Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipatia nafasi kuweza kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Wizara, Mheshimiwa Dkt. Mpango, pamoja na Naibu wake kwa kuwasilisha, lakini pia watendaji wakuu kwa maana ya Katibu Mkuu - Ndugu James Doto na wengineo, kwa bajeti nzuri ambayo imeandaliwa na kupunguza baadhi ya tozo na ada mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi napenda nichangie kwenye huu ukurasa wa 81 wa hotuba ya Waziri Mheshimiwa Dkt. Mpango ambapo anazungumzia hatua za kisera na kiutawala katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ambapo hapa amependekeza kuweka utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini ambapo wananchi wa kawaida wataruhusiwa kutoa mizigo bandarini bila kuwa na ulazima wa kutumia Wakala wa Forodha kwa maana ya Clearing and Forwarding Agent. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu nizungumzie hapo kidogo na tujadili pamoja na Mheshimiwa Waziri hapa atuambie, mimi ninavyofahamu uwepo wa hizi agencies za freight clearing and forwarding, kwanza uwepo wao wapo kwa Sheria ya East African Community Customs Management Act ya mwaka 2004 as amended time to time. Lakini pia makampuni haya yanapokuwa yanafanya usajili wake, kwanza yanafanya mitihani katika Chuo cha Kodi na hawafanyi tu mitihani kwa maana huwezi kumchukua mtu yeyote akaenda kufanya mtihani wa kodi pale akafaulu.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaofanya mitihani utakuta makampuni zaidi ya 1,000 yanaomba yapate leseni ya kufanya kazi ya u-agent ya kutoa mizigo bandarini ama airport na sehemu zingine bandari kavu. Utaratibu huu wa kufanya mitihani inahitaji upate kijana aliyesomea, aliyebobea na kijana aliyesomea aliyebobea anasomea kati ya miezi nane mpaka miaka mitatu kazi ya kutoa mizigo bandarini, kazi ya kutoa mizigo katika bandari kavu, kazi ya kutoa mizigo katika viwanja vyetu vya ndege. Ni kazi iliyosomewa na yenye weledi wa hali ya juu sana, siyo kazi kwamba unaweza kuifanya mtu yeyote kirahisi kama ambavyo inaweza kuzungumzwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naweza nika-declare interest; mimi mwenyewe nimeisomea hiyo kazi, kwa maana ninaifahamu by profession. Kwa hiyo, ninapozungumza naizungumza kwa maana naielewa nje/ndani. Unapofanya registration, unapokwenda kufanya mtihani kati ya makampuni 1,000 yanayokuja kupata leseni hayazidi makampuni 100, kati ya 1,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya makampuni ambayo yanapata leseni ndiyo yanaweza kupewa leseni ya kufanya kazi hii ya kutoa mizigo bandarini. Lakini pamoja na kupewa leseni lazima waweke bond kwa maana ya kwamba chochote kikitokea aidha fraud au chochote, bonds zao zinakuwa ni security ya kulinda kazi zao au kampuni yao au kulinda upotevu wa fedha za kodi katika Serikali Kuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni haya yanaajiri vijana wasomi, ambao wamesoma. Leo ukiniambia tu kila mtu afanye as huge, utapata makanjanja wengi sana, upotevu wa kodi ya Serikali utakuwepo mkubwa sana, kwa sababu makampuni haya pamoja na kufanya kazi ya clearing agent, yanafanya kazi ya kukusanya kodi ya Serikali. Kwa hiyo, yanapokusanya yanasimama kwa niaba ya Serikali, at the same time hawalipwi na Serikali, lakini wanaisaidia Serikali kukusanya kodi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuwepo kwa ma- agents hawa tuwaboreshee mazingira yawe mazuri zaidi kwa sababu Serikali inahamasisha katika uwekezaji, inahamasisha katika kuwepo kwa viwanda, inahamasisha kuwepo kwa makampuni. Leo kampuni inaweza kuajiri na katika field hii wapo zaidi ya vijana 15,000 wameajiriwa. Leo ukisema kiholela maana yake ajira za vijana waliosoma zaidi ya 15,000 watapoteza kazi zao. Kwa hiyo, unapoteza ajira katika kazi hizo za ukusanyaji wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vipo vyuo vinavyotoa kozi za ku-clear mizigo, kwa mfano Chuo cha Kodi Dar es Salaam wanafundisha pale miezi nane lakini mpaka mwaka mmoja, mpaka miaka mitatu, wanatozwa ada, makampuni yanalipa ada za wanafunzi hao. Leo unavyosema kila mtu akajifanyie, hivi unafikiri ni kazi rahisi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza unaambiwa ukatoe mzigo wako, lazima ufanye classification ya mzigo wako, je mwananchi wa kawaida kutoka Choma cha Nkola anaweza ku-classify mzigo wake? Maana ku-classify mzigo kuna HS Codes, codes za mizigo, lipo likitabu likubwa sana, nani atafanya? Maana yake utaanza kutafuta vishoka wafanye kazi hizo kienyeji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, lazima ufanye valuation ya mzigo, valuation hawezi kufanya huyo mwananchi wa kawaida, hawezi. Lakini bado lazima ufanye documentation; nani mwananchi wa kawaida anaweza kufanya documentation. Bado uingie kwenye mfumo wa ASYCUDA ama hii system wanatumia sasa hivi ya TANCIS.