Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Siha

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kusema kwamba mpaka 2100 yaani miaka 81 kutoka sasa Tanzania inakadiriwa kuwa ni nchi ya sita kwa idadi ya watu duniani lakini itakuwa ni nchi ya pili kwa Afrika ikiongozwa na Nigeria, tukifuatiwa na DRC, Ethiopia na Uganda. Kwa hiyo, mambo yote ambayo tunayafanya leo na mipango ambayo tunaipanga leo ni kujipanga kwa ajili ya kupokea hiyo idadi ya watu na changamoto kwa ajili ya hiyo idadi ya watu. Kwa muda mrefu tulikuwa tukitamani Serikali inayofikiri miaka 100 mbele siyo inafikiri kwa miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali kubwa linaloendelea hapa ni kwamba Serikali hii imekuwa akipanga bajeti kwa ajili ya vitu na sio kwa ajili ya watu. Nianze kwa Wilaya ya Siha, nikija kwenye eneo la barabara, Serikali hii imepeleka shilingi bilioni 52 na barabara ya lami inaendelea kujengwa ndani ya Wilaya ya Siha. Ukienda kwenye TARURA, barabara za kuunganisha vijiji kuna kata moja ya Ivaeni pamoja na Kashashi ilikuwa ili watu waliotofautiana mita 200 kukutana wanazunguka kilometa saba. Serikali hii imepeleka shilingi milioni 960 na sasa wananchi wanaungana kwa kupitia daraja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni nini? Leo utakuta Mbunge anasimama hapa anasema kwamba Serikali hii inapeleka fedha kwenye vitu hapo hapo analalamika kwamba bei ya petroli imepanda kijijini kwa sababu barabara imekatika, unashindwa kuelewa huyu kiongozi anataka nini kifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Wilaya ya Siha, Serikali hii na bajeti hii, Wilaya ya Siha ina vijiji 100 umeme umefika vijiji vyote, ina vitongoji 168 umeme umefika vijiji 125 bado vitongoji 43, ni Serikali hii hii ya Chama cha Mapinduzi. Hii maana yake ni nini? Ukipeleka umeme vijijini wananchi wataongezea mazao yao thamani na watapata karibu huduma zinazohitaji umeme na hata mzunguko wa fedha unaongezeka kwenye vijiji vyao. Hiyo ndio maana yake, tunaposema tunawekeza kwenye umeme mfano Stigler’s Gorge tunapandisha thamani ya maisha kule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata leo ukiangalia Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini, Korea ya Kusini ni tajiri kuliko Korea ya Kaskazini hata kama unapita usiku utaiona Korea ya Kaskazini kuna giza lakini utaiona Korea ya kusini kuna mwanga wa kutosha. Maana yake umeme ndiyo chanzo kikubwa sana cha kusisimua maendeleo ya wananchi. Kwa maana hiyo, tunaposema tunawekeza kwenye umeme wa uhakika na kwa sababu umeme wa maji ndiyo wa bei rahisi mpaka sasa hakuna mwingine, dunia sasa hivi inafanya utafiti namna ya kuwekeza kwenye umeme huu wa uranium na kuweka ndani ya bahari ambapo ni salama zaidi na utatoa umeme rahisi na sisi wangetufikirisha pamoja na sisi kuwekeza kwenye huu umeme wa maji sasa tuanze kufikiria na kujifunza wenzetu wanafanya nini kwenye uranium, hilo ndilo tungelitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye afya kwenye Wilaya ya Siha. Bajeti hii na Serikali hii imepeleka shilingi bilioni 9 Hospitali ya Kibong’oto na shilingi bilioni 1.75 tunajenga Hospitali ya Wilaya. Maana yake ukipunguza magonjwa, huduma ya akina mama na watoto na life span inaongezeka, hiyo ni michango ya kugusa maendeleo ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unakwenda kwenye maji, kwenye kata zingine imepelekwa shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya vijiji 17 na shilingi bilioni 1.75 kwa ajili ya vijiji 13. Maana yake ukipeleka maji vijijini unapunguza magonjwa lakini akina mama muda wa kwenda kuchota maji unapungua. Baada ya muda hata muda wa kufanya kazi za maendeleo unaongezeka lakini magonjwa ambukizi yanapungua na unaongeza maisha ya watu na uzalishaji. Kwa hiyo, hoja ya kusema hii bajeti ni ya vitu siyo ya watu ni uongo uliotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye umwagiliaji sisi kwetu tuna shilingi milioni 380 kwenye Kata ya Levishi na shilingi milioni 450 kwenye Kata ya Kashashi. Maana yake ni kwamba wananchi wanaenda kumwagilia mazao yao kwa kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, maana