Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, naanza kwanza kwa kukupongeza wewe uliyenipa nafasi hii ya kuchangia. Wewe ni Spika wa kiwango cha hali ya juu, lakini pia mwenye weledi, mwadilifu, mwenye busara na ni mchapakazi. Nakupongeza kwa dhati hasa kwa sababu ya utendaji wako mzuri wa kazi, lakini pia kwa ajili ya Bunge mtandao.

Mheshimiwa Spika, mimi binafsi imenisaidia sana. Kwanza imenisaidia kuongeza uelewa, lakini pia imenisaidia kuondoa mabegi na viroba vya vitabu ambavyo vilikuwa vinajazana nyumbani kwangu. Ahsante sana. Sasa hivi nyumba imekuwa na nafasi ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wangu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais anayetokana na Chama cha Mapinduzi, Chama ambacho kina sera nzuri, chama imara, kinakubalika na sera zake zinatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nawapongeza wasaidizi wake, Makamu wa Rais pamoja na Waziri Mkuu. Waziri mkuu amekuwa akifanya kazi nzuri sana. Tumemwona kila maeneo ya nchi yetu. Kama kuna jambo lolote linajitokeza, basi mara moja anatokea na kuweza kufanya suluhisho la jambo hilo ambalo liejitokeza. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mungu akujaalie kila la kheri, akupe uzima na afya njema na Bunge lijalo urudi ukapate kura za kishindo, ikiwezekana upite bila kupingwa Ruangwa. Hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina kila sababu ya kuendelea kupongeza Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo anasaidiwa na wanawake wawili mahiri sana; Mheshimiwa Jenista Joachim Mhagama na Waziri Angellah Kairuki. Hawa akina mama wanafanya kazi vizuri sana.

Mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Katiba na Sheria ambaye ninafanya kazi sana na Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunaona namna ambavyo wamekuwa wakijibu hoja zetu Waheshimiwa Wabunge ambao ni Wanakamati na pia tumeona umahiri wa utendaji wao wa kazi. Hongereni sana, wanawake, tunaweza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo ndiyo maana wameweza kukidhi maono ya Mheshimiwa Rais; kwanza kwa uratibu mzuri ambao wamekuwa wakiufanya na usimamizi mzuri. Hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, progaramu ya kukuza ujuzi kwa vijana ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imetekelezwa vizuri sana. Kutokana na ufinyu wa ajira, lakini Wizara hii imekwenda mbali zaidi, vijana wengi wameweza kupelekwa kwenye mafunzo ya Vyuo vya Ufundi Stadi ikiwepo VETA na vyuo vingine kama Don Bosco. Vijana wamepata mafunzo mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, tunapozungumzia suala la ajira kwa vijana huwezi kuacha kuzungumzia suala la vitalu nyumba ambayo inaitwa greenhouse, ambapo kwa mapana na marefu sana sisi tumekwenda tumekagua miradi mbalimbali ya vijana kwenye kila Halmashauri, miradi hii imewekwa. Niseme tu baada ya muda mfupi, inawezekana kabisa tukawa tumefikia uchumi wa kati tunaoutarajia kupitia hawa vijana. Vijana hawa pia wamejikita katika shughuli za viwanda vidogo vidogo vya utengenezaji wa chaki, pamoja na kutengeneza mafuta na mambo mengine mengi. Kwa kweli Ofisi hii iko makini sana.

Mheshimiwa Spika, miradi mikubwa ambayo inaendeshwa katika nchi yetu inayotekelezwa kwa sasa ikiwemo miradi ya barabara za lami lakini pia reli ya umeme, standard gauge, Stiegler’s Gorge, bomba la mafuta, umeme wa REA na usafiri wa anga, kwa kweli imeleta tija sana katika nchi yetu. Miradi hii imefungamanisha maendeleo ya watu, uchumi wa nchi pamoja na kipato cha kila mmoja. Miradi hii imeongeza ajira. Uchumi wa sekta binafsi kwa kutoa huduma umekua.

Mheshimiwa Spika, miradi hii pia imesababisha wananchi kupata kipato kupitia katika shughuli mbalimbali, mfano; kwenye suala la ujenzi, wananchi waweza kupeleka kokoto, wameweza kuuza cement, kukusanya mchanga na kupeleka maeneo ya ujenzi. Kwa hiyo, hii imesaidia sana kukuza kipato kutokana na miradi hiyo mikubwa.

Mheshimiwa Spika, nachelea kusema miradi hii ina tija na niseme tu kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kutoa mafunzo mbalimbali ili hawa vijana waweze kuendelea kuwekeza na kupata tija zaidi katiak maisha yao.

Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Tume ya Uchaguzi kwa sababu imetekeleza takwa la kikatiba na kisheria kwa kuboresha daftari la kudumu. Hata sasa tunavyozungumza wananchi wapya zaidi ya milioni saba wameweza kujiandikisha katika daftari la kudumu. Sasa niseme tu, kwa wale wenzetu wenye tabia ya kuchukua mpira na kuweka kwapani, safari hii tunaomba sana msichukue mpira kuweka kwapani na kukimbia uwanjani. Twendeni uwanjani, uchaguzi upo, twende tukapambane uwanjani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa, naomba nichukue nafasi hii kumpongeza sana Kamishna Mkuu wa TRA, Dkt. Mhede, kwa kazi nzuri sana ambayo anaifanya ya ukusanyaji wa mapato. Amekuwa mbunifu na tumeshuhudia mwezi Desemba amekusanya mapato na kufikia shilingi trilioni 1.9, haijapata kutokea. Pongezi nyingi sana kwake. Namwomba tu Rais wangu kipenzi, Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, ikibidi huyu Dkt. Mhede ampe zawadi nono.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia suala la kukua kwa maendeleo, ni muhimu sana tukazungumzia pia barabara ambazo ziko pembezoni kwenye mikoa ya pembezoni ili kuweza kufungua mawasiliano ya kiuchumi na uchumi wetu uweze kukua kwa pamoja, usiende kukua kwa upande upande. Kwa mfano hapa, nitazungumzia barabara ambayo ina urefu wa kilometa 124, inayotoka Songea Mjini kwenda Mkenda. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Jacqueline.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naunga mkono hoja.