Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Joram Ismael Hongoli

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Dkt. Merdad Kalemani, Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Nishati kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kutumikia Watanzania kwa kuhakikisha kaya zote nchini zinapata umeme. Mungu awabariki sana. Pia nawapongeza Watendaji wote wa Wizara kuanzia Katibu Mkuu, Dkt. Khamis Mwinyimvua, Wakurugenzi na Mameneja wote wa Mikoa.

Mheshimiwa Spika, sekta ya umeme au nishati ni muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda nchini. Ukuaji wa sekta ya viwanda unategemea sana uwepo wa nishati ya umeme wa kutosha na wa bei nafuu. Nchi kama Marekani, China, Japan na South Korea zimepiga hatua katika maendeleo ya viwanda ni kutokana na uwepo wa vyanzo vingi vya umeme.

Mheshimiwa Spika, kasi ya usambazaji wa umeme kwa baadhi ya maeneo ni nzuri lakini kuna maeneo kasi ya usambazaji ni ndogo sana. Mfano, katika Jimbo la Lupembe speed ya Mkandarasi wa REA ni ndogo sana. Tuna vijiji 22 havina umeme lakini tangu mwaka jana 2018, Mkandarasi ameanza kusambaza umeme katika vijiji viwili tu na kila kijiji amesambaza kwenye mtaa mmoja tu katika Vijiji vya Ihang’ana na Iyembele. Pia amepeleka nguzo katika Kijiji cha Ninga tangu mwezi Januari lakini mpaka sasa kazi haijaanza.

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Lupembe kuna wakulima wengi wa mazao ya chai, matunda, miti ya mbao, mahindi na parachichi. Mazao haya yanahitaji viwanda vya kuongeza thamani lakini tatizo limekuwa umeme. Mfano, wakulima wamenunua kiwanda cha sembe katika Kijiji cha Ninga tangu 2016, lakini hakijaanza kufanya kazi kutokana na kukosekana kwa umeme. Pia wakulima wa nanasi wa Kijiji cha Madeke wana kiwanda cha kuchakata nanasi, lakini kiwanda hakifanyi kazi kutokana na kukosekana kwa umeme. Hivyo ni muhimu kuangalia uwezo wa hawa Wakandarasi kwani wanakwamisha juhudi zote za Waziri na Naibu Waziri za kuwaletea maendeleo wakulima kupitia huduma ya umeme.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto kwenye maeneo ya viwanda umeme unapokuwa umekatika kutokana na kuungua kwa transformer. Wawekezaji wamekuwa wakiambiwa wanunue transformer wenyewe na wajiunganishie, hii imekuwa ikiwaathiri wakulima. Mfano, Jimboni kwangu Lupembe tuna viwanda viwili vya chai na kutokana na eneo la Lupembe kuwa na mvua nyingi zinazoambatana na radi hupatwa na tatizo la kuungua kwa transformer na kiwanda kutoendelea kufanya kazi mpaka transformer ipatikane, wakati mwingine huchukua wiki mbili mpaka tatu.

Mheshimiwa Spika, hii imekuwa ikiathiri wakulima wa chai na kupoteza uchumi wa wakulima hawa, hivyo nashauri Wizara kwenye maeneo ya viwanda tuwe na transformer za ziada au za akiba ili pindi kunapotokea kuungua kwa transformer kufanyike replacement mapema ili kuokoa uchumi wa wakulima hawa. TANESCO wapeleke transformer na wafunge kuliko kuwaachia wawekezaji wajitafutie transformer zao wenyewe.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze Wizara kwa kutoa offer ya punguzo la bei ya kuunganishiwa umeme kwa bei ya shilingi 27,000 kwa REA na TANESCO, hili litaharakisha usambazaji wa umeme vijijini. Nashauri Mheshimiwa Waziri awaagize Mameneja wote wa TANESCO kwa kutoa waraka maalum na Wabunge wapate nakala yake. Hii ni kutokana na kwamba bado wananchi kwa baadhi ya maeneo wanakataliwa kulipia, wanaambiwa kulipia mpaka kuwepo na nguzo ya kuingizia umeme kwenye nyumba yake kumbe wangelipia hizi fedha zingesaidia kununua waya, nguzo na vifaa vingine, lakini pia wananchi wengi wakipata umeme wananchi watalipia bili za umeme na shirika litaongeza makusanyo ya fedha.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Umeme wa Makaa ya Mawe wa Mchuchuma; mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya viwanda nchini. Mradi wa Mchuchuma ukianza utatusaidia kupata umeme wa bei nafuu na wa kutosha, lakini kupitia mradi huu tutapunguza makatizo ya umeme yanayotokea wakati wa kiangazi au mvua inapopungua na shughuli za uzalishaji zitaendelea vizuri kwa kuwa kutakuwa na umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Spika, scope ya miradi ya umeme kwa baadhi ya maeneo ni ndogo sana. Wakandarasi wamekuwa wakieleza kwamba usambazaji wa umeme unategemea scope waliyopewa. Kuna vijiji ni vikubwa sana mfano, katika Jimbo la Lupembe, scope ikiwa ni kilometa mbili maana yake itatosha kitongoji kimoja tu na hivyo eneo au kitongoji kilichokosa umeme kuanza kulalamika kwa kutopata umeme hivyo ni muhimu kuangalia na aina ya kijiji chenyewe ili angalau kuwapa umeme wananchi wote waliopo kwenye kijiji hicho. Hii itasaidia kuondoa lawama na manung’uniko kwa sisi viongozi wa kuchaguliwa.

Mheshimiwa Spika, mwisho, narudia kuwapongeza sana Waziri na Naibu Waziri kwa kujituma kwao katika kuhakikisha kila kaya inapata umeme. Wanafanya kazi kwa kujituma kama vile ni kazi zao binafsi, kwa kweli wamekuwa mfano mzuri wa kuigwa na Wizara nyingine. Mungu awabariki sana.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.