Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. David Ernest Silinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduma

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na mimi kunipa fursa hii kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Spika, naomba nianze kwa kum-quote Makamu wa Rais wa Ghana, Dkt. Mahamudu Bawumia, anasema; “Huwezi kuendesha uchumi kwa propaganda.” Never, haijawahi kutokea, haitakuja kutokea, kwa sababu hali halisi ya maisha ya wananchi itakuumbua. Maswali madogo tu sisi mioyoni mwetu tunaridhika na namna Wizara ya Fedha inavyoendesha uchumi wa nchi hii? Mioyoni mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wabunge tukiwa tumekaa kantini, tukiwa Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kila taasisi inayokuja tumewapelekea bango kitita, taasisi zote, hakuna inayoridhika, watu wanalalamika. Tuna uwezo wa kusema propaganda kadri tunavyoweza, lakini uchumi hauendeshwi kwa propaganda, uchumi ni fact. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Fedha iliyo chini ya Mheshimiwa Dkt. Mpango. Dkt. Mpango yule wa Tume ya Mipango leo wakikutana na Mheshimiwa Dkt. Mpango wa Wizara ya Fedha leo, ni watu wawili tofauti. Hakuna mahali wana-merge, yaani huwezi kuwakutanisha, yaani yule wa Tume ya Mipango wana-differ kwenye kila kitu, ndiyo ukweli, whether mnakubali ama mnakataa, ndiyo ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo Wizara ya Fedha na Mipango, mwaka jana mimi nilizungumza hapa Bungeni, inafanya mambo ya reallocation ya fedha bila mamlaka ya Bunge. Kosa hilo hilo wamelirudia tena mwaka huu, wametengeneza revised budget zaidi ya bilioni 355, Bunge halijapitisha wala hakuna reallocation warrant kwenye vitabu vyetu. Huko wamekiuka Sheria ya Bajeti… (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Nchi.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
naomba tu nimpe taarifa mchangiaji, pamoja na hizo personal attacks kwa Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Dkt. Mpango hapa yuko kama Waziri na kanuni zinamtaka amu-address kama Waziri na siyo Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Spika, lakini nataka nimpe taarifa kwamba kifungu cha 28(2) cha Sheria ya Bajeti, Sura ya 439 kimempa Waziri wa Fedha mamlaka ya kufanya uhamisho baina ya mafungu kwa kiasi kisichopungua asilimia tisa. Hiyo bilioni 355 anayoisema ni asilimia moja tu ya hizo asilimia tisa ambazo Mheshimiwa Waziri wa Fedha amepewa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninataka nimpe taarifa Mheshimiwa Silinde, asi-take advantage ya haya yanayojiri kupotosha fulani hivi, hiki kiasi cha fedha cha hizo bilioni 355 kiko ndani ya sheria na kanuni hiyo niliyoisema ambayo inampa mamlaka Waziri wa Fedha kufanya hayo aliyoyafanya. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Silinde ni taarifa kwako hiyo, iko ndani ya uwezo wake.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Bahati mbaya Waziri hakuelewa na Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Waziri wa Fedha unajua.

