Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hoja hii ya bajeti kuu ya Serikali ya mwaka huu 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kasi kubwa ambayo sote tunaishuhudia, tunaiona ya ukuaji wa uchumi wa taifa letu la Tanzania; nampongeza sana. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, yeye pamoja na Naibu wake; na nipongeze timu nzima ya wafanyakazi wa Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya pale. Tumeona safari hii wametujia na bajeti ya trilioni 33.11 ikiwa ni ongezeko la takriban asilimia 1.9 kutoka kwa bajeti ya mwaka jana ya trilioni 32.48; nawapongeza sana kwa kazi kubwa hiyo mliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo mimi nianze kabisa kwa kuunga mkono hoja hii ya Wizara ya Mipango ambayo imeletwa mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzijadili kwa kina Bajeti za Wizara mbalimbali na tukazipitisha, leo tunajadili Bajeti Kuu. Bajeti Kuu ambayo ndiyo muunganiko wa bajeti zote za Wizara zote ambazo tulizipitisha hapa siku za hapa karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulisomewa taarifa na Waziri wa Mipango kwamba wanajipanga vipi kukusanya hizi trilioni 33.11 zitakazokwenda kukidhi haja ya bajeti ya Wizara zote kwa mwaka huu 2019/2020. Mimi kwa upande wangu naunga mkono hatua zote na njia zote ambazo zimependekezwa. Tumeshuhudia kuna maeneo kodi zimetolewa, tumeshuhudia kuna maeneo tozo zimetolewa lakini kuna maeneo pia zimeongezwa kiutaalam na kukidhi haja, ya kwamba bajeti hii ikawe kweli ni bajeti ya mfanyakazi wa chini hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sana miradi mikubwa ya Serikali ambayo imewekwa kama kipaumbele. Mradi wa SGR, SGR ni ujenzi wa reli ya kisasa, mwendo wa kasi, yenye uwezo wa kufanya kazi kubwa ya kubeba mizigo ambayo itapungua matumizi ya barabara zetu ambazo zimekuwa zikiharibika kwa kubeba mizigo mikubwa sana. Napongeza sana kwa sababu usafiri ni kitu muhimu sana katika kuleta maendeleo ya nchi yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana mradi wa Stiegler’s Gorge, kwa maana ya kupata umeme. Tunapozungumzia kutaka kuivusha nchi yetu kutoka katika uchumi wa chini hadi uchumi wa kati hakuna namna na namna ambayo sisi tumeichagua ni kupitia viwanda. Viwanda bila umeme tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Tunahitaji umeme mwingi na nafuu ili viwanda vyetu viweze kuzalisha bidhaa ambazo zina bei inayoweza kuchukulika na mfanyakazi wa kiwango cha chini hapa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tunazihitaji fedha kwa ujumla wake ili tuweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini. Tunahitaji fedha ili tuweze kutekeleza miradi ya REA. Wamezungumza wengi humu ndani kwamba REA imeonesha dhahiri kwamba ni eneo ambalo limemnufaisha Mtanzania wa kawaida. Umeme umefika vijijini maeneo mengi ya nchi yetu hadi kufikia sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli usiopingika kwamba ya REA si nzuri, inasuasua kwa kiasi kikubwa sana. Tunahitaji tupate pesa ili Serikali ielekeze pesa hizi kwenye maeneo ambayo bado REA haijafika ikafike ili angalau kulingana na mpango wetu kufika 2021 vijiji vyote na vitongoji vyote nchi hii viwe vimeshapata umeme. Naogopa kwa kasi hii tuliyonayo sasa huenda hilo lisitimie, lakini naomba sana; nawaamini sana, Dkt. Mpango kwa mipango yako mikubwa unayoiweka hapa basi suala la REA liangalie kwa macho ya karibu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili nizungumzie barabara. Barabara kwa maana ya TARURA kwa maana ya TANROADS, mgao wa fedha kati ya TANROADS na TARURA wengi wameunzungumza hapa; na mimi niwe mmoja wapo wa kuzungumza. Nakuomba tuangalie namna ya kuweza kuwaongezea angalau kidogo TARURA kutoka asilimia 30 wanazozipata sasa angalau wapate asilimia 40 ili nao waweze kufanya kazi inayotegemewa kwa ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA wanabeba eneo kubwa sana la barabara hapa Tanzania, tena barabara ambazo ni za udongo, barabara ambazo kila mvua ikinyesha zinaharibika, barabara ambazo kila mwaka lazima zifanyiwe matengenezo; tofauti hata na TANROADS, TANROADS wanashughulikia barabara kubwa ambazo kwa kiasi kikubwa zimeshatengenezwa kwa umakini mkubwa, zina lami haziharibiki mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Wizara iliangalie hilo kwa manufaa ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji fedha ili tuweze kutekeleza miradi ya kilimo. Wengi wamezungumza hapa ndani kwamba ili tuweze kuivusha nchi na jinsi tulivyojipangia sisi wenyewe, kwamba tunataka kuivusha nchi toka uchumi wa chini hadi uchumi wa kati kupitia viwanda vinavyotegemea kilimo. Tutegemee kilimo, tukizungumzia kilimo cha kutegemea mvua hapa tutakuwa tunajidanganya. Tunahitaji kuzungumzia kilimo cha umwagiliaji, chenye uhakika hivyo tunahitaji mabwawa ya uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza baadhi ya watu waliopita kwamba maeneo mengi ya Tanzania hasa haya ya kati mvua si za uhakika sana, lakini ardhi yetu ni bora, nzuri na ina rutiba ya kutosha, shida ni maji; lakini maeneo haya haya tunayoyazungumza maji yapo karibu; tunaweza kutengeneza mabwawa na kuchimba visima. Kwa hiyo niombe sana fedha zipatikane ili suala zima la kilimo cha umwagiliaji lipewe umuhimu wake kama tunavyolizungumza hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maji; tunahitaji fedha tupeleke kwenye miradi ya maji; maji safi na salama. Watanzania tunahitaji tumtue ndoo mwanamke, mambo ya kutembea kilometa na kilometa; na kwenye vijiji vyetu kuna maeneo; mimi kuna kijiji cha Nzali wananchi wa Kitongoji cha Mapinduzi akina mama kazi yao ni kuondoka alfajiri kurudi saa 9 hadi saa 10; hii sio. Pamoja na kwamba kuna mambo mengine yanachengesha; tumekwenda mara mbili tunawachimbia visima pale hatupati maji; sasa wenyewe wanasema kwamba kuna wazee hawataki maji yapatikane. Sasa hilo nalo ni jambo lingine lakini kwa hakika tunahitaji kumtua ndoo mwanamke. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo nizungumzie kuhusu miradi ya elimu. Tunahitaji watoto wetu waende shule ili taifa letu liweze kwenda huko kwenye uchumi wa kati, tunahitaj liende kwenye uchumi wa kati likiwa na wananchi wenye kuelimika. Watoto wetu waende shule, madarasa yapatikane, maabara zipatikane na nyumba za walimu zipatikane; zote hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji miradi ya afya pia iweze kutekelezeka. Tupate zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata na hospitali za wilaya ili wananchi tuweze kuwa na afya njema ili tuweze kuifanya kazi ya kuweza kuvusha nchi kutoka hapa tulipo kwenda uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache, naunga mkono tena hoja kwa asilimia 100. Ahsante sana. (Makofi)