Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi nzuri anayowafanyia Watanzania. Hongera sana Mheshimiwa, tuko pamoja nawe, hatuna wasiwasi kabisa kwamba kazi inafanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kwanza ni ujenzi wa barabara ya Mpwapwa – Kongwa kwa kiwango cha lami. Kwanza nishukuru sana Serikali kwamba bajeti iliyopita ambayo tunamalizia mwezi Juni ilitenga fedha kidogo kwa ajili ya kuanza kutengeneza barabara ya lami kutoka Mpwapwa - Kongwa lakini barabara hiyo mpaka sasa haijaanza kutengenezwa. Nina wasiwasi hata fedha haijatolewa, sasa naomba maelezo kwa nini fedha haijatolewa. Mheshimiwa Waziri Mkuu mwaka huu nina hakika atatenga fedha za kutosha kwa ajili ya utengenezaji wa barabara ya lami Mpwapwa - Kongwa.

Mheshimiwa Spika, lakini barabara ya Mpwapwa inaanzia Mbande kwenda Kongwa, kuna barabara inatengenezwa kuanzia Mbande kwenda Kongwa na ilianza kutengenezwa mwaka 2012 mpaka leo hii haijakamilika. Tatizo Mheshimiwa Waziri Mkuu wakandarasi hawalipwi. Kwa hiyo, naomba wakandarasi walipwe na hii barabara inayokwenda kwa Mheshimiwa Spika kutoka Mbande kwenda Kongwa iweze kukamilika na barabara ya kutokwa Kongwa junction mpaka Mpwapwa nayo itengenezwe kwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la pili ni fedha kuchelewa kufika katika mikoa yetu pamoja na Halmashauri za Wilaya. Suala hili linatuathiri sana katika Halmashauri, miradi mingi sana imelala. Ujenzi wa madarasa, vituo vya afya na zahanati umekwamba. Kwa sababu fedha zimechelewa kupelekwa mikoani na wilayani kuna viporo vingi sana katika Jimbo la Mpwapwa, Jimbo la Kongwa, pamoja na Jimbo la Kibakwe. Kwa hiyo, naomba fedha zitolewe mapema kwenye mikoa na Halmashauri za Wilaya ili ile miradi iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni kuhusu mapato ya Halmashauri pamoja na madeni ya Madiwani. Mwezi Februari, Waziri wa TAMISEMI aligawa mashine za kukusanyia mapato katika Halmashauri lakini jambo la kushangaza bado Halmashauri nyingi mapato ya ndani (own source) ni kidogo sana na own source ndiyo uhai wa kila Halmashauri. Ni kweli Serikali inatenga fedha kwa ajili ya Halmashauri lakini fedha zinachelewa kufika na zinazofika ni kidogo sana. Kwa hiyo, mapato ya ndani yakikusanywa vizuri nina uhakika kabisa miradi ya maendeleo katika Halmashauri itatekelezwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, suala la nne, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa ina madaraja matatu, Daraja la Godegode ambapo namshukuru sana Waziri wa Ujenzi ametenga fedha kwa ajili kujenga daraja lile, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri na Daraja la Nghambi la Kinyasungwi nalo vilevile limebomoka.

Mheshimiwa Spika, wiki iliyopita Daraja la Mpwapwa Mjini limebomoka. Kwa hiyo, kutoka Posta kwenda Mpwapwa Mjini hakuna daraja, magari hayawezi kupita. Jana kuna daraja lingine tena la kutoka Hospitali kwenda Godegode nalo limechukuliwa na maji. Sasa sina madaraja, magari yatapita wapi?

Mheshimiwa Spika, naomba msaada wa Serikali na kama inawezekana Waziri wa Ujenzi kesho au keshokutwa au Jumamosi atume Naibu Waziri atembelee Daraja lile la pale TANESCO kuona kama kuna uwezekano liweze kufanyiwa angalau matengenezo. Niliomba angalau Barry Bridge ili magari yaweze kupita kwa muda. Kwa sasa hivi mvua bado zinanyesha lakini mkituwekea Barry Bridge katika daraja lile la kutoka Posta kwenda Mjini pamoja na Daraja la Godegode ili magari yaweze kupita. Ni tatizo kubwa sana kwa wananchi wa Mpwapwa, naomba msaada wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja kwa asilimia 100 bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)