Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba radhi sauti yangu ina shida kidogo lakini nitajitahidi ili Waheshimiwa Wabunge waweze kusikia majumuisho.

Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nimshukuru Mungu kwa Baraka ya upendeleo kwa siku nyingine ya leo ambayo nimepewa kwa ajili ya kutumikia.

Mheshimiwa Spika, tarehe 13 Juni, 2019 niliwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu Taarifa ya Hali ya Uchumi ya Mwaka 2018, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2019/2020 na Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka 2019/2020; na kwa muda wa siku saba za kazi tangu tarehe 17 hadi leo tarehe 25 Waheshimiwa Wabunge wamepata nafasi ya kuzipitia hotuba hizo pamoja na viambatisho vyake na kutoa maoni na ushauri juu ya namna bora ya kujenga uchumi unaogusa wananchi wengi na kufanikisha utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi lakini pia Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuendesha mjadala huu vizuri na kwa kweli unatarajiwa kuhitimishwa leo hii kwa kura ya wazi ya kila Mbunge kama ulivyosema.

Mheshimiwa Spika, jumla ya Wabunge 236 wamechangia hoja niliyowasilisha, na kati ya hao 189 wamechangia kwa kuzunguza, 41 kwa maandishi. Aidha, Waheshimiwa Mawaziri wanne, Naibu Mawaziri wawili akiwemo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango wamechangia kwa kutoa ufafanuzi kwa baadhi ya hoja zinazogusa sekta wanazosimamia, ninawashukuru sana. Vile vile nina washukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yenu, hakika mmetekeleza wajibu wenu wa Kibunge vizuri sana.

Mheshimiwa Spika, na kipekee napenda kutambua na kupongeza uchambuzi na ushauri wa Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe.

Mheshimiwa Spika, lakini pia namshukuru Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kwa maoni na ushauri aliousoma kwa niaba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

Mheshimiwa Spika, wakati wa mjadala wa hituba nilizowasilisha, Waheshimiwa Wabunge wengi walimpongeza Mhehsimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uongozi makini na kwa kusikiliza kero za makundi mbalimbali ya jamii na kuelekeza ufumbuzi wa kero hizo. Aidha, walipongeza na kuunga mkono bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha kwa maelezo kwamba bajeti ikaakisi matarajio ya Watanzania na inazingatia maslahi ya taifa na wadau wengi. Kwa niaba ya Serikali nimepokea kwa unyenyekevu shukurani na pongezi zote zilizotolewa kutoka ndani na nje ya Bunge juu ya bajeti hii. napenda niahidi kwamba baada ya bajeti hii kupitishwa rasmi na Bunge, Serikali itafanya kila linalowezekana kuitekeleza kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, yako aadhi ya maeneo mapya ambayo yaliungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge wengi nitasema machache tu:-

i. Kwanza ni hatua ya Serikali kufuta au kupunguza ada na tozo 54;

ii. Serikali kukutana na wafanya biashra na kuanza utekelezaji wa blueprint;

iii. Kuanza na kuendeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati

iv. Kutopandisha ushuru wa bidhaa kwa mazoea na hususani sigara na bia;

v. Kuielekeza TRA kubadilika ili kuwa na urafiki na walipa kodi na kupunguza utegemezi wa kibajeti na pia hatua za kikodi kulinda viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Spika, yapo maeneo mengi ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameishauri Serikali iyawekee msukumo wa kipekee katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha na bajeti zinazofuata. Naomba napo nitaje machache tu:-

i) Ni kuweka mkazo zaidi kwenye kilimo hususani utafiti, mbegu bora, huduma za ugani, pembejeo, kuongeza thamani, kutafuta masoko na kilimo cha umwagiliaji

ii) Kuwezesha upatikanaji wa taulo za kike kwa gharama nafuu

iii) Kukwamua upatikanaji wa mikopo ya kugharamia miradi muhimu ya maendeleo Zanzibar; na

iv) Uanzishwaji wa wa mfuko wa pamoja wa fedha za Muungano.

