Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi ya kuweza kutoa mchango wangu wa mawazo katika bajeti hii. Awali ya yote nitoe shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimwa John Pombe Magufuli kwa kuweza kutekeleza ahadi kubwa na muhimu kwa wananchi wangu wa Nanyumbu hasa Kata ya Mikangaula na Kijiji cha Mikangaula kwa sababu Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alitoa ahadi ya kituo cha afya pale Mikangaula. Nami kama mwakilishi wao wananchi nilikuwa naendelea kuwasiliana na Serikali kuhakikisha kwamba ahadi inatimia. Hatimaye kwenye bajeti hii tumeshatengewa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kuanza ujenzi huo wa kituo cha afya. Kwa niaba ya wananchi wale natoa shukrani za dhati kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge nami nimeona niweze kuchangia eneo moja tu la kusisitiza namna ya kukusanya mapato ili Serikali yetu iweze kuwa na uwezo wa kuweza kutoa huduma kwa jamii. Eneo lenyewe ni namna ya kulinda vyanzo vyetu vya mapato. Hapa nakwenda kukiangalia chanzo cha ajira kwa sababu watumishi wanaoajiriwa na Serikali na kampuni za watu binafsi pia wanachangia katika kulipa kodi ya Serikali. Sasa ni vizuri Serikali ikawa makini kuhakikisha kwamba hao watu ambao wanaajiriwa wanalindwa ili wasipotee kwa sababu wakipotea Serikali inakuwa imepoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kutoa mfano mdogo tu ambao naomba Mheshimiwa Waziri auzingatie. Wakati natunga Sheria ya TASAC hapa, Sheria ile ilikwenda kuwaondoa watu wanaitwa watu wa tallying. Watu wa tallying ni kama mashuhuda wa mwenye mzigo, mwenye mzigo akiwa nje akileta mzigo wake hapa anataka watu anaowaamini yeye wauthibitishe kama mzigo kabla haujapokelewa na bandari kama umekuja kama alivyoagiza yeye. Pia kama kuna mzigo unaondoka Tanzania kwenda nje labda majani ya chai, anataka mtu anayemwamini yeye akaungalie mzigo kama ni kweli ndiyo unaopakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tumekwenda kuwaondoa mashuhuda hawa ambao watu wa nje wanapenda kuwaamini. Sasa hii kitu ina athari nyingi, kwanza tunaondoa ajira lakini pili tunakwenda kupoteza kodi ambayo Serikali ingeweza kupata, tatu Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ilikuwa imeahidi kuhakikisha kwamba tunaongeza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nishauri Mheshimiwa Waziri ahakikishe kwamba suala hili la TASAC, kitendo cha kuwaondoa watu wa tallying tunakwenda kufanya makosa makubwa ambayo yataathiri maeneo mengi na makubwa. Kwa hiyo naomba atakapokuja hapa aangalie uwezekano wa kuleta mapendekezo ya kubadilisha sheria ili itakapofika mwezi Julai kama ambavyo wamewaahidi wasije wakawaondoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakwenda kuangalia kule jimboni kwangu na kutoa ushauri mchache, naanza kwenye suala la umeme, umeme Nanyumbu ni shida; Nanyumbu ina umeme usiozidi asilimia 30 ya vijiji vyote ambavyo vina umeme. Nanyumbu tulipata umeme kwa mpango maalum wa Serikali laini REA I Nanyumbu haikupatikana, REA II haikupatikana, REA III tukapata vijiji 13. Kwa hiyo, nashauri Serikali inapoona kuna wilaya au eneo ambalo limekosa umeme kwa kiasi kikubwa basi tunapokwenda kugawa huu umeme watu kama hawa wanatakiwa wapate zaidi kuliko wale wengine. Kwa sababu kuna watu wana asilimia 90 ya vijiji vyao, kuna watu wana asilimia 80 lakini Nanyumbu ina chini ya asilimia 30. Kwa hiyo, nilitegemea bajeti iliyopita tungepata vijiji vingi, kwa hiyo, leo nakwenda kuunga mkono hii bajeti lakini nataka nione kwamba vijiji vyangu vingi vinapata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukija Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu pale Mangaka ukitembea mita 20 nje ya barabara hakuna umeme. Kuna Kitongoji kimoja kinaitwa Mchangani, kama Mbunge naona aibu kupita kule kwa sababu ni mjini pale pale hakuna umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba hawa watu wanapoanza kushuhulikia haya mambo wahakikishe kwamba maeneo makubwa kama Makao Makuu ya Wilaya tuhakikishe umeme