Mheshimiwa Spika, hawa watu hii ni sheria, Sheria ya Bajeti iko wazi, Sheria ya Fedha iko wazi. Sisi baada ya muda wako kuisha tutakutana mahakamani kule kwa hii kazi. Wasikudanganye, utafungwa kwa mambo haya. Sheria haifi, criminal huwa haifi. Mheshimiwa Waziri hajaelewa ni bahati mbaya sana. Watu wanaokushangilia sana usiwafurahie kuliko wanaokuambia ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba mimi niendelee na hoja za msingi ambazo nilikuwa nazungumza, kwamba makosa haya ya revised budget bila kuleta kwenye Bunge mamlaka aliyonayo ya kwenye mafungu ile asilimia moja hayo yanaeleweka. Lakini tutakwenda mwisho wa siku haya, sisi tunarekodi tu, tunaweka kwenye rekodi, utawala utakavyobadilika watakuja kusema akina Mheshimiwa Silinde mlituambia na mlitushauri vizuri na utawala siyo lazima aje CHADEMA nawaambia huko huko ndani, umenielewa. Kwa hiyo, hicho ndicho tunachokisema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, Wizara ya Fedha imeshindwa kusimamia sera zake nyingi za fedha na tunapojadili hapa, tatizo la nchi hii, sera za nchi tulizonazo lazima ziendane na malengo (objectives) ambayo tumejiwekea. Sasa leo ukiangalia Sera ya Fedha, Sera ya Biashara, Sera ya Kilimo zinatofautiana kabisa when it comes to industrialization. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunajadili uchumi wa viwanda lakini nenda kaangalie Sera ya Fedha, angalia Sera ya Biashara na Kilimo yaani hivi vitu vitatu tu vinatofautiana. Sasa unajiuliza unafikiaje malengo ya uchumi wa viwanda ambao tunauhubiri humu ndani wakati sera zenyewe zinatofautiana.

Mheshimiwa Spika, Serikali ikaja na blueprint, mkaleta opinion hapa kwamba twende na blueprint; leo kila unayemuita sasa twendeni tukatekeleze hakuna hata mmoja ambaye yuko tayari. Kuna mikanganyiko kibao mule ndani.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Silinde, taarifa, Mheshimiwa Angellah Kairuki nimekuona.

T A A R I F A

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, nimuombe tu Mheshimiwa Silinde aache kupotosha. Tayari tumeshatoa taarifa, mpango kazi wa blueprint uko tayari na kuanzia Julai mwaka huu utekelezaji unaanza na hakuna anayepinga hilo na hata sekta binafsi yenyewe, bahati nzuri tarehe 28 Mei, nilikuwa nao, wanasubiri kwa hamu utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini si hilo tu, yako maeneo ambayo tayari utekelezaji umeanza. Ukiangalia katika kufuta tozo mbalimbali za OSHA, zaidi ya tozo tano; ukiangalia katika Wizara ya Madini katika uzalishaji wa chumvi zaidi ya tozo tisa zimefutwa. Lakini pia Wizara ya Afya kupitia TFDA, TBS, kwenye Bodi ya Nyama na Maziwa na bodi nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuombe sana kwa kweli Mheshimiwa Silinde asitumie hadhara hii kuweza kufanya upotoshaji huo na niwahakikishie wananchi na wafanyabiashara wawe macho, Serikali inatambua kwamba wao ndiyo engine ya ukuaji wa uchumi, tuko pamoja nao, tunawathamini, tutawalea na kuhakikisha kwamba wanafanikiwa na hata Mheshimiwa Rais muda si mrefu anakutana nao kuhakikisha kwamba mambo yao yanakwenda vizuri. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Silinde taarifa hiyo ipokee.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, uzuri hawa watu ukipiga kwenye fact huwa lazima wajitokeze. Mimi napokea taarifa yake, naipokea kwa sababu ndicho ninachokizungumza. Hii taarifa ya blueprint tangu mwaka 2016, leo nasema hata Bunge halijui ndiyo taarifa inatolewa humu ndani kwa kushtukiza. Hii biashara ya kushtukiza kila kitu itaendelea mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mimi nasema naipokea, lakini bado ukiona vitu anavyovitaja ni vitu petty, yaani vitu vidogo vidogo. Kuna haja na ndiyo maana moja ya proposal yangu kwenye mchango wangu kabla huyu haja interfere nilitaka nikuombe uunde Kamati Maalum itakayopitia ile blueprint kuishinikiza Serikali ianze utekelezaji wake kwa sababu mambo mengi yanakwama, ndilo jambo ambalo nilikuwa nauliza.

