Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru sana kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii ya Bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza naomba nitoe shukurani na najua wewe mara nyingi unasahau kwa sababu unawahudumia wengi, unawasaidia wengi. Mimi umenisaidia sana kufika hapa nilipo, ulikuwa chachu ya mimi kugombea Ubunge kutoka katika Bunge la Katiba.

Mheshimiwa Spika, katika Bunge la Katiba nikukumbushe wakati Wapinzani walipokataa hati ya Muungano na wakawa tatizo kubwa sana na hata mlipotupa Hati ya Muungano, Wapinzani wakasema imefojiwa, mimi nilishawishi nichangie kutoka katika lile kundi la 221 na nikasema mimi na mtu mmoja wa upinzani wanipe hiyo hati tuipeleke Ubalozi wa Marekani tukaangalie tu wino kwa sababu walikuwa na uwezo wa kusoma wino wa miaka kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, watuambie tu huo wino umeandikwa lini wakati marehemu Karume yupo au baada ya kufariki marehemu na ikawa ndiyo maziko ya suala la Hati ya Muungano iliyofojiwa, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika,tangu nimeingia hapa Bungeni huu ni mwaka wa nne, umenisaidia mambo makubwa mawili. Kwanza nilileta Muswada Binafsi wa Sheria ya Sekta ya Ulinzi. Kwa kweli ulinisaidia sana, uliupokea Muswada ule ukafanyiwa kazi na Bunge na mapendekezo yakaenda Serikalini, Serikali wakauchukua Muswada huo watauleta kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani. Hiyo ni kumbukumbu ya mambo uliyonisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hivi karibuni nimekuletea Hoja Binafsi ya kutaka lugha ya Kiswahili itumike kama lugha ya kufundishia. Bunge limeifanyia kazi na kuniandikia mimi tena nilipeleke suala hilo au hoja hiyo kwanza ipate maoni ya Chama change. Chama changu wanalifanyia mchakato hoja hii na baadaye wataniarifu itakuwaje. Haya ni mambo makubwa sana kwangu mimi na nitakuwa nimeweka alama kubwa katika Bunge lako kwa msaada wako. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,pia naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais na hasa kwa matendo yake makubwa ya kusaidia nchi hii kuipeleka mbele katika miaka mitano ambayo amekuwa Rais na kitaifa lakini pia katika Jimbo langu amefanya mambo makubwa sana. Ameniletea maji kwenye vijiji vyangu vyote karibu asilimia 48, umeme wa REA, kituo cha afya, hospitali ya Wilaya, kituo cha VETA shilingi bilioni 5 na ananijengea Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi katika Kata yangu ya Magiri, Kijiji cha Malampaka. Mambo haya siyo madogo, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho, namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kitendo chake cha kuishi ndani ya mambo aliyoyafikiria Mheshimiwa Marehemu Baba wa Taifa hasahasa misingi ya Azimio la Arusha na mimi ninalo. Hili hapa ndiyo Azimio la Arusha ambalo lipo na kila nikilisoma hili linanikumbusha mambo yangu ya miaka 1965 nilipotembea kilometa 50 kuunga mkono Azimio hili. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuliamsha dudu hili la Azimio la Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa niende kwenye mambo muhimu ya kuchangia katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza nimshukuru Waziri Mkuu kwani yeye ni tofauti na Mawaziri Wakuu wote niliowafahamu. Nakiri kwamba nimefanya kazi na Mawaziri Wakuu waliopita lakini Waziri Mkuu huyu ni muungwana, mpole lakini anayependa watu.

Mheshimiwa Spika, hata nilipokuwa nalalamikia tumbaku ndani ya jengo hili na hata nilivyofanya kosa la kwenda kumshtaki kwake Waziri wa Kilimo hakuchukua hatua yoyote mpaka alipokwenda Tabora kuthibitisha niliyoyasema na baadaye akachukua hatua nzuri sana na tukauza tumbaku. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni mtu wa watu, anapenda wanyonge, amefanana sana na Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,pia nimshukuru Mheshimiwa Jenista Mhagama, huyu binti wa Kingoni, mweupe maana sisi Wanyamwezi watu weupe, mara anikatishe tamaa aniite baba, mara aniite kaka, akikumbuka mambo yangu ya zamani kwamba nilikuwa Rais wa Afrika ananiita bosi, mara aniite mzee hata sijui ananiita nani sasa. Namshukuru sana kazi maana zake ni nzuri sana na ameongoza Wizara hii kwa nguvu sana. Mimi jina langu kwake na roho yangu nyeupe ni mtani wangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika,lakini pia ana Mawaziri wadogo wawili…

SPIKA: Nataka kumwambia tu Mheshimiwa Jenista, Wanyamwezi hawazeeki.

