Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Juma Kombo Hamad

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Wingwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nimshukuru Mwenyezi Mungu nami kunipa fursa hii ya kupata kuchangia angalau mawili matatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha atakapokuja kufanya majumuisho, atujibu masuala au mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni mambo ambayo yamekuwa yakileta mkanganyiko na utata katika taarifa mbalimbali ambazo zinatoka hususan kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii. Sasa ili tujiridhishe, naye kwa sababu ndiye msemaji wa Wizara ya Fedha, basi atakapokuja ana wajibu wa kutuweka wazi ili tujue kipi ni kipi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni mgao wa Zanzibar kwenye mapato ya Muungano, kwa sababu kila siku tunapiga kelele hapa kwamba kuanzishwe account ya pamoja ya fedha ili suala hili lisiwe na utata. Ikianzishwa account ya pamoja ya fedha ina maana ni kusema kwamba mgao utakuja kwenye bajeti na itaonekana kwamba haya ndiyo makusanyo ya Muungano na huu ndiyo mgao kwamba Tanzania Bara ilipata hiki na Zanzibar ilipata hiki, kwa hiyo hilo ni suala la kwanza ambalo namuomba sana Waziri wa Fedha atakapokuja aje atujibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili, ni hilo la mgao lakini sasa kupitia mikopo ya nje, kwamba suala la mikopo ya nje ni suala la Muungano sasa aje atuambie Tanzania, Mwaka 2018/2019 na 2019/2020 inategemea kukopa nini na ilikopa nini na Zanzibar ilipeleka nini. Ninachomuomba sana aje awe mkweli kwa sababu ilitokea mwaka jana kusema katika ile 1.5 trillion kuna bilioni kadhaa zilikwenda Zanzibar, baada ya kutamka hivyo Waziri wa Fedha wa kule akasema kwamba huku hakuna shilingi tano ambayo imekuja sasa utakapokuja Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mpango uje utuambie uhalisia na ukweli ulivyo kwenye mikopo ya nje inayohusu Muungano, umekopa kiasi gani na Je, katika mkopo uliokopa ile 4.5 umeipeleka? Uje utuambie na utuambie ukweli kabisa katika jambo hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, jana Zanzibar kuliwasilishwa bajeti na katika bajeti iliyowasilishwa Zanzibar kukatajwa miradi mitatu na bajeti ile ikasema wazi kwamba katika miradi hii mitatu imekwamishwa na upande wa pili wa Muungano kwamba haijatekelezwa kwa sababu mkwamo huu umetokana na upande wa pili wa Muungano:

Mheshimiwa Naibu Spika, moja; suala la barabara ya Wete-Chake ambayo ina mradi wa BADEA. Hii barabara ina udhamini na ufadhili wa BADEA na bahari mbaya sana tunapofuatilia tunakuta kwamba miradi ya BADEA kwa upande wa Bara hata ukienda Mkoa wa Kagera kuna miradi kadhaa ambayo imefadhiliwa na BADEA lakini barabara hii moja kutoka Wete-Chake ambayo ni kilometa hazizidi 40 mradi huu Mheshimiwa Mpango umeletewa barua ukakumbushwa unatakiwa uweke sign tu kwa ajili ya utekelezaji wake lakini umeshindwa kuweka sign. Umeshindwa kwa sababu hauna interest na hii barabara, lakini wewe ujue Mheshimiwa Mpango wewe ni Waziri wa Fedha inawezekana Wizara ya Fedha siyo ya Muungano lakini unasimamia fedha ambazo ni za Muungano, unasimamia Benki Kuu ambayo ni ya Muungano, unasimamia Hazina ambayo inadhibiti fedha ambayo ni jambo la Muungano. Waziri unapojivua ukasema kwamba mimi ni Waziri wa upande mmoja wa Tanzania Bara na ukajaribu kujikita zaidi kwenye mambo yanayohusiana na Tanzania Bara hapa utakuwa unapotea Kaka yangu na siyo sahihi kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati unasimamia jambo linalohusu pande mbili za Muungano lazima ulisimamie kama vile ni Waziri unayehusiana na pande zote mbili. Unapokuja mradi upo Zanzibar na unataka sign yako kwa nini unapata kigumumuzi? Mheshimiwa Waziri suala moja ni hilo uje utujibu sasa kwamba barabara hii pamoja na kukumbushwa siyo mara moja, wala mbili, wala tatu, ufadhili upo unataka sign yako kwa nini unakwama uje utujibu.(Makofi)

