Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Godfrey William Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GODFREY W. MGIMWA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi uliyonipa kuweza kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Awali nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini pia nimshukuru Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na nikushukuru wewe binafsi kwa kazi nzuri ambayo unaendelea kuifanya hapa Bungeni. Vilevile niendelee kuwashukuru na kuwapongeza Mawaziri; Mheshimiwa Jenista Mhagama, Naibu Waziri Mheshimiwa Mavunde lakini vilevile na Mheshimiwa Ikupa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hotuba ya Waziri Mkuu lazima niseme kwamba imesheheni mambo makubwa na ya msingi sana na nasema hivi kwa sababu kuna baadhi ya mambo ambayo yameelezwa kwenye hotuba hii ambayo nitaenda kuyagusa, naamini kabisa kwa upana wake tunaweza tukabadilisha mtazamo wa nchi lakini vilevile kama tutajikita vizuri katika hotuba hii tunaweza tukapata majibu mazuri kwa changamoto mbalimbali ambazo ziko mbele.

Mheshimiwa Spika, labda nianze tu kwa kusema kwamba nitaanza kwa masuala mtambuka hasa kwenye hotuba ambayo kidogo imegusa kwenye masuala ya UKIMWI. Tatizo tunalolipata katika Taifa letu ni maeneo mbalimbali ambayo yanaguswa kwa kiasi kikubwa na maambukizi ya UKIMWI lakini vipaumbele vinapelekwa katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, nasema hivi nikiwa na takwimu za mikoa kadhaa. Kwa mfano kwa Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya na hasa sasa hivi Mkoa wa Dodoma ambapo tunaona maambukizi ya Ugonjwa wa UKIMWI yanazidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa. Miaka mitano iliyopita Mkoa wa Dodoma ulikuwa kwenye asilimia 3.5, leo hii Dodoma tunazungumza asilimia 5.8, haya ni maambukizi ambayo yanakwenda kwa kiasi kikubwa na hivyo basi napenda kuishauri Wizara husika kwamba, tunavyoangalia tatizo hili la UKIMWI linavyoendelea kukua katika mikoa mbalimbali basi tupeleke nguvu pale ambapo kuna tatizo kubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa unakuta Asasi nyingi za Kijamii na za Kiraia zinaenda kupeleka misaada mbalimbali kwenye maeneo ambayo takwimu zinaonesha kwamba maambukizi ya ugonjwa huu yapo chini. Sasa kwenye maeneo kwa mfano Mkoa wa Iringa ambapo kwa kweli tatizo ni kubwa, lishe duni na mambo ambayo yanaendana na hayo, naomba sana Nyanda za Juu Kusini iweze kutazamwa vizuri kwa sababu kule ndiko kwenye matatizo makubwa sana. Naamini kabisa Mheshimiwa Jenista tumekuwa naye kwenye Kamati mara kwa mara, ni msikivu na ataendelea kufanya kazi vile ambavyo fedha zitaendelea kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba kuna tatizo kubwa kwenye Mfuko wetu wa ATF. Ukiangalia mwaka jana unakuta Serikali ilitenga fedha za kwenye Mfuko wa ATF shilingi milioni 804 lakini ilitoa shilingi milioni 705. Sasa maeneo mengi ambapo Mfuko wa ATF ulitakiwa uimarishwe labda hauimarishwi kwa sababu maeneo yenye matatizo haya ni mengi na ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba fedha ambazo zimetolewa na wadau au ambazo zinaendelea kutolewa na wadau, kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati kwamba wadau wanaanza kujitoa. Sijui kama nchi tunajipanga vipi kuhakikisha kwamba Mfuko huu wa ATF ambao ulikuwa mahsusi kabisa kwa ajili ya kuboresha suala hili la UKIMWI tunafanyaje kuhakikisha tunaongeza fedha kwa kiasi kikubwa ili tuweze kujimudu wenyewe kama nchi. Naomba sana eneo hili tuweze kuliwekea mkazo ili fedha ziweze kupatikana na Serikali ya Tanzania tuweze kuona namna gani sasa tunaweza kujiimarisha wenyewe bila kutegemea wageni. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwambabajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni endelevu. Nilikuwa nikitizama bajeti ya mwaka jana 2018/2019 nikilinganisha na hii, nasema endelevu kwa sababu gani? Bajeti ya mwaka jana ilikuwa inaonesha kwamba vijiji ambavyo tunavyo Tanzania ni 12,268. Kwenye upande wa REA peke yake mwaka huo kulikuwa kuna vijiji 5,746 ambavyo vilikuwa vimeunganishwa na umeme lakini kwa upande wa asilimia tulikuwa tuna asilimia 47. Mwaka jana 2019/2020 vijiji vimeongezeka kutoka 5,746 mpaka 9,001, hii ni sawasawa na asilimia 73. Kwangu mimi naona lazima tuipongeze Serikali kwa juhudi kubwa ambazo inazifanya kuhakikisha kwamba umeme unapelekwa vijijini na wananchi wetu wanapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwenye maji, maji pia kulikuwa kuna miradi 65 sasa hivi 2020 tuna miradi 94 ambayo ukiangalia kwa ujumla wake ni asilimia 64. Kwa hiyo, tunaona ambavyo Serikali imejikita moja kwa moja kwa wananchi kuhakikisha kwamba inaondoa tatizo la maji na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna baadhi ya maeneo kwenye maliasili tunaona kwamba miradi mbalimbali imeongezeka lakini mapori mengi yameongezwa na yamepandishwa hadhi kwa mfano Burigi, Ibanda na Rumanyika. Nilipata nafasi ya kwenda kule Rumanyika na Ibanda kwa kweli, ukiangalia unaona Serikali imejikita kuhakikisha kwamba inaongeza mapato yake kwa kiasi kikubwa kupitia maliasili na utalii. Kwa hiyo, tuendelee kui- support Serikali ili tuweze kupata fedha za kigeni za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa upande wa vijana, mwaka 2018/2019 mikopo ilitolewa kwa jumla ya shilingi bilioni
4.2 lakini mwaka uliofuata mikopo ilishuka kwa vijana ikatoka kutoka shilingi bilioni 4.2 ikaenda shilingi bilioni 3.2. Nashauri Serikali iangalie eneo hili la vijana ambao ndio Taifa la leo na kesho kuhakikisha wanapata ajira za kutosha na wanajisimamia wenyewe. Vilevile kuhakikisha kwamba ujasiriamali ambao wao binafsi wameamua kujiwekeza basi tunawaongezea nguvu na tunawapa namna ya kuhakikisha kwamba wanaweza kujikimu na kuendelea kufanya kazi kwa ajili ya ujenzi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni suala la ugonjwa wa Corona. Kwa kweli, ugonjwa huu ni janga kubwa kwa sababu ukiangalia Marekani, Uingereza, Italia, Hispania, ni mataifa makubwa ambayo yana uchumi mkubwa lakini kwa namna moja yameshindwa kuzuia ugonjwa huu. Tatizo nalolipata mimi ni kwamba, je, Serikali yetu ya Tanzania tunafanyaje kuhakikisha kwamba wananchi wanapata elimu ya kutosha ili kufahamu ukubwa wa tatizo hili? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika maeneo mbalimbali ya starehe, vijana sasa hivi unakuta kuanzia saa moja, saa mbili mpaka usiku wa manane wako katika maeneo ya starehe. Sasa maeneo kama yale tukishindwa kuyazuia sijui tukipata tatizo hili tutakuwa katika hali gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lazima tuangalie uchumi ambao tunao katika nchi yetu. Lazima tuwe na dawa na lazima tuweze kuwapeleka waathirika wa ugonjwa huu katika maeneo ambayo yatakuwa yametengwa. Sasa tunawawezeshaje watu hawa kielimu kuhakikisha kwamba wanaweza kuepukana na tatizo hili?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)