Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza nitumie fursa hii kukushukuru sana wewe mwenyewe umeongoza kikao hiki toka asubuhi na umerudi mchana tunakushukuru sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini, naomba pia nitambue michango ambayo imetolewa na Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake - Mheshimiwa George Boniface Simbachawene, Makamu Mwenyekiti - Mheshimiwa Mashimba Ndaki, Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kuzungumza na kwa maandishi na bado tunaendelea kupokea hata maoni mengine nikiwa hapa mezani nimepokea maoni ya maandishi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge wawili.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jumla ya Wabunge 22 niliyo nao mpaka sasa wamechangia hii hoja na kati yao, waliochangia kwa maandishi sasa ni 11 na waliochangia pia kwa kuzungumza ni 11. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli nafurahi kwamba michango ni mizuri ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge wote na nitaeleza kwa muhtasari majibu ya hoja mbalimbali ambazo zimetolewa, ingawa sijui kama nitaweza kujibu hoja zote zilizosemwa kwa sababu ya muda, lakini naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba majibu ya hoja zote zilizochangiwa tutaziwasilisha kwa maandishi kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano huu wa Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nianze na baadhi ya hoja ambazo zimechangiwa na Kamati ya Bajeti, moja lilikuwa ni lile la ukiukwaji wa taratibu katika kuanzisha tozo, ada na ushuru kwa baadhi ya Wizara na Mamlaka ya Serikali za Mitaa na ambazo zimeendelea kuleta kero kwa baadhi ya wananchi, lakini pia wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, pana ukweli kiasi fulani na Wizara ya Fedha na ikijumuisha hivi karibuni tumeziandikia Wizara zote na mamlaka nyingine wahakikishe kwamba wanazingatia utaratibu uliobainishwa katika Sheria ya Bajeti. Pia kwa kawaida mwezi Desemba tunawaandikia wadau ndani na nje ya Serikali kuwasilisha mapendekezo ya tozo, ada na ushuru kabla hazijaanzishwa ili ziweze kuchambuliwa na tuweze pia kuziwianisha ili kuondoa migongano. Wizara inaitisha pia maoni ya wadau mbalimbali kuhusu hizo kodi ambazo zinapendekezwa kuanzishwa au kuzifuta ili kuondoa kero kwa wananchi. Kubwa hapa ni kwamba ndugu zangu wote Serikalini wazingatie huu utaratibu ambao ni wa kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilibaini baadhi ya taasisi ambazo zinapokea mishahara kutoka Serikali Kuu, lakini bado zinatumia utaratibu wa retention. Ushauri wa Kamati umepokelewa na kwa mujibu wa sheria zilizoanzisha hizi taasisi, Bodi za taasisi hizo zimepewa mamlaka ya kuidhinisha bajeti husika katika ngazi ya awali. Vilevile Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 na hususan kifungu kile cha 17 na kifungu cha 22 vimetoa mamlaka kwa Msajili wa Hazina na Katibu Mkuu Hazina kupitia na kuidhinisha bajeti za taasisi na mashirika hayo ambayo tumeyaona. Tutalitazama tunavyokwenda mbele tuone namna ya kuondoa upungufu huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilitupongeza tunawashukuru sana kwa jitihada ambazo tunaendelea kuhakiki na kulipa madeni ya wafanyakazi, wazabuni, watoa huduma na wakandarasi na ni kweli suala hili limekuwa ni la muda mrefu. Pamoja na kupokea ushauri wa Kamati, niseme tu kwamba Serikali inaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kulipa madeni ambayo yamehakikiwa kila mwaka. Baada ya uhakiki kukamilika taarifa ya matokeo ya uhakiki huwa inawasilishwa kwa Maafisa Masuuli ambayo inaonesha wadai ambao madeni yao yamekubaliwa na wale madai yao yamekataliwa na sababu za kukataliwa kwake.

Kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwataka Maafisa Masuuli kuwajulisha wahusika ambao walikuwa na madai lakini madai yao yalikataliwa, maana wao ndiyo wanaowafahamu. Uhakiki wa madeni ya mwaka 2017/2018 na 2018/2019 umeanza na tunatarajia kwamba itakapofika mwezi wa nane, Serikali itakuwa imemaliza na tutaanza utaratibu wa kuyahakiki kwa kila robo mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ilishauri Serikali kutenga fedha za kutosha kwa ajili ya Kitengo cha Udhibiti wa Fedha Haramu ili kiweze kufanya majukumu yake kikamilifu. Ni kweli kabisa tunatambua umuhimu wa kitengo hiki na kwenye mwaka ujao wa fedha Fungu 13 ambayo ndiyo kitengo cha udhibiti wa fedha haramu, kimetengewa jumla ya shilingi bilioni 2.01 kwa ajili ya OC na shilingi milioni
200.29 kwa ajili ya maendeleo. Tunatenga fedha hizi kwa kuzingatia kiwango cha makadirio ya mapato kwa mwaka ujao wa fedha, lakini pia vipaumbele vya kimkataba ambavyo tunavyo ikiwa ni pamoja na Deni la Taifa lakini pia mishahara ya watumishi wa umma. Kwa hiyo, kwa kuzingatia umuhimu wa kitengo hiki, tutaendelea kukitengea fedha, lakini tunafungwa tu na mapato ambayo yanaweza yakapatikana katika mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilihoji juu ya Sheria ile ya Udhibiti wa Fedha Haramu ya mwaka 2006 ambayo inataja kiwango cha juu cha fedha ambazo mtu anaweza kukibeba kama fedha taslimu kuwa ni shilingi milioni 10 tu na kwamba kwa biashara na hususan biashara ya dhahabu kwamba hiki kiasi ni kidogo sana.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Kusimamia Usafirishaji wa Fedha Taslimu ambazo zinavuka mipaka ya nchi (The Anti-Money Laundering (Cross Border Declaration of Currency and Bearer Negotiable Instruments Regulations) ya mwaka 2016 wasafiri wakiwa na fedha taslimu, sawa na dola za Marekani 10,000 au zaidi wanatakiwa kutoa taarifa kwa Maafisa Forodha.

Naomba ifahamike kuwa kanuni hizi hazimzuii mtu kubeba fedha taslimu zaidi ya kiwango kilichotajwa, lakini tunachosema ni kwamba ni lazima a-declare, lazima atoe tamko kwa Maafisa Forodha ili tuweze kudhibiti usafirishaji wa fedha haramu kupitia mipakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilionesha kwamba pamoja na kuwa Tume ya Pamoja ya Fedha imeanzishwa tangu mwaka 2003 mpaka sasa Akaunti ya Pamoja bado haijafunguliwa, japokuwa jambo hili linafanya kazi ni muhimu tuliharakishe. Naomba tu niseme kwamba tarehe 9 Februari, 2019 Mheshimiwa Makamu wa Rais aliongoza kikao hapa Mjini Dodoma na moja ya ajenda iliyojadiliwa katika kushughulikia changamoto za Muungano lilikuwa ni hili. Maelekezo ambayo sisi tulipatiwa ni kwamba tuandae Waraka mpya wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kufungua akaunti ya pamoja. Naomba kulijulisha Bunge lako tukufu kwamba utekelezaji wa maagizo hayo unafanyiwa kazi hivi sasa, kwa hiyo muda si mrefu Serikali itaweza kutoa maamuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia ilibaini kwamba kumekuwa na mifumo mingi sana ambayo inasimamiwa na Wizara yangu ikiwemo IFMS, GPG, GSSP, GAMIS na kadhalika; mifumo yote inasimamiwa na Wizara yangu, uendeshaji wake una gharama kubwa na kwamba ni muhimu sana sasa tuone namna ya kuiwianisha na kuiunganisha na hasa ile ambayo inafanya kazi moja. Pia Kamati ilitusisitiza tuharakishe mchakato wa kujenga mifumo yake na kuondokana na mifumo mingine kutoka makampuni au watu binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitengeneza mifumo kulingana na mahitaji mbalimbali ambayo hayaingiliani katika business process. Hata hivyo kupitia mradi wa PFMRP tayari Wizara imeanza kuunganisha mifumo mbalimbali ya ndani na taasisi nyingine za kifedha ili kubadilishana taarifa na kupunguza gharama za uendeshaji wa mifumo. Pia Serikali imeanza kutengeneza mifumo yake na