Mhehsimiwa Spika, haya tu ni baadhi lakini yako mengi sana; na kwa kuwa tutaleta majibu kwa maandishi ili kila Mheshimiwa Mbunge asome tutayaorodhesha yote ili Waheshimiwa Wabunge waweze kuona mamambo makubwa ambayo tuliyachukua.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kuanza kutolewa ufafanuzi hoja na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge. Kama nilivyotangulia kusema mjadala wa siku saba ni vigumu kuutolea ufafanuzi kwa dakika 50; kwahiyo tutaleta ufafanuzi wa hoja zote na kila Mheshimiwa Mbunge atapata ufafanuzi.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza, naomba nianze na hiiambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameieleza kwa kirefu, kwamba msamaha wa kodi wa ongezeko la thamani uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike zinazotambulika kwa HS code 9619.00.10 kwamba urejeshwe na Serikali ichukua hatua za maksudi kuhakikisha wafanya biashara wa bidhaa hiyo wanashusha bei au wanawekewa bei elekezi.

Mheshimiwa Spika, Serikali imetafakari sana juu ya mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu hitaji hili muhimu kwa mtoto wa kike na wanawake kwa ujumla. Kwa kuzingatia maoni na ushauri uliotolewa, napendekeza mambo matatu yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kama vile ambavyo nilieleza kwenye Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali tarehe 13 Juni, 2019; kwamba ni kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni (Corporate Income Tax) kwenye Sheria ya Kodi ya Mapato kutoka asilimia 30 mpaka asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020/2021 kwa wawekezaji wapya wa viwanda vya kuzalisha taulo za kike. Lengo la hatua hii ni kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa hii bidhaa muhimu sana pamoja na kuongeza ajira na mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hatua ya uwekezaji inaweza kuchukua muda kiasi, na ni nia ya Serikali kuhakikisha kuwa hatua hii inaleta manufaa kwa haraka, Serikali pia imeamua kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020/2021 kwa viwanda vilivyopo vinavyozalisha bidhaa hiyo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, narudia tena. Serikali pia imeamua kupunguza kiwango cha kodi ya mapato ya makampuni (Corporate Income Tax) kutoka asilimia 30 hadi asilimia 25 kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia mwaka ujao wa fedha hadi mwaka 2020/2021 kwa viwanda vilivyopo hivi sasa hapa nchini ambavyo vinavyozalisha bidhaa hii. Aidha, ni matumaini ya Serikali kuwa hatua hii itasaidia viwanda hivyo kuongeza uzalishaji wa taulo za kike na kupunguza bei ya taulo hizo. Kwa upande mwingine itaongeza matumizi ya pamba inayozalishwa hapa nchini, na pia itaongeza ajira, na hii ni pamoja na hatua nyingine ambazo Mheshimiwa Naibu Waziri amezieleza; kwa maana ya ujenzi wa viwanda kimoja na MSD na kingine kule Simiyu kwa ajili ya kuzalisha bidhaa hii muhimu kwa ajili ya watoto wetu wa kike na wakina Mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatua ya tatu inabaki ileile kwamba tunafuta msamaha wa VAT uliokuwa unatolewa kwenye taulo za kike kwa kushindwa kuwezesha upatikanaji wa bidhaa hiyo muhimu kwa bei nafuu kwa walengwa badala yake kuwanufaisha wafanyabiashara. Kwa kweli lengo la Serikali ni kumnufaisha mtoto wa kike na sio wafanyabiashara kujilimbilikizia faida kubwa.

Mheshimiwa Spika, napenda kutumia nafasi hii kusisitiza kwamba dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba bidhaa hiyo muhimu inapatikana kwa bei nafuu na hivyo kuwawezesha watoto wa kike na wanawake kuinunua. Kwa msingi huo tutaingia mkataba wa makubaliano yaani performance agreement na kila mwekezaji atakayenufaika na punguzo hili la kodi ya mapato ambao utaainisha wajibu wa kila upande, lakini sasa Serikali itafuatilia pia mwenendo wa bei za hizo taulo za kike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa kwamba Serikali iboreshe maslahi ya Watumishi wa Umma. Serikali inathamini sana mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya nchi yetu na si kweli kwamba Serikali imewasahau watumishi kama ilivvyozungumza na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge. Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa maslahi ya Watumishi wa Umma yanaboreshwa. Katika mwaka 2016/2017 Serikali ilipunguza kodi kwenye mishahara yaani payee kutoka digit mbili mpaka digit moja. Aidha, mpaka kufikia bei mwaka 2018/2019, Serikali imelipa madai mbalimbali ya watumishi jumla ya shilingi bilioni 64.97 na pia ilipandisha madaraja watumishi wote waliokuwa wanastahili, ambapo jumla ya shilingi bilioni 14.55 zilitumika kufika Mei, 2019.

Mheshimiwa Spika, naomba nilitaarifu Bunge lako kuwa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kuboresha maslahi ya wafanyakazi iko pale pale kama alivyoahidi wakati wa kuadhimisha Sherehe za Mei mosi mwaka huu 2019 kule Jijini Mbeya.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa kupunguza kodi kwenye mishahara ya watumishi, naomba nilitaarifu niwaatarifu Waheshimiwa Wabunge kuwa Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikifanya maboresho ya mifumo ya kodi, tozo na ada mbalimbali ili kuongeza mapato; kuboresha mazingira ya kufanya biashara lakini pia mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii yanayoguswa na mfumo huo. Hata hivyo muundo wa uchumi (economic structure) umebadilika sana tangu miaka ya 90. Aidha, mahitaji ya fedha za kugharamia matumizi ya kawaida ya Serikali na ya miradi ya maendeleo kwa ustawi wa jamii yetu umeongezeka, lakini pia gharama za maisha kwa wananchi na hususani wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba, Serikali inakusudia kuunda timu maalum ya kufanya uchambuzi wa kina utakaohusu kupitia mfumo wa viwango vya kodi, tozo, ada na matumizi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, Taasisi na Mashirika ya Umma kwa lengo la kuviwianisha au kuvibadili ili viendane na wakati. Kazi hiyo pia itapendekeza marekebisho ya sheria na miundo ya taasisi husika. Kazi kama hiyo ilifanyika mara ya mwisho mwaka 1991, miaka 28 iliyopita. Aidha, kwa kuwa kazi hiyo itahusisha kupitia mfumo mzima wa kodi na namna inavyogusa wafanyakazi na makundi mbalimbali ya jamii, wawakilishi wa Vyama vya Wafanyakazi watashirikishwa kikamilifu katika zoezi hilo. Mapendekezo mengine ambayo yanaweza kutekelezwa kwa taratibu za kiutawala yatatekelezwa kupitia nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa kwamba deni la Serikali limeendelea kuwa kubwa mwaka hadi mwaka na hivyo kuathiri uchumi wetu na maisha ya wananchi kwa ujumla. Katika kipindi cha mwaka ulioishia Aprili, 2019, deni la Serikali liliongezeka kutoka trilioni 49.86 na kufikia shilingi trilioni 51.03 Aprili, 2019, ambayo ni ongezeko la asilimia 2.35. Pia ikumbukwe kuna utaratibu madhubuti wa kuhakikisha kuwa mikopo inayochukuliwa inazingatia vigezo vyote vya uhimilivu, makadirio ya fedha zitakazotokana na chanzo hiki yanaidhinishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, ongezeko la deni limetokana na mikopo mipya kama nilivyosema kwenye Bajeti Kuu ya Serikali na imetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo bomba la gesi, ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli na mitambo ya kufua umeme na kadhalika. Hata hivyo, mwenendo wa deni katika nchi zenye mazingira karibu sawa na Tanzania nao unaonesha kuwa nako madeni yanaendelea kuongezeka hususan kutokana na mahitaji makubwa ya kujenga miundombinu na huduma muhimu za jamii. Ukiangalia takwimu za Ghana, Ethiopia, Uganda, Kenya na Rwanda unaona, mwenendo ni kama huu wa kwetu.