yake ni bajeti ya watu na inayoenda kukugusa maisha ya watu siyo bajeti ya vitu kama ambavyo wenzetu wanataka kutuaminisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo wenzetu walewale leo wanasema kwamba idadi ya watalii kwenye Taifa hili haiongezeki na wanasema pato la utalii haliongezeki. Watu wamefanya utafiti wameona kwamba wenzetu ambao tunashindana nao kwenye utalii wana ndege na wanasafirisha watalii kwa ndege zao wanaanza kupitisha kwenye nchi zao ndiyo watalii waweze kuja Tanzania. Maana yake sisi Watanzania pesa ya kwanza wanayotoka nayo Ulaya wanapita nazo kwanza kwenye nchi yetu chenchi ndiyo inafika kwenye nchi yetu. Sasa leo tumenunua ndege anaibuka yule yule anayesema kwamba pato na idadi ya watalii haiongezeki anasema kwamba unanunua ndege haigusi maisha ya watu. Haya ndiyo mambo tunayoyasema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia suala la ajira, tunatakiwa tufikiri sana na tunawekeza kwenye elimu, tunaenda kwenye dunia ya artificial intelligence, vitakuja viwanda hapa mtu atakuja na roboti tatu halafu anahitaji watu wenye uwezo wa kufikiri. Ndiyo maana Mheshimiwa Profesa Ndalichako kuna hela nyingi zimewekezwa kwenye elimu na mabweni yanajengwa kwenye maeneo mbalimbali, uwekezaji unafanyika kwenye elimu ili tufike hapo kwa sababu ajira ijayo ndugu zangu siyo hii mnayoipigania hapa ambayo leo inagharimu asilimia 43 ya pato la TRA, ni ajira ambayo inahitaji mtu kufikiri siyo kufanya casual job. Miaka ijayo artificial intelligence, roboti ndiyo zitakuwa zinafanya kazi sasa wanatakiwa watu creative na innovative. Twendeni tukatengeneze watu creative na innovative kwa sababu ndiyo ajira itakayokuwepo siyo aina hii ya ajira ambayo tunaifikiria sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina malalamiko kutoka kwa wenzangu wazuri wa CHADEMA wameniambia jambo niombe kuwasaidia na Watanzania wazuri. Wameniambia kwamba kuna kiongozi wao mmoja mkubwa amekopa ndani ya chama shilingi milioni 600 akaenda kuwekeza Morogoro lakini huo mradi ulivyoshindikana anataka sasa kugeuka hiyo pesa iwe ulikuwa ni mradi wa CHADEMA usiwe tena mradi wa kwake yeye binafsi. Wakaniambia nisaidie hapa kuiokoa hiyo mali ya CHADEMA na tuiombe TAKUKURU iende pale na hata ikiwezekana kwa sababu tunataka maendeleo yanayogusa watu basi hayo matrekta ambayo yanabadilishwa majina na hizo mali kwa sababu hizo pesa ni ruzuku na ni kodi ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango umekusanya, sasa hiyo kodi ambayo Mheshimiwa Dkt. Mpango umekusanya ikaenda CHADEMA halafu mtu mmoja amechukua anataka kuwapakazia CHADEMA baada ya yeye kukopa tunataka ikachunguzwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mashamba ya ushirika kule Siha na Hai tunataka sasa yale matrekta yachukuliwe yaende kwenye hayo mashamba na ichunguzwe tuletewe ukweli hapa. Wakati kule Hai tunaendelea kuchunguza, Sabaya anaendelea kuchunguza kale kataasisi cha kihuni, tuendelee kufanya na hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwenzangu anapenda kusema kansa hapa. Kansa maana yake ni nini? Cell zote za mwili zinakuwa controlled na central nervous system. Maana yake cell moja iki-jump ikawa haisikiliza ubongo inakuwa inajigawanya bila kusikiliza ubongo unataka nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia Serikali ya Tanzania na Chama cha Mapinduzi kuna control system kutoka juu mpaka chini na akisema Mheshimiwa Rais basi chini tunafuata lakini CHADEMA sasa hivi wanatafutana wamekuwa kansa wenyewe, kila mmoja yuko kivyake kama cell ya kansa. Kwa hiyo, kufafanua vizuri kansa ni CHADEMA wala siyo kama yeye anavyofikiri ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namsikia Kiongozi Mkuu, namheshimu sana kaka yangu Mheshimiwa Selasini lakini naunga bajeti mkono, hebu rekebisha kansa kwenye chama chako watu wasikilize kama central nervous system. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi kusema namsikia kiongozi namheshimu sana Mheshimiwa Selasini, lakini naunga bajeti mkono hebu rekebisha kansa kwenye chama chako watu wasikilize kama sisi tulivyosikiliza. (Makofi)