nashukuru Kamati ya Bajeti imeliona hili, ili tuweze kupunguza gharama kubwa mno ambazo tumekuwa tukilipa wakandarasi mbalimbali. Kwa hiyo, tumetumia wataalam wetu ndani ya Serikali kutengeneza mifumo ya GPG, GSPP na GAMIS, lakini pia mfumo wa kiuhasibu. Pia kwa kutumia wataalam wetu wa ndani tunaendelea kutengeneza mifumo mingine ya nje iliyobaki ili kuondokana na utegemezi wa malipo ya leseni (subscription fee) pamoja na utegemezi wa utalaam kutoka makampuni binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia iliona kwamba pamekuwepo na mwingiliano wa majukumu baina ya baadhi ya taasisi za Serikali na hususan GPSA ambao ni Wakala wa Huduma za Ununuzi Serikalini, lakini PPRA - Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi Umma, lakini pia Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi Tanzania na Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma. Walitushauri kwamba ni vizuri majukumu ya taasisi hizi kuwa wazi na tuhakikishe zinatekeleza majukumu yake kama ambavyo zimebainishwa kwenye sheria zilizozianzisha. Kamati pia iliona zipo changamoto za wataalam wa ununuzi waliosajiliwa na Bodi ya PSPTB kwenye taasisi na mashirika ya Serikali na hivyo inakwenda kinyume na sheria na suala hilo lazima Serikali ilifanyie kazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme tu kwamba tunapokea ushauri wa Kamati na Wizara yangu kwa kushirikiana na hizo taasisi tutapitia na kuchambua majukumu ya kila mmoja ili kubaini maeneo yenye muingiliano kwa lengo la kurekebisha ili taasisi hizo ziweze kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria iliyozianzisha. Bodi kuendelea kutoa elimu kwa waajiri na waajiriwa juu ya matakwa ya Sheria ya PSPTB inayowataka kuwaajiri au kuajiriwa wataalam wa ununuzi na ugavi waliosajiliwa na hii Bodi. Lakini bodi itawachukulia hatua waajiri wanaoajiri Maafisa Ununuzi na Ugavi ambao hawajasajiliwa kwa mujibu wa Sheria Na. 23 ya PSPTB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nianze kutolea ufafanuzi baadhi ya hoja ambazo zilitolewa; kwanza Mheshimiwa Obama Ntabaliba tunazipokea pongezi zake kwa Serikali na hususan Mheshimiwa Rais, viongozi wa Wizara lakini pia Mamlaka ya Mapato na Benki Kuu ya Tanzania. (Makofi)

Suala la Ofisi ya Msajili a Hazina, Mheshimiwa Naibu Waziri ameshalitolea maamuzi. Naomba niseme kuhusu hotuba yangu niliyoitoa asubuhi imejaa hatua za udhibiti (controls) na hakuna hatua ambazo zinaleta faraja kwa wafanya biashara, naomba Mheshimiwa Obama na Bunge lako wasubiri kidogo, wavute subira hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali itasomwa alasiri ya tarehe 13 Juni, 2019 na baadhi ya haya mambo atapata majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la wale walikuwa wanaendesha maduka ya kubadilisha fedha za kigeni na wapo wachache ambao walikuta wanaendesha hiyo biashara kwa mujibu wa sheria na taratibu za lesini zao, hoja ilikuwa kwamba hawa waruhusiwe kuendelea na biashara yao. (Makofi)

Naomba nilifahamishe Bunge lako tukufu kwamba baada ya Benki Kuu kukamilisha lile zoezi kwa baadhi ya maeneo, wote waliokutwa wanafanya biashara hiyo kwa mujibu wa leseni, masharti ya leseni zao waliruhusiwa kuendelea na biashara zao. Ni wale tu ambao walikutwa wanafanya kinyume cha taratibu hizo ndiyo walifungiwa kuendelea na biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Obama pia alituambia kwamba malipo ya wastaafu yanachelewa sana na pengine tuangalie kwa macho makali kile kitengo kinahusika. Naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba hivi sasa tunaweka mfumo wa kielektroniki ambao utapunguza sana ucheleweshaji, lakini hususan shida kubwa iko kwenye kumbukumbu (records). Kwa hiyo, sisi tunaamini kwamba njia hiyo itaturahisishia na muda si mrefu suala la kuchelewesha malipo ya wastaafu