Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amina Saleh Athuman Mollel

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru sana. Awali ya yote nitoe pole kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Waandishi wa Habari na wapenzi wote ambao wanafahamu kazi kubwa inayofanywa na Waandishi wa Habari kwa kifo cha Mwanahabari nguli hapa nchini Marin Hassan Marin. Hakika ni pigo kwetu wote na ni pigo kwa Serikali.

Mheshimiwa Spika, Marin anafahamika kwa jitihada zake katika kuhabarisha Umma wa Watanzania. Binafsi kama miongoni mwa niliofanya naye kazi, imeniuma sana. Niliingia TBC mwaka 2008 baada tu ya kumaliza Chuo Kikuu, Marin Hassan alinipokea na alinifundisha usomaji wa habari. Kwa kweli kwangu mimi pia, moyo wangu unalia kwa maumivu. Ombi langu ni kuiomba Serikali imuenzi Marin Hassan Marin kwa mchango wake mkubwa.

Mheshimiwa Spika, kutokana na janga hili la ugonjwa wa Corona mwanamuziki Michael Bulton katika wimbo wake wa “Learn on Me,” anasema kwamba sometimes in our lives we have all pain, we all have sorrow, lakini katika yote hayo anasema kwamba daima kuna kuwa na kesho. Nami naamini kwamba katika ugonjwa huu wa Corona Mwenyezi Mungu atatujalia na tutavuka salama. Taifa letu kupitia jemedari Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kazi aliyoifanya, ugonjwa huu ukija, naamini kabisa kwamba utatikisa. Kwa pamoja tumwombe Mwenyezi Mungu ili ugonjwa huo upite.

Mheshimiwa Spika, katika ugonjwa huu kweli tahadhali imetolewa, lakini siku zote nakwenda mbele zaidi hasa kama mwanamke mwenye ulemavu nawaangalia watu wenye ulemavu; je, elimu imewafikia vya kutosha? Kwa mfano, tumeweka tahadhali kwamba kila mmoja wetu aweze kunawa. Je, kwa yule mtu asiyeona na hakuna watu pale wanaoweza kumsaidia, je, ataweza kujikinga na tahadhari hii?

Mheshimiwa Spika, siyo hao tu, hata viziwi huko mitaani, hawafahamu. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali na ninaishauri kuona umuhimu pia kwamba twende sote kwa pamoja kuhakikisha elimu inayotolewa hakuna anayeachwa nyuma ili basi maambukizi haya yasije kuwa athari kubwa pia kwa watu wenye ulemavu.

SPIKA: Mheshimiwa Amina nakubaliana na wewe kuhusu elimu, ni muhimu sana. Maana wako watani zangu fulani wanauliza, hiyo sanitizer wanakunywa vijiko vingapi? Kwa hiyo, elimu ni muhimu sana. Endelea Mheshimiwa Amina Mollel. (Kicheko)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana. Kwa kweli ninaipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Jemedari, legendary Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ndani ya miaka minne aliyoifanya.

Mheshimiwa Spika, pia nampongeza Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na Baraza lako la Mawaziri, kazi kubwa mmefanya. Wewe pia nikupongeze kwa moyo wa dhati kabisa kwa kazi kubwa uliyoifanya. Mimi ndani ya miaka minne nimejifunza na kushuhudia mambo mengi katika Bunge hili yakifanyiwa mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nakupongeza wewe; na hasa nilipofika kwa mara ya kwanza, sikuwahi kupanda ghorofa ya nne na mara nyingi nimekuwa nikisumbua. Nakumbuka katika mojawapo ya bajeti nilishika shilingi huku kusema kuhusu lile jengo la utawala na ukaahidi kwamba litawekwa lift.

Mheshimiwa Spika, wewe ni mtendaji na unaposema, kinafanyiwa kazi. Hongera sana, kwa mara ya kwanza hatimaye niliweza kufika ghorofa ya nne kwa sababu wakati mwingine mbali ya wasaidizi, kuna mambo ambayo inabidi tufuatilie sisi wenyewe.

Mheshimiwa Spika, kwa nini naipongeza Serikali hii? Naipongeza kwa sababu nimezungumza mara kwa mara humu ndani, kwamba tangu tumepata uhuru, kwa kweli masuala ya watu wenye ulemavu yalikuwa nyuma sana na kipaumbele changu mimi katika Bunge hili tangu nimeingia, ukiniuliza; namba moja ni walemavu, namba mbili ni walemavu na namba tatu ni watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, Ofisi hii ya Waziri Mkuu, kupitia kwa Jemedari wetu hatimaye alikuwa na jicho la ziada na kuhakikisha kwamba ndani ya Baraza la Mawaziri kunakuwa na mtu mwenye ulemavu ambaye pacha wangu Mheshimiwa Ikupa ninakupa pongezi kwa kazi kubwa uliyoifanya katika kuhakikisha kwamba unawashauri Mawaziri wenzako, unaishauri Serikali na mara kwa mara tumekuwa tukiwasiliana na kuziwasilisha kero mbalimbali ambazo leo hii ninajivunia na kusimama kifuambele kwamba yamefanyiwa kazi. Hongera sana kwa hilo, Bunge litakukumbuka na Watanzania watakumbuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, fungu Na. 65 linahusu masuala ya watu wenye ulemavu. Katika Bunge la 2017, Februari 2, niliishauri Serikali juu ya kitengo cha watu wenye ulemavu. Vilevile Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu leo hii nasimama hapa na kusema ahsante kwa Serikali yangu kwa kuwa yote haya yamefanyiwa kazi. Naomba tu sasa badala ya kuwa kitengo, hatimaye sasa ije kuwa Idara kamili katika Bunge lijalo.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017 nilishauri pia kuhusu Mfuko wa Watu Wenye Ulemavu kwa sababu haukutengewa fedha. Ninaposimama hapa leo hii ninatoa ushuhuda kwamba mfuko huu kazi nzuri imefanywa na umeweza kutengewa bajeti.

Mheshimiwa Spika, tarehe 14 Novemba, 2017 niliuliza swali na kuitaka Serikali kuleta Mkataba wa Marrakesh. Mkataba huu unawawezesha watu wenye ulemavu, wasioona kuweza kupata kutafsiri, yaani vitabu na majarida mbalimbali yatakayowawezesha wao kupata elimu. Ninaposimama hapa mwaka 2019 Mkataba huu wa Marrakesh uliletwa na hatimaye Bunge hili likaupitisha. Naipongeza sana Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2016 katika Wizara ya Afya nilileta marekebisho ya kifungu cha Sheria nikiwataka, nanukuu: “Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wa mwaka 2016 ambao katika bodi itakayoteuliwa na Mheshimiwa Waziri na kwa sababu nafahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu, kifungu cha 7, nilipendekeza kifungu cha 3 kiletewe mabadiliko…

(Hapa kengele iilia kuashira kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Amina.

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba nimalizie tu kwa kusema kwamba Serikali hii imefanya kazi kubwa sana, ninaipongeza sana, Mheshimiwa Waziri Mkuu nakupongeza kwa kuwa na jicho la ziada na kuweza kutoa ushirikiano mkubwa kwa Mheshimiwa Ikupa na hatimaye naye ameonesha kwamba kuwa na ulemavu siyo kulemaa, watu wenye ulemavu tunaweza.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)