Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Wilfred Muganyizi Lwakatare

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Bukoba Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwanza nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyotolewa hapa na nishauri Serikali chini ya Mawaziri wake wote wawili na washauri wao ni vyema wakachukua ushauri ambao umetolewa na Kambi ya Upinzani kwa manufaa ya bajeti nzuri kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili; Waheshimiwa nizungumze kauli ambayo nimewahi kuitoa hata tangu nikiwa kiongozi wa Kambi ya Upinzani huko nyuma na sasa nairudia kwamba vipindi mfululizo ambavyo tumekuwa ndani ya Bunge hili na mpaka leo hii sijawahi kuona upande wa pili ukisema hii bajeti ni mbaya na kwamba siyo bajeti ya wanyonge, bajeti zote tunaambiwa ni bajeti za wanyonge pamoja na kwamba zinakua kwa kiasi mwaka baada ya mwaka lakini matatizo yanabaki vilevile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwangu mimi nakwenda mbele zaidi ya kuhoji capacity ya wataalam wetu na watu wanaotutengenezea bajeti hizi, kwamba nashauri Researchers wetu, wataalam wetu, taasisi zinazojenga capacity na hata taasisi zinazosaidia capacity building ya sisi Wabunge, wajaribu kuangalia tatizo letu la msingi liko wapi; kwa nini tunatengeneza bajeti ambazo miaka nenda, miaka rudi hazioneshi effectiveness kwa kuondoa umaskini ule unaolengwa wa kipato kwa watu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna masikio, tuna macho, tuna mikono, tunasafiri na leo nilikuwa naangalia kwenye ma-group, naangalia watu waliokwenda Egypt wanatuonesha mahali walipo, wanakopita. Kwangu mimi kinachokuja ni kwamba mambo yote tunayoyaona kwenye runinga au ukienda kwenda geographical ile TV ukaona mambo watu wanayofanya, ile ni brain, brain ndiyo inayofanya mambo yote hayo. Sasa na mimi najiuliza, brain ya sisi Watanzania na wataalam wetu ikoje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi kweli Mheshimiwa Dkt. Mpango, Naibu Waziri, Mawaziri wetu, Wabunge; huko tunakotoka vijijini tunapozungumzia suala la umaskini wa watu wetu, kweli tunahitaji Wazungu ndio waje watuoneshe umaskini wa watu wetu? Hivi mtu atoke hapa aende kilometa 20 tu kutoka ndani ya Dodoma, aone kama hajui umaskini unafananaje, aende aone; hivi tunaridhika na hizi bajeti tunazotengeza kwamba kweli zinajielekeza kubadili hali ya watu wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kabisa, kuna nchi ambazo early 50s kuja mpaka 90s, Nchi kama Indonesia, Malaysia, Philippines, Thailand, Vietnam na sasa Botswana, hata Rwanda hapa jirani ambao tulikuwa tunalingana na wengine wako nyuma ya uchumi wetu wakati tunapata uhuru, wamefanya maajabu gani mbona wana vichwa kama vyetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mbona akina Mheshimiwa Dkt. Mpango ndio wanakwenda katika nchi kule, tena Watanzania wanasifika sana wakienda kwenye mitihani au kuandika thesis wanapata A nyingi, lakini inapokuja kwenye kutafsiri elimu wanayoipata kuja kwenye matendo tunapotelea wapi, mbona mambo hayabadiliki? Naomba hilo tujielekeze tuangalie matatizo yetu kimsingi yako wapi. Tulete Researchers wajaribu kutafiti vichwa vyetu vinaharibikiwa wapi, kutuhamisha akili tulizonazo kwenda kwenye vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba mbili, naomba Mheshimiwa Dkt. Mpango wakati tukieleka Jumanne kupiga kura, nataka aniridhishe na kitu kimoja ambacho hapa katikati kinaweza kunipa ushauri wa kupiga kura; aniridhishe kwamba bajeti hii inakwenda kufanya maajabu gani, anakwenda kufanya maajabu gani tofauti na experience ambayo tumeipata katika bajeti hii inayokwenda kumalizika mwisho wa mwezi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiwa na maana gani; kwamba bajeti iliyopita kwa mapato ya kodi kwamba tuliambiwa kwamba kila mwezi wanapata average ya 1.2 pamoja ni nje ya trilioni 17 ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anazizungumzia. Sasa ukija kwenye average tumekuwa tunaelezwa wanajaribu kupata 1.2 trillion kila mwezi. Kwa bajeti hii inaonekana lazima tutakwenda katika average ya kutaka kukusanya at least 1.4 – 5 trillion kwa kila mwezi kama tutakuwa tumekwenda vizuri, ili tupate ile 19 ya mapato ya kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa experience iliyoonekana hapa kupata hata hiyo 1.2 ni kwamba Mheshimiwa Dkt. Mpango na wasaidizi wake na TRA na taasisi nyingine wametumia mitulinga isiyo ya kawaida. Maana yake wame-pull forces zote kadri walivyoweza; maana yake pale polisi wameshiriki, mgambo wameshiriki, TISS imeshiriki, wajasiriamali nao na vitambulisho wameshiriki, yaani kuna watu wengine hata mpaka wakawekwa ndani na wengine wakawekewa hata kesi za money laundering, yaani hata kwa forces zote hizo lakini amepata average ya 1.2 trillion. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa wakati tukielekea tena kwenye hii bajeti naiita bajeti ya uchaguzi, yaani kupata 1.5 trillion, kama kule alikuwa anatumia viboko nafikiri safari hii atatumia rungu au inabidi atumie SMG kabisa mtaani na vinginevyo mimi naitafsiri kwamba inaweza ikawa bajeti ya mateso na maumivu kwa wananchi wetu na wafanyabiashara. Maana yake tusidanganyane; wananchi watarajie hilo. Vinginevyo kama ni tofauti napo anieleze anakwenda kufanya maajabu gani ili kuwaepusha watu na mambo ambayo mimi nayaota kwamba yatatokea. Kama wafanyabiashara walikuwa wanakimbizana na TRA sasa watahama hata nchi kabisa kwa sababu hali kusema kweli haivutii.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ambalo nataka kumaliza nalo; mimi natoka Bukoba Town na kwa Bukoba Town na wananchi wa Kagera sisi meli, unapomwambia mwananchi wa Kagera meli wameijua tangu wakati wa Mkoloni, kumekuwepo na Mei MV Victoria ile ililetwa tangu wakati wa Mwingereza. Kwa hiyo kwa mwananchi wa Kagera meli ni maisha, meli ni uchumi. Kwa sababu leo mwananchi wa Kagera njia pekee ambayo anapata huduma na kuwa supplied na vitu mbalimbali ni kutumia barabara. Ukitumia barabara tunajua expenses za ku-transport mizigo kwenda mpaka Kagera kwa njia ya barabara, kwamba ni very expensive.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi naomba, tuliona bajeti iliyopita, kwenye upande wa huduma za meli ni kwamba zilikuwa zimetengwa 20 billion, lakini zilizotoka mpaka mwezi wa Nne ni only three billion. Na mwaka huu nimeona zimetengwa 70 billion. Sasa ile 20 ilishindikana na zikatolewa tatu kwa bajeti ya kutafuta kwa mitulinga, sasa hii ya sasa 70 billion sijui zitapatikana wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalizungumza kabisa. Bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Mpango ni Muha na Waha ni wajukuu zetu maana yake ile ya Wahaya babu zao, sisi tunaitwa Wahaya tulipoona mjukuu asilingane na babu tukaondoa ya ikabaki Waha. Hata Mheshimiwa Engineer Nditiye nafikiri anatoka kule na shemeji yangu, Naibu Waziri, sisi Bukoba tunataka meli. Kama meli mpya imeshindikana watupe Victoria yetu aliyoacha Mwingereza, hebu wajaribu kuikarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kwa sababu meli sisi wakati inafanya kazi mfuko wa simenti ulikuwa 17,000, 16,000, lakini sasa hivi kwa barabara simenti 20,000. Sisi Kagera wamekuwa wepesi kutuambia sisi ni mkoa maskini sasa hivi. Ni lazima tutafute tuliharibikia wapi Kagera, Kagera ulikuwa ni mkoa ambao unasifika dunia nzima. Ule mkoa hata wakati tunapata uhuru Mwalimu Nyerere aliwekewa guarantee gari la kwanza kutoka kiwandani na BCU (Chama cha Ushirika cha Kagera). Kwa hiyo huu umaskini wa Kagera mimi nafikiri umetengenezwa tunahitaji Marshall Plan ya Kagera ili mkoa urudi katika nafasi yake, wasianze kutuambia ninyi ni watu wa matatizo, sijui mafuriko huko, matetemeko huko. Sasa turudi katika kuutengeneza huo mkoa ili urudi mahali pake. (Makofi)