Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi kwa kunipa nafasi jioni hii ili niweze kuchangia walau maneno machache kuhakikisha kwamba bajeti yetu inakuwa ni bajeti bora kama ambavyo tumeipokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nianze kwa kuwapongeza na kumshukuru Mheshimiwa Waziri na timu yake yote kwa namna ambavyo wamekuwa wakitenda kazi na wajibu wao sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba moja kwa moja nijikite kwenye suala zima la hali halisi ya viwanda. Tunafahamu kwamba Serikali yetu inayo dhamira njema ya kuhakikisha viwanda vyote vilivyoko nchini vinapata nguvu, vinawezeshwa, lakini viwanda vyote ambavyo vinategemewa kujengwa hapa nchini vijengwe kwa misingi ya kuzalisha lakini kwa misingi ya kutoa ajira na kuifanya nchi yetu kuwa nchi ya viwanda halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwanza tuna viwanda vya samaki karibia saba mpaka nane. Hivi tunavyozungumza leo ni viwanda takribani vitatu au vinne peke yake ndiyo vinafanya kazi na vyenyewe havifanyi kazi kwa ufanisi unaotakiwa. Lipo tatizo moja kubwa, mwanzo baada ya operesheni tunafahamu kabisa Serikali ilikuja na bei elekezi ya samaki kuanzia karibia shilingi 5,500 mpaka shilingi 6,000. Leo kilo moja ya samaki inauzwa shilingi 3,800. Huyu mvuvi ili akavue wale samaki sawasawa na kuwaleta anagharamikia zaidi ya lita moja ya mafuta kama unavyofahamu kwa sasa ni shilingi 2,480 hadi 2,500.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kusema kuwa Serikali imeachaniza hii sekta ya viwanda vya samaki, imewaacha wenyewe wafanyabiashara na wenye viwanda wahangaike kutafuta masoko, wahangaike kutafuta bei ambazo zinaweza kuwasaidia kwenye mafuta, wahangaike wenyewe kuona namna ambavyo wanaweza kuendesha viwanda hivi. Kiwanda kimoja peke yake kilichokuwa na uwezo wa kuajiri wafanyakazi zaidi ya 700 leo kinaajiri wafanyakazi 50 mpaka 90 kwa shift moja, kilikuwa na uwezo wa kukata tani 70, leo kinakata tani 15 peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali haitawekeza jicho huku na nimuombe sana Mheshimiwa Waziri hasa Waziri wa Uvuvi warudi nyuma waangalie kushiriki na wavuvi hao wote ili waweze kushughulikia suala hili la viwanda vya samaki, vinginevyo vitakufa, tutaendelea kupoteza ajira na wafanyabiashara ndogo ndogo sio kwamba wanapenda kuweo wengi, wanakuja kwa sababu hakuna kazi za kufanya ndiyo maana wanatafuta mitaji ya shilingi 200,000 waingie sokoni ili waweze walau kuuza bidhaa yoyote ile wajikimu na maisha yao.

Kwa hiyo, niombe sana bidhaa hii jhasa bei ya samaki lazima irudi kuwa elekezi ili wavuvi nao wanakovua kule waone umuhimu na faida ya kwenda kukesha kwenye maji na kurudi nchi kavu kufanya biashara na viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nilitaka kuzungumzia Wakala wa Barabara (TARURA). Nimekuwa nikisema siku zote kwamba mimi ni muumini mzuri wa TARURA, kwenye bajeti iliyopita tumeongeza fedha kwa ajili ya bajeti ya TARURA, inakadirika shilingi bilioni 30 baadae tena ikaongezwa karibia shilingi bilioni 60 hivi na mimi nataka kusema jambo moja; TARURA kama tutaijali, kama tutaichukulia kama chombo ambacho tumekitengeneza kwa ajili ya kuja kutoa suluhisho kinaweza kufanya kazi nzuri sana. Suluhisho tunalolizungumza hapa kwenye chombo hiki ni lazima fedha zote zilizotengwa na fedha zilizoongezwa kwenye bajeti zielekezwe TARURA ili waweze kutoa mgawanyo ambao ni sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ukichukua kwa mfano Wilaya mbalimbali zilizoko kwenye Jiji la Dar es Salaam na Wilaya zilizoko kwenye Majiji mengine kama Mwanza, leo ukichukua Kinondoni na Nyamagana ni kama vile tunalingana lakini ukija kwenye mgao Nyamagana inapata kidogo, Kinondoni inapata zaidi na hii sio sawa kwa sababu hata miji yote iliyoko pembezoni inahitaji kufunguliwa mtandao wa barabara ili tuweze kwenda sawa na mazingira tunayoyapigania sasa. Vinginevyo tutabaki kupiga kelele humu, fedha ziongezwe halafu fedha zisipokwenda hata utekelezaji wa miradi yenyewe hautafanana na kile ambacho tunakipigania kelele na tunachokiombea kila siku hapa.