Mheshimiwa Spika, ilitolewa hoja kwamba Serikali kukopa ndani kinawaathiri sana wananchi hasa wajasiriamali na kushindwa kupata mikopo kwenye mabenki na taasisi za fedha na ilidaiwa kwamba ni kutoka kwenye taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Naomba kutoa maelezo kwamba Serikali inakopa katika soko la fedha la ndani kwa utaratibu wa kutoa hatifungani na dhamana za Serikali kwa muda mfupi kupitia minada. Amana hizo zinanunuliwa na watu binafsi, mabenki, mifuko ya hifadhi ya jamii, mashirika ya bima pamoja na taasisi mbalimbali. Kiwango cha kukopa katika soko la ndani kinazingatia uwezo wa soko, kiwango cha ukwasi katika uchumi pamoja na kuhakikisha kuwa haipunguzi uwezo wa taasisi hizo kukopesha sekta binafsi.

Mheshimiwa Spika, sekta ya benki imeendelea kuwa imara na benki zina ukwasi wa kutosha ambao unakadiriwa kuwa takribani asilimia 30% ya mahitaji ya malipo mbalimbali ikilinganishwa na ukomo wa chini wa asilimia 20%. Kiwango hiki kinatosha kutoa mikopo kwa wateja na kuwekeza katika maeneo mengine ya uzalishaji, lakini pia Benki Kuu imeshusha kiasi cha amana ambacho mabenki yanatakiwa kuweka Benki Kuu (statutory minimum reserve) kutoka asilimia 10% mpaka asilimia 7.5% na hiyo imeongeza ukwasi katika mabenki kwa ajili ya kukopesha na kuwekeza katika maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, ilikuwepo hoja kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha imekuwa ikifanya mabadiliko kwenye bajeti iliyopitishwa na Bunge kimya kimya bila kuomba ridhaa ya Bunge, this is very serious allegation. Mpaka kufika Machi 2019 Serikali ilitoa mgawanyo wa matumizi ya kawaida kwa Wizara na Idara Zinazojitegemea, Mikoa na Halmashauri kiasi cha shilingi bilioni 355.815 zaidi ya bajeti iliyokuwa imepitishwa na Bunge ya shilingi trilioni 20.468 na kufanya jumla ya fedha iliyotolewa kuwa shilingi trilioni 20.824 na kwamba hii inakiuka sheria ya bajeti kwa kubadili matumizi ya fedha tofauti na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge.

Mheshimiwa Spika, napenda kutoa maelezo yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, baada ya Bajeti ya Serikali kuidhinishwa na Bunge ikiwa ni pamoja na kuidhinisha sheria ya matumizi ya mwaka (Appropriation Act) hatua inayofuata ni utekelezaji wa bajeti ambapo Waziri mwenye dhamana ya fedha amepewa mamlaka ya kusimamia na kudhibiti utekelezaji, ufuatiliji na tathmini kwa mujibu wa kifungu cha 10(2)(b) cha Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015. Kifungu hiki kinasomeka kwamba nanukuu:

“The Minister shall be responsible for controlling and supervising the preparation, execution and monitoring of the budget including adjustment to the budget”.

Mheshimiwa Spika, vilevile Sheria ya Bajeti namba 11 ya mwaka 2015 imetoa Mamlaka kwa Waziri wa Fedha na Maafisa Masuuli kufanya marekebisho ya bajeti iliyopitishwa na Bunge wakati wa utekelezaji wabajeti. Marekebisho haya hufanywa ili kuwezesha Mafungu kutekeleza baadhi ya shughuli ambazo makadirio hayatoshelezi kwenye vifungu vilivyotengwa wakati wa maandalizi ya bajeti. Kwa upande wa Maafisa Masuuli ni kifungu cha 27(1) cha Kanuni za Sheria ya Bajeti ambacho kinawapa Mamlaka ya kufanya uhamisho wa ndani ya mafungu yao kwa kiwango kisichozidi asilimia 7% ya bajeti iliyoidhinishwa.