Mbili; suala jingine ni Airport ya Zanzibar Terminal II, kwa kweli tunasikitika sana na tunasikitika sana Mheshimiwa Mpango kuwa ni sehemu ya mtu ambae unakwambisha maendeleo ya Zanzibar. Airport hii inataka kupatiwa mkopo kwa ajili ya kufanyiwa finishing. Imeshajengwa, takribani imeshakamilika inataka kufanyiwa finishing inahitaji fedha kidogo tu, inahitaji mkopo lakini bado Wazanzibar na kupitia bajeti ya jana Baraza la Wawakilishi imesema wazi kwamba wewe ndiyo umekwamisha mradi huu. Kwa maana tunaposema ni wewe tunasema ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano imekwamisha kwa sababu Serikali ya Jamhuri ya Muungano inakopa kwa niaba ya pande mbili za Muungano, suala la mikopo ni suala la Muungano sasa wewe unapokopa kwa uoande mmoja ukasahau upande mwingine lawama zinakuja kwako, hilo ulijue.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo suala hili nalo ukija uje utujibu mkwamo uko wapi, maana yake kuna taarifa kwamba hawa watu walikula hela, wataje! Kama mlipeleka hela zikaliwa watajwe mbona humu Bungeni wanatajwa waliokula hela? Watajwe ili tujue nini cha kufanya lakini usijibebeshe wewe msalaba ambao haukuhusu, kama haukuhusu, kama unakuhusu basi hapa tutakusulubu wewe.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu na muhimu sana ni suala la Bandari ya Mpigaduri. tatizo la Zanzibar ni uchumi, tatizo hasa la Wazanzibar ni uchumi na tatizo la Zanzibar ni umaskini, kinachotukwaza sisi ni umaskini sasa umaskini huu wa Zanzibar unanasibishwa kwamba umesababishwa na upande mwingine wa Muungano. Kwamba upande mmoja wa Muungano unaweka vipaumbele vyake, unaweka miradi yake, unaweka taratibu zake zinakwenda lkini upande wa pili kule unakwamba. Kwa mfano, Bandari ya Mpigaduri ipo ni mwaka zaidi ya 10 na wafadhili wapo, wahisani wapo, wawekezaji wapo ambao wako tayari kuwekeza katika Bandari ya Mpigaduri hata Wachina karibuni miaka miwili, mitatu walikuja pale kufanya survey kutaka kuwekeza Bandari ya Mpigaduri lakini ukija ukiombwa sasa na bahari nzuri sana deni la Zanzibar ni bilioni tano, Zanzibar nzima inadaiwa bilioni tano. Bilioni mbili ni mikopo ya ndani, bilioni tatu tu ni mikopo ya nje hata tukichanga wenyewe tuna uwezo wa kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango unadaiwa trilioni 50 na bado unakopa tunadaiwa bilioni 300, tukikuambia huu hapa mkataba sasa unataka kujazwa mara umeandikwa kwa kiarabu, ulisema ufadhili huu wa Serikali ya Oman, Bandari ya Zanzibar kwa asilimia 80 ilikuwa idhaminiwe na Serikali ya Oman ukataba ukaingiwa, uliandikwa kwa kiarabu, ulipoletewa ukasema umeandikwa kwa kiarabu ukatafsiriwa kwa Kiingereza umeletwa huna jibu hivi tufanye nini? tatizo hasa nini? Miradi imekuja imeikuta miradi kama hii lakini imetekelezwa upande mmoja wa Muungano upande ule kule visingizio haviishi, hivi ninyi hamna watu wa tafsiri wa Kiarabu katika Serikali nzima ya Jamhuri ya Muungano siyo kweli hilo nalo linahitaji jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bandari kwa upande wa Zanzibar ni uchumi, Bandari kwa upande wa Zanzibar ni suluhisho na ni ajira. Bandari ambayo ilikuwa ijengwe na Serikali ya Oman ilikuwa na uwezo wa kuweza kuchukua meli 16 kwa mara moja. Meli kubwa, meli za kisasa ambazo wanaziita wenyewe ni 4G meli ambayo inaweza kubeba makontena 400 mpaka 800 lakini kisingizio chako na Wizara yako na wataalam wako na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha hili analizungumza wazi wazi kwamba eti ikijengwa Bandari ya Zanzibar itaua Bandari ya Tanganyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha anasema kwamba kujenga Bandari ya Zanzibar itaua Bandari ya Tanzania Bara lakini kuimarisha Bandari ya Tanzania Bara haitaua Bandari ya Zanzibar ambayo ndiyo uchumi wa Zanzibar, hivi ninyi Watanzania Bara mna mangapi ambayo mnaimarisha? Mna madini, mna ardhi kubwa, mna kilimo, mna ufugaji, mna uvuvi, hivi kujenga Bandari Zanzibar ni kosa kwamba kuimarisha uchumi wetu leo ni kosa? Huo umuhimu wa kuwa ndugu, umuhimu wa kuimarisha Muungano uko wapi? Hivi mnatueleza nini, mnajenga taswira gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana na hili niseme wazi kwamba ndani ya Bunge hili kuna Wabunge wanatokea Zanzibar na walikuwa ni viongozi wakubwa kule inafika mahali mtu ni Mtendaji Mkuu wa Serikali anasimama Bungeni humu anatumia dakika 10 anaona aibu na anaona haya kuitaja Zanzibar halafu kesho na keshokutwa mwaka 2020 eti anajinasibu anagombea Urais! Wazanzibar siyo mapoyoyo kiasi hicho watakuhukumu. Unaona haya kwa sababu unategemea Urais!

