Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Richard Phillip Mbogo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kupongeza Serikali, nipongeze Wizara na watendaji kiujumla na taasisi zote zilizoko chini ya Wizara hii ya Nishati kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya, na Waziri na Naibu wake wanazunguka sana katika Nchi yetu hii ya Tanzania kuhakikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi unaenda vyema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaenda kwenye hoja zangu za jimboni, naomba kidogo kuna masuala niweke sawa. Nianze na alipoishia kaka yangu, Mheshimiwa Simbachawene, kuhusiana na rafiki yangu Mheshimiwa Silinde; katika mchango wake amezungumzia gharama za umeme hususan kwenye gesi pamoja na matumizi ya bomba, linatumika kwa asilimia 6 pamoja na