Mheshimiwa Spika, Kifungu cha 28(2) cha Kanuni za Sheria ya Bajeti kinampa Waziri wa Fedha Mamlaka ya kufanya uhamisho wa bajeti kati ya Mafungu kwa kiwango kisichozidi asilimia 9% ya bajeti yote ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, mpaka kufikia mwezi Aprili uhamisho wa fedha ndani ya mafungu umefikia shilingi bilioni
964.6 ambayo ni sawa na asilimia 2.7 ya bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge kwa mwaka huu wa fedha. Aidha, uhamisho wa Fedha kati ya mafungu ni shilingi bilioni 660.78 sawa na asilimia 2.03 ya bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge kwa mwaka 2018/2019, hivyo marekebisho ya bajeti yaliyofanywa kwa mwaka huu wa fedha yako ndani ya wigo unaoruhusiwa kisheria.

Mheshimiwa Spika, Bunge huwa linapewa taarifa ya uhamisho wa fedha kwa mafungu namba moja na namba mbili kwa mujibu wa kifungu cha 41(8) cha Sheria ya Bajeti. Katika mwaka 2018/2019, taarifa hizo za uhamisho wa nusu mwaka yaani Julai mpaka Disemba, ziliwasilishwa kwenye kikao cha Bunge cha mwezi Januari 2019 na nimebeba hapa nakala ya statement of reallocation between vote, reallocation namba moja ya mwaka 2018/2019 ambayo ilishagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja kwamba tuanze sasa kutumia mfumo wa uchumi wa soko jamii hapa nchini na kwamba mfumo huu umefanikiwa kuziimarisha na kuendeleza nchi mbalimbali duniani na wakati huo kuwaondoa wananchi wa nchi hizo kwenye umaskini na kuwapatia fursa za ajira zenye uhakika. Nafikiri hapa Waheshimiwa Wabunge naomba waniazime masikio kidogo kwa sababu nataka kutoa darasa kidogo. Mfumo wa uchumi wa soko jamii yaani social market economy ni mfumo wa uchumi ambao unaendeshwa kwa kuchanganya misingi ya uchumi wa soko pamoja na dola kutoa huduma za jamii bure kwa wazee, wagonjwa, wasiojiweza, maskini na wasio na kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumo huu uliasisiwa Ujerumani na Australia ukijulikana kwa jina la Kijerumani, sasa bahati mbaya sijui Kijerumani. Baadhi ya nchi za Ulaya na zilifanyika hivyo kushughulikia hifadhi ya jamii, huduma za afya kwa makundi ya jamii kama hao niliowataja. Sasa msingi wa uchumi wa soko jamii ni soko huria lakini pia utoaji wa social safety net na ili mfumo wa uchumi jamii uweze kufanya kazi ipasavyo, yapo walau masharti matatu ambayo ni lazima yatekelezwe.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kwamba Serikali iwe na uwezo wa kukusanya mapato ya kutosha kuendesha Serikali, kugharamia miradi, shughuli za maendeleo na matumizi ya umma na hususan miundombinu ya msingi ya usafirishaji, nishati, afya na kadhalika, lakini mapato ya ziada kuweza kugharamia progam za jamii yaani welfare programmes, hilo ndio sharti la kwanza. Sharti la pili ni lazima nchi iwe na usimamizi madhubuti wa fedha za umma na sharti la tatu lazima pawepo utaratibu wa wazi na wa haki katika kugawa rasilimali na mapato ya nchi kwa makundi ya nchi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia maelezo hayo kuhusu huo mfumo wa uchumi wa soko jamii ni wazi kuwa mazingira ya mfumo huo ili ufanye kazi ipasavyo, bado yanahitajika kujengwa hapa nchini na Serikali ya Awamu ya Tano imeweka nguvu kubwa katika kujenga misingi hiyo. Serikali ya Awamu ya Tano imeelekeza nguvu kupanua wigo wa mapato kupitia ajenda ya kujenga uchumi wa viwanda na kuongeza ukusanyaji wa mapato sambamba na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato. Pia Serikali imeweka mkazo katika kusimamia matumizi ya fedha za umma. Serikali pia imechukua hatua kuhimiza kila mtu afanye kazi na kulinda rasilimali za nchi ili ziwanufaishe Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo nawasihi wenzetu upande wa pili wasikimbilie kuiga yaani copy and paste bila kujenga misingi ya mfumo huo kuweza kufanya kazi katika mazingira na tamaduni za Mtanzania. Ni vyema pia kutambua kwamba mfumo huo una upungufu na athari zake, kwa mfano watu wanaoishi kwa kutegemea social protection huko kwingine, wanadharauliwa na kuonekana ni wavivu, wenye akili ndogo na wanaishi kwa jasho la wengine. Pia mfumo huo unaweza kuuwa kabisa utaratibu wetu mzuri wa jamii au familia kusaidiana (social capital) kwa mfano katika kusomesha watoto wa kaka au wa wadogo zetu. Kwa hiyo ni muhimu kidogo tuwe waangalifu, tusiende tu kubeba kilichofanikiwa Ujerumani tukakileta hapa kwetu sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nihamie kwenye hoja moja nzito ambayo ilisemwa sana na ndugu zetu kutoka Zanzibar na hususan ikihusu kuchelewa kusainiwa kwa mkataba wa mkopo wa Saudi na BADEA kuhusu ujenzi wa barabara ya Wete Chakechake, kuchelewa kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Serikali ya Muungano na Exim Bank of China utakaogharamia mradi wa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume, Terminal Two, lakini pia kuchelewa kusainiwa kwa mkataba wa mkopo kati ya Serikali ya Muungano na Exim Bank ya China kugharamia ujenzi wa Bandari ya Mpiga Duru.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na mkataba wa mkopo wa Saudi na BADEA kuhusu ujenzi wa barabara ya Wete Chakechake. Kwanza mradi huu unajumuisha ukarabati wa barabara ya Wete hadi Chakechake ambayo ina urefu wa kilomita 22.1. Mradi huu unategemea kufadhiliwa kwa fedha za mkopo kutoka BADEA dola za Marekani milioni 10, Saudi Fund dola za Marekani milioni 11.4, Serkali ya Mapinduzi Zanzibar dola za Marekani milioni 3,000,000 na hivyo kufanya jumla ya dola kuwa milioni 24.4. Licha ya Serikali kusaini mkatana na BADEA, mkataba wa Saudi fund umekwamishwa na kifungu katika mkataba kinachoitaka Serikali kuweka mali zake kama dhamana ya mkopo, mali zilizotajwa katika kifungu hicho ni pamoja na mali za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, mali za Benki Kuu ya Tanzania, Malikale (cultural heritage), mali za kihistoria (historical objects) na mali za Ubalozi, lakini pia mali nyingine zilizoainishwa katika sheria ya Tanzania.

