Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti yetu ya mwaka 2019/2020. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya njema ya kuweza kusimama katika Bunge hili. Nichukue fursa hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na watendaji wao ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuandaa mpango na bajeti ya mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti yetu imeangalia utekelezaji wa Chama chetu cha Mapinduzi, imengalia Mpango wa Miaka Mitano kuanzia 2016-2021 na pia umeangalia kero za wananchi na misingi ya kukuza uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niipongeze Serikali kwa kuendeleza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge, kwani ujenzi wa reli ni miongoni mwa vipaumbele katika mpango wetu wa miaka mitano, mpango wa maendeleo ambapo katika mpango wetu wa maendeleo tulisema kabisa uendelezaji wa miundombinu na ukarabati ni suala muhimu sana kwa maendeleo endelevu ya uchumi wetu. Kama tunavyofahamu reli ndiyo usafiri rahisi sana wa mizigo na hata abiria kushinda usafiri mwingine wa aina yoyote ile. Kwa hiyo sina budi kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuhakikisha kwamba hili suala la standard gauge linajengwa na linakamilika.

Pia nipongeze kwamba mchakato wa kujenga reli ya kutoka Mtwara mpaka Liganga na Mchuchuma uko katika hatua nzuri, upembuzi yakinifu umeshafanyika na nimeona katika mpango na bajeti kwamba, mchakato unaendelea vizuri. Kwa hiyo mimi naipongeza sana Serikali kwa hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naangalia katika bajeti ya upande wa pili, mapendekezo wanasema kwamba bajeti iangalie maendeleo ya watu na siyo maendeleo ya vitu. Unapozungumzia reli, unapozungumzia barabara, unapozungumzia standard gauge, yote hayo ni vitu vinavyolenga maendeleo ya watu. Huwezi kutenganisha maendeleo ya watu na vitu, utakuzaje uchumi kama usafiri wako si wa uhakika. Kama hauna umeme wa uhakika, maendeleo ya watu unayafikiaje?

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nikasema kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano kipaumbele cha kwanza kilikuwa ni kuhakikisha tunapata umeme wa uhakika. Umeme wa uhakika ndiyo utakaowezesha maendeleo ya viwanda, umeme wa uhakika ndiyo utakaohakikisha kwamba kilimo chetu kinakuwa bora na kinakuwa kwa sababu utaruhusu usindikaji wa mazao katika viwanda vyetu na ndiyo utakaoruhusu kilimo cha umwagiliaji, kusuma pump za kusukuma maji. Sasa ni lazima uwe na pa kuanzia, pa kuanzia ni kuhakikisha kwamba una miundombinu muhimu ya kuhakikisha uchumi wako unakuwa, ndipo hapo watu watakapokuja kuingia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hakuna umeme wa uhakika ina maana viwanda havitafanya kazi kwa uhakika, hakuna watu watakaowekeza kwenye viwanda na kama watu hawatawekeza kwenye viwanda ajira hizo unazitoa wapi. Kwa hiyo maendeleo ya watu na vitu vinakwenda kwa pamoja, lakini unaanza kuboresha miundombinu, kuhakikisha una umeme wa uhakika, ukiwa na umeme wa uhakika mambo mengine yatajipa yenyewe. Ajira zitakuja, maisha ya watu yataboreka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi niipongeze sana Serikali kwa kuhakikisha tunakuwa na umeme wa uhakika. Katika Mpango wa Miaka Mitano tuliridhia kwamba kipaumbele chetu namba moja ni kuhakikisha tunapata nishati ya umeme ya gharama nafuu na ya uhakika. Sasa inapatikana katika chanzo kipi nadhani hilo ni suala la watendaji na Serikali. Sio mtu umwambie wewe ni golikipa, halafu umwambie uangukie kushoto na usidakie upande wa kulia, hizo si kazi zetu. Sisi tunachopaswa ni kuridhia ile mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali kwa kuendeleza bandari zetu ikiwemo Bandari ya Dar es Salaam, Bandari ya Tanga na Bandari ya Mtwara. Kazi inayofanyika katika kuzipanua bandari zetu hizi itaifanya nchi yetu kuwa lango kuu la kibiashara ambapo tutaweza kufanya biashara na nchi ambazo hazina bandari au hazina bahari. Kwa hiyo, itakuza uchumi wetu, itapunguza gharama za usafiri na itatufanya pia kuwa kitovu cha kibiashara na tutaweka mazingira mazuri ya kibiashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali katika suala zima la kujenga na kukarabati viwanja vya ndege, tukianzia na Kiwanja cha Ndege cha Dar es Salaa, Mwanza, Tabora na Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi hizo, ningependa maeneo machache nayo nipate ufafanuzi. Nimuombe Waziri wa Uvuvi na Mifugo baadae naye aje atutolee ufafanuzi baadhi ya maeneo. Nimeangalia katika bajeti yake, nimeangalia katika hotuba ya Waziri wa Fedha, kwa kweli nimewapongeza sana eneo la mifugo au eneo la ufugaji, tozo nyingi sana zimeondoshwa, napongeza katika hilo. Lakini nilivyoangalia upande wa uvuvi, tozo zimebaki v ilevile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kusafirisha kaa nje ya nchi leseni ni dola 2,500 na zamani ilikuwa unatoa leseni moja tu 2,500 umemaliza sasa hivi kila zao unalipa dola 2,500, ukitaka kaa dola 2,500, prawns dola 2,500, lobster dola 2,500 kwa hiyo kama unasafirisha mazao manne ujiandae dola 10,000. Lakini kila kilo ya zao unaposafirisha unalipa dola moja. Kwa kweli tutafanya wafanyabiashara katika eneo hilo washindwe kusafirisha mazao ya bahari na tushindwe kuvuna mazao ya bahari. Kwa hiyo, nitaomba Mheshimiwa Waziri wa eneo hilo uje ututolee ufafanuzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nilitaka kupendekeza kwenye Serikali, niipongeze kwa kuongeza tozo kwenye mafuta ghafi kufikia asilimia 25 kwa yale ambayo bado hayajachakatwa kabisa na asilimia 35 ambayo yamechakatwa mpaka hatua ya mwisho. Mheshimiwa Waziri, mimi naona bado hiki kiwango ni kidogo, hakitoshi. Kama kweli tunataka kuendeleza viwanda vyetu vya ndani, tuwe tunaangalia na soko la dunia linaendaje. Soko la mafuta ya chakula kila mwaka limekuwa likishuka zaidi. Kwa hiyo, mazao ya mafuta ya nje ni rahisi sana ukilinganisha na gharama za huku ndani. Pamoja na kuweka hizo asilimia, muwe mnaangalia na mwenendo wa mazao haya ya mafuta katika soko la dunia ili muwe mnafanya kama tunavyofanya diesel na petrol, bei zake ziwe zinabadilika na asilimia ya ku-charge iwe inabadilika kutegemeana na bei ya zao kule nje. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mheshimiwa Waziri nipongeze kwa Serikali kuamua kuingia makubaliano na viwanda vya kuzalisha taulo za kikekwa sababu hiyo ndiyo itakuwa njia ya kuwanufaisha akina mama na sio kwa kupunguza zile kodi kwa sababu hakuna manufaa ya moja kwa moja kupitia msamaha wa kodi. Lakini kwa kuingia makubaliano, ina maana mtakubaliana mpaka bei hiyo ndiyo itawakomboa akina mama pamoja na watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)