Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Mimi nitakuwa na masuala mawili. La kwanza ni la Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, imetaja kazi nzuri sana alizofanya Mheshimiwa Rais katika nchi yetu na kila mtu anajua kwa sababu kuna uchaguzi, mimi nilikuwa natoa tu mapendekezo; ili kasi hii iendelee, nawaomba Watanzania wote tumpitishe Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli katika uchaguzi ujao ndani ya chama na kwenye Uchaguzi Mkuu ili aweze kugombea peke yake, kwa sababu kazi aliyoifanya ni kubwa, kubwa, kubwa sana na ya kupigiwa mfano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu alikuwa anamsaidia vizuri sana Mheshimiwa Rais, nawaomba wapiga kura wa Jimbo la Ruangwa, pamoja na demokrasia, apite bila kupingwa. Vile vile wa tatu; na hili simung’unyi maneno; katika miaka mitano ndani ya Bunge hili, Mheshimiwa Spika, wetu, Bunge hili umeliongoza vizuri sana, sana, sana na mabadiliko tumeyaona. Nawaomba wapigakura wa Kongwa na wanisikie hao Wagogo watani zangu wakupitishe bila kupingwa ili kusudi kasi hii iliyopo iweze kuendelea. Baada ya huo utangulizi, nilisema nitazungumzia mambo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, wachangiaji wote waliosimama wamezungumzia kuhusu homa kali ya mapafu (Corona Virus); nami nitajikita hapo hapo mwanzo mpaka mwisho, kwa sababu ugonjwa huu unatesa dunia.

Mheshimiwa Spika, naomba tuungane na Mheshimiwa Rais kuliombea Taifa letu ili shetani huyu Corona Virus aweze kuishia huko aliko. Naomba tusilete siasa katika ugonjwa huu. Ugonjwa huu ni mbaya, ni mbaya sana. Kirusi hiki ni tofauti na virusi vingine. Ni kirusi ambacho hakionekani, hakishikiki na wala hakijulikani, kiko kimya, kinaambukizwa kwa mfumo wa hewa. Naomba sana, hili tumwombe Mwenyezi Mungu atusamehe, atuepushe na ugonjwa huu hatari wa Corona Virus.

Mheshimiwa Spika, nimekuwa nikisikiliza mara nyingi katika mitandao na ili tusaidiwe, tuombe wataalamu wetu; najaribu kumtazama hapa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla ambaye ni mtaalamu wa milipuko, simwoni, wangetusaidia pamoja na Mheshimiwa Dkt. Ndugulile. Tunaambiwa kwamba ugonjwa huu unaambukizwa kwa hewa; mtu anapopiga chafya, anapokohoa. Sasa hizi masks ambazo tunatakiwa tuvae usoni kuziba midomo na pua, lakini hizi masks bei yake ni kubwa sana. Mtanzania wa kawaida wa kule Sumve, Ruangwa na Kongwa hawezi kumudu kuzinunua.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu na ninafikiri unakubalika; nimemsikiliza mtaalamu jana anasema kwamba tunaweza tukatumia vitambaa kama mask. Bahati nzuri kama utaruhusu na kwa sababu shule nyingi zimefungwa sasa na baadaye zitafunguliwa, nina mfano wa mask kwa ajili ya watoto wa shule ambazo ni kitambaa. Bei yake ni chini ya shilingi 500/= kwa mask moja ya kitambaa ambayo inazuia.

Mheshimiwa Spika, pili…

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Ndassa.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Naam.

SPIKA: Eeh, pokea kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa msemaji ambaye anaongea kwa lengo la kumsaidia tu katika mchango wake kwamba kwanza ugonjwa wa COVID 19 hausambazwi kwa njia ya hewa. Ni ugonjwa ambao unasambazwa na kutokana na maji maji ambayo yanatokana na chafya kwenye pua au mdogo wake yanapomfikia mtu mwingine na au akishika maeneo ambayo mtu amepigia chafya au maji maji yale ya kutoka kwenye mdogo yatapokuwa yamedondokea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika maambukizi haya, yeyote kati yetu akipata maambukizi ni kwamba, moja alikuwa karibu na mtu ambaye alikuwa na ugonjwa huu akampigia chafya au akamkoholea au ameupata kwa kushika sehemu ambazo mtu alipiga chafya au akakohoa naye akashika uso wake, akashika macho, pua au mdomo. Ndiyo maana wakati tunaingia hapa nimewaambia Waheshimiwa Wabunge, ukipata ugonjwa huu, hiyo ni kati ya mikono yako. Usafi wa mikono yako ndiyo inaweza ikakukinga.

Mheshimiwa Spika, la pili ambalo nataka nilitolee ufafanuzi, masks za vitambaa havizuii virusi wala bacteria. Havimkingi mtu kupata virusi vya Corona. Kwa hiyo, tuwe waangalifu sana na aina ya masks tunazozitumia. Kuna masks ambazo ni surgical mask na N95 ambazo zimethibitishwa pasipo shaka kwamba zinaweza zikazuia virusi au kumkinga mtu.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya kwa taarifa hiyo muhimu. Tunakushukuru. Hii taarifa ni kwa wote, wala siyo kwa Mheshimiwa Ndassa peke yake. Mheshimiwa Ndassa endelea.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru Mheshimiwa Dkt. Ndugulile kwa maelezo ya ziada hayo, lakini nilikuwa najaribu tu kuona namna nzuri zaidi ya kuzuia kwa sababu unapozungumzia hizi masks za box, twende kwenye uhalisia, Mheshimiwa Waziri wa Afya na Naibu Waziri wa Afya, kwenye uhalisia hizi masks za box kwanza uwezo wake kwa mujibu wa wataalamu wanasema zinatakiwa zivaliwe ndani ya masaa manne. Zaidi ya hapo, yenyewe inabeba ule uchafu tena na hiyo mask ya box huwezi kuifua ni lazima uitupe.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa huyu mwananchi wa kawaida, mwananchi wa kawaida uwezo wa kununua mask kila siku ni mdogo, tofauti na hizi mask 95 Mheshimiwa Dkt. Ndungulile anaifahamu, najaribu kuzungumzia uhalisia kwamba ili tuwasaidie wananchi wetu hasa waliopo chini ni lazima tuangalie namna nyingine mbadala na namna nyingine mbadala wenzetu wa Wizara ya Afya mnaweza kutasaidia ili tutafute na namna nzuri zaidi ya kuzuia haya maambukizi ya corona virus.

Mheshimiwa Spika, lingine nishauri tu kama nilivyoshauri mwanzo na mimi kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Ndungulile amesema hazizuii. Lakini bado Mheshimiwa Dkt. Ndungulile, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya nitakupa hizi sample uende nazo kwa wataalam wako ili wakadhithibitishe kwa sababu nia hapa ni kuzuia, ni kuzuia huko vijijini maambukizi haya leo tunaona kama ni kitu cha kawaida lakini ugonjwa huu ni hatari sana kwa Taifa letu. Haya mafanikio ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyaeleza ya SGR, Reli ya kati hiyo hatuwezi kuyapata kama Watanzania ni wagonjwa niombe sana, niombe sana lazima Serikali yetu ilitazame kwa makini sana suala hili la ugonjwa wa corona.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu.