Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. SEIF KHAMIS SAID GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. Kwanza napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa kumpa nafasi hii Waziri dada yetu, Mheshimiwa Dkt. Ndalichako. Mheshimiwa Ndalichako una historia ndefu sana katika Wizara hii ya Elimu. Tunaamini toka hapo kabla hujapata nafasi hii ulikuwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Elimu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, Mheshimiwa Waziri, sisi kazi yetu kama Wabunge ndani yetu, umoja wetu, ikiwa Wabunge wa Upinzani au Wabunge wa CCM, kwa ujumla wetu, kazi yetu ni kukusaidia wewe Mheshimiwa Waziri. Siyo kukubebesha mizigo ya lawama ambayo haina sababu za msingi. Sisi kazi yetu ni kukusaidia kujua namna gani utaweza kwenda kwenye mfumo wako, kuurekebisha au kuboresha ili watoto wetu wapate elimu bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kumsaidia Mheshimiwa Waziri. Sehemu moja viko vitabu vinavyotolewa shuleni na baadhi wamezungumza wenzangu, unakuta shule „X‟ inatumia kitabu fulani na shule „B‟ inatumia kitabu fulani; vitabu hivi ni tofauti lakini somo ni moja. Halafu wanakwenda kufanya mtihani mmoja ambao unatofautiana mafunzo ya vitabu vyenyewe. Nakuomba Mheshimiwa Waziri ukaliangalie hili tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwe kitabu kimoja nchi nzima, kama Darasa la Kwanza, kitabu cha Kiswahili cha mwandishi fulani, basi nchi nzima kiwe na mfanano wa syllabus zote iwe mfumo mmoja. Isiwe huku syllabus tofauti huku syllabus tofauti, tukienda kwenye mtihani, watoto hawa wanaenda kukutana na paper ambazo hawajawahi kukutana nazo katika kufundishwa kwao. Kwa hiyo, naomba Wizara iangalie hili, wataalamu wanatusikia, wakalifanyie kazi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, linguine, kuna tatizo la ufujaji wa mitihani. Kuna kipindi fulani ikifika mitihani ya Kidato cha Nne, Form Six unasikia mitihani imevuja na kunakovuja mitihani huku kunaathiri sana watoto wote wa nchi nzima waliofanya mitihani. Wako wenye dhamira njema na wale ambao dhamira yao siyo njema. Wanaovujisha mitihani ni Watumishi ambao wanafanya kazi ndani ya Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilipata kufanya mtihani wa Form Four 2004, mtihani ulivuja. Ulipovuja, wakati wengine hatukupata hata hiyo paper, tulipoenda kwenye mtihani unakutana na paper wanakwambia mikoa mingine ambayo wamepata maendeleo paper ile tayari wanayo. Wakaenda kufanya mtihani wakapata marks za juu, kuna watoto ambao wanaenda kufanya hata paper hawakuwahi kuiona, lakini Wizara ama wataalamu wanao-standardize matokeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ku-standardize matokeo mnapelekea kuwaumiza watoto wengine ambao hawakuweza kupata hata huo mtihani. Hamwangalii nguvu kazi iliyotumika kwa watoto ambao wametoka katika mazingira magumu hasa ya vijijini. Watoto wa Mjini wanapata paper, wanajua jinsi gani wanavyozipata katika Wizara. Mwangalie hao watumsihi ambao sio wema, siyo kuwapa maonyo, ni kuwafukuza kazi na ikiwezekana wachukuliwe hatua za kisheria za kufukuzwa kazi na kuwekwa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo la Walimu. Napenda kuzungumzia Walimu. Walimu wanagawanyika katika maeneo mbalimbali katika nchi yetu. Yako mazingira mazuri ya Walimu wanayofanyia kazi, lakini yako mazingira ambayo siyo mazuri ambayo Walimu wanafanya kazi. Kwa mfano, katika Wilaya yetu ya Igunga Jimbo letu la Manonga, eneo kubwa ni vijijini. Walimu hawa wanakuja kule vijijini lakini allowance zozote zile, promotions za kuwafanya waishi mazingira yale, hawapewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iangalie hao Walimu wanaokwenda kufudisha katika maeneo hatarishi, maeneo ambayo siyo rafiki kwao, muwape promotion ya kiwango fulani ya fedha ambazo zitaweza kuwashawishi kuweza kumudu kuishi katika mazingira haya. Haiwezekani mshahara na posho ufanane kwa kila kitu. Mwalimu anayefundisha Chomachankola na Mwalimu wa Shule ya Msingi anayefundisha Temeke au Kinondoni. Haiwezekani! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ni lazima mliangalie na mlitilie nguvu kuhakikisha kwamba hili tatizo mnalitatua haraka ili ku-promote hata Waalimu wanaofundisha Kinondoni wawe wana hamu sasa ya kuja kufundisha Choma, Simbo na maeneo mengineyo ya vijijini. Hii itaweza kurahisisha upatikanaji wa Walimu na kuondoa hii kero ya Walimu; kila wakifika Kijijini wanakaa muda wa mwezi mmoja, wanaomba uhamisho. Anakwambia mama yake mgonjwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)