Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kwa kukushukuru wewe na nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi ya kuweza kusimamia na kutoa machango wangu katika hoja hii muhimu ya Hali ya Uchumi wa Taifa, Taarifa ya Utekelezaji wa Bajeti Iliyopita pamoja na Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Mwaka wa Fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuunga mkono hoja kwa sababu zifuatazo;

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na viambatisho vyake imeandaliwa vizuri sana kwa sababu imejielekeza kwa uwazi kabisa wapi tulipotoka wapi tulipo katika kutekeleza ilani ya CCM 2015 na utekelezaji wa Mpango wa Taifa uliozingatia pia Mpango wa Maendeleo Endelevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa kuwa katika mwaka huu wa fedha tunaomaliza kesho kutwa Serikali imefanya kazi nzuri ya kukusanya mapato, kudhibiti mapato, yaliyokuwa yakipotea pamoja na kupeleka fedha katika miradi ya maendeleo. Mwaka huu kila mkoa umepata fedha nyingi ukilinganisha na miaka mingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa sababu bajeti hii imegusa maeneo yote ambayo Mheshimiwa Rais ameyawekea mkazo tangu achaguliwe; Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana kupitia hotuba yake ukurasa wa 16.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono kwa sababu bajeti ya 2019/2020 imepunguza utegemezi kwa kiwango kikubwa. Naunga mkno kwa sababu kodi zote zaidi 54 zilizokuwa vikwazo katika kukuza uchumi zimeondolewa. Naunga mkono kwa sababu vipumbele vilivyowekwa vinalenga kukuza uchumi wa taifa na kutoa huduma kwa wananchi waliotuchagua. Naunga mkono kwa kuwa bajeti hii 2019/2020 ni bajeti ya matumaini.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo haya naomba nijielekeze katika maeneo machache niliyoyachagua kuyatilia mkazo ambayo yanagusa wananchi ninaowawakilisha ambao ni wanawake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ambao walio wengi ni wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Kilimo. Zaidi ya Watanzania 65 wanaotajwa kujihusisha na kilimo asilimia 80 ni wanawake ambao wanalima kilimo cha kujikimu tu, kilimo cha kutegemea mvua, kilimo cha jembe la mkono, kilimo bila utaalamu, mbegu duni, kilimo ambacho mazao yao hayajaongezewa thamani na mazao yao kukosa soko na kukosa mitaji ya kuwekeza katika kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu; pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya kuhakikisha kilimo chetu kinaleta tija kwa wanawake, wananchi na taifa kwa ujumla naomba kushauri yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwaondoa wanawake katika kilimo cha jembe la mkono na kutumia nyenzo za kisasa, kama vile majembe ya kukokotwa na ng’ombe, matrekta pamoja na kupatikana tena kwa pembejeo za kilimo na kwa wakati; na hapa benki ya kilimo ihusike kikamilifu kwa sababu lengo la kuanzisha benki hii lilikuwa ni kuwakomboa wakulima wanyonge ambao wengi wao ni wanawake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kilimo cha umwagiliaji Serikali kwa kushirikiana na Sekta binafsi iongeze wigo wa kujenga miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 475.052 hadi kufikia hekta 1,000.000, ikiwa ni hatua muhimu ya kutekeleza mpango ulioandaliwa na Wizara ya Maji 2018/2019. Kwa kutekeleza mpango huu kilimo chetu kitakuwa ni kilimo chenye kuleta tija.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kuongeza wataalam wa kilimo na kuwawezesha watekeleze wajibu wao kikamilifu. Serikali ipeleke pembejeo za kilimo tena kwa wakati. Serikali kuhakikisha inawawezesha wanawake na wananchi kupata masoko ya mazao ya ndani na nje. Serikali ihakikishe kunakuwepo na viwanda vya kusindika mazao ya wakulima. Serikali iwawezeshe wanawake mitaji ya kutosha katika sekta ya kilimo ili waweze kuanzisha miradi mikubwa. Serikali itoe elimu kwa wakulima juu ya kilimo bora ili wanawake na wananchi waweze kuzalisha mazao yenye viwango vyenye ubora.

