Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kukupongeza sana wewe. Nakumbuka wakati tumekuchagua, ulipokuwa unaeleza vipaumbele vyako, moja ya kipaumbele ulichotueleza ni kwamba baadaye sisi Wabunge hatutahangaika tena na makaratasi, utaleta Bunge mtandao. Tunakushukuru sana. Hata mimi mwenyewe sasa hivi sibebi karatasi, nami pia nimekuwa wa kisasa. Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nakaangalia ka Msigwa sijui kameenda wapi, kwa sababu unajua mimi huwa najiuliza, yaani haya maneno yanazungumzwa na mtu anaitwa Mchungaji,…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: …anatuaminisha tuache kufuata maelekezo ya Madaktari, watu walioumiza vichwa, wakasoma wanajua kinga ya Corona, anatuaminisha kama Mganga wa Kienyeji, halafu kenyewe kanatoka kanaenda kunawa pale. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hawa watu ni watu wa hatari sana na tusikae kimya Waheshimiwa Wabunge. Sisi tunaelekeza kusikiliza maelekezo ya Madaktari, watu wanaojua; na tutanawa. Tunaiomba Serikali ongezeni hata ndoo barabarani tuendelee kunawa. Hawa watu kama akina Msigwa hawa, anapiga porojo humu anakaa kwenye you tube, kenyewe kamepita mlangoni pale kamenawa maji kameondoka.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba sana watu kama hawa tusiwafumbie macho, lazima tupate muda wa kuwaambia, hili siyo suala la mizaha. Kuna watu wetu kule vijijini walishaamini kabisa na tunanawa mara tatu au nne, anakuja kutueleza Wazungu wananawa maji. Wazungu wa wapi aliowaona wananawa kila dakika? Hata ukiingia kwenye washroom zao kuna makaratasi, halafu mtu anakuja kutuambia mambo ya kihunihuni. Naomba sana watu kama hawa tuweze kuwakemea. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana watu wa Mkoa wa Dar es Salaam. Tunaona na kweli Watanzania wameelewa. Jana nilikuwa naangalia kwenye TV, ule mlundikano wa kwenye daladala umeisha automatically. Kwa hiyo, tunaomba na Wakuu wa Mikoa wengine waige mfano kama ule wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nikupe mfano mmoja; mimi na mwenzangu Mheshimiwa Tizeba na Mheshimiwa Ngeleja hapa; ili wapiga kura wetu Mwanza, pale kuna pantoni. Ukiondoa ile pantoni ya Serikali kuna ferry za mizigo kule Kamanga Ferry. Hizi ferry zinabeba watu zaidi ya 1,500 wakati uwezo wake wa kubeba labda ni watu 300 au 400. Malori humo humo, mafuta humo humo. Kwa hiyo, naomba Serikali iangalie namna kwa watu wetu ambao wanatumia hicho kivuko. Ikiwezekana Mheshimiwa Engineer Kamwelwe kama yuko hapa aweke watu wasimamie, zile ferry zinatakiwa zibebe watu 300, haiwezekani ukalundika watu 1,000. Tusije tukasababisha mambo mengine kwa wapiga kura wetu.

Mheshimiwa Spika, lingine, kwanza tunaishukuru sana Serikali. Tumepata taarifa kwamba mmepata mkono ule ambao watu walisafiri kwenda kuupinga. Kitu ambacho nitawashangaa, kama watu walitumia mamilioni kwenda kuharibu tusipewe hela, halafu sasa hivi zimekuja hela, umpelekee mgao wa hizi hela, nitawashangaa Mawaziri. Ninaomba kabisa sisi ambao tulikaa kimya na kuomba kila siku kwa Mungu tupate huo mkopo, mtuangalie, sisi tuna shida na shule zetu. Hao watu ambao walienda kuponda, achaneni nao msiwape.

Mheshimiwa Spika, lingine, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, tumepata Halmashauri kwenye vijiji vyetu. Ni kweli Serikali ina wazo zuri kabisa, imepeleka huduma kwa wananchi, lakini naomba kama kuna uwezekano, Serikali ione dharura yoyote, kule tulikohamia hakukuwa na maandalizi na hatukuwa na bajeti. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona dharura sasa, zile Halmashauri ambazo zimegawanywa ziweze kupelekewa hela ili waweze kuandaa makazi na ofisi za kufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lingine nilijaribu kuingia siku moja kwenye Kamati ya TAMISEMI, nikawa nasikiliza, kwa mfano Mkoa wa Dar es Salaam; tunapiga kelele kila siku hapa tupeleke hela kwa vijana, watu wenye mahitaji maalum na akina mama, lakini ukisikiliza mpango mzima, tunatengeneza Taifa la watu wajinga tu. Hakuna mtu anapewaga hela ya bure. Zile hela za Halmashauri ni kama tunazitupa tu bila kuwa na mkakati wowote wa kuhakikisha fedha inarejeshwa.

Mheshimiwa Spika, hata kule Bungeni nilikuwa nawasikiliza Wajumbe mle hakuna aliyesema zimelipwa ngapi? Tunang’ang’ana kulundika tu. Mkoa mmoja wa Dar es Salaam peke yake umetoa kama shilingi bilioni nne, hamna mtu anayezifuatilia hizo hela. Mnawaza tu tena na mwakani kulundika. Tutakuwa tunatengeneza watu wajinga tu baadaye hawana akili ya kutafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kama kuna utaratibu, basi tuangalie baadhi ya mikoa yenye uwezo tuweze kuzilinda hizi hela, tufungue hata taasisi ambaoo tutaweka watu wenye kazi hiyo hiyo kwa ajili ya kushughulika na masuala ya kukopesha na kudai kuliko kuwa tunachukua hela, tunalundika, watu wanaenda kuolea. Hii naona kama haijakaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, suala la afya. Serikali imefanya vizuri sana kwenye afya. Tumepata Vituo vya Afya na Hospitali za Wilaya. Naomba sana, mimi kwangu kule ninakotokea, hospitali nzima ya Wilaya nina Madaktari watatu kwenye population ya watu 600,000. Hicho kitu hakiwezekani. Kwa hiyo, naiomba Serikali, yale mazingira ambayo tumepewa hospitali mpya, basi waangalie kwenye huo mgao hao madaktari walioajiriwa watupatie Madaktari kwa sababu unakuta ikama inataka labda watu 20, una Madaktari watatu utafanyaje?

Mheshimiwa Spika, tumepewa x-ray na vitu vyote kama echo machine na kadhalika halafu hakuna mtumishi. Mpaka leo unakuta labda zina miaka miwili yamelundikwa tu ndani lakini hakuna mtaalam wa kuzitumia. Kwa hiyo, naiomba Serikali tunapokuwa tunanunua vitu, tuandae na mpango mzima wa kuweza kusimamia zile hela.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, limezungumzwa suala la Ofisi za Wabunge, kwa kweli ni shida. Waheshimiwa Wabunge wengi hapa ukiwaangalia hapa, Ofisi zao ni magari na wananyanyasika kweli kwa Wakurugenzi. Mkurugenzi mwenyewe hana Ofisi, iwe wewe Mbunge! Kwa hiyo, naomba kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Bajeti, ni vizuri suala hili likasimamiwa na Bunge, tuache kupeleka TAMISEMI, hatutapata Ofisi. Unakuta mtu ameniga tai halafu Ofisi iko kwenye gari. Kwa hiyo, ni vizuri walivyopendekeza Kamati, basi mrudishe kwenye Bunge, halafu Bunge lenyewe ndiyo lisimamie kutengeneza Ofisi za Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)