Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Josephat Sinkamba Kandege

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalambo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa
Spika, nakushukuru kwa fursa ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu ambao wamepongeza hotuba nzuri sana ambayo imewasilishwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwa dakika tano na hoja ambazo zimeibuka kuhusiana na Wizara ya TAMISEMI sina uhakika nitagusa ngapi lakini kwa sababu tarehe 8/4/2020 Mheshimiwa Waziri wa Nchi atakuwa na fursa ya kuwasilisha hotuba yake, ufafanuzi tutautoa na tutakuwa na muda wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, sasa niruhusu nipitie machache katika kutoa ufafanuzi. Kuna hoja ambayo ilikuwa imeibuliwa na Mheshimiwa Engineer Chrisotpher Chiza ambayo ilikuwa inahusu ushauri katika majengo ya Serikali na hasa katika maeneo ambayo kuna matukio mengi ya radi, akashauri Serikali ianze kuweka vitega radi. Naamini katika maeneo ambayo yanapata tatizo kubwa ni pamoja na Mkoa wa Kigoma na mikoa mingine. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanatoka maeneo ambayo kuna usumbufu mkubwa wa radi, wazo hili sisi kama Serikali tumelichukua na tulishaanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika majengo yote ya Taasisi za Umma ambayo yataendelea kujengwa tutahakikisha kwamba tunaweka vitega radi, kwa sababu pale ambapo radi inatokea athari zake zinakuwa kubwa. Ni vizuri pia hata wananchi sisi Waheshimiwa Wabunge tutumie fursa kuelimisha wananchi kwa sababu gharama yake wala sio kubwa sana katika kuweka vitega radi.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambayo ilikuwa imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi kidogo akiwepo Mheshimiwa Vulu, Mheshimiwa Bobali Hassan, Mheshimiwa Christina Ishengoma, Mheshimiwa Livingstone Lusinde ikiwa inaongelea suala zima la TARURA pamoja na kazi nzuri ambayo inafanyika, lakini wameomba kwamba ikiwezekana bajeti ya TARURA itazamwe.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba maeneo mengi TARURA imekuwa ikifanya kazi vizuri ukiachilia mbali huo ufinyu wa bajeti, lakini pia ni vizuri pia tukakumbushana kwamba pamoja na kwamba TARURA inahudumia takribani kilometa 108,942, pia TANROAD nayo ambayo ina mzigo mkubwa kwa sababu barabara zake nyingi ambazo zinajengwa ni zile za kiwango cha lami ambayo gharama yake ni kubwa, lakini ni ukweli usiopingika na baada ya hili Serikali kulitambua tumeanza kupitia formula ambayo itasaidia.

Mheshimiwa Spika, pia ni ukweli usiopingika kwamba tukitegemea bajeti hii ambayo tunatenga kila mwaka kwa ajili ya kujenga Taasisi kubwa kama TARURA, fedha hii haitoshi. Ndiyo maana Serikali inatumia vyanzo vingine kuhakikisha kwamba tunaijengea uwezo TARURA kama ambavyo hata mwanzo TANROADS ilijengewa uwezo ikasisimama vizuri ili iweze kufanya kazi kama ambavyo inatarajiwa na Watanzania.

Mheshimiwa Spika, ni ukweli usiopingika kwamba tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015 bajeti imekuwa ikiongezeka kwa kadri inavyopatikana. Tunaendelea kuijengea uwezo TARURA ili ifanye kazi nzuri kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wengi wamesifia kazi nzuri ambayo inafanywa na TARURA.

Mheshimiwa Spika, iko hoja ambayo iliibuliwa na Mheshimiwa Mohamed Omar Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji ambayo inahusu Jimbo lake ambako kumepatikana mafuriko makubwa sana, lakini kipekee akawa anaomba kwamba Kituo cha Afya kile ambacho hakiwezi kutumika hata baada ya kwamba mafuriko yameondoka, basi ni vizuri Serikali ikatazama uwezekano wa kujenga Kituo cha Afya kipya.

Naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge, avute subira kama ambavyo nimesema kwamba kuanzia tarehe 8, bajeti yetu itawasilishwa, atapata ufafanuzi ulio mzuri kuhusiana na nini ambacho tumepanga kufanya.

Mheshimiwa Spika, kuna hoja pia ambayo imeibuka ambayo ni vizuri nikatumia fursa hii kutoa ufafanuzi; kuna Kampuni ambayo inajenga Stiegler’s Gorge kule ambapo kumekuwa na ubishano, service levy ilipwe wapi? Je, inatakiwa ilipwe sehemu ambayo Ofisi iko kwa maana ya Kinondoni au ilipwe sehemu ambayo mradi unatekelezwa?

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa maelekezo mahususi; Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeelekeza service levy inatakiwa ilipwe kule ambako mradi unatekelezwa na wanufaika ni Rufiji pamoja na Morogoro vijijini. Kwa hiyo, hoja ya kwamba Ofisi iko Kinondoni ndiyo eti service levy ikalipiwe Kinondoni, siyo sahihi hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)