Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. ENG. GERSON H. LWENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na viongozi wote wa Wizara ya Fedha kwa kutuletea hotuba nzuri ya bajeti na ameanza kwa kutoa quotation nzuri kwenye Biblia, kawabariki watu ambao wanamuombea. Basi naomba niongeze tu kwa sisi Waheshimiwa Wabunge, tunatakiwa tuwe wamoja, umoja huu ndiyo unatufanya tuweze kusonga mbele na Mwalimu wetu Julius Nyerere aliwahi kusema kwamba umoja ni nguvu, utengano ni udhaifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kuna mambo mengi makubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Tano imeyafanya. Ninukuu mambo saba, yapo mambo mengi, tukitaka kuyataja yote katika miaka mitatu tutakesha hapa kuonesha kwamba kwa kweli wanafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kutoa elimu bure, kila mwezi bilioni 23 zinapelekwa kwenye shule zetu kwa ajili ya elimu bure, ni kitu kikubwa sana. Kununua ndege nane kwa mara moja na kufufua Shirika la ATCL, kupeleka umeme katika vijiji 7,000 katika mpango wa REA, kuanza ujenzi wa SGR Dar es Salaam – Morogoro, kilomita 722 ni jambo kubwa. Kuhamia Dodoma na kujenga mji wa Serikali, Wizara zote zimejengwa katika muda mfupi zimejengwa ofisi za Serikali na kujenga vituo 352 vya afya na hospitali 67 katika muda mfupi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ndugu zangu kama mtu huwezi kuzungumzia haya na kupongeza Serikali ya Awamu ya Tano, ukajisita katika vitu vidogovidogo ambavyo ni kweli vinahitajika lakini haya makubwa ambayo yameanza ni lazima tuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiri pamoja na haya ambayo nimeyasema na Serikali hii imeonesha kuthubutu, ninaomba sana ithubutu katika miradi mitatu; kwanza mradi wa Liganga na Mchuchuma, hapa panahitaji maamuzi magumu ya kuthubutu, hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda bila kuwa na chuma, chuma ndiyo nguzo muhimu katika viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima Serikali ithubutu kuanzisha mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, kama kuna majadiliano basi yasiwe yanachukua miaka kumi bado mnajadiliana. Kama kitu hakiwezekani basi tunajua hakiwezekani tunatafuta mbadala mtu mwingine tukaweza kujadiliana nae ili huu mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kuanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi mwingine ambao niliona ni muhimu na upo kwenye mpango wa miaka mitano ni ujenzi wa Bwawa la Kidunda. Ndugu zangu Bwawa la Kidunda lisipojengwa, Dar es salaam muda si mrefu itakuwa haina maji. Kwa hiyo, tunahitaji sana tujenge Bwawa la Kidunda ili tuwe na maji endelevu katika Mji wa Dar es salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nilikuwa naomba Bwawa la Farkwa kwa ajili ya Mji wa Dodoma, ni mradi muhimu sana ambao tunahitaji Serikali hii ithubutu tuweze kujenga Bwawa la Farkwa. Sasa ili tuweze kufanya mambo haya tunahitaji kupanua wigo wa makusanyo yetu ya mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nashauri kwenye kodi ya majengo, miundombinu ambayo ilitengenezwa na halmashauri zetu, wanaweza wakakusanya kirahisi zaidi kuliko TRA. Hii kodi ya shilingi 10,000 kila nyumba ni rahisi sana zikakusanywa na halmashauri zetu. Kuwe na mfumo tu kwamba zile fedha akikusanya ziingie kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, naona jambo hili kidogo Mheshimiwa Mpango mnasita kulifanya lakini litatusaidia, tutapata fedha nyingi katika kodi ya majengo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la service levy kwa mfano kwenye hoteli na guest house, kutoza asilimia 10 kwenye mauzo, nafikiri