Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. William Mganga Ngeleja

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa fursa hii na naungana na wenzangu kumuunga mkono mtoa hoja Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Hotuba hii ni elekezi kwa maana ya utendaji Serikalini lakini pia mengi yaliyozungumzwa sisi ni mashahidi yanavyoendelea katika maeneo yetu tunakotoka. Ni ukweli ambao haufichiki kwa kweli, nikisema almost kila Jimbo limeguswa labda nitakuwa nazungumza kwa niaba ya wenzangu ambao mahali pengine sina taarifa sahihi, lakini ukweli ni kwamba, mambo makubwa sana ndani ya miaka mitano hii yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano tu, sisi huko Sengerema kwa mfano kwenye bajeti hii ambayo tunaihitimisha tarehe 30 mwezi Juni, tumetengewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya jambo jema kabisa kama ambavyo zimo halmashauri nyingine 26 ukijumlisha na kwetu tunakuwa na 27. Taarifa ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inaonesha kwamba kwenye bajeti hii ambayo 2018/2019 kulikuwa na hospitali za halmashauri 69 zimejengwa, kwa hivi ni jambo kubwa ambalo hatukuwahi kulifanya miaka mingi toka nchi yetu ipate uhuru.

Mheshimiwa Spika, pia huko Sengerema wamenituma niipongeze Serikali kwa kutenga fedha shilingi milioni 750 kwenye bajeti ambayo itaanza tarehe 01Julai, mwaka huu kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala, jengo la Mkurugenzi pamoja na ofisi nyingine. Sisi tunasema ahsanteni sana Serikali kwa kutujali, kwa kutukumbuka, kama ambao mnawakumbuka maeneo mengine, hatuwezi kuyazungumza yote kwa sababu mijadala ya kisekta inakuja.

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu waliochangia kukupongeza wewe kama Kiongozi wetu Mkuu wa Mhimili huu, wewe pamoja na Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge hili Tukufu wakisaidiwa na Watendaji wakiongozwa na Katibu wa Bunge, Ndugu Kagaigai mmefanya kazi kubwa sana. Ni vyema tuweke kumbukumbu sahihi, pamoja na kwamba Bunge hili majukumu yake ya msingi ni ya kutunga sheria na kuisimamia Serikali, lakini yako mambo ya msingi wewe uliyoyafanya ni vyema taifa likaendelea kuyakumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja, umelifanya Bunge hili litoke kwenye utengaji kazi wa analogy tukahamia kwenye digital, tunafanya kazi kwa kutumia mitandao, umelifanya Bunge liwe e-parliament ni jambo la msingi sana tunakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ukisoma hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye ukurasa wa 18 aya 32 utaona pale Serikali inakiri yenyewe kwamba michango ya Bunge lako Tukufu imesaidia sana kuanzisha Mfuko wa Maji, lakini pia tukatengeneza utaratibu wa kuanzisha chombo maalum kwa ajili ya maji vijijini (RUWASA) jambo la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa tunakupongeza wewe na wasaidizi wako kwa namna ambayo ulisaidia kusimamia hii hoja hatimaye Serikali kwa kushirikiana na wewe, kwa kushirikiana na Bunge Tukufu hili tukafanikiwa kuanzisha hiki chombo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ambalo tunakukumbuka wewe, Mheshimiwa Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wetu ni kwa kuanzisha na mimi nazungumza hapa nikiwa na interest, kuianzisha ile Kamati ya Sheria Ndogo, naomba Waheshimiwa Wabunge wanisikilize vizuri hapa, simaanishi kwamba Kamati ya Sheria Ndogo ni ya muhimu sana, lakini wenye historia ya Bunge hili wanafahamu hii ni kamati ambayo imekuwa ikiingia na kutoka. Tunafahamu ilishaingia huko nyuma ikatoka, ikarudi ikatoka na sasa imeingia tena.

Mheshimiwa Spika, umefanya jambo kubwa sana tunakupongeza kwa sababu yale ambayo tunayafanya sisi chini ya uongozi wetu wa Mheshimiwa Chenge kwa kushirikiana na Waheshimiwa Wabunge kwa ujumla kama kusingekuwa na kamati mahsusi maalum kuzungumzia mambo haya na hii ni Kamati inayoshughulika na Sheria Ndogo. Masuala ambayo kila siku ndiyo yanasimamia uendeshaji wa maisha ya Watanzania, ina maana kwamba wananchi kwa kiwango kikubwa wangekuwa wanaumia kwa yale ambayo Serikali ilipitiwa ama kwa kutoyaona au kwa kutoyapa tu nafasi yake na sisi tunakuja kuyabaini na kuyafanyia kazi. Kwa hiyo tunakupongeza sana, lakini tujipongeze wote kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la nne ambalo napenda kuliweka kwenye kumbukumbu zaidi ni kwa namna ambavyo una-support suala la michezo. Suala la michezo si la mchezo, suala la mchezo ni fursa lakini suala la mchezo ni afya na suala la mchezo ni kiwanda kinachotembea. Tukizungumza kwa muktadha wa hapa Bungeni mimi ni Mwenyekiti wa Bunge Sports Club, nakupongeza na kukushukuru sana kwa namna ambavyo umetupa support kwa miaka mitano yote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze jambo moja ambalo nimelibaini kwenye hotuba hii. Ukisoma mafungu haya na hasa uchambuzi wa Kamati ya Bajeti. Wanasema kwenye bajeti makadirio ya fedha iliyotengwa mwaka mpya wa fedha unaokuja hatujatenga fedha kwa ajili ya ushiriki wa michezo kwa Bunge hili, kwenye mashindano ya Mabunge ya Afrika Mashariki. Nina ushauri, ni jambo la kawaida kwamba na tunafahamu wenye historia nzuri katika mashindano haya kwamba kwa kila nchi ambayo inakuwa ndani ya mwaka huu wa mashindano ina Uchaguzi Mkuu taratibu zinaruhusu nchi hiyo isishiriki.

