Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya Waziri wa Fedha na Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, napenda nianze kwa kukupongeza kwa uongozi wako mahiri wa Bunge letu kama ulivyojidhihirisha pia hivi karibuni ulipotuongoza kwenda Misri pamoja na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Naibu Waziri, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha pamoja na timu nzima ya Wakurugenzi, Kamishna wa Bajeti na wengineo kwa kuandaa bajeti hii ya Serikali ambayo imesomwa vizuri na Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Spika, yamezungumziwa masuala mbalimbali ya Muungano katika michango hii na mimi nitapenda kujikita katika mambo kadhaa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika kujibu hoja atajibu mahsusi kuhusu miradi iliyotajwa na iliyochangiwa na Wabunge ambayo walipenda kupata maelezo, mradi wa Bandari ya Mpigaduri, jengo la uwanja wa ndege, barabara ya Chake na miradi mingineyo, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anayo maelezo mazuri na atayatoa. Mimi niongee kwa ujumla tu kuhusu masuala ya Muungano na hasa namna tulivyouzungumzia Muungano humu ndani ya Bunge letu.

Mheshimiwa Spika, wewe unafahamu kwamba Tanzania na sisi sote tuliomo ni nyumba na ni nyumba ya urithi kwa kweli kwetu sisi sote kwa sababu imejengwa na watu wengine na sisi tumeirithi, tunaishi katika Tanzania iliyojengwa na watu wengine na viongozi wetu walioijenga wametangulia mbele ya haki. Namna tulivyouzungumzia Muungano katika michango hii kwa baadhi ya Wabunge maneno yanajenga lakini maneno pia yanabomoa. Baadhi ya maneno yaliyotumika, baadhi ya lugha zilizotumika hazichangii kujenga nyumba yetu hii tuliyoirithi kwa viongozi wetu waliotangulia mbele za haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya maneno humu yametuhumu, yametusi na kwa kweli yameleta fadhaa kubwa. Mimi naomba kwa heshima ya Bunge lako, nchi yetu na kwa dhana nzima ya kuimarisha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwetu, baadhi ya maneno kwa kweli ifike mahali yasiruhusiwe kutumika ndani ya Bunge lako Tukufu hasa maneno ambayo yanachangia kuweka ufa katika Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilipata bahati ya kwenda kuhudhuria bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati inasomwa siku ya Alhamisi wiki iliyopita na niliisikia bajeti imesomwa na Waziri Balozi Ramia. Baadhi ya mchango humu ndani katika bajeti yetu hii kuu ya Serikali ya Muungano imenukuu kwamba bajeti iliyosomwa Zanzibar ilirejea na kuzungumza na kwamba Waziri Mpango na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina roho mbaya, haina nia njema kwa Zanzibar ina hasada, wivu, chuki na kwamba Waziri Mpango na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wamegoma kufanya masuala ambayo yataleta maendeleo kwa Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwepo kwenye bajeti ile, hayo maneno yaliyonukuliwa kwamba yamezungumzwa na Waziri wa Fedha wa Zanzibar hayakunukuliwa hivyo, siyo sahihi. Bajeti ile ilisomwa kwa staha, kwa ustaarabu na ilieleza mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mimi napenda nimpongeze Waziri wa Fedha wa Zanzibar pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuandaa na kusoma bajeti nzuri na ya kujasiri ambayo ina nia ya kuleta maendeleo ya Zanzibar. Kwa hiyo, tusiwatie maneno midomoni viongozi wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kusukuma ajenda zetu za kuleta mgawanyiko katika Muungano wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi kama nchi tumeweka utaratibu wa kushughulikia masuala ya Muungano, yanapojitokeza tunayazungumza na tunayafanyia kazi. Napenda niseme kwa taarifa kwamba kuna ndugu yangu kutoka Pemba alizungumza jana nadhani Mheshimiwa Mohamed Amour na sisi tunaotoka Tanga watu wa Pemba tuko karibu nao, ni ndugu zetu kwa sababu unapanda mashua tu unavuka, unafika Pemba. Ndugu yangu alitumia lugha ngumu kidogo kumsema Waziri Mpango na kuwasema viongozi wa Serikali na kukisema Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, ilichukua uvumilivu kwa baadhi yetu kutohamaki na ilikuwa inazungumzwa ni barabara kwamba kuna barabara ya kilometa 20, kilometa 40 imechelewa kujengwa kwa hiyo basi kwa sababu hiyo watu wote huku wana chuki, wivu, hasada. Kuna masuala mengi sana ya maendeleo ya Zanzibar, yanapojitokeza na mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unapohitajika kuna utaratibu mzuri uliowekwa ambao unatumika katika kuyawasilisha na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mimi nilipata bahati ya kuwa Msaidizi wa Rais Kikwete, mwaka 2005 – 2006 kulikuwa na changamoto ya umeme