hii siyo sawasawa. Na nadhani hata kama mtu unafanya biashara 10% kupata faida ni ngumu sana lakini fedha ile yote inachukuliwa na manispaa yetu na halmashauri. Kwa hiyo, naomba hili jambo mliangalie ili kusudi kwa kweli watu waweze kuwekeza kwenye eneo hili la huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni hivi vitambulisho vya wajasiliamali ambavyo vinatozwa kwa elfu 20 lakini utekelezaji wake unatofautiana kati ya mkoa na mkoa, naomba jambo lihuishwe na pia iainishwe ni aina gani ya biashara za hao watu watakaokuwa na vitambulisho. Mama ntilie anapika supu naye anatakiwa alipe elfu 20 kwa mwaka, ni fedha kubwa sana. Mama amepanga nyanya anauza kwa siku hata 1,000 hapati, na yeye aweze kuwa na kitambulisho cha elfu 20, nafikiri siyo sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tungetengeneza category kama tatu kama mtu anafanya mauzo kwa mwaka yasiyozidi 500,000 hii asihitajike kuwa na kitambulisho. Yule mtu ambaye ana 500,000 – 1,000,000 angalau tumpe kitambulisho cha 10,000, tutapata mapato mengi sana. Halafu wale wanaozidi sasa 1,000,000 – 4,000,000 ndiyo tuweke 20,000. Nina hakika kabisa tukiweka mageuzi haya tutapata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Wanging’ombe pia ina nafasi ya kuweza kuchangia kuweza kupata mapato. Tunalo eneo ambalo ukifika pale Wanging’ombe kuna jiwe ambalo kuna ramani ya Afrika, yaani Mwenyezi Mungu aliweka ramani pale, ukienda pale unapata ramani ya Afrika. Sasa hili tunaweza tukapata, tukiboresha barabara inayotoka Njombe mpaka Iyai tukaweka lami, watalii watakwenda kuangalia hii ramani ya Afrika ambayo Mwenyezi Mungu alikwenda kuiweka kwenye Wilaya yetu katika Kijiji cha Igodiba, tutapata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Msitu wa Asili wa Nyumbanitu ambao unapita barabara hiyohiyo, kuna kuku weusi ambao pengine huwezi kuwapata maeneo mengine duniani utawapata Wanging’ombe. Sasa tutaongeza mapato kwa sababu watalii watakwenda wataangalia wale kuku wa ajabu wapo kwenye Msitu wa Wanging’ombe, karibuni sana muweze kufika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mwekezaji ambaye anataka kuwekeza kuchakata matunda ya parachichi katika Wilaya ya Wanging’ombe toka mwaka jana mwezi wa 8 anazungushwa kuweza kupata leseni na makontena na kila kitu kipo bandarini. Ilikuwa mpaka mwezi wa nne kile kiwanda kiwe kimeshaanza kufanya kazi. Kwa hiyo, naomba sana urasimu upunguzwe katika hizi taasisi mbalimbali zinazohusiana na process ya wawekezaji kuweza kuanza kupata vibali vya kujenga viwanda ambavyo vitatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia sana suala la kukuza kilimo na kuomba bajeti iongezwe lakini ni vizuri tukaangalia tunaongeza bajeti kwenye eneo gani. Kuna wengi wamesema vizuri sana kwamba lazima tuweke nguvu sana katika mbegu na mbolea pamoja na viuatilifu, hapa ndiyo tungeongeza bajeti na tuondoe vikwazo vile vya kuanzisha hizo biashara za kusambaza mambo ya mbegu bora na viuatilifu pamoja na mbolea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiondoa vikwazo nina hakika sana kilimo kitapanda juu na pia tuangalie mazao yale ambayo yanaendana pamoja na viwanda vile tunavyovianzisha. Kwa hiyo, hili jambo ni muhimu sana tuweze kuunganisha ili kusudi ndugu zangu kilimo kikue lakini pia na viwanda viweze kuanzishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo pia tulifanyie nguvu sana ni katika suala la kutafuta masoko ya wakulima. Wakulima wetu wamekuwa wanahangaika sana kwa kuweza kupata masoko ya mazao yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka nichangie machache, naunga mkono hoja hii, ahsante sana. (Makofi)