Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa fursa ili niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo ipo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, napenda kuungana na wenzangu kumpongeza Mheshimwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha hotuba yake ya bajeti kwa umahiri mkubwa sana. Pia napenda kuungana na wenzangu kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa ambayo amefanya kwa miaka minne hii. Serikali hii mtu atabeza atafanya nini lakini kazi waliyofanya ni wamefanya mapinduzi. Mapinduzi ambayo mtakapomaliza hii kazi nchi yetu hii itaingia kwenye uchumi wakati. Mungu awabariki muendelee kupiga mzigo namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, pia naomba niungane na wenzangu kwanza kukushukuru wewe, pamoja na uongozi wote wa Bunge, Naibu Spika, Katibu wa Bunge na viongozi wengine, kwa tahadhari ambayo mmeichukua hapa Bungeni kuhusu ugonjwa huu wa corona, nawashukuru sana sana. Mmetukinga Wabunge na Wafanyakazi wa Bunge, tuchukue tahadhari kubwa kwa sababu ugonjwa huu upo.

Mheshimiwa Spika, pili, napenda kuishukuru Serikali, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Afya kwa maelekezo ambayo wanatupa na wanawapa wananchi kuhusu ugonjwa huu, nawashukuru sana. Nawaomba wananchi wa Chunya, wananchi wa Mkoa wa Mbeya na Watanzania, tufuate maelekezo ambayo viongozi hawa wanatupa. Tuyafuate kweli kweli uongojwa huu upo na unaua. Nawaomba sana yote ambayo wamesema tuyatuate kwa umakini sana.

Mheshimiwa Spika, nataka katika hayo ambayo viongozi wetu wametupa niongeze kimoja kidogo nacho nisimu ya mkononi. Nawaomba sana simu ya mkononi kuanzia sasa ibaki yako wewe mwenye simu usiseme shika mwenzangu shika kidogo angalia clip hii hapana, ibaki kwako mwenyewe kwa sababu nayo inaweza kuwa njia ya kuambuakiza. Unaponawa mikono unatumia sanitizer chukua kitambaa cheupe safi na simu uisafishe kwa sababu nikwambie mimi nakuapia Watanzania tungekuwa tunashika dini zetu kama tunavyoshika simu, moto wa huko ungeishia kuchoma mahindi, nakwambia kweli kabisa. Kwa hiyo naomba niongezee hapo kwamba tuwe makini sana na simu, simu yako ibaki yako, usimpe mwenzie, aangalie clip au apige salio limeisha, ubaki nayo na uisafishe mara kwa mara.

SPIKA: Waheshmiwa Wabunge mmemsikia Senator ushauri wake? Simu ibakie yako na watanzania pia kwa ujumla hasa wanawake wanapenda simu za wenzao. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwambalaswa endelea.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunisaidia na kuniongezea uzito kwenye hoja hii. Nikiongelea hilo la simu Mheshimiwa Rais wetu katika ushauri wake ameongezea kwamba tutubu kwa Mwenyezi Mungu, tumfuate Mwenyezi Mungu tutubu dhambi zetu. Ukiona huko Italia wanateseka sasa hivi, wanaoana wanaume kwa wanaume, mtu jitu zima linamwingia mtoto wa miaka mitato wakati watu wakubwa wapo chungu nzima, ni dhambi ambazo Mungu amekasirika.

Mheshimiwa Spika, naomba uniruhusu nikiwa katika hilo niende kwenye kitabu cha Mungu. Nachukua Biblia watu nasikia wanasema bibilia, hapana, ni Biblia, katika wafalme wa zamani mfalme wa zamani mwana wa Daud. Baada ya kutawazwa kuwa mfalme alifanya vitu vingi vizuri unique.

Mheshimiwa Spika, cha kwanza alienda kuteketeza sadaka kumshukuru Mwenyenzi Mungu na Mungu akaongea naye akamwambia nikupe nini? Akamwambia unipe maarifa na uelewa ni waatawale watu wako vizuri. Hakuomba nguvu za kijeshi hakuomba utajiri, Mwenyenzi Mungu kampa vyote kampa hekima, kampa nguvu za kijeshi kampa na utajiri.

Mheshimiwa Spika, cha pili, alimjengea Mungu nyumba nataka nianzie hapo. Sasa ukienda kwenye kitabu cha Mambo ya Nyakati wa pili nianzie sura ya saba, aya kumi na moja baada ya Suleiman kumjengea nyumba Mungu. Hivyo basi, Suleiman akaimaliza nyumba ya bwana na nyumba ya mfalme na yote yaliyomwingia Suleiman moyoni mwake ayafanye mwa bwana. Bwana akamtokea Suleiman usiku akwamwambia nimesikia uliyoyaomba na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu anasema Mungu sasa na Suleiman.

Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi au nikiwapelekea watu wangu tauni kama corona nikiwapeleka watu wangu tauni ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu watajinyenyekesha nakuomba na kunitafuata uso na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao na kuiponya nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tumuunge Mheshimiwa Rais ametuambia hili tumrudie Mungu tuache dhambi ugonjwa huu utapita. Baada ya hilo naomba ningelee hilo ambalo wachimbaji wangu wa dhahabu wadogo wadogo wa Chunya wamenituma.

Mheshimiwa Spika, kwanza wachimbaji hawa wanaishukuru sana Serikali kwa kuweka soko la dhahabu pale Chunya, soko lipo vizuri, linaenda vizuri, wachimbaji wanapata pesa yao, Serikali inapata pesa yake na halmashauri inapata pesa yake. Sasa hii tafrani ambayo imetukuta sasa hivi wachimbaji wadogo wamekaa na dhahabu mkononi hawana kwa kuuza kwa sababu broker wa pale Chunya ni wale wenye mitaji midogo midogo na kwa kuwa sasa hivi ndege haziendi nje, kwa hiyo kwamba anunue dhahabu akauze Dar es Salaam arudi kununua tena hawana uwezo huo. Naiomba Serikali iingilie kati, hili kuna dhahabu nyingi sana zipo mikononi mwa wachimbaji wadogo wadogo naomba tuchukue hatua interim period, ijue aidha benki ziwakopeshe wale brokers au benki kuu iende kununua in the interm period ili wananchi wetu waende kufanya biashara kama kawaida.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nimeona kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri Mkuu kufufua kilimo na ushirika. Naongelea ushirika kwa kifupi, nimeshukuru sana nilipoona Serikali imemtuma TAKUKURU kwenda kukagua ushirika nchi nzima, nimefurahi sana. Kwa sababu ushirika ndio umeua kilimo upo wapi ushirika wa zamani KNCU, upo wapi ushirika wa Nyanza Co-operative wa zamani, upo wapi ushirika wa Bukoba au wa Mbeya? Viongozi wa ushirika wameua ushirika, kwa hiyo umeua kilimo chetu. Nimefurahi sana kwamba Serikali imeliona hilo, imeanza kulishughulikia. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Naibu Waziri wakomae sana katika hili, vilevile kumuachia COASCO yeye ndiye anakagua ushirika, hapana, naomba akague lakini na CAG naye aende kukagua ili kujiridhisha.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)