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana kuna vitu hapa tunaweza tukaulizana maswali, nchi hii kwenye masuala ya sera kuna swali tumewahi kujiuliza siku moja, hivi leo kwa mfano Wizara ya Kilimo isingekuepo watu wasingekuwa wanalima humu ndani, hii nchi watu wasingekuwa wanalima? Au Wizara ya Viwanda na Biashara isingekuepo watu wasingefanya biashara? Wangefanya. Sijui kama umenielewa.

Mheshimiwa Spika, lakini sasa angalia hawa wataalam walikokaa kule, ndiyo wanatumika kama kuvuruga utaratibu. Sasa ukipitia, hii nilikuwa najaribu kuiunganisha kwa sababu sera yetu ya sasa ni sera ya uchumi wa viwanda. Sasa hivi vitu vitatu vikubwa nilikuwa naona ni vitu ambavyo lazima ilikuwa tuvi-merge ili kuhakikisha tunaisaidia.

Mheshimiwa Spika, kwenye Kamati ya Bajeti amekuja Waziri wa Viwanda na Biashara wanalalamikia kuhusu mtiririko wa makodi, amekuja Waziri wa Fedha na wenyewe wanawalalamikia watu wa upande mwingine. Kwa hiyo, imekuwa ni lawama juu ya lawama ya kila moja wao. Kwa hiyo, hilo nikasema ni bora kulisema.

Mheshimiwa Spika, lakini cash economy is very expensive na Mheshimiwa Dkt. Mpango anajua. Wakati Dkt. Mpango anaanza kuwa Waziri alisema bajeti yetu ni kasungura, sasa hivi amebadilisha kutamka yeye mwenyewe sasa hivi anatamka kwamba unajua uchumi wetu sasa ni kasimbilisi, kwamba makusanyo ya fedha ni madogo. Sasa tunapoiambia Wizara ya Fedha irekebishe, iongeze uzalishaji maana yake tunataka kodi, wigo wa kodi uongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na ndiyo maana lengo letu lilikuwa ni nini, Wizara ya Fedha ni lazima i-promote, iweke incentives kwenye private sector ili kuongeza uzalishaji na wigo wa kodi. Lakini Wizara ya Fedha inajikita kwenye kodi peke yake, yaani yenyewe inafikiri kwamba kodi baada ya kodi ndiyo suluhisho.

Mheshimiwa Spika, kuna maswali ya kujiuliza hapa, swali namba moja, kwa mfano hivi kupunguza kodi ndiyo suluhu ya kupata kodi nyingi? Jibu linaweza kuwa ndiyo au hapana. Kwa sababu gani, moja, unaweza kuangalia efficiency, kama kukiwa na efficiency nzuri mtakusanya kodi, lakini efficiency ikiwa mbovu kodi itakuwa hakuna.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, uchumi unakwendaje? Kama uchumi ni mbovu hiyo kodi haiwezi kupatikana, mtahangaika haitakusanywa mahali popote. Ni masuala ambayo tunapaswa tuangalie. Jambo la tatu, compliance, mazingira ya kibiashara. Wakati mwingine wafanyabiashara hawataki wapunguziwe hata kodi, ni bureaucracy iliyokuwepo mle ndani, kuna kanuni zinakwenda contrary na sheria ambazo tumepitisha ndani ya Bunge.

Mheshimiwa Spika, sasa haya yote ndiyo kazi yetu sisi kuishauri Wizara ya Fedha iyafanyie kazi ili ku-rescue uchumi wa nchi. Lakini hapa watu wanataka kusikia zile lugha za kupendeza tu, jamani reli imepata, Stiegler’s imekwenda hivi, sijui nini; hizo lugha hazisaidii, tunaangalia mapungufu ili yarekebishwe, nchi iende mbele na hiyo ndiyo kazi yetu kubwa ambayo tunaifanya humu ndani. Sasa bahati mbaya binadamu huwa hapendi kusikia maneno mabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mwalimu Nyerere wakati anaondoka madarakani…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Silinde.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)