Mheshimiwa Naibu Spika, Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi. Pamoja na kwamba wanawake ndio wazalishaji wakubwa, wanawake pia ndio walezi wa familia, wanawake ndio hata wanapopata kipato walio wengi kipato hicho hukielekeza katika familia zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuipongeza Serikali kwa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia fursa mbalimbali, bado wanawake walio wengi ni masikini na hata wanachokizalisha hawanufaiki nacho.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Manunuzi. Swali; Bunge tulipitisha Sheria ya Manunuzi iliyoweka kifungu kwamba kila manunuzi yatakayofanyika au tenda zitakazotolewa asilimia 30 zielekezwe kwa wanawake. Pia tumepitisha sheria ya kuzitaka kila halmashauri kutenga asilimia 10 kwa ajili ya kuwezesha vikundi vya kiuchumi. Pamoja na kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri hiyo bado lipo tatizo la baadhi ya taasisi hizi kutekeleza Sheria ya Manunuzi kwa kiwango cha asilimia 70 kama ilivyoainishwa kwenye sheria baadhi ya halmashauri zinashindwa kutekeleza sheria ya kutoa asilimia 10 ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Vilevile mchango wa wanawake unaotolewa katika kulea familia haujathamanishwa katika kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali; ningependa kujua tangu sheria hii imeanzishwa wanawake wangapi wamenufaika na Sheria hii ya Manunuzi na katika maendeleo? Ni ujenzi wa barabara, ujenzi wa reli nakadhalika. Swali tumepitisha sheria ya kutenga asilimia 10 ya wanawake na vijana na watu wenye ulemavu. Tangu sheria hii imepitishwa ya kila halmashauri kutenga asimilia 10 ya mapato yake ya ndani ni wanawake wangapi wamenufaika ukilinganisha na kabla ya sheria haijarekebishwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali; wanawake wengi wameanzisha vikundi vya kiuchumi; tatizo lao kubwa ni kukosa mitaji, hii ni kwa sababu baadhi ya halmashauri mapato yao yako chini hivyo vikundi havipati mikopo ya kutosha ya kuweka misingi imara ya kiuchumi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzisaidia halmashauri kuongeza vyanzo vya mapato na kufanya uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji katika halmashauri nyingi zinazotegemea mapato yanayotokana na kilimo cha kutegemea mvua? Zikiwemo halmashauri za Musoma Vijijini, na Butiama kupitia Bonde la Bugema na Mto Mara?

Mheshimiwa Naibu Spika, Huduma ya Maji kwa Wanawake na Wananchi Katika Kuchangia Uchumi wa Taifa. Kama nilivyotangulia kusema kuwa wazalishaji wetu wakubwa katika taifa ni wanawake. Wanawake walio wengi wanashindwa kufanya kazi za uzalishaji mali kutokana na tatizo la maji. Ushauri; Serikali iendelee kutafuta fedha kwa ajili ya kuwekeza katika miradi ya maji ili kuwawezesha wanawake kuacha kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji na badala yake washiriki kufanya kazi zitakazowakomboa kiuchumi. Ushauri; kwa kuwa kwa mujibu wa taarifa ya Mheshimiwa Waziri deni la Taifa linahimilika, Serikali iendelee kutafuta mikopo na fedha za ndani kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji. Huduma hii ya maji ikiboredhwa itawakomboa wanawake ambao ndio wazalishaji wakubwa na itachochea uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Upotevu wa Fedha za Miradi ya Maji. Fedha za miradi ya maji zimekuwa zikipotea na miradi kutokamilika kwa sababu za usanifu mbaya wa miradi hiyo na kupewa kandarasi wasio na sifa. Swali; ningependa kujua, je, Serikali imejipangaje kupata wataalamu wa kusanifu miradi na wakandarasi wenye uwezo wa kujenga na kusimamia miradi ya maji?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mchango wa Wanawake Unaotolewa Katika Kulea Familia. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika kulea familia. Je, ningependa kujua kama mchango wa wanawake umethaminiwa na kuingizwa katika mchango wa taifa wa kukuza uchumi? Nimeomba kujua kwa sababu wanawake walio wengi wanatoa mchango katika kulea familia lakini kwa bahati mbaya mchango wao haujathaminika; hivyo, wamenituma niulize, je, Serikali inautambua?

Mheshimiwa Naibu Spika, ukusanyaji wa mapato pamoja na kuipongeza Serikali kwa kukusanya mapato na kuiwezesha Serikali kutekeleza malengo yake ikiwa ni pamoja na kuliona mishahara na kutekeleza miradi ya maendeleo ni na ushauri kidogo katika eneo hili. Serikali iendelee kufuatilia kwa karibu mianya yote ya upotevu wa mapato katika bandari, uwanja wa ndege, bandari bubu, bandari kavu, mipakani pamoja na kwenye manunuzi ya umma hasa katika miradi ya maendeleo nakadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, taulo za watoto wa kike. Nashauri Serikali iwezeshe wanawake wajenge viwanda vidogo vya kuzalisha taulo za kike na kutoa bei elekezi. Fedha inayopelekwa halmashauri kwa ajili ya maelekezo ya kununua taulo za kike ipelekwe kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.