Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali ya yote napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu…

SPIKA: Sasa Mheshimiwa Mwakajoka amehamia mbele; tunakushukuru Mheshimiwa. (Makofi/ Kicheko)

Ahsante. Mheshimiwa Dkt. Chegeni endelea.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nafurahi kumuona rafiki yangu Mheshimiwa Mwakajoka amesogea mbele kwa wito wa Mheshimiwa Mtulia.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli mimi nampongeza sana yeye na timu yake na Mawaziri wa Nchi wawili ambao ni Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Angellah Kairuki na Naibu Mawaziri wawili; Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa.

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imeangalia mambo mengi kwa upana mzuri sana, na kwa kweli ukiangalia jinsi ambavyo ameweza kuiainisha kwa kuangalia misingi ya bajeti yake, lakini mambo ambayo yamefanyika kama nchi, unaona kabisa kwamba hotuba hii imejikita katika kuelezea Watanzania nini azma ambayo Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. John Pombe Magufuli, anayo kwa Watanznaia. Napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais pamoja na wasaidizi wake wakiwemo Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu na wale wote wanaomsaidia.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kuna janga la Corona. Corona hii imekuja kama magonjwa ya mlipuko, lakini magonjwa ya mlipuko yanakuwa na madhara yake kwa upande wa ugonjwa na upande wa uchumi. Napongeza sana jitihada ambazo Mheshimiwa Spika wewe binafsi pamoja na wasaidizi wako katika Bunge hili na Kamati ya Uongozi kwa kufikia katika maamuzi ambayo sasa Bunge tunaendelea na shughuli zetu kama mihimili mingine lakini kwa kuangalia tahadhari zote na kuelimisha Waheshimiwa Wabunge na wananchi namna sahihi ya kujiepusha na maambukizi ya Ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimiwa Spika, huo ni upande mmoja, lakini pili najaribu kuangalia kwamba kama Serikali inafurahisha kuona kwamba mkakati wa Serikali daima, na hasa kufuata tamko la Mheshimiwa Rais kuwaambia Watanzania kwamba sasa tuko kwenye vita ya ugonjwa wa Corona, kila mmoja achukue tahadhari. Aliwasihi Watanzania, lakini pili akasema kwamba Watanzania lazima tukubali kwamba, tuko kwenye mapambano hatuwezi kufunga nchi yetu lazima tusonge mbele, uchumi wetu unahitaji kuwa-supported na Watanzania, lakini tuchukue tahadhari.

Mheshimiwa Spika, hili ni jambo ambalo kwa kweli baadhi walibeza na hali inavyokwenda tunaimani kwamba, pamoja na kwamba ni suala la kisayansi lakini kama kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake ni sehemu kubwa sana ya kupata ushidni wa ugonjwa huu wa Corona kwa Tanzania kwa sababu mpaka leo kwa takwimu ambazo tumezipata bado tuko vizuri.

Naomba Mwenyezi Mungu naye atie mkono wake kwa Watanzania wote, tuheshimu maagizo ya Serikali, kila mmoja wetu tutii uamuzi na tuzingatie masharti ambayo yatatufanya sisi tujiepushe na ugonjwa huu.

Mheshimiwa Spika, huo ni upande wa kwanza. Upande wa pili ni wa kiuchumi. Sasa hivi ni lazima tukubali duniani kote mambo ya uchumi yamepangaranyika, kila mahali mambo yamedorora na sisi hatuwezi kuwa exceptional, we are part and parcel.

Mheshimiwa Spika,mimi niombe kupitia Waziri wa Fedha na Ofisi ya Waziri Mkuu, tuone namna gani nzuri ya kutafuta a rescue package itakayowasaidia Watanzania tuendelee kupambana na janga hili lakini vilevile tukubali namna sahihi ya kuweza kuimarisha uchumi wetu. Tunahitaji kuishi pamoja na kwamba kuna tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii biashara nyingi zimedorora wala siyo siri lakini ni kwa sababu hali yenyewe duniani ime- shut down. Sisi tunaendelea kadiri tunavyoweza, tunaomba sasa kupata support ya Serikali ili sekta ambazo zitakuwa zimeathirika zaidi kuwe na rescue package ya kuweza kusaidia.

Mheshimiwa Spika, leo hii kuna watu ambao wana marejesho yao kila mwezi. Sasa hivi hali ilivyo mbaya watashindwa kurejesha. Nimeona jitihada za Serikali ambazo zinaendelea kufanyika lakini kuna haja ya kuona ni namna gani kuja na mkakati mzuri wa kuwawezesha Watanzania hawa waweze kupata nafasi nzuri ya kuweza kuondokana na tatizi hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali yetu ni tulivu, ni sikivu na yote haya inayafanyia kazi vizuri. Nakumbuka jana nilikutana na Mheshimiwa Mpango akasema Mheshimiwa Mbunge subiri, wala msipige kelele subiri. Akasema, nakuja na mkakati mzuri kwa namna gani kama Serikali tutajaribu kuhimili na kufufua uchumi wetu na kulinda mdororo huu wa uchumi kwa Watanzania wote. Napongeza sana mawazo ya Mheshimiwa Mpango na mawazo ya Serikali ambayo yatakuja hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo nilitaka nilizungumzie, tunapambana na Corona lakini kuna magonjwa mengine nyemelezi na magonjwa mengine ambayo yanaendana na tatizo hilo lazima tuyape kipaumbele, tusiyasahau. Kwa sababu Wizara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu inasimamia mambo kama haya, ugonjwa wa HIV – UKIMWI, kuna TB na magonjwa mengine lazima yaendelee kupewa kipaumbele kwa sababu na yenyewe ni sehemu mojawapo ya tatizo hili la Corona.