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Juma Kombo Hamad kila Mbunge ana haki ya kuchangia aonacho ni bora, huwezi ukaanza kusema mtu anaona haya unajuaje aliona haya? Kwa sababu bajeti hii ni Bajeti Kuu na Wabunge wengi tu wanazungumza habari za Majimbo yao hamna mtu anawakataza lakini wakati wa kuzungumzia Majimbo ulishapita, ni kwenye ajeti za kisekta ndiyo tunazungumzia Majimbo, sasa hivi unazungumza Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mbunge, wewe ukiamua kutaja Zanzibar ni sawa lakini kiongozi mwingine akiamua kutokutaja usitake wewe kumuwekea maneno kana kwamba yeye amekosea sana mchango wake kwa sababu wewe mawazo yako ndiyo bora, siyo sawasawa. Mheshimu kama yeye anavyokushimu wewe, heshimu mawazo yake na mchango kuhusu Mbunge huyo mwingine aliyechangia unaondoka kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, suala la bandari ambalo kwa mujibu wa takwimu itazalisha ajira karibu 80,000 kwa Zanzibar ni jambo kubwa sana, bandari ambayo itajengwa Zanzibar ile dhana kama kuna dhana, kama kuna tongo za masikio watu zinawatoka wanasema itaua bandari ya Tanzania Bara siyo kweli. Bandari ambayo inaenda kujengwa Zanzibar ni kisaidizi cha bandari ya Tanzania Bara au ni partner wa bandari ya Tanzania Bara. Nchi hii si ni moja? Si tunashirikiana kwenye masuala ya biashara? Si tunashirikiana kwenye masuala ya uchumi? Tunategemeana kwa masuala ya uchumi? Hivi kwa nini huku ni sawa huku siyo sawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango kwa dhana hiyo ya umoja na juzi tumepitisha sheria hapa kwamba mtukopee, sheria ile ikapitishwa humu kwenye Bunge walioipitisha ni sawa, walioikataa ni sawa, sasa leo kama kutukopea hamtaki mnachokihitaji ni nini? Baraza la Wawakilishi sasa hivi kule Zanzibar lina Wajumbe wa CCM watupu lakini inafika mahali Mheshimiwa Dkt. Mpango unaambiwa bajeti ya Zanzibar ndiyo umekwamisha miradi hii, hivi tukueleweje? Maana kama ni mpinzani ni sawa, lakini bajeti ya nchi, bajeti ya Zanzibar inaenda kukusulubu wewe kwamba hawa ndiyo waliokwamisha miradi, hivi hamna haya? maana yake lazima tufike mahali tuambiane ukweli siyo sisi ni bajeti ambayo ilisema kuwa miradi hii minne imekwamishwa na hawa. Bandari ya Mpigaduri, barabara ya Wete-Chake na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kudumisha umoja wetu, kwa kudumisha Muungano wetu haya mambo lazima yaondoke, lazima yashughulikiwe ipasavyo. Mheshimiwa Dkt. Mpango huna budi ushughulike kama Waziri unayehusika na pande zote mbili hata kama Wizara ya Fedha siyo ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo inashangaza umetuletea bajeti, juzi nchi za Afrika Mashariki zimewasilisha bajeti zote zimewasilisha bajeti, nikashangaa nilikuwa najiuliza, humu haujataja Zanzibar umetaja mara mbili wakati unampongeza Dkt. Shein na umekuja kuitaja tena Zanzibar wakati unazungumzia VAT ya umeme, nadhani uliitaja ili ionekane tu umeitaja, lakini haujazungumzia chochote kingine! Sasa mimi nikajiuliza, Zanzibar haiwasilishi bajeti kwa sababu siyo nchi miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki ni sawa, lakini basi tunawasilisha bajeti ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania basi hata kutaja angalau hicho ambacho kinapatikana kule Zanzibar, kwa nini kisiwemo ndani ya hii bajeti? Kwa hiyo Mheshimiwa Mpango mimi nakuomba sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la utalii na hili niseme kwamba suala la utalii siyo suala la Muungano kiukweli, lakini nimestuka wakati tunalalamikia masuala ya biashara tulilalamika kwamba biashara Zanzibar…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)