Mheshimiwa Spika, nataka nitofautishe ushiriki na mashindano haya yanakofanyikia mwaka huu, mwenyeji wa mashindano haya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka huu ambayo yatafanyika mwezi wa 12 yanafanyikia Jijini Arusha na wenyeji wa mashindano haya ni Bunge la Afrika Mashariki. Kiutaratibu wenyeji ni EALA, lakini kiuhalisia yanafanyikia Tanzania. Naomba Bunge lako Tukufu litafakari vizuri na hasa Kamati ya Bajeti, ile nadharia ya kwamba nchi ambayo ina Uchaguzi Mkuu isishiriki mazingira ya mwaka huu ni tofauti. Jambo la pili juu ya hilo ni kwamba gharama zake kwa mwaka huu kwa sababu mashindano yanafanyika ndani ya nchi ni ndogo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, nafanya hesabu tu rough hapa, sisi kwa mahesabu tuliyofanya kwa ushiriki wa mwaka huu tukichukulia wachezaji 100 ambao wanaweza kwenda kushiriki pale Arusha gharama yake haifikii hata silimia 50 kama mashindano yangefanyika nje ya nchi. Kwa hivyo, najaribu kuzungumzia hili jambo tulitafakari vizuri wakati tunaendela kufanya majadiliano kadri ambavyo majadiliano yanaendelea, kwa sababu kadri tunavyozungumza kwa mfumo tulionao wa bajeti, ndipo pia tunaweza kupata fursa nyingine za kurekebisha mahali hapa ama kule. Kwa hiyo tulikuwa tunaomba sana turuhusiwe.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo napenda kulizungumzia ni lile ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelizungumzia kuhusu mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara Tanzania. Ni kweli takwimu zinaonesha kwamba tumesogea kidogo kutoka namba ya 144 tukasogea nafasi ya 141, lakini hii inaonesha mazingira yetu ya ufanyaji biashara na uwekezaji bado tuna changamoto kubwa. Ile blueprint ambayo imetayarishwa na wataalam wetu nashauri kwamba ifanyiwe kazi, tuitekeleze rasmi kwa sababu inafungua fursa lakini pia inarekebisha kasoro nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho kasoro moja, mimi ni mpenzi wa kuwa na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na umma kikanda. Tunafahamu Dodoma kuna Chuo Kikuu cha Serikali, Dar es Salaam vipo, Nyanda za Juu Kusini Mbeya kipo, Arusha kipo, lakini mikoa saba ile ya Kanda ya Ziwa hatuna. Pale Sengerema Sekondari Mheshimiwa Profesa Ndalichako Waziri wa Elimu yuko hapa ni shahidi, kwa maboresho yaliyofanyika kwenye shule kongwe Tanzania na Sengerema Sekondari ni eneo lisilopungua ekari 143, linafaa kabisa kama Serikali itaamua kutafakari vizuri. Tuigeuze ile Shule ya Sekondari kuwa Chuo Kikuu, lakini hilo naiachia Serikali itaendelea kutafakari.

Mheshimiwa Spika, la mwisho Corona; naomba uniongezee dakika moja katika hili, nataka nizungumze kama mwananchi wa kawaida ambaye sina taaluma yoyote katika masuala ya afya, lakini nataka nizungumzie jambo moja la kimapokeo. Tumekuwa tukielezwa kwamba iko tiba ya mafua ambayo ni ya kienyeji ile ya kujifukizia, sijaelewa ni kitu gani ambacho kimetukumba kama Taifa, sina taarifa sahihi lakini mimi nafahamu pale Muhimbili hasa MUHAS pale kuna Kitengo cha Tiba Mbadala. Yaliyotokea China leo wamedhibiti ugonjwa wa corona huu hatufahamu siri zake kwa sababu siri zote hazijitokezi. Ninachotoka kusisitiza na kuliomba Bunge lako Tukufu, wewe unaweza kutumia Kanuni ya 5 kutoa mwongozo kwa Serikali ama Serikali itafakari. Kwa nini hii tiba mbadala ya kimapokeo ambayo wengi tumetibiwa na tukapona kwa miaka mingi hatuipi nafasi katika vita hii.

Mheshimiwa Spika, tuna corona hapa ambayo ni janga la kidunia.

SPIKA: Mheshimiwa Ngeleja, malizia.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, hili janga naomba kila nchi ipambane na hali yake kwa mazingira iliyonayo. Kama tulivyosema China hatujajua kitu gani kimewafanya wakadhibiti, lakini kama hili jambo halina madhara kuli-promote kwa maana ya Serikali kulizungumza Watanzania wakafanya.

Mheshimiwa Spika, chukulia mfano kila mtu ajifukizie asubuhi yeye na familia yake, kuna hasara gani kama tumejifukizia na tukapata nafuu lakini itatokea nini kama inawezekana kujifukizia kunatibu halafu sisi hatuipi nafasi hii fursa, maana yake ni nini.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, narudia tena kuunga mkono hoja, lakini naomba jambo hili mlitafakari vizuri. Ahsante.