Pemba, kulikuwa na shida kubwa likaletwa kama suala kwamba Pemba kuna shida kubwa ya umeme katika utaratibu tuliouweka hayakutumika matusi, kejeli wala kudhalilishana. Lilivyochukuliwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikatafuta msaada Norway dola milioni 88 ukawekwa waya chini ya bahari kutoka Tanga kwenda Pemba kupeleka umeme. Huo ni msaada ambao Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliutafuta. Umeme ukapatikana Pemba bila matusi, kejeli au kudhalilishana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya katika miaka ya hivi karibuni ule umeme umeleta changamoto. Mimi ni kiongozi ninayetoka Tanga, watu wenye viwanda Tanga walikuja kutulalamikia mbona Tanga mnasema tujenge viwanda lakini umeme hautoshi? Tukaenda kuwauliza TANESCO jamani mbona umeme Tanga hautoshi? Wakasema, jamani eeh mtuwie radhi, tumewapelekea wenzetu Pemba line moja ya umeme kwa sababu kuna tatizo. Hilo limefanyika bila matusi, kejeli au kudhalilishana. Kwa hiyo, Serikali hizi zinafanya kazi pamoja vizuri, zinashirikiana, hakuna haja ya kuja hapa Bungeni na kusema watu wana chuki, hasada, wanafiki na kadhalika. Maneno hayo yanabomoa nyumba yetu hii ya Tanzania ambayo sisi tumeirithi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala la Sheria ya Mikopo kwamba mabadiliko yameleta changamoto. Naomba niwataarifu Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wiki iliyopita suala hilo imelileta rasmi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limeingizwa katika utaratibu wetu wa kawaida wa kushughulikia masuala ya Muungano. Hapa Bungeni siyo kwamba ndiyo linaletwa kwa mara ya kwanza na Wabunge, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yenyewe imelileta na tayari Serikali zote mbili zinalifanyia kazi na litatolewa taarifa kuhusu namna linavyoshughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais na Rais Shein kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu kuimarisha Muungano wetu. Mimi nakuomba na nakusihi sana Mzee wangu unayenipenda, naomba utusaidie Bunge lako lisiwe chanzo cha kuweka ufa katika Muungano wetu wacha watu wengine huko barabarani wafanye lakini siyo Wabunge, tena wakiwa ndani katika nyumba hii Tukufu na kula kiapo cha kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka mwaka 1992 ndani ya Bunge lilijitokeza kundi la Wabunge 55 ambao walitaka kuchukua hatua ambayo ingesababisha kuvunjika kwa Muungano wetu (G55), wakasema kuwepo na Serikali ya Tanganyika jambo ambalo kwa hakika lingesababisha kuvunjika kwa Muungano. Mwalimu Nyerere muasisi wa Muungano na baba wa Taifa letu aliingilia na akakaa na Wabunge pamoja na Wajumbe wa NEC, sisi tunafundishwa kwamba ni mara chache Mwalimu Nyerere ametoa chozi hadharani ni pale alipopokea mwili wa Sokoine, alipokuwa anamuelezea Mheshimiwa Kawawa na alipokuwa anataka Muungano huu udumu kwa kuwazuia wale watu 55 wasichukue hatua waliyokuwa wanataka kuichukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusingependa kauli hizi zinazotoka humu zikataka kuleta hisia kama zile za mwaka 1992. Tunaomba utuongoze, ninyi ndiyo wazee mliobaki, mwalimu hayupo. Baadhi ya kauli zinazotoka humu zitafanya miili ya waasisi wetu ndani ya makaburi yao ianze kuzunguka kutokana na maneno yanayotoka ya kutaka kuivunja nchi yetu. Tunaomba sana utuongoze, uhodari wa kuwasema wengine ili kupata mtaji wa kisiasa, uhodari wa kuunajisi Muungano kwa maneno machafu ili kupata umaarufu wa kisiasa usikubalike. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni jambo ambalo linakubalika kabisa kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina bajeti yake, ina Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na kuna Ilani ya Chama cha Mapinduzi kwa upande wa Zanzibar. Tunafahamu kabisa kwamba vyote hivyo vinahitaji rasilimali ili kutekelezwa na tunafahamu kabisa kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzana inayo nafasi katika kuhakikisha kwamba Zanzibar inapata uhakika wa rasilimali hizo. Hilo linafahamika na viongozi wetu wanalifahamu na wanalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimalize kwa kusema kwamba tumechagua viongozi mahiri kwa pande zote; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar, tuwaamini kwamba dhamira yao ni kufanya yote yanayopaswa kufanyika kuimarisha Muungano wetu. Tusishindane kwenye uhodari wa kuusema Muungano kama namna ya kuulinda. Tuwachie viongozi wetu na sisi kwa kauli zetu na kwa matendo yetu tuwasaidie katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inabaki moja ili kizazi hiki kiirithishe nchi yetu kwa kizazi kijacho bado ikiwa inaitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)