Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Rev. Peter Simon Msigwa

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Rais akifanya mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri akimtoa aliyekuwa Waziri wa Viwanda alisema moja ya kazi aliyowapa ni kufanya biashara na sio kupeperusha bendera tu. Mheshimiwa Rais ninaamini amewateua Mawaziri kwa ajili ya kumsaidia na kumpa ushauri, ili kuweza kuhakikisha Taifa letu lina-flourish, tunasonga mbele kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema mahali hapa kwamba if you are lost, speed is useless (ukiwa unakimbia mwendokasi na umepotea, ule mwendokasi hauna maana). (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango ni miaka minne sasa hivi tunajadili kuhusu maendeleo ya nchi yetu na toka bajeti ya kwanza mfumo na mpango mzima mliokuja nao humu ndani Wabunge wengi kwa wingi wetu tulipinga namna ya uendeshaji uchumi na mipango mliyokuwa mmepanga. Na nimesema Rais anapowachagua anataka mka-add value na ndio maana alisema sikuwachagua kupeperusha bendera tu. Kwamba ninyi ni wachumi, mnazijua kanuni za uchumi, mnajua mki-violate kanuni a uchumi ita-backfire. Kodi jinsi mlivyokuwa mnakusanya tulitoa ushauri kwenye bandari hamkutusikiliza, tulitoa ushauri kwenye watalii hamkutusikiliza, tulitoa ushauri namna ya ukusanyaji kodi kwa bunduki, kwa task force hamkutusikiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa leo miaka minne mmebadilisha lugha sasa hivi mmekuwa laini as if sio ninyi. Mimi nilitaka Mheshimiwa Mpango kama mchumi, mmoja wa watu wanaoheshimika katika nchi hii, hebu tuambie ule ushauri ambao Bunge na Wabunge wengi humu ndani tulishauri kwamba hiyo njia unayokwenda sio sahihi kwa nini mlikuwa mnakataa? (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa ongea na Kiti. Ongea na Kiti.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, niliomba Waziri wa Fedha aseme kwa nini walikuwa wanakataa na walikuwa wanataka ku-achieve nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, yote tuliyozungumza sasahivi wamegeuka kwa mlango wa nyuma wanatekeleza yaleyale baada ya kulitumbukiza Taifa kwenye matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi mimi nailinganisha na timu inayocheza mpira kwenye uwanja ambao hauna magoli, mnapiga mashuti makubwa ambayo huwezi ku-major, you are going no where kwa sababu ya miradi mikubwa ambayo mmeweka... (Makofi)

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa kuna Taarifa. Mheshimiwa Julius Kalanga

T A A R I F A

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya kazi kubwa ya Bunge ni kuishauri Serikali. Bunge hili limekuwa likiishauri Serikali mambo mengi ikiwepo kuondoa VAT kwenye umeme wa Zanzibar na maeneo mengine, kwa hiyo, Serikali imechukua ushauri wa Bunge ambao ni ajnibu wake kwa hiyo, Mbunge hana sababu ya kuhoji kwa nini Serikali inatekeleza yale ambayo Bunge limeshauri ni kazi ya Bunge. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru, kumbe ili Serikali isikie inachukua miaka minne, yaani mnakuwa mmemaliza muda wa miaka minne ndio mnasikiliwa. Nachukua uchauri wako kwamba, ni kuishauri, lakini tumewashauri four years, mambo ya miaka minne ndio wanasikiliza leo na mwakani ni uchaguzi na mkataba wenu na wananchi ni miaka mitano, yani mnashauriwa miaka minne ndio mnasikiliza, thank you. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema miradi mikubwa na ukilinganisha kiukweli Waziri wa biashara amekaa karibu siku mia mbili na kitu, ametumbuliwa kwa maana ya kwamba hajamsaidia Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukiniuliza mimi watu ambao kwa weledi wao na heshima kubwa ambayo Rais aliwapa, waliotakiwa kutumbuliwa ni pamoja na Mheshimiwa Mpango na Waziri Kabudi. Kwa sababu kwa nini nasema? Nitatoa sababu kwa nini nasema hivyo? (Makofi/Kicheko)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa kuna taarifa nyingine. Mheshimiwa Amina Mollel.

