiba hapa aongezewe miaka mitano mingine mbele ili aweze kukamilisha ndoto za Watanzania ambazo amepanga ziweze kutimia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija na ndugu yangu Mheshimiwa Jafo ambaye ndiye anasimamia Wizara hii, kwa kweli mdogo wangu Mheshimiwa Jafo amefanya kazi kubwa sana, pamoja na wanaokusaidia Naibu Mawaziri wawili, Katibu Mkuu na wataalam wote katika Wizara hii. Ukiangalia ukurasa wa 54 unasema tulikuwa na vituo 535 sasa tuna vituo 968 vikiwepo na vya Makambako. Kwa hiyo, Mheshimiwa Jafo amefanya kazi kubwa sana. Kwa sababu amewafanyia kazi Watanzania naye tunamwombea kwenye Jimbo lake kule asitokee mpinzani upite bila kupingwa pamoja na wanaokusaidia nao wapite bila kupingwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wapo wasaidizi wa Rais akiwepo Waziri Mkuu, kazi kubwa anayowafanyia Watanzania kwa kuzunguka, jana tu tumemwona alikuwa Zanzibar, anawazungukia Watanzania kutekeleza shughuli ambazo Rais amezipanga. Naye Waziri Mkuu kule Ruangwa, mimi na Wabunge tunakuombea upite bila kupingwa. (Makofi/Vigelelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile na dada yangu Mheshimiwa Jenista kwa kazi anazozifanya namwombea kule Peramiho apite bila kupingwa ili aendelee kuwatumikia Watanzania. Pia Spika wetu Job Ndugai kwa kazi kubwa anayoifanya ndani ya Bunge hili kuwatumikia Watanzania naye tunamuombea apite bila kupingwa. (Makofi/ Vigelegele)

MBUNGE FULANI: Naibu Spika kule Mbeya.

MHE. DEO K. SANGA: Lakini na wewe Naibu Spika mdogo wangu, Mheshimiwa Tulia tunakuombea kule Mbeya upite bila kupingwa ili uweze kuwatumikia Watanzania. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maombi haya, nirudi sasa kwenye Jimbo langu la Makambako.

MBUNGE FULANI: Na wewe upite bila kupingwa.

MHE. DEO K. SANGA: Watanzania wakiwepo wa Jimbo la Makambako nawapenda sana, wanajua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye Jimbo la Makambako. Miradi iliyotekelezwa kwenye jimbo langu ni mingi sana. Ombi langu ni dogo tu kwa Watanzania hususani Jimbo la Makambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tuna mradi mkubwa ule wa fedha za kutoka Serikali ya India kwa mkopo nafuu. Mradi ule tumewaambia wananchi mara nyingi sana na kwa muda mrefu kwamba mradi utatekelezwa. Kwa sababu Wizara inayohusika wako hapa, naomba waone namna ya mradi ule kuweza kuanza katika mji wetu wa Makambako. Tunashukuru kwamba kuna miradi ipo inayoendelea ikiwepo pale Mawande, Lingala, Nyamande na pale Ikeru. Miradi hii inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, nikija kwenye Vituo vya Afya, ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri, pale kituo chetu kipya cha Lyamkena kimeshafikia asilimia 99. Tunaomba vifaa tiba pamoja na wataalam ili kituo hiki kianze kufanya kazi iliyokusudiwa ikiwepo pia na hospitali ya Halmashauri yetu ambayo imejengwa pale Mlowa na imefikia asilimia karibu 100. Tunaomba kupata vifaa tiba ili ianze iweze kuhudumia Wanamakambako.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile upande wa Kituo cha Afya cha Makambako cha zamani, nimemwambia Mheshimiwa Jafo mara nyingi kwamba hatuna wodi ya wanaume; na wanaume wanaugua. Kwa hiyo, ombi langu tuone namna ya kupata fedha tuwapelekee tuweze kujengewa wodi ya wanaume.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija upande wa umeme wa REA, Waziri mwenye dhamana, haki ya Mungu nitoe neno la shukrani kabisa. Kwenye Halmashauri yangu kimebaki kijiji kimoja tu kupata umeme. Naomba kwa sababu nacho ni kimoja, kiweze kumalizwa. Nacho ni Mtanga. Vijiji vingine vyote tumeshapata umeme. Kwa hiyo, kilichobakia ni maeneo madogo madogo ya Vitongoji kuwapelekea. Kwa hiyo, tunakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na timu yako kwa namna ambavyo mnatujali kupitia Rais wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni watu wa NIDA, Waziri mwenye dhamana yuko hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Spika, basi baada ya maelezo haya, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nakushukuru sana, ahsante sana.