Mheshimiwa Spika, ni dhahiri sharti hili ni kinyume cha sheria za nchi na nasema kweli siwezi kusaini mkataba kwa niaba ya Watanzania kwa sharti hili. Wanaosema nina roho mbaya sana, sawa ni maoni yao, lakini mimi Philip Mpango kamwe sahihi yangu haitatumika kuuza nchi. Pia miradi ya Bara inayosemekana imesainiwa kwa sharti hilo kwa hakika haikukopewa kwa sahihi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na miradi ya Bara inayosemekana imesainiwa kwa sharti hilo kwa hakika haikukopewa kwa saini yangu.

Mheshimiwa Spika, katika kutatua mkwamo huu Serikali inaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Saudi Arabia kama ilivyoshauriwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili waweze kuondoa sharti hili. Napenda niwakumbushe pia kwamba kwa mujibu wa Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana, Waziri wa Fedha na Mipango anashauriwa na kamati mbili; Kamati ya Kitaalam (TDMC) na Kamati ya Kitaifa ya Usimamizi wa Madeni (National Debt Management Committee) ambazo zote zina wajumbe kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hakuna mradi hata mmoja wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambao kamati hizi zilinishauri nikope kwa niaba ya Serikali nikakataa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, Mkataba wa Mkopo Kati ya Serikali ya Muungano na Exhim Bank of China kugharamia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Amani Abeid Karume, Terminal Two. Serikali imekuwa ikifanya majadiliano na Benki ya Exhim ya China ili kupata mkopo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume, (Terminal Two) kwa kiasi cha Dola za Marekani milioni 60. Majadiliano ya kwanza na benki hiyo yalifanyika Disemba, 2018. Exhim iliialika Tanzania kwa majadiliano ya pili ili yafanyike China mwezi Aprili, 2019.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, majadiliano hayo hayajafanyika kwa vile Serikali bado inafanyia kazi masharti hasi kwenye rasimu ya mkataba. Na tunachotaka sisi ni kurekebisha kifungu cha mkataba ambacho kama ilivyo kwenye mradi niliotangulia kuuelezea nacho kinaitaka Serikali kuweka dhamana baadhi ya mali zake zikiwemo mali za Jeshi la Wananchi wa Tanzania, mali za Benki Kuu ya Tanzania, mali kale, mali za kihistoria, mali za ubalozi na mali nyingine ambazo zimeainishwa katika sheria za nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, lakini pia tumewataka waondoe sharti la kuhusisha mkopo huu na deni la kiwanda cha urafiki. Kwa hiyo, Serikali inaendelea na majadiliano ya kidiplomasia, ili kitatua mkwamo huo.