MHE. ALMASI A. MAIGE: Ni kweli kabisa. (Kicheko)

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Maige. (Kicheko)

MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniongezea hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niwashukuru Mawaziri wadogo wawili, ndugu yangu Mheshimiwa Mavunde na Mheshimiwa Ikupa. Hawa nimewajua mimi nikiwa Mwenyekiti wa Waajiri Tanzania.

Mheshimiwa Spika,katika mchango wangu nitachangia mambo ya kazi na ajira lakini pia mambo yanayohusu tozo zile za SDL. Nianze na suala la kazi na ajira. Sisi waajiri na naomba ni-declare interest kwamba mimi ni mwajiri na ni Mkandarasi Daraja la Kwaza, bado tunategemea kwamba Serikali itafanya mpango wa kupunguza SDL kutoka asilimia 4.5 iliyopo sasa mpaka asilimia 2 kulingana na watu wengine walioko huko Duniani hasa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana tulikuwa tumepanga kwenye bajeti hii ya Wizara ya Kazi na Ajira kurekebisha sheria za kazi ambazo zimepitwa na wakati. Sheria hizo hazikurekebishwa na mapungufu yake tunayaona sasa. Wakati huu imetokea Corona tunafunga biashara, tunafanya watu wasiende makazini lakini hakuna nafuu kwa mwajiri, tunaendelea kulipa mishahara na hii tunaona kwamba siyo sahihi. Kama ingekuwa sahihi basi kwenye hili la force majeure kwa maana ya jambo lililotokea nje ya waajiri na wafanyakazi ilitakiwa tupewe nafuu wote wawili.

Mheshimiwa Spika, lipo suala la Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), mimi na wenzangu waajiri tunaamini kwamba bado Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kuendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu ni makosa. Mwanzo iliwekwa vile kwa sababu tulikuwa tunatafuta hela za mikopo ya wanafunzi sasa hivi tunakusanya hela zinakwenda kwenye central account, kwa hiyo sababu ile imekufa, siyo muhimu tena. Tunaomba VETA kwa sababu ni Vyuo vya Ufundi Stadi vinafundisha wafanyakazi wetu ambao wako chini ya Wizara ya Kazi na Ajira virudishwe tena chini ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa maana hakuna sababu ile kubwa iliyokuwepo ya kukusanya hela kwa ajili ya mikopo kwani hela zinakwenda kwenye central account.

Mheshimiwa Spika, sasa niongelee Mfuko wa Fidia. Mfuko wa Fidia ulipoanzishwa tuliunga mkono na ulikuwa na wigo wa matawi mawili tu kwamba utakusanya tozo kwa waajiri wa umma yaani public na sekta binafsi. Sasa sisi tukawashauri kwamba hapana wapanue wigo ili waajiri wenye kazi za hatari na zenye madhara walipe zaidi halafu waajiri wenye kazi salama na hazina madhara walipe kidogo kwa mfumo huo huo kwamba wale wa public na wale wa binafsi.

Mheshimiwa Spika, tulifanya stadi Waziri aje na matokeo ya stadi hiyo ilisemaje. Sisi Waajiri tunaamini kwamba ni muhimu sana sana kuwe na sababu ya kupanua wigo ili hela nyingi zikusanywe kwa sababu ya kufidia wafanyakazi wetu watakaoumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwishoni nina ukakasi. Uwakilishi ndani ya Bunge letu katika muktadha wa ajira na kazi ni wa utatu na utatu huu unasajiliwa na kusimamiwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) ambao ni wa Serikali, Waajiri na Wafanyakazi. Nauona huu uwakilishi katika Bunge lako kwa theluthi mbili. Naiona Serikali chini ya Waziri Mkuu na Mawaziri wake, nawaona wafanyakazi, Majimbo mawili ina maana Wabunge wawili walioingia humu Bungeni kupitia wafanyakazi lakini siwaoni waajiri.

Mheshimiwa Spika,najua tulipotokea siku za nyuma ilitakiwa iwe hivi kwa sababu waajiri ndiyo waliokuwa mabepari na makabaila na tulitaifisha mali zao lakini yameshapita hayo, tusiendelee kuganga yaliyopita. Hivi kwa nini hivi sasa kusiwe na uwakilishi wa waajiri humu ndani? Kasoro itakuwa nini? Iam thinking loudly, tatizo ni nini kuweka uwakilishi wa waajiri?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja hii na kwa kweli naunga mkono mambo yote yatakayoongelewa katika hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na Wizara ya Kazi na Ajira.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)