Kwa hiyo mimi niombe sana, narudia; TARURA ni chombo muhimu na TARURA wameanza kuonesha njia. Kama watapewa fedha kama ambavyo tumekubaliana kwenye Bunge hili wakati wa bajeti iliyopita ya kisekta sina shaka TARURA wanaweza kufanya kazi yao vizuri na mgawanyo narudia tena, uwe sawa kulingana na mahitaji ya kwenye kila mji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili liende sambamba na ahadi zilizokuwa zimetolewa na Mheshimiwa Rais hasa kwenye maeneo haya am bayo sasa yamekabidhiwa TARURA, mimi nina barabara karibia tatu za ahadi ya Mheshimiwa Rais, niombe sana barabara ya kutoka SAUT – Luchelele; Igoma – Kishiri kutokea Buhongwa; hizi ni ahadi za Mheshimiwa Rais na barabara hizi zimerejeshwa TARURA ni lazima sasa TARURA waje na mpango wa kutuambia barabara hizi zinajengwaje na Serikali ipeleke fedha hizi ili barabara hizi zijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la umeme; tunafahamu REA haitoi huduma wala ujenzi wa miradi ya umeme kwenye majiji kwa maana majiji haya yote yana mitaa na hayana vijiji, lakini mimi nimuombe sana Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Nishati wafikirie jambo hili, tunachukua umeme tunapeleka vijijini, hatukatai, ndiyo mfumo. Leo wamekuja na umeme wa mradi wa peri-urban, huu mradi wa peri-urban kama hautakuja kutekelezwa sawasawa, miji yetu itabaki kuwa na giza ilhali watu wamejitoa na wamejenga majumba kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Kwa hiyo mimi niombe mradi wa peri-urban utakapoanza uelekezwe kwenye maeneo ambayo ni very strategic na hii ni biashara, TANESCO wanafanya biashara hapa, wanaingiza fedha. Sioni sababu unapeleka transfoma mbali kwa miaka miwili wameunganisha watu wanne badala yake tunapoteza fedha. Walete hizi transfoma mjini watu wamejenga zaidi ya kaya 15,000/20,000 kwenye kila kata ili tuweze kupata suluhisho la mambo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho tumejikita kwenye miradi mikubwa sana na sasahivi Serikali inafikiria kwenda kujenga mradi mkubwa wa kuhifadhi mafuta kwa pamoja. Tunakwenda tunafikiria tutatumia zaidi ya dola bilioni 22 lakini sisi tuna wadau, tuna PUMA na TIPER, hawa sisi tuna hisa asilimia 50 kwa kila kampuni. Lakini kama ndiyo msimamo wa Serikali, hebu tusubiri kwanza tuimarishe hii miradi mikubwa tulinayo, hiyo dola milioni 22 ukiipeleka kwenye Stiegler’s Gorge, ukiipeleka kwenye standard gauge tutakwenda mbali zaidi kuliko kufikiri kujenga matenki ya mafuta leo na huku ni ku-frustrate wadau tulionao.

Kwa nini tusikae na hawa wadau? Maana shida ya Tanzania sio kuwa na reserve ya mafuta, shida ya Tanzania tulikuwa na uhaba mafuta yanapotoka yanaletwa na nani. Sasa tumeshamaliza mfumo huo, mafuta yanaagizwa kwa pamoja, yanakuja kwa pamoja. Bado iko tatizo, hata leo ukienda bandarini pale tunajenga flow meter mpya. Hivi ile flow meter ya zamani kule Mji Mwema ina matatizo gani?

Mheshimiwa Naibu Spika, tumechunguza matatizo yake? Tumebaini matatizo yake? Haitoshi, tunafanya ujenzi mpya, tume-engage mkandarasi mshauri, hatumtumii, tunamuacha kama alivyo, leo tunafikiria kuwekeza mradi mwingine tuwatengenezee watu kichaka kipya na hii ndiyo maana tunaambiwa sisi tunaotunga sera na kuzisimamia tuanzidiwa sana maarifa na watu wanaofanya baishara hizi kule nje na hii sio sawa. Ni lazima maarifa ya watunga sera na wanaozisimamia sera yawe na weledi mkubwa kuliko hawa walioko nje ili tuweze kwenda sambamba na kazi ambayo tunaifikiria na kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema tunatamani sana miradi hii mikubwa ikamilike kwa wakati, Stiegler’s Gorge, standard gauge ikifika Mwanza wananchi wa Mwanza watakuwa na ahueni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naomba kuunga hoja mkono asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)