Mheshimiwa Spika, mradi wa tatu ni Mkataba wa Mkopo kati ya Serikali ya Muungano na Exhim Bank of China kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri. Mradi huu unatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za Marekani milioni 200 ambazo zitakuwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exhim ya China; na Serikali ya Muungano iliomba ipatiwe nakala ya upembuzi yakinifu ya mradi huu ili ufanyike uchambuzi na vyombo husika.

Mheshimiwa Spika, hatua ya Serikali kufanya uhakiki imekuwa ikifanyika kwa miradi mbalimbali inayofadhiliwa kwa mikopo nafuu ili tujiridhishe kabla ya kusaini mikataba husika; na hii tunafanya kwa miradi yote. Lengo letu ni kuepuka kuingia gharama kubwa zisizoendana na thamani ya mradi ili tuhakikishe kuwa Serikali inanufaika vyema na mkopo wa masharti nafuu.

Mheshimiwa Spika, taarifa zote hizi nilizozieleza tulizitoa kwenye kikao cha kujadili changamoto za muungano kilichoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Mkamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutolewa maelekezo kuwa kila linalowezekana lifanyiwe kazi ili tufikie mwisho haraka iwezekanavyo. Taarifa za kikao hicho zipo tena kwa maandishi, kwa hiyo inashangaza kweli kwa nini wenzetu hawakupewa hiyo taarifa yake na badala yake ninavikwa roho mbaya sana, naomba tu Mwenyezi Mungu awabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja pia kwamba Sera za Uchumi na Fedha za Tanzania Bara zina athari za moja kwa moja kwenye uchumi wa Zanzibar bila Zanzibar kuwa na intervation yoyote, lakini pia kwamba hadi sasa Serikali haijaunda Kamati ya Pamoja ya Fedha ya Muungano na hivyo kuvunja Katiba na pia kwamba mapato ya Zanzibar ni asilimia mbili na mapato ya Bara ni asilimia 98, asilimia 68 mapato yote yanatumika Tanzania Bara wakati asilimia 32 yanatumika kwenye taasisi za muungano; na kwa hiyo Zanzibar inatakiwa ilipwe trilioni 4.6 kutoka kwenye mapato ya muungano kwa kutumia formula ya mgawo wa asilimia 4.5.

Mheshimiwa Spika, naomba nitoe maelezo kwamba, Sera za Uchumi na Fedha za Jamhuri ya Muungano ni jumuishi na zinazingatia mahitaji ya Zanzibar na Tanzania Bara. Sera hizo zinahusisha hali halisi ya uchumi ya pande zote mbili za muungano. Sera ya Uchumi na Bajeti inapitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano ambalo linajumuisha Wabunge wa pande zote za muungano. Aidha, Sera ya Fedha hupitishwa na Kamati ya Sera ya Fedha (Monetory Policy Committee) ambayo ina uwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kuhusu akaunti ya pamoja; ni kweli Ibara ya 133 ya Katiba inazungumzia uwepo wa akaunti hiyo ya pamoja ambapo zitawekwa fedha zote zitakazochwngwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume ya Pamoja ya Fedha kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Mungano kwa mambo ya muungano.

