Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye bajeti hii. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Philip Mpango, nampongeza na Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji, Makatibu Wakuu na watendaji wote kwa kazi nzuri na kwa bajeti nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, unaposikia hapa tunakuja tunatamba kwamba kuna mafanikio makubwa ndani ya Sekta ya Afya, tumepata mafanikio makubwa ndani ya elimu, tumeweza kutengezea miundombinu mikubwa ya barabara, ndege, ni kwa sababu Wizara ya Fedha inafanya kazi nzuri. Wameweza kukusanya kodi, wametafuta fedha wakaweza kusimamia, nafikiri kule hakuna mchwa na miradi yote ikaweza kutengenezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hii bajeti ni nzuri kwa sababu inalenga wananchi na inalenga maendeleo ya wananchi. Vilevile inalenga kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na namna ya kuwashawishi wawekezaji waweze kuja katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Waziri kwa kuweza kuhakikisha kwamba bajeti yake inaondoa sasa tozo zaidi ya 54 ambazo zilikuwa ni kero kwa wafanyabiashara. Nikitoa mifano tu; mnakumbuka hapa wakulima walikuwa wanahangaika wanashindwa kuuza karanga zao, wanashindwa kuuza mahindi kwa sababu yanaingiliwa na sumu kuvu, lakini sasa hivi kwa kuondoa VAT kwenye vifaa vya kukaushia ina maana kwamba basi wataweza kukausha hayo mazao na kuyauza yakiwa vizuri na yakiuzika vizuri kwenye masoko ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile taulo za watoto (baby diapers) ushuru umepungua kutoka asilimia kumi mpaka sifuri, ina maana kwa akina mama wengi ambao wanaendelea kuzaa watakuwa wamewapunguzia matumizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mashine za EFD wamezipunguzia ushuru kutoka asilimia 10 mpaka sifuri, kwa maana hiyo wafanyabiashara wengi watapenda kununua hizi EFDs, kwanza zinakusaidia kutunza hata kumbukumbu za biashara yako. Kwa hiyo wamefanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashangaa watu ambao wamesimama hapa wanasema kwamba bajeti hii haijapunguza tozo kwenye mifugo na uvuvi. Naomba waende wakaangalie kwenye hotuba ya Waziri, ukurasa wa 78 na wa 79, zimetolewa tozo zaidi ya 15 kwenye mifugo na uvuvi na zote zina mashiko.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa zamani mtu ulikuwa unajichimbia kisima chako nyumbani lakini unatakiwa kulipa ada ya maji ya 100,000; sasa imefutwa. Wanaoanza biashara wamepewa angalau miezi sita waanze kujiandaa tangu unapopewa TIN unakaa miezi sita unaandaa biashara yako ndiyo uanze kulipa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri vilevile katamka kwamba tangu sasa hakuna mfanyabiashara kufungiwa biashara yake kwa sababu labda hajalipa kodi, labda kwa kibali maalum. Kwa hiyo nasema nawashangaa wote wanaosema hii bajeti siyo nzuri, naomba wote tuiunge mkono kwa sababu ni bajeti ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ushuru wa Forodha umeongezwa kwenye bidhaa kutoka kwenye asilimia 25 mpaka 35 kwenye vibiriti, peremende, chokoleti, chewing gum, soseji, hata ushuru wa maji umeongezeka kutoka kwenye asilimia 35 mpaka 60. Nawashangaa ambao wanabeza juhudi hizi za Serikali, hawajaelewa Serikali inataka kutuambia nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niwaulize Wabunge wenzangu; tuna miti kibao ndani ya Tanzania, kwa nini tuagize njiti za vibiriti, kwa nini tuagize vibiriti kutoka nje? Vilevile tunafuga ng’ombe, kuku, nguruwe; kwa nini tuagize soseji kutoka nje? Tunalima kokoa, tunalima kahawa, tuna maziwa, tuna jibini, tunalima miwa kwa maana hiyo tuna sukari; kwa nini tuagize pipi na chokoleti kutoka nje? Pia tuna unga wa mihogo, tuna unga wa ngano, tuna unga wa mtama, tuna maziwa, tuna mayai; kwa nini tuagize biskuti ambazo tunaona akinamama sasa hivi wanatengeneza kwa kutumia unga wa muhogo?