Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RICHARD S. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi, kwanza nianze kumshukuru Mungu na niombe tu watanzania tuendelee kumwomba aendelee kutuepusha na hili janga ambalo linasumbua dunia la Covid 19.

Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba nipongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri ambayo anaifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwenye kazi ya kuendeleza nchi yetu na watanzania kiujumla. Pia naomba niwapongeze mawaziri wote watatu Waziri mwenyewe Mheshimiwa Jenista na Manaibu Mheshimiwa Anthony na dada yangu Ikupa na watendaji wote makatibu wakuu na watendaji wote chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, ni vyema tuseme kwa hii miaka mitano Waziri Mkuu kwenye hotuba yake ameweza kueleza vyema kila sekta na kila wizara kwa maana nyingine ni jinsi gani ambavyo tumeweza kufanya kazi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni kufatisha mpango wa maendeleo pamoja na ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo inaelekeza nini kifanyike kwa wananchi. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa namna ambavyo wamefanya kazi kubwa sana ndani ya miaka mitano na takwimu zinajionyesha kwa vitu ambavyo vimefanyika vingi na vya thamani kubwa tofauti na miaka iliyopita ikiwa ni mabadiliko yaliyotokana na uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, baada ya kueleza hilo naomba nianze na suala la majanga ambayo yametokea kwenye nchi hii. Mwaka huu 2020 na tangu mwaka jana 2019 Tanzania tumebarikiwa kuwa na mvua nyingi sana ambazo kwa miaka hii mitano kwa kweli haijapata kutokea. Kwa hiyo, mafuriko ambayo yametokea Rufiji kwa Mheshimiwa Mchengerwa na pia hata sisi Mkoa wa Katavi kuna baadhi ya maeneo yalipata mafuriko lakini siyo makubwa kama haya na yamepelekea baadhi ya nyumba za wananchi kuweza kubomoka.

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri Mkuu natumainia taarifa imefika ofisi kwako sasa hivi usafiri wa njia ya reli haupo kwenye Wilaya Mpanda, au Mkoa wa Katavi kutokana na tuta la Mto Ugala takribani mita 120 kubomoka baada ya kuwa mto umejaa sana na mvua zilivyo nyingi.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hiyo wito wa wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaomba kwenye fedha za dharura na vyanzo vingine chini ya Wizara kwamba punde tu baada ya kuwa mvua zimesimama basi tuta liimarishwe kwa kuwa midomo mingi ambayo itaweza kupitisha maji na madhara haya yasitokee tena kwa masika zinazofata. Kwa hiyo, hiki ni kilio kikubwa sana kwa wananchi wa Katavi tunakumbuka miaka ya nyuma tumewahi kukulilia sana kuhusu njia hii ya reli ni msaada mkubwa sana kwa Mkoa wetu wa Katavi. Tunalima pamba, tunalima mazao ya chakula, Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa ile minne inayotoa sana chakula na kulisha nchi hii pia tunalima tumbaku sasa ubebaji wa haya mazao unahitaji sana hii njia ya reli na ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yetu na uchumi wa wananchi wa Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi sasa hivi Mheshimiwa Waziri Mkuu njia zinazotumika kutoka nje ya Mkoa wa Katavi ni kupitia Sumbawanga kuja Mbeya na kupitia Uvinza kuja Kigoma kuja Tabora. Ni hizo tu kwa hiyo, njia ya reli haipo nah ii njia ya kuja Tabora Sikonge na kwenye pale kwenye daraja la mto Ukoga na lenyewe limefungwa muda mrefu kutokana na kujaa sana na kuhatarisha maisha ya wananchi. Kwa hiyo, pia tunashukuru Mheshimiwa Rais mwaka jana alivyohimiza Air Tanzania na inafanya mara tatu kwa wiki na yenyewe pia ni njia ya usafiri inayotumika. Lakini hizi njia kuu mbili ni muhimu sana kwa Mkoa wa Katavi kwa hiyo tunaomba sana kwenye fedha za dharura mtuangalie tuweze kutengeneza hili tuta kwenye mto Ugana.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la uwezeshaji. Kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri Mkuu umezungumza vizuri na hatua ambazo zimeweza kuchukuliwa na lakini pia kupitia halmashauri zetu na majiji na manispaa wametekeleza vyema kupeleka fedha zile zinazotengwa kutoka kwenye mapato ya hizi halmashauri mapato ya ndani asilimia 10 ambayo inaenda kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, nikianza na vijana tunajua rika la vijana mwisho ni miaka 35 lakini changamoto ambayo tumekutana nayo ni kwamba kuna watu wanazidi umri huo kwa hiyo wanakuwa hawako kwenye sifa za kuunda vikundi na kupata mikopo hii. Sasa tunajua mna vyanzo takribani taasisi 19 ambazo zinafanya uwezeshaji na ukopeshaji katika nchi hii lakini kwenye hili la vyanzo vya halmashauri kwenye asilimia 10 ya mapato ya ndani tuliondoa pia riba ambayo mmeweka sana unafuu. Kwa hiyo, tuombe sasa Serikali tuangalie Mheshimiwa Waziri Mkuu ile mifuko iliyo chini ya Ofisi yako ni namna gani sasa iende ikasaidie kundi la wanaume ambako wanakuwa hawako kwenye kundi la vijana ambao wamezidi miaka 35.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ndio hao ambao wanakwama kwa sasa hivi kuwa na sifa ya kuweza kukopeshwa. Kwa hiyo, kama ule mfuko wa self na hii mifuko mingine ambayo ni ya kuwezesha vijana basi tunaomba tuongeze aidha tuongeze rika angalau tuweke kwamba vijana na watu wenye umri wa kati ambao labda wanafika hata miaka 50 hii itasaidia sana na ndio kizazi hichi ambacho ndio cha uzalishaji ni kinachangia sana kwenye pato la Taifa. Kwa hiyo tunaomba marekebisho ya sera hii au sheria ili tuongeze umri kwa upande wa vijana tuwabebe na watu wanaofkisha mpaka umri wa miaka 50 au la tuwezeshwe kwenye mifuko mingine na iende kukopesha bila riba.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kwenye uwezeshaji hapa hapa kuna halmashauri ambazo zina mapato ambayo yako chini sana ni chini ya bilioni moja. Kwa hiyo, kile kiwango ambacho kinakuwa na uhitaji pia hakitoshi, kwa hiyo, tunahitaji sana hii mifuko pia iendelee.

