Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Dalaly Peter Kafumu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo hoja ya Waziri Mkuu. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, speech yake kwa kweli imeeleza juhudi ambazo Serikali imezifanya, ni juhudi nzuri. Kwa kweli mnyonge mnyongeni, haki yake mpeni. Serikali imefanya kazi kubwa. Nikiangalia kwenye Jimbo langu, Serikali imetuletea maji kutoka Ziwa Victoria. Kata zaidi ya 11 sasa zina maji. Tumepata fedha shilingi bilioni mbili na zaidi tunajengewa VETA pale.

Mheshimiwa Spika, tumejengewa Kituo cha Afya cha Igurubi, tuna daraja la Ngutu ambalo tulijengewa. Kwa kweli ni mambo mengi mazuri wananchi wa Igunga wanashukuru. Kwa niaba yao, naomba niseme ahsante sana kwa Serikali kutufanyia haya mambo mazuri kabisa.

Mheshimiwa Spika, suala la umeme nisilisahau, bado nina kata tano tu ambazo hazijapata umeme. Naomba basi itakapofika wakati ziweze kupewa umeme. Kwa maana hii, naomba niishukuru sana Serikali, nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yote kwa kazi nzuri hii. Bado tuna changamoto kidogo kidogo ambazo kwa kweli ndiyo wajibu wetu Wabunge kusema. Kama Wabunge wengi walivyosema, nami naomba niseme, hizi changamoto basi tuzifanyie utaratibu.

Mheshimiwa Spika, nianzie na janga hili ambalo liko pamoja nasi, Waheshimiwa Wabunge wamesema, nami naomba kuishauri Serikali kwamba kwa sababu limetukuta tuko kwenye bajeti, ni lazima tunapoendelea kuchakata bajeti yetu tuendelee kuiangalia. Hatujafika mwisho, ikiwezekana tuweke utararibu wa kibajeti kupambana nalo.

Mheshimiwa Spika, pamoja na maelekezo yote haya ambayo wananchi tunaendelea kuyafuata lakini tusisahau kama Serikali kwamba janga hili ni kubwa na hata ikibidi kubadilisha bajeti yetu kidogo, tusione aibu kwa sababu ni jambo kubwa limetukuta.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kidogo kuhusu kilimo. Sisi ni wakulima wa pamba kule Igunga, tunazalisha mbegu kwa ajili ya wakulima wa pamba wote Tanzania. Mwaka 2019 tumepata taabu sana ya kuuza zao la pamba na mpaka sasa kuna baadhi ya wananchi bado wanadai hawajalipwa. Zaidi ya shilingi milioni 200 hazijapelekwa kwa wananchi. Tunaomba basi kama inawezekana Serikali imalizie, nadhani siyo Igunga tu, lakini wakulima wa pamba wote hii taabu iliwapata sana. Tukumbukeni Mheshimiwa Waziri Mkuu, wananchi wetu wanakata tama kidogo. Mwaka huu nadhani nilizungumza na Naibu Waziri, kuna marekebisho kidogo kwenye jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo ningependa kusema ni madhara ya mvua ambazo zimenyesha. Tunashukuru tumepata mvua na chakula ni kingi kama ulivyosema. Tuna chakula kule kwetu kingi sana, mahindi na kadhalika. Sehemu chache ambazo zilikuwa za chini kule, maji yamechukua mpunga na nini, lakini sehemu nyingi wamepata chakula, ila imeleta madhara makubwa sana. Kweye Jimbo langu kuna barabara ambayo huwa nalalamika kila siku, tulipata fedha, lakini wameshindwa kujenga kwa sababu mvua imenyesha kubwa. Nilikuwa naomba basi tuangalie utaratibu wa kubadilisha, kuongeza bajeti kwenye hizo barabara kwa sababu zimekatika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la umeme kama nilivyosema, wananchi wa Igunga wanashukuru sana. Bado Kata tano tu; Kata ya Mtungulu, Kinungu, Kininginila, Mwamashiga na Kata ya Isakamaliwa, bado hazijapata umeme hata kidogo. Mheshimiwa Waziri wa Nishati, tunaomba basi mtutazame kwa namna ya pekee.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili kutoka mwisho ni usala la uwekezaji katika nchi yetu. Tunataka kwenda kwenye nchi ya viwanda na Mheshimiwa Chegeni amesema kidogo kwamba tunahitaji sana tuhahamasishe uwekezaji wa ndani na wa nje. Blueprint ile hebu tuitekeleze kama alivyosema Mheshimiwa Soni, ni muhimu sana. Kwa sababu tusipofanya hivyo, tunaweza tusiifikie nchi ya viwanda kwa sababu wawekezaji wengi wanakata tamaa. Wengine wanaondoka, wengine wanaogopa kwa sababu ya matatizo ambayo yako katika kuendesha biashara na kuanzisha biashara katika nchi yetu imekuwa taabu sana.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nizungumze kuhusu Sekta ya Madini ambapo kwa kweli naipongeza sana Serikali. Wamejitahidi wamefanikiwa jambo moja kubwa ambalo sisi lilitushinda la kuwapatia machimbaji wadogo masoko. Serikali imefanikiwa sana na ninawashukuru sana. Jambo moja dogo limebaki ni kuhamasiha Sekta ya Uchimbaji Mkubwa. Sekta ya Uchimbaji Mkubwa imekufa kwa sababu utafutaji umepotea kabisa. Utafutaji ndiyo engine ya kuleta migodi mingine.

Mheshimiwa Spika, naiomba Serikali na Waziri wa Nishati na Madini, tutazungumza kwenye Wizara yake, ahamasishe utafutaji mkubwa wa madini kwa watafutaji wa ndani na wa nje ili migodi iweze kuanzishwa siku za usoni. Hii migodi mitatu iliyobaki, ikifungwa hatutakuwa na migodi tena na migodi inaleta ajira kweli. Inaleta zile effects za watu ku- supply migodini, kufanya kazi kule ni muhimu sana. Kuna nchi zinaendeshwa na uchumi wa migodi. Kwa hiyo, nasi tukihamasisha utafutaji, tutakuwa na hali nzuri sana ya kuweza kupata uchumi kutoka katika madini yetu haya. Tumeweza kuya-control, tumeweza kuhakikisha kwamba wachimbaji wadogo hawayatoroshi ovyo ovyo. Kwa hiyo, lazima tuyachimbe kwa ku-benefit uchumi wetu.

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Naishukuru tena Serikali, endeleeni kufanya hivyo, nasi wananchi tunapokea na tutafanya kazi pamoja nanyi.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mungu awabariki. (Makofi)