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali inachotaka kutuambia kwa kuongeza ushuru kwenye hivi vitu ni kwamba tusiagize hivi vitu kutoka nje. Inajaribu kulinda viwanda vya ndani, inajaribu kuwashawishi Watanzania tuweze kuanzisha hivi viwanda, tutengeneze peremende, biskuti na tutengeneze hizo soseji hapahapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwamba Serikali sasa akinamama hizi biashara wanaziweza, kwa kupitia Mabaraza na Mifuko ya Uwezeshaji wanawake wako kwenye vikundi mbalimbali wawezeshwe, wapewe utaalam, wapewe mitaji, waweze kuanzisha viwanda vidogovidogo, waweze kutengeneza hizi bidhaa ndani, hakuna haja ya kuagiza hizi bidhaa kutoka nje. Kwa hiyo nawapongeza kwa kuongeza huo ushuru wa forodha kwenye hizo bidhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta Binafsi ni sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi. Kwenye Sekta Binafsi hukohuko ndiko tunapotegemea viwanda tunavyosema vijengwe, vitakuwa hukohuko, hukohuko ndiko tunapotegemea ajira za vijana wetu, hukohuko ndiko Serikali inakotegemea kupata kodi kwenye Sekta Binafsi. Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kwamba sasa inawatengenezea mazingira mazuri ili waweze kufanya biashara yao katika mazingira yaliyotulia, wawe na mfumo mzuri wa kodi, sera, sheria na taratibu ziwe ni zile zinaoeleweka lakini zile ambazo hazibadiliki mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Rais wetu ambaye ameweza kuita kikao akakutana na wafanyabiashara akasikiliza kero zao na namshukuru Mheshimiwa Dkt. Mpango na Naibu wake kwa kuona kwamba sasa kero nyingine zimeanza hata kutatuliwa ndani ya bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Mheshimiwa Rais aliacha agizo pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwamba sasa hii mikutano iende ifanyike kwenye ngazi ya kanda. Napendekeza ianze kufanyika kwenye ngazi za mikoa wafanyabiashara waweze kueleza kero zao. Vilevile kwa sababu tunajua kodi lazima walipe ndiyo, lakini lazima wafanye biashara wapate faida na wao walipe kodi. Kwa hiyo waweze kuleta mapendekezo yao ambayo yatasaidia kuboresha mfumo wa kodi ndani ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakulima wa Mkoa wa Kagera wanategemea zao la biashara ambalo ni kahawa na kwa miaka mingi kahawa imekuwa ikichochea na kuleta fedha za kigeni katika Tanzania. Kwa sasa kahawa ilishakuwa tayari imeshakauka, wanayo majumbani, msimu ulishaanza tangu tarehe Mosi, Mei, ni takribani miezi miwili, hakuna kahawa hata moja imeshanunuliwa Mkoa wa Kagera kwa sababu Vyama Vikuu vya Ushirika hawana fedha, Benki ya Kilimo haijatoa hela ya mikopo kwa Vyama vya Ushirika ili waweze kununua hizo kahawa kutoka kwa wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu ni kwamba sasa hawa wakulima wana shida, wanazo kahawa ndani, watashawishika wataanza kuziuza butura, wataanza kufanya magendo wataharibu kazi nzuri ambayo imeshafanywa na Serikali, ikasimamiwa na wakuu wa wilaya wote katika Mkoa wa Kagera pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, kazi ya utokomeza magendo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe basi Serikali kwamba Benki ya Kilimo iongezewe mtaji na kwa haraka sana wapeleke hela kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoa wa Kagera ambayo ni Ngara Farmers, KDCU na KCU ili sasa pamoja na kwamba tumeshachelewa miezi miwili, waruhusu kahawa zianze kununulia na mkulima akiuza kahawa anakuta hela iko pale analipwa palepale, kutakuwa hakuna manung’uniko. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri atueleze hizo hela za Benki ya Kilimo kwenda kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika Mkoa wa Kagera zitaenda lini.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nawasilisha kilio cha wazabuni. Wazabuni hawa walitoa huduma ya vyakula katika shule mbalimbali, labda hata katika hospitali na nini, lakini tangu mwaka 2011 leo hii ni mwaka 2019, wengine hawajalipwa kwa maana ya Mkoa wa Kagera, wanadai zaidi ya milioni 600 na kitu, haya ni madeni ya wazabuni ambayo yalishahakikiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hawa wazabuni walifanya makosa gani? Walitoa huduma kwa Serikali, na Serikali wale watoto kama ni shuleni wakala, wakaendelea kusoma; hawa wazabuni walikopa hela kutoka kwa watu mbalimbali kwamba labda niamini hela nitaleta, hawakuleta, kwa hiyo hawaaminiki tena. Hawa wazabuni walikopa katika mabenki…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)