Mheshimiwa Spika, pia kuna suala la vikundi sasa hivi tunaambiwa idadi ya vikundi imeongezwa kutoka watu 5 mpaka 10 sasa imekuwa inaweka mkanganyiko kwa wananchi kwa sababu wingi wao pia ile fedha wanayokopeshwa ni ndogo halafu wanakuwa wako wengi na wengi hawana biashara ya pamoja wanachukua halafu wanagawana. Kwa hiyo, hiki kiwango kilichoongezwa cha watu 10 tunaomba kipunguzwe na angalau pia tuangalie sheria hii kama kuna uwezekano wa kukopeshwa mtu mmoja pia na yenyewe pia iweze kuangaliwa na ambayo itasadia sana. Kwa mfano kwa watu wenye ulemavu kuna wengine wana ulemavu viungo vinatofautiana na aina ya kazi ya kufanya. Kwa hiyo, watu wenye ulemavu iangaliwe kukopeshwa mtu mmoja mmoja kwa sababu wengine kuna kijiji wako wachache na aina ya ulemavu na kufanya biashara kila mmoja inatofautiana.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la uwekezaji, liko chini pia ya ofisi ya Waziri Mkuu lakini naomba turejee kwenye suala la tafiti mbalimbali na kwa nini tulikuwa tuna SIDO na kwa nini tulikuwa tuna TIRDO. Mpaka sasa hivi SIDO na TIRDO zimefanya, malengo yake wamefanya kwa asilimia gani kwa nini wamefeli na kama wamefeli tunawakwamua vipi ili waende mbele. Maana tunapozungumzia uwekezaji lazima tuangalie na taasisi ambazo zinaenda kusaidia uwekezaji hususani watu wa ndani na viwanda vikiwepo tunasaidia pia kutumia fedha zetu za kigeni ambazo tunazo kwa ajili ya manunuzi mengi kutoka nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni suala la ajira. Tunaona kwenye kilimo tunaajiri watu wengi lakini ile kada ya vijana bado hatujachukulia vyema kwenye upande wa kilimo. Uwezeshaji wa mitaji, uwezeshaji wa elimu na ujuzi na uzoefu bado upo kwa kiwango cha chini kwa hiyo tuombe Serikali kwa mfano PAMATEC wana matrekta mengi sana pale na wana mkataba lakini namna gani ya kuyatoa moja ya nyenzo za kuwasaidia watu kwenye kilimo bado linasuasua. Kwa hiyo, tuombe Waziri Mkuu uliingilie hili matrekta yako pale wana mkataba na mzalishaji wa Poland kwa hiyo, hawajatimiza ile kiwango ili sasa kiwanda kiweze kujengwa hapa Tanzania. Kwa hiyo, tunaomba uingilie kati na uweze kusaidia suala hilo.

Mheshimiwa Spika, la mwisho ambalo niligusie ni kuhusiana na Corona kama wenzetu ambavyo wamechangia Wabunge. Tunaomba sasa Serikali kwenye maeneo ya mikusanyiko kwenye vyomboo vya usafiri kabla abiria hawajaingia basi vipulizwe dawa na kikifika kipulizwe dawa pia stand zote kwa sababu zina mageti kwa nini maafisa wetu wa afya wasiwepo pale kama wanawapima kama sisi vile Wabunge tunavyoingia hapa ndani na tunapimwa. Ukienda Stand ya Ubungo, stand ya Usamvu zote hizo tuongeze usimamizi wa hali ya juu.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. RICHARD P. MBOGO:Mheshimiwa Spika, nashukuru naunga mkono hoja.