unapatikana. Kuna wilaya zina umeme wa kutosha kwa nini Nanyumbu iwe hivyo. Kwa hiyo, napendekeza TANESCO wapewe uwezo wa kuweza kukabiliana na hili eneo langu la Nanyumbu ili wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu wapate umeme, wasiwe watu wa kulalamika kwa sababu sasa wanajisikia vibaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maji yanayotumika pale Mangaka yanatoka kwenye Kijiji kimoja kinaitwa Mara, ni kilomita kama nane kutoka Makao Makuu ya Wilaya. Yale maji tunatumia jenereta laini umeme upo kilomita nane, sasa jenereta zinaharibika wananchi wanakosa maji lakini hata hivyo gharama za uendeshaji ni kubwa, maji yanauzwa kwa bei kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kwenye bajeti hii umeme upelekwe haraka pale kwenye chanzo cha maji ili wananchi waweze kupata maji kwa bei nafuu lakini pia kwa uhakika. Umeme uliotoka Mangaka kuelekea Tunduru hapo katikati pana vijiji vingi sana lakini umeme umeteremka Kijiji cha Mnazi Mmoja pale Michiga peke yake, lakini vijiji vyote vya njiani vimekosa umeme laini kubwa zipo lakini umeme umekosekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri na kuomba Serikali kabla hatujaanza kutoa vijiji vingine tuhakikishe vijiji hivi ambavyo vinapitiwa na laini kubwa vinapata umeme. Kwa mfano Likokola ni Makao Makuu ya Kata hakuna umeme, pana zahanati; Lumesule Makao Makuu ya Kata hakuna umeme lakini pana zahanati. Kwa hiyo, naomba tuvipatie umeme vijiji hivi ili wananchi hawa nao wapate umeme kwa sababu umeme ndiyo maendeleo bila umeme kimsingi huwezi kuwa na maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka nilichangie ni TARURA, TARURA hao ukiwachunguza matatizo yao wana fedha ndogo sana. Wilaya yangu haipati zaidi ya milioni 800 ukilinganisha na ukubwa wa barabara ambazo zipo Nanyumbu hii kitu hawawezi kukabiliana nayo. Kwa hiyo, wananchi wanakuja kuilaumu Serikali, wananchi wanakuja kukilaumu hiki chombo cha TARURA hata sometimes Madiwani kwa sababu bado wananchi hawajaelewa vizuri huu mtenganiko. Kwa hiyo, Madiwani wanapata lawama ambayo siyo yao, sasa naomba sana tuongeze fedha kwa hizi barabara za vijijini lakini pia hata hiyo fedha ndogo ambayo tunawapa kuna tabia ambayo ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Watendaji hawa wa TARURA wa Ofisi Kuu Mkao Makuu TARURA wanatenga labda milioni 800 Nanyumbu, lakini baadaye wakati Nanyumbu imeshingia mikataba ya kutengeneza ile barabara TARURA wanawaandikia barua kwamba sasa mtatumia milioni 600. Sasa hawa wameshaingia mkataba, kwa hiyo tunasababisha mgogoro kati ya TARURA na wakandarasi, tunasababisha mgogoro kati ya TARURA na Madiwani na wananchi hatimaye Serikali yote inakuwa imepata lawama ambazo siyo za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana Serikali tunapotenga hata hicho kidogo ambacho tumekisema kiende, kwa sababu unaposema kisiende wakati wameingia mkataba ni hatara sana. Tunaweza kusababisha hata kushtakiwa na hao wakandarasi, nashukuru sana wakandara wanakuwa wastaarabu lakini kimsingi wanaweza wakatuchoko. Hilo suala naomba sana Serikali iliangalie kwa makini ili tusije tukasababisha migogoro ambayo kimsingi tunaweza tukaiepuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo sikutaka niongee mengi ila nirudi tena kwenye swali langu la mwisho kabisa la umeme. Nanyumbu kama nilivyosema tupo chini sana, ninaunga mkono bajeti hii nihakikishe kwamba Nanyumbu kwenye umeme tutakuwa tumepata vijiji vingi kwa sababu ya nature ya tulikotoka Tulisahauliwa, kwa hiyo tukipendelewa ni sahihi siyo Nanyumbu peke yake, wale wote walioachwa nyuma wakipiwa mwingi awamu hii ni halali yao kwa sababu kuna watu wana vijiji vingi sana. Hilo suala naomba sana Serikali katika awamu hii, na naunga mkono hoja hapa ya bajeti kwa matumaini hayo Mheshimiwa Dkt. Mpango. Nahakikisha kwamba tunaunga mkono bajeti lakini ikatimize haya ambayo wananchi wanategemea wayaone. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru sana muda wangu nimeutumia vizuri naunga mkono hoja, ahsante. (Makofi)