litakuwa ni historia, lakini pia tunapokea ushauri, tutakitazama pia kitengo hiki kwa karibu, kwa maana ya mahitaji ya watumishi lakini pia vitendea kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Dkt. Kamala alisema vizuri sana kuhusu ukuaji wa uchumi na zile sekta ambazo zinakuwa kwa kasi. Ni kweli kabisa sekta ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Mwakyembe ndiyo inayokuwa kwa kasi zaidi kuliko nyingine kwa hivi sasa. Kwa upande wa kilimo naomba kwa kweli niwapongeze sana wakulima wa nchi hii, siyo tu wanatupatia chakula, lakini wanatupatia fedha nyingi za kigeni kupitia mazao ambayo tunauza nje. Kwa mwaka 2016 kilimo kimeendelea kutoa takribani asilimia 27.4 ya pato la Taifa, mwaka 2017 kilichangia asilimia 28.8 na mwaka 2018 kimechangia asilimia 28.2. Hata ukiangalia kwenye mauzo yetu nje kwa wastani kwa hiyo miaka mitatu kwa kila mwaka mazao ya kahawa, pamba, katani, chai, tumbaku, korosho na cloves, kwa ujumla kila mwaka zinaliletea taifa letu mapato ya takribani dola milioni 4197. Hii unaondoa fedha ambazo tunapata kutoka kwenye mauzo ya samaki na yanayotokana na samaki, lakini pia mazao ya mboga mboga na hata mazao ambayo yameongezewa thamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kutumia takwimu mpya za pato la Taifa kwa kweli tumeona, hapo zamani kilimo kilikuwa kinakuwa kwa karibu asilimia 3/3.2. Kwa takwimu mpya kilimo kimekuwa kwa asilimia 4.8 mwaka 2016, asilimia 9.2 mwaka 2017 na asilimia 5.3 mwaka 2018. Kwa hiyo kwa kweli wamefanya vizuri sana wakulima wetu wanastahili pongezi. Ukienda kwenye mchanganuo kilimo cha mazao ndiyo kinaongoza kwa kasi kubwa ambacho kimekuwa kwa wastani wa asilimia 5.0 mwaka 2018 na kinafuatiwa na mifugo ambayo nayo sekta ndogo ya mifugo nayo ilikuwa kwa asilimia 4.9, uvuvi imekuwa kwa kasi zaidi ya asilimia 9.2 mwaka 2018. Tunawapongeza sana wavuvi wetu ambao wameleta mafanikio hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mfumuko wa bei katika nchi hii unachangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumuko mdogo wa bei za chakula. Kwa hiyo Mheshimiwa Balozi Kamala alikuwa anasema ni vema nieleze mikakati ya Serikali kusaidia wakulima ambao ndiyo wanachangia kushusha mfumuko wa bei katika nchi yetu. (Makofi)

Naomba niseme tu kwa kifupi kwamba, maelezo yalitolewa wakati wa hatuba ya bajeti ya Wizara ya Kilimo lakini siyo vibaya nikarudia kwamba sisi kama Serikali tunajielekeza kuhakikisha kwamba pembejeo muhimu zinawekewa fedha kwenye bajeti ya Serikali kupitia bajeti ya Wizara husika, hizi zote zinazohusika na mazao, mifugo na uvuvi, lakini pia kwa upande wa misitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia, mkakati mwingine ni kuondoa kodi na tozo za kero. Kodi na tozo za kero kwa wakulima wetu tumekuwa tunazifuta kwa miaka yote mitatu na mimi kabisa ninaamini kwamba tutaendelea na jitihada hizi katika mwaka ujao wa fedha. Lingine ni kuwatafutia mikopo nafuu, na hii tumekuwa tunafanya kwa kuzungumza na taasisi mbalimbali ikiwemo African Development Bank lakini pia Kuwait Fund ambao tumekuwa na majadiliano nao ili watupatie fedha kwa ajili ya miradi ya umwagiliaji, lakini pia ADB kwa ajili mradi ambao utaweka kongani za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, lakini pia jitihada za kuongeza na kutafuta masoko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba kidogo nijielekeze kwenye Deni la Taifa ambalo limesemwa na watu wengi na naomba nimshukuru sana Mheshimiwa George Boniface Simbachawene kwa darasa zuri sana ambalo amelitoa kuhusu Deni la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Sika, labda nianze na hili ambalo alilisema Mheshimiwa Kamala maana yeye hakuwa na shida sana na sisi kukopa, lakini suala alikuwa na wasiwasi kwamba viashiria vya uhimilivu wa deni vimeanza kuwaka na hivyo Serikali ipunguze kasi ya kukopa. Pia alihoji kwamba tuna mkakati gani wa kuhakikisha kwamba Deni la Serikali haliendelei kukua sana kwa kuwa tunajua tutaendelea kukopa kugharamia miradi yetu mikubwa ya maendeleo, SGR, umeme Mto Rufiji na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, kwa maana ya mkakati, napenda kusisitiza kwamba mikopo ambayo inapewa kipaumbele katika kukopa ni ile yenye masharti nafuu. Ile ya kibiashara kwa kweli tunakuwa waangalifu sana, we are very very cautious na tunapokopa mikopo ya kibiashara tunaielekeza kwenye maeneo mahsusi ya kuchochea uchumi. Kwa hiyo, hatukopi tu mikopo ya kibiashara tukaipeleka popote, hapana.

Mheshimiwa Spika, la pili tumejielekeza sana kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na lengo letu ni kuwa sehemu kubwa ya bajeti iwe inagharamiwa na fedha za ndani na wakati huo huo tukifanya jitihada kupunguza matumizi ambayo yanaepukika. Lakini mkakati wa tatu ni kufanya marekebisho ya Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura ile ya 134 ili dhamana ya Serikali ambayo inatolewa itolewe tu kwa taasisi za Serikali ambazo zinajiendesha na ambazo tuna uhakika zinaweza zikarudisha deni.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine ni kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Deni la Taifa ndiyo sababu kila mwaka ni lazima tufanye uchambuzi wa uhimilivu wa deni (debt sustainability assessment) kila mwaka ndiyo maana nilitoa taarifa kwamba Desemba, 2018 tumefanya assessment hiyo na bado tunaona kwamba kwa vigezo vyote vya Kimataifa bado tuko vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine tunaendelea majadiliano na majadiliano nan chi ambazo sio wanachama wa Paris Club na lengo letu hapa ni kuona kama tunaweza tukafikia makubaliano ili nao waweze kutusamehe madeni yao kama ilivyokuwa wakati ule wa HIPC kwa nchi ambazo ni za Club ya Paris.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mikopo ya ndani, tunazingatia uwezo wa soko na pia tunazingatia liquidity katika uchumi, lakini pia tunafanya hivyo, tunapokopa tunahakikisha kwamba hatupunguzi uwezo wa taasisi m balimbali kuikopesha sekta binafsi ya ndani. Kama mnavyofahamu, tumeruhusu pia nchi za Afrika Mashariki kushiriki kwenye ununuzi wa dhamana kwenye soko letu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema vigezo vyote vya uhimilivu tuko vizuri kabisa na niseme tu kwamba kumtoa wasiwasi Mheshimiwa Dkt. Kamala na wengine ni kwamba tunapofanya ule uchambuzi wa uhimilivu wa deni tunafanya kitu tunaita debt stress test na hizi maana yake ni kwamba tunaweka zile namba zote ambazo tunakuwa tumezikusanya kwamba deni letu liko hapa hivi sasa. Je, kama ikitokea tatizo kubwa labda tumepata tatizo kubwa moja ya mazao yetu yanayotuingizia fedha za kigeni imeporomoka, kwa hiyo mwenendo wa upataji fedha za kigeni unakuwaje na mwenendo wa deni letu la Taifa utakuwaje. Kwa hiyo, tunatumia vigezo mbalimbali kujiridhisha kwamba bado tutabakia sawasawa na kwa hiyo, tunapotoa taarifa kwamba deni letu ni himilivu tunakuwa pia tumezingatia debt stress test ambazo tumekuwa tumefanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nirudie kusisitiza kukopa sio dhambi ilimradi mikopo hiyo ielekezwe kuongeza uwezo wa kuzalisha mali nchini na pia izingatie uwezo wa nchi yetu kulipa. Nadhani hicho ndicho kitu cha msingi na bahati nzuri ni kwamba Serikali imeendelea kulipa kulingana na mikataba ya madeni hayo kila yanapoiva. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda naomba nilisemee hili tena kwa Mheshimiwa mdogo wangu Zitto Kabwe ambaye alituambia usimamizi wa Deni la Taifa ni tatizo na kwamba kuna upotoshaji kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ambayo alikuwa anainukuu. Naomba niseme, tena yupo, afadhali!

