Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kipekee kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu kwa muda huu kunipa tena pumzi ya kuweza kuchangia mambo ya maendeleo katika nchi yangu, nchi yenye amani, huru na ambayo inaheshimu raia wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue muda huu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kutuletea bajeti nzuri tofauti na bajeti zote na hata huko nje wanasema walizoea kusikia nyongeza kwenye pipi, karanga, kilevi, mafuta, leo mambo ni tofauti kabisa. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wangu huyo, Dkt. Philipo Mpango, Mheshimiwa Naibu Waziri, Dkt. Ashatu Kijaji na mimi nasema kwa kweli hizo PhD zao ni za uhakika. Nampongeza Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu na timu yao yote. Zaidi sana nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliosimama na kuchangia bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa sijaitendea haki nafasi yangu kama sitakishukuru chama changu cha CCM kilichopitisha jina langu mara kilipopokea jina hilo kutoka kwa wanawake wa Kilimanjaro. Nawashukuru sana wanawake hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunazungumzia keki ya Serikali. Keki hii sasa iko kwenye mgawanyo lakini inapatikanaje? Bajeti ya Serikali au bajeti yoyote ile ina pande mbili, ina makadirio ya mapato na matumizi, kwenye mapato tuna kodi, mikopo, misaada na pia kwenye bajeti ya Tanzania tunayo pia nafasi ya kupata gawio kule Serikali ilipowekeza. Hapa niwapongeza sana CRDB kwa kutoa gawio la shilingi bilioni 9.9 zikiweko shilingi bilioni 6.7 za Serikali na zile nyingine kwenye taasisi. Pia NMB walitoa na nadhani mashirika mengine machache yametoa. Naomba huo uwe ni mwendelezo. Upande mwingine wa bajeti una matumizi yanayotumika kwenye social services, vichocheo vya maendeleo ikiweko mindombinu kama barabara lakini yote hayo ni kwa ajili ya maendeleo na mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walipa kodi ni wananchi wote tukiwemo sisi na wale wa chini na ili kodi iongezeke inabidi wale wafanyabiashara wadogo wasaidiwe ili waweze ku-graduate wawe wafanyabiashara wakubwa. Tumeona Serikali yetu imetoa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ili ikifika mahali sasa na wao watakuwa wakubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana kutoa vitambulisho ni moja lakini waendelee kutoa elimu kwa watu hawa ili waweze kuja kuwa wafanyabiashara wakubwa. Hata hivyo, niiombe Serikali yangu sikivu, katika kuwalea hawa wafanyabiashara wadogo na kati wawalipe pia wazabuni, hao ni wafanyabiashara wa kati wanaoenda kuomba mikopo benki, wanatoa huduma Serikalini lakini wakati wa kulipwa inachukua muda sana na watu wale wengine wanakata tamaa au wanaondoka kabisa kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, niiombe Serikali yangu sikivu ilipe pia madeni ya wale wanaotumia utility, wanaotumia huduma za maji na umeme, walipe yale mashirika yanayotoa huduma hizo. Hapa nawaombea sana Mamlaka za Maji ikiwemo Mamlaka ya Maji ya Moshi (MUWSA), deni lake sasa ni takribani shilingi bilioni 2, limeshahakikiwa lakini bado hawajalipwa; DAWASCO imelipwa na pia Arusha imelipwa. Mheshimiwa Waziri wa Mipango na Fedha ametenga fedha, naomba katika ile awamu ya kwanza ya kulipa watu hawa waweze kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme wazi kwamba naunga mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri ili nisije nikasahau. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nina mambo mawili ambayo ni maombi sasa. Naomba ili wafanyabiashara hao katika kuwafanyia mambo yawe rahisi kibiashara, wa kati na wakubwa, ile Blue Print tuliyoambiwa hapa sana chonde chonde iletwe na tufanyiwe semina na wananchi waeleweshwe ili wajue jinsi gani watarahisisha mambo yao kwenye biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ambalo linasumbua sasa hivi, mwaka jana tuliliona ni zuri tukasherehekea ni kuhusu sanitary pads za wanafunzi au wahitaji ambao ni mabinti. Kweli hakuna jambo ambalo ni bure na sisi kila tukisimama hapa tumeona ambavyo Wizara hiyo imepata shida na ilipo-test imeona kwamba jambo hilo halikuwa kwa manufaa ya wahusika. Basi nami nije pia na pendekezo langu, naomba kuwepo na vocha, tunasema kuwe na tozo kama tulivyofanya kwenye chandarua (hati punguzo), ikiwezekana taulo hizi za kike kwa wanafunzi wetu zipatiwe hati punguzo. Tuliona jinsi ambavyo awamu iliyotangulia ilishughulikia malaria ikatoa hati punguzo kwenye chandarua, kiwanda kikaweza kupata msamaha kiasi lakini pia mhitaji anakwenda na hati punguzo kununua. Hawa ni wanafunzi, wapatiwe vocha waende wakapatiwe hati punguzo hiyo waweze kununua pungufu ya bei, kwa ujumla wake tutakuwa tumechangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda mtauliza kwa nini haswa? Mimi ni jinsi ya (K), ni mwanamke, najua shida tunazozipitia toka utoto mpaka kufikia hapa. Kuanzia miaka 15 mpaka kufikia miaka 55, hilo jambo halikwepeki lakini hatuangalii kwa wote tunaangalia kwa wanafunzi na hasa wanafunzi wale ambao wanatoka katika mazingira duni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wanafunzi ambao kwa siku tano hawaendi darasani kwa vile ila hali inakuja na mambo mengi, kichwa kitauma, maumivu ya tumbo, kichefuchefu, lakini sio hiyo tu hata ile kutoka ni shida. Kwa hiyo, ili nisifafanue zaidi kwa sababu wote wanaelewa, naiomba Serikali yangu sikivu iangalie itakachoweza kufanya ili watu hao wanufaike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kuhusu bajeti hii ni kwenye kilimo. Kweli kila aliye humu ndani amepitia eneo la kilimo. Mimi nimetokea eneo ambalo kahawa ndiyo zao la biashara lakini pia kuna ndizi na mazao mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema nini kuhusu kahawa? Wako waoteshaji kahawa wenye mashamba makubwa pembeni yake yuko mtu wa kawaida ambapo shamba lake dogo lakini shamba la mtu yule ni choka mbaya yaani limekata tamaa, shamba na mwenyewe wamekata tamaa. Naiomba Serikali yangu iweze kuzungumza na hawa wakulima wakubwa kama wataweza kuungana sasa na wale ambao wanawazunguka kama inavyofanyika Kilombero kwa out growers wa miwa ifanyike hivyo Kilimanjaro kwa wale wakulima wa kahawa ili tuweze kuwa na kahawa nzuri na tuongeze pato la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye utalii, nataka nizungumzie tu kwamba kuna kodi ambazo wamepunguziwa lakini pia kuna kodi ambazo bado zipo lakini wale waliokuja kama wadau kwenye Kamati ya Bajeti shida yao siyo ile tozo ya kodi. Juzi Mheshimiwa Waziri amepunguza ule ukiritimba wa kwenda kulipa tozo nyingi. Namwomba ikiwezekana kwenye utalii aangalie ili kuwaweka kwenye one stop center wakifika walipe ili watalii hawa wapate tena hamu ya kurudi Tanzania na kuja kutembea bila kufikiria shida zilizopo za kuanza mahangaiko hapa na pale. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)