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima usomee, unaingia kwenye computer unafaya log documents zinakwenda TRA wanakujibu. Leo mnataka kuturuhusu kila mtu apige simu TRA kuuliza HS Code ya mzigo wangu ni ngapi? Sasa TRA watafanya kazi ya kutoa huduma ya kutoa HS Codes badala ya mawakala wafanye hizo kazi? Hili suala namuomba Mheshmiwa Dkt. Mpango aliangalie kwa makini, lakini atambue uwepo wa mawakala hawa. Wanafanya kwa mujibu wa East African Community Customs Management Act. Kwa maana hiyo kama tunataka kila mtu ashiriki maana yake turekebishe sheria zetu za customs za Afrika Mashariki ndiyo twende pamoja. Kwa sababu suala hili halifanyiki Tanzania peke yake; uwepo wa mawakala Uganda wapo, Kenya wapo, dunia nzima wapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tutambue kwamba kazi hizi, makampuni haya yanapokuwa yanafanya yanaleta ajira. Lakini pili, makampuni yanalipa kodi kama Corporate Tax, PAYE, VAT, Withholding Tax, vyote vinaigiza katika Serikali, inakusanya mapato, leo ukiondoa hizi kodi zote utazikosa. Lakini kingine makampuni haya yana-deal na shipping line, yana-deal na ICDs, TBS, TFDA, Government Chemist; mwananchi wa kawaida ataweza kufuatilia vitu vyote hivi?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango liangalie suala hili kwa undani zaidi. Nikuombe sana tusiliendee kichwa kichwa maana yake leo utapitisha hivyo, mwaka unaokuja utakuja utarekebisha tena; tutakuwa tunakwenda mbele au tunarudi nyuma?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tutambue kwamba mizigo inapokuwa kwenye manifest ni lazima sheria za forodha zi-apply, sheria za kimataifa zi-apply, sheria za uchukuzi zinataka utumie Mawakala wa Forodha. Sasa kama mzigo ukishakuwa kwenye manifest leo umwambie mtu wa kawaida tu aka-clear mzigo wake, anau-clear vipi? Maana yake manifest, Sheria za Uchukuzi za kimataifa zinaelekeza utumie agent; sheria za uchukuzi zinaelekeza utumie agent; sheria za forodha zinaelekeza utumie agent, haiwezekani tu mtu wa kawaida. Lakini utaua makampuni, utapoteza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini utambue mfumo unaotakiwa kimataifa according to World Trade Organization, World Customs Organization wa kuondoa mizigo bandarini ni kutumia mawakala na sisi kama Tanzania tumesaini kwamba tutatumia mawakala, leo unakwenda kuondoa nguvu ya mawakala ama agents.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo changamoto za mawakala, lakini changamoto hizo tu-set down, zipo Wizara wanasema hata hawa makampuni hawajawaajiri hawa vjana wetu; tufuatilie kwa sababu sheria inaeleza kwamba makampuni hayo yaajiri. Kwa hiyo, Wizara ifuatilie kwenye makampuni hayo iangalie mikataba ya ajira ya vijana wetu ili wawe na uhakika wa soko lao. Otherwise tutazalisha vijana wanaozurura mitaani, tutazalisha vishoka mitaani, lakini tutaongeza rushwa katika TRA, tutaongeza makanjanja mitaani, kutokuwepo kwa kumbukumbu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango, leo unaweza ukaifuata kampuni yoyote kwa sababu kwa mujibu wa sheria kampuni lazima itunze kumbukumbu zake ndani ya miaka mitano. Unaweza kufuata ukamwambia hebu lete niangalie mizigo ndani ya miaka mitano mmefanya nini. Je, mtu wa kawaida utampata wapi akupe kumbukubu za ku-clear mzigo wake kwa miaka mitano, ama mnataka kuruhusu wafanyabiashara au wengine, leo atatumia jina la Seif ku-clear mzigo wake, kesho atatumia jina la Gulamali ku-clear mzigo wake, keshokutwa ataenda Juma Athumani, hutapata kumbukumbu itakuwa ni kupoteza tu. Hata ikitokea fraud utamkamata nani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Mpango, kwa hiyo nikuombe sana uliangale hili kwa mapana yake kwa maana siyo suala la kuingia kichwa kichwa. Pili, linatunza ajira za vijana wetu. Huko mitaani vijana wako wengi sana wanasoma, wame-qualify. Lakini siyo tu kuajiriwa ndani ya nchi yetu, Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango, hii ni fani unapoiua maana yake unapoteza vijana wa Kitanzania ambao wanaajiriwa, siyo kufanya kazi ndani ya Tanzania, wanafanya kazi katika dunia. Ukienda Ufaransa utakutana na watu hawa, ukienda Uingereza utakutana na watu hawa, ukienda China utakutana na watu hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo yako masomo na curriculum katika vyuo vyetu yanafundishwa masuala ya kutoa mizigo yetu bandarini. Ukiua kwa urahisi namna hii maana yake unaondoa vijana wetu katika mfumo rasmi, unakwenda kuwafanya wawe sasa katika mfumo, hata mimi ambaye namlipia ada mtoto wangu nitamwambia kwa sababu Serikali imesema mtu yeyote, kwa hiyo achana na masuala ya shule. Kwa hiyo, badala sasa ya kumuweka katika mfumo rasmi, unamuondoa kwenye mfumo rasmi unampeleka awe kanjanja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, nakuomba sana katika marejeo yako utakapokuja ninakuomba uje utoe ufafanuzi wa kina juu ya suala hili. Naomba sana Serikali tusiende katika mkanganyiko ambao tunauona huko mbeleni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. Ahsante sana, naunga mkono hoja, hotuba ya Mheshimiwa Waziri, ahsante. (Makofi)