Naomba niseme allegation aliyoitoa ni very serious. Mheshimiwa Zitto Kabwe allegation aliyoisema ni very serious, haiwezekani Taifa kama letu tukatunza takwimu za Deni la Serikali kwenye counter book. Hii si kweli na ni udhalilishaji wa Serikali. Kwa kweli Mheshimiwa Zitto Kabwe ulitakiwa ufute kabisa yale maneno, hayafai, sio sahihi na ninajua unafahamu kwamba hatuweki takwimu za Deni la Taifa kwenye counter book. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kutunza kumbukumbu za Deni la Taifa, Wizara ya Fedha inatumia mfumo wa kielektroniki wa kutunza kumbukumbu za Deni la Serikali ambao unajulikana kama Commonwealth Secretariat Debt Recording and Management System (CSDRMS) na mfumo huu unatumiwa na nchi za Jumuiya ya Madola na unahuishwa mara kwa mara kulingana na mahitaji. Aidha, mfumo huu kwa Tanzania ulianza kutumika toka mwaka 1996 mpaka 1997. Kwa hiyo, Mheshimiwa Zitto Kabwe hilo sio sahihi, usipotoshe umma hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, takwimu za deni letu ni sahihi, lakini pia niseme CAG hazuiliwi kufanya ukaguzi wa Deni la Taifa na wala sio mara ya kwanza amefanya, kwa hiyo, kwa mujibu wa taratibu zake alizojipangia akitaka kuhakiki Deni la Taifa atafanya hivyo. Sasa labda niseme tu inawezekana pengine pakawa na tofauti, alikuwa anasema inawezekana kabisa kwamba wale waliotukopesha wana namba tofauti na sisi hili ni jambo la kawaida, tofauti zinaweza kuja kwa sababu ya matumizi ya exchange rate, lakini inawezekana pia hata just human error katika uandishi wa zile takwimu, lakini kikubwa ni kuhakikisha kwamba ile marginal of error inakuwa ni kidogo na kwetu sisi marginal of error ndogo na inakubalika. Hata kukiwa na error baadae reconciliation inafanyika. Kwa hiyo hili sio tatizo hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba pia nitoe maelezo ya nyongeza pale alipoishia Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu ukusanyaji wa mapato ya kodi. Mheshimiwa Zitto Kabwe mimi nakumbuka wakati ule, nadhani siasa inakuchanganya kidogo siku hizi. Wakati ule ukiwa darasani kwangu nadhani ungeweza kuona kwa urahisi kabisa. Uwiano wa mapato ya kodi kwa Pato la Taifa kwa nchi yetu ni kweli umepungua kama Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema, lakini ni rahisi tu, tax effort tunachukua makusanyo ya kodi unagawanya kwa Pato la Taifa. Sasa kilichofanyika baada ya kufanya rebasing ni kwamba GDP imeongezeka kwa kasi kuliko kasi ya ongezeko la kodi na kwa hiyo ndiyo maana utaona kwamba tax effort imepungua, lakini ni kwa sababu ya mabadiliko ambayo tumefanya kwenye Pato la Taifa kwa sababu ni muhimu pia. Ni muhimu kwamba Pato la Taifa liweze kuendana na hali halisi ya uchumi. Wakati ule tulikuwa tunatumia Pato la Taifa kwa kizio cha mwaka 2007 sasa toka mwaka 2007 mpaka mwaka 2019 pametokea tofauti kubwa sana katika structure ya uchumi wetu na ndiyo maana unaona kwamba sekta anayoongoza Mheshimiwa Mwakyembe sasa imekuwa ni sekta ambayo inakua kwa kasi kuliko zote wakati hapo nyuma tu haikuwa hivbyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni rahisi tu kama denominator inaongezeka kwa kasi zaidi kuliko numerator ni hesabu za kawaida tu Mheshimiwa Zitto Kabwe unatakiwa ukumbuke tu hiyo. Lakini pia ni muhimu kuzingatia kwamba baadhi ya nchi za Afrika Mashariki bado hazijakamilisha rebasing na katika makubaliano tuliyonayo tumekubaliana kwamba tutafanya rebasing ya nchi zote za Afrika Mashariki kwa pamoja na hapo ndiyo unaweza ukafanya ulinganifu mzuri wa hiyo tax effort kwa maana ya uwiano wa mapato ya kodi na GDP.

Mheshimiwa Spika, labda niseme pia kuhusu rai ya Mheshimiwa Peter Serukamba, tunaisaidiaje Benki ya Maendeleo iweze kufanya vizuri zaidi, lakini pia benki zingine kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya uchumi katika Taifa letu. Labda tu niseme kwamba pamekuwepo changamoto za mtaji na hususan kwa benki zetu mbili zile za TIB Corporate na ile ya Maendeleo. Lakini tumekuwa tunashirikiana na benki hizi kama Wizara ili kushughulikia suala la mtaji na ukwasi ili kuweza kuleta tofauti na mafanikio yameanza kuonekana. Mikopo ya mashirika ya umma iliyokuwa hailipwi kwa ushrikiano wa karibu na Ofisi ya Msajili wa Hazina sasa mikopo hii imeanza kurejeshwa. Pia benki imefanikiwa kupata vibali stahiki kutoka kwa Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam kwa aili ya kutoa hati fungani ya kiasi cha shilingi bilioni 135 na mpango huu unatazamiwa kukamilika ndani ya mwezi Juni ambao tumeanza, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nataka tu kusema kwamba zipo jitihada za makusudi kabisa ambazo Serikali inafanya ili kuweza kuhuisha utendaji wa benki hizi.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nisemee juu ya marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani. Kama utakumbuka palikuwepo na udanganyifu ambao umekuwa ukijitokeza kwa baadhi ya wafanyabiashara wanapodai kurejeshewa kodi ambazo hawastahili na ndiyo sababu tuliamua kwamba ni lazima tufanye uhakiki wa marejesho hayo kwa kiwango cha asilimia 100 na kwa hiyo, tunahakiki nyaraka zote ambazo zinawasilishwa na mwombaji, lakini nyaraka zote pia ya yule aliyemuuzia bidhaa au huduma muombaji wa marejesho na uhakiki wa nyaraka zilizowasilishwa kwa kiwnago cha asilimia umefanyika na hatua inayoendelea sasa ni uhakiki wa nyaraka za muuzaji wa bidhaa iliyonunuliwa yaani third part verification. Tunachukua hatua hii kwa waombaji wote wa marejesho ya kodi ya ongezeko la thamani ili tujiridhishe kwamba hakuna uwezekano wa kurejesha fedha zaidi ya kiwango sahihi kinachostahili. Ili kukabiliana na changamoto ya ucheleweshaji, Serikali kupitia TRA imefanya maboresho ya mifumo yake ya usimamizi wa kodi ikiwemo EFDMS ili kuweza kutoa risiti moja moja kwa kila muamala badala ya mfumo wa zamani wa kutoa risiti kwa makundi mwisho wa siku. Mfumo huu utaweza kusomana na mifumo mingine kama i- tax ambao unatumika kuwasilisha return za VAT na hivyo kufanya uhakiki kuwa rahisi.

Mheshimiwa Spika, kiasi cha madai yaliyopokelewa ni maombi 1,854 ambayo yana thamani ya shilingi bilioni 697.2 na kati ya hayo, madai yaliyohakikiwa ni 451 ambayo yana thamani ya shilingi bilioni 22.6 na madai ambayo hayajahakikiwa ni 1292 ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 713.2. madai yaliyolipwa mpaka sasa ni 152 ambayo yana thamani ya shilingi bilioni 10.6 na madai haya ni takwimu hadi kufikia mwezi wa Aprili, 2019.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa malipo ya ile asilimia 15 kwa waingizaji wa sukari, napenda niseme tu kwamba Serikali imelifanyia kazi na hivi karibuni Serikali itatangaza kwa umma juu ya hatua stahiki ambazo zitachukuliwa kuhusiana na eneo hili.

Mheshimiwa Spika, naomba pia nitolee ufafanuzi kidogo juu ya suala la vitambulisho vya wajasiriamali. Niseme tu kwa sababu kulikuwa na allegation hapa kwamba ile tozo/ gharama ya kitambulisho kwamba haipo kisheria, sio sahihi kabisa kabisa. Suala hili ni kwa mujibu wa sheria na linaratibiwa na kutekelezwa kwa asilimia 100 na Wizara yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, labda niseme tu kwamba Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura 438 pamoja na marekebisho yake ambayo yalifanywa na Bunge hili tukufu mwaka 2017 katika kifungu cha 22(a) kilimpa mamlaka Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara wadogo na watoa huduma ambao ni washereheshaji, machinga, mama lishe, baba lishe na wengineo ambao mauzo ghafi hayazidi shilingi milioni nne.

Kwa hiyo, hili jambo liko kisheria kabisa. Wafanyabiashara wadogo na watoa huduma wanaoangukia kwenye Sekta isiyo rasmi hivyo huweka mazingira ya ushirikiano na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na TRA katika mchakato wa ugawaji wa vitambulisho, ni utaratibu wa makusanyo ya malipo ya gharama ya vitambulisho na ushirikiano huo umegawanyika katika sehemu mbili; kwanza ni kutumia mtandao mpana wa kiutawala ambao uko kule TAMISEMI katika kuwatambua wajasiriamali wadogo pamoja na kugawa hivyo vitambulisho kwenye huo mtandao. Ndiyo uliotumika kugawa hivyo vitambulisho.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa pili ni ule sasa ambao unahusu ukusanyaji wa fedha na gharama za vitambulisho na Wizara ya Fedha kupitia TRA ndiyo inafanya kazi hiyo na fedha zinazokusanywa zote zinapelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nirudie tena kwamba jambo hili liko kisheria na sheria ilipita hapa Bungeni, kwa hiyo, ni suala tu la mgawanyo wa majukumu na kama Serikali ni lazima tutumie mtandao mpana wa Serikali kule kwa wale ambao wanaweza kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

Mhesimiwa Spika, Mheshimiwa Nsanzugwanko nilishatolea maelezo juu ya suala la tax refunds.Hili la kutumia wataalam kunishauri tutalitafakari, lakini pia nikuhakikishie kabisa kwamba Serikali inafanya jitihada kuhakikisha kwamba yale mashirika ambayo Serikali inahisa kama Naibu Waziri alivyozieleza tunajitahidi ku-maximize mapato yanayotokana na taasisi hizo kwa kuzingatia uwekezaji wa Serikali na pia kwa kuzingatia kama ulivyosema umuhimu wa kulinda ajira lakini pia michango ya hayo mashirika. Tunafanya jitihada kubwa na wewe mwenyewe umeona mabadiliko makubwa katika kipindi kifupi kwamba hata sasa hata taasisi ambazo kwa miaka mingi zilikuwa hazileti chochote Serikali sasa zimeanza kuleta gawio.

Mheshimiwa Spika, rai ya kwamba TRA iwe rafiki kwa wafanyabiashara, ahsante kwa kutupongeza kwamba walau mnaona tunaanza kusikiliza, lakini ni rai yangu kwamba tutaendelea kulitilia mkazo ili TRA kweli iwe rafiki wa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ujenzi wa Ofisi ya TRA Kasulu na kule Kongwa kwa Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, nitalitazama kwa jicho la karibu tunavyokwenda mbele katika mwaka ujao wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja mbalimbali kutoka kwa Mheshimiwa Katani, labda tu niseme kwamba tulipochagua ule mradi wa kimkakati kule Mkuranga nadhani ilikuwa timing problem, lakini tutaliangalia kuhusu mradi wa kimkakati wa kujenga ghala kule Tandahimba kwa kuwa tunatambua kweli Tandahimba ni moja ya Wilaya ambazo zinazalisha korosho kwa wingi. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri ahsante, sasa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo nakushukuru tena kwa nafasi, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, naafiki.