Mheshimiwa Spika, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa pamoja hivi sasa zinaandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri na hili ni agizo kutokana na kile kikao tulichofanya mwezi Februari chini ya Mheshimiwa Makamu wa Rais; kuhusu utaratibu wa kuchangia gharama za muungano na kugawana mapato ya muungano ili kuwezesha kuwepo utaratibu wa kudumu wa kuchangia gharama za muungano na kugawana mapato ya muungano.

Mheshimiwa Spika, uamuzi huo wa pamoja utakapofikiwa utawezesha kufunguliwa kwa akaunti ya fedha ya pamoja na kwa kuwa, mapendekezo ya uanzishwaji wa akaunti ya pamoja yapo katika ngazi ya uamuzi makubaliano yaliyopo ni kwamba mapato yanayotokana na utekelezaji wa mambo ya muungano yanayokusanywa Zanzibar yatumike Zanzibar kwa ajili ya kuimarisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kule visiwani.

Mheshimiwa Spika, aidha, mapato ya muungano yanayokusanywa Tanzania Bara yatumike kugharamia mambo ya muungano na yasiyo ya muungano Tanzania Bara. Kutokana na makubaliano hayo pande mbili za muungano zimeendelea kunufaika na mapato ya muungano yatokanayo na kodi yanayokusanywa na TRA. Mapato hayo ni kodi ya mapato, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. Pia kila upande wa muungano umeendelea kunufaika na mapato yanayotokana na misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo pamoja na gawio la Benki Kuu. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa inarejesha mapato ya kodi yanayotokanayo na mishahara ya watumishi (pay as you earn) wa muungano wanaofanya kazi upande wa Zanzibar. Maeleozo yote haya yapo kwenye kumbukumbu za mikutano ambayo tunafanya kwenye vikao rasmi kabisa baina ya Serikali zote mbili kuhakikisha kwamba muungano wetu unadumu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa nchi (Mazingira) ameeleza vizuri; maana palikuwa na hoja kwamba bajeti hii ya Serikali haijaeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo upande wa Tanzania Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, nirudie tena kusisitiza miradi ya maendeleo ambayo inatekelezwa nchini inatokana na hatua za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao ni sehemu ya Mpango Elekezi wa Miaka 15 wa kutekeleza Dira ya Taifa. Kwa upande wa Zanzibar kuna dira ya maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020 ambayo inatekelezwa na SMZ kupitia Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini (MKUZA), na sasa ni MKUZA III. Hivyo, utekelezaji wa miradi ya maendeleo upande wa Zanzibar unaainishwa na kutekelezwa kupitia MKUZA III na Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Miradi ya maendeleo kwa upande wa Zanzibar inatekekelezwa baada ya kuidhinishwa na Baraza la Wawakilishi.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, kwamba hoja ni nyingi sana, nitazileta kwa maandishi. Naomba uniruhusu niweze kuhitimisha.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Dokta John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anavyotuambia mara kwa mara, kwamba, maendeleo hayana chama. Tena ameendelea kusisitiza kwamba Tanzania ni nchi yetu wote. Hivyo naomba nihitimishe kwa kusema kuwa bajeti ni nyenzo muhimu ya kufikia matarajio ya wananchi wetu. Na ninawaomba kila mmoja wetu, Waheshimiwa Wabunge, aipigie bajeti hii ya nne ya Serikali ya Awamu ya Tano kura ya ndiyo ili tukaitekeleze kwa manufaa ya Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nitumie nafasi hii kukushukuru tena na pia kuwashukuru viongozi wote wa Wizara ya Fedha na Mipango, bila kumsahau Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango ambaye pia ni Care Taker Minister, Dkt. Ashatu Kijaji na viongozi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Fedha, Wakurugenzi, Wataalam, Watumishi wenzangu wote kwa kujitoa kunisaidia katika kulitumikia taifa letu na wananchi wake usiku na mchana hadi kufikia hatua hii; ninamuomba Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, asante sana kwa fursa hii ya kuhitimisha mjadala huu na asante sana kwa Mungu kwa baraka na nguvu na uwezo alionikirimia kufanya kazi yake mpaka dakika hii.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naafiki.