Mheshimiwa Spika, nikimaliza hapo nakuja kwenye suala la uwekezaji. Kwa vile Wizara ya uwekezaji iko chini ya Waziri Mkuu bado kuna tatizo na sintofahamu kubwa sana, namna gani ya kufanya coordination ya Wizara ya Uwekezaji na Wizara nyingine ili iweze kuleta matokeo chanya kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, leo hii bado kuna kukinzana kati ya TIC - Kituo cha Uwekezaji na TRA. Mwekezaji anapokuja hapa nchini anapata tax incentives kupitia TIC, akienda TRA wanamwambia hapana kuna kodi lazima ulipe. Kwa hiyo, kuna haja ya ku-harmonise mambo kama haya na kupunguza unnecessary delays katika kufanya maamuzi kwa sababu haya yanatusababisha tunapoteza wawekezaji kwa sababu ya ukiritimba ambao hauna sababu wala tija. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri wa Uwekezaji kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu atusaidie ku-harmonise TRA na TIC ili ziweze ku-facilitate uwekezaji katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais kila siku anazungumza lazima tuvutie uwekezaji wa ndani na nje ya nchi. Hata hivyo, leo hii ukitaka kutengeneza working permit ya mfanyakazi tozo la labor ni dola 1,100 ukipitia TIC; ukienda Immigration ni dola 2,050, kwa hiyo, utatumia dola 3,150 kupata permit ya mfanyakazi hapa nchini, it is too expensive. Mimi nashauri Serikali ijaribu ku-review hizi fees kusudi tuweze kupata wawekezaji wengi na wafanyakazi wengine ambao wana sifa za kufanya kazi hapa nchini ili iweze kuchangia katika uchumi wetu. Uchumi lazima uendeshwe na watu wote, tuchanganye expertise ya ndani na nje.

Mheshimiwa Spika, kingine ninachokiona ni kuhusu maamuzi, tatizo la maauzi bado ni ugonjwa. Mchuchuma na Liganga leo tuna miaka nenda rudi lakini hadithi na ngonjera zilezile, maamuzi hayafanyiki. Naomba kama Serikali tujitahidi sana kufanya maamuzi tusije tuka-frustrate uwekezaji ambao tunauhitaji hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kingine kuna issue ya BRELA. Leo hii ukienda BRELA ukitaka kusajili kampuni wanakambia lazima uwe na NIDA, ukienda NIDA hawatoi vitambulisho. Sasa unashindwa ku-register makampuni na kufungua biashara nyingine nyingi kwa sababu ya NIDA. Nashukuru kwamba Serikali imeweza kuweka utaratibu mzuri sasa kwamba angalau NIDA wataweza kutoa vitambulisho kwa uharaka zaidi. Hii ni hatua moja muhimu ya Serikali kupongezwa; imetambua hilo na ni vema ilisimamie lifanyike kwa uharaka zaidi.

Mheshimiwa Spika, pia vitambulisho vyetu ni vingi mno, tujaribu ku-synchronize vitambulisho. Leo una kitambulisho cha NIDA, Driving License, una sijui cha wapi ni vingi mno. Tujaribu kuwa na kitambulisho ambacho mtu akiwa nacho kimoja kina-cover kumpa information mtu yeyote na mahali popote pale, itasaidia sana.

Mheshimiwa Spika, lakini kingine nachokiona ni suala la returns za BRELA. Sasa hivi ukienda BRELA kama una kampuni ina miaka mingi haijafanya return siku za nyuma unaambiwa ulipe returns za miaka 10 iliyopita…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ni kengele ya pili Mheshimiwa malizia.

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, namalizia. La kumalizia ni suala la wakulima wa pamba. Mimi kwangu katika Wilaya ya Busega wakulima wa pamba mpaka leo hii wanadai shilingi milioni 450 hawajalipwa. Hawa watu wameuza pamba toka mwezi Mei na Juni, 2019 mpaka leo hawajalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu amefanya kazi kubwa sana ya kuwaunganisha wanunuzi wa pamba na hawa wakulima na kadhalika lakini bado Mheshimiwa Waziri Mkuu nikuombe chondechonde hawa wakulima wa pamba walipwe ni muhimu sana. Hawa wakulima toka mwezi Juni, 2019 pesa hajalipwa, hata tukisema wazalishe tena mwaka huu afanye vizuri, haiwezekani tunamnyonya mkulima. Naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu hili alisimamie. Najua anafanya kazi kubwa sana, aendelee kufanya kazi hiyo vizuri sana.

Mheshimiwa Spika,baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii. (Makofi)