Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mpango, pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Ashatu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango wangu nilioutoa kwa kuzungumza, naomba niongezee kidogo katika Sekta mbili za Mifugo na Uvuvi pamoja na Utalii. Naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja kuhitimisha hotuba yake anipatie majibu ya maswali kadhaa ambayo naona yana ukakasi kwangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tunaagiza maziwa ya unga kutoka nje ya Tanzania ilhali Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya kuwa na ng’ombe wengi Barani Afrika baada ya nchi ya Ethiopia? Mheshimiwa Waziri atueleze tunapoteza kiasi gani cha mapato kwa kuruhusu uagizaji wa maziwa haya ya unga; kwa kilo moja ya unga ina uwezo wa kuzalisha boksi nne za lita nne nne.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanini Serikali imeruhusu matumizi ya imported milk kwenye ofisi za Serikali badala ya kuelekeza matumizi ya maziwa ya ndani kama tulivyofanya katika eneo la furniture? Moja ya malengo ya kutoza kodi (import tax) ni ku-protect home industries, lakini tumepunguza sana kodi kwenye eneo hili; tunalindaje viwanda vya ndani ambavyo vinatoa ajira kubwa kuanzia kwenye ufugaji, soko mpaka viwandani?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini Serikali isishushe export levy ya ngozi ghafi kuliko kuendelea kuacha ngozi ghafi nyingi kuendelea kuoza ilhali viwanda vya ndani havina uwezo wa kutumia ngozi ghafi yote tuliyonayo?

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ni eneo la maliasili na utalii. Ni vyema Serikali ikawekeza sana kwenye eneo hili. Kwa mfano kwenye Hifadhi zetu za Taifa (TANAPA) tulikuwa na hifadhi 16 na ni tano tu ndizo zilizokuwa zina- break even point. Tumeongeza hifadhi nyingine tano, jumla sasa tunazo 21, na bado zinazo-break even ni tano (5) tu. Kwa hiyo tumeiongezea mzigo mkubwa TANAPA. Ombi; gawio linalopelekwa Hazina lisitishwe au lipunguzwe. Tuongeze mkakati kuhakikisha tunaongeza hifadhi zingine zinazo-break even kwa kukuza utalii wa ndani kwa kurekebisha na kuboresha miundombinu ya barabara na maeneo ya kuishi (makambi).

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni Msitu wa Sao Hill. Eneo hili linaingiza pesa nyingi kwenye Pato la Taifa lakini kuna tatizo kubwa sana kwenye eneo la miundombinu; barabara hazipitiki kabisa na ndiko kwenye eneo kubwa la uvunaji wa misitu. Ni vyema sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha akapeleka pesa kwa ajili ya kuboresha barabara za Mtili, Ifwagi, Mdafuro, Ihemu, Isipii – Mpangatuzwa mpaka Mrimba – ambako kuna pareto, chai pamoja na msitu mkubwa bila kusahau eneo la umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, naunga mkono hoja.