T A A R I F A

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kumfahamisha Mheshimiwa Msigwa kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ana imani kubwa na Dkt. Mpango na ndio maana mpaka sasa Waziri Mpango bado yupo akitekeleza majukumu yake kama Waziri wa Fedha.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unapokea taarifa hiyo?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, wala sipotezi, ananipotezea muda tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema waliotakiwa kutumbuliwa ambao wameleta shida ya kutunigiza kwenye matatizo ni Mheshimiwa Mpango pamoja na Mheshimiwa Kabudi. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Kabudi alitoa ushauri kwenye masuala ya madini, leo kama Taifa we are stuck, yamebaki machimbo madogo madogo, machimbo makubwa ukienda Bulyankulu kume-stuck, we are not going anywhere tumekaa haturudi nyuma, hatuendi mbele, akatuambia kutakuwa na kishika uchumba, wala kishika uchumba hakionekani mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa report ya Profesa Osoro kulikuwa na ngoma na ngonjera na praise and worship kila mtu alikuwa anashangilia. Leo tunataka mtuambie what is it going on? Mheshimiwa Kabudi where is our money? Mheshimiwa Kabudi alisema haya mambo, ametuletea hasara na amemshauri Rais vibaya. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Taarifa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, mtu wa pili ambaye nasema ni Mheshimiwa Mpango…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa taarifa ya mwisho kwa Mheshimiwa Msigwa. Mheshimiwa Stanslaus Nyongo.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa tu Mheshimiwa Msemaji kwamba sekta ya madini anavyosema ime-stuck, naomba nimtaarifu tu kwamba, sekta ya madini haija-stuck, unless otherwise unazungumza kitu kingine.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya madini kwa taarifa yako ni kwamba, sasahivi imekuwa ndio iliyoongeza mchango wa Taifa. Na tumechangia zaidi, tumekusanya maduhuli zaidi ya bilioni mia tatu na kumi na kitu ambayo imetokea kwa mara ya kwanza toka tumepata uhuru wa nchi yetu. Masuala ya kishika uchumba anayoyazungumza huyu Mheshimiwa ni kwamba, hiyo commitment kweli ipo na mazungumzo yanaendelea…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA MADINI: …tuendelee kusubiri pale taarifa rasmi itakapokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwamba sekta ya madini inaendelea kukua na hata sasa hivi ni kwamba watu wanaona ni jinsi gani sekta ya madini ilivyoweza kuingiza kipato cha Taifa katika nchi yetu, asipotoshe aananchi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Msigwa unaipokea taarifa hiyo?

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Serikali imekiri kwamba, kishika uchumba bado kinajadiliwa, ndio nilichokuwa nazungumza kwamba wameendelea kwamba, kishika uchumba mpaka leo. Ndio maana nimesema Mheshimiwa Kabudi anamshauri vibaya Rais na kwa bahati mbaya amekuwa sasa kwenye masuala ya kidiplomasia ameendelea kuwa arrogant, wala haisaidii nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mpango toka umekuwa Waziri wewe Makamishna wanazidi kuondoka na wewe ndio msimamizi, there must be something wrong. Aidha, una-violate principle za uchumi wewe mwenyewe huzifanyi na watu waungwana wana-step down kama principle zile walizosoma za uchumi hazifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunasifu na kuabudu hapa kwamba uchumi unakua, economics. Economies obout the walfare of people, the well being of people, kuhusiana na uchumi wa watu, hatuwezi tukawa tunaimba mnachozungumza takwimu mnasema uchumi unakua, takwimu zenu zinakwenda hivi wananchi wanakwenda kushoto, sasa hizo ni takwimu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yani tukubaliane kwamba, wale IMF ni waongo, uchumi unakuwa kwa asilimia saba kama mnavyosema ninyi maana mtatufunga tukisema zingine. Sasa maisha ya Watanzania yakoje? Ni kwa nini maduka yanafungwa? Kwa nini watu wanashindwa kusomesha watoto shule? Kwa nini kunywa chai maeneo mengine imekuwa luxury? Wananchi huko chini wanataka waone maisha ya kawaida, mnaweza mkatangaza kwamba uchumi unakua kwa asilimia 15, that is fine, lakini kule nyumbani hayo ndio maisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri mnaotoa, purchasing power ya mwananchi wa Tanzania iko chini kwa kiwango kikubwa sana. Mheshimiwa Mpango hasara aliyoileta Mheshimiwa Kakunda, wewe na Mheshimiwa Kabudi ni kubwa zaidi kwa sababu ninyi ndio mnamshauri Rais kwa karibu kuhusiana na uchumi wa nchi hii. Yale yote tuliyosema mliyakataa miaka minne iliyopita, halafu hapa tunabaki kusifu na kuabudu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo suala la korosho; suala la korosho kwa kawaida korosho msimu ukifika wale wanunuzi wa nje huwa wanaleta makontena wakinunua korosho zinaingizwa kwenye makontena zinasafirishwa kwenda nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi zimekuwa zikisafirishwa kwenda nje kwa sababu sisi hatuna uwezo wa kutunza korosho. Watu wa nje wakinunua hizo korosho kule kwao wana ma-godown ambayo yanaweza yaka-regulate temperature. Sasa ninyi washauri wa Mheshimiwa Rais mlimshauri Rais, mkapeleka Jeshi kwenda kukusanya korosho, mkaziweka kwenye ma-godown ambayo mengine yananyeshewa na mvua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesea mwanzoni kwamba, if you are lost, speed is useless na tumepotea mnaendelea ku-accelerate, tunaenda kwenye chaka ninyi mnaendelea kuongeza mafuta, uchumi unakua, uchumi unakua, huku mnapotea njia. Tusipokuwa waangalifu hizi korosho tutavuruga hata msimu unaokuja watu wa nje watashindwa kununua korosho zetu kwa sababu taarifa nilizonazo, watanisaidia watu wenye maeneo hayo, korosho asilimia kubwa zimeanza kuharibika na zinaoza maeneo mengine na zikioza hizi korosho maana yake wateja wa nje wanakuwa na wasiwasi kuja kununua korosho kwenye nchi yetu na zinashuka thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakaribia kwenda msimu mwingine. Mimi nishauri jambo moja, aidha korosho zile ziuzwe kwa bei ya chini ili tuziondoe kwa sababu Trade World Organisation ina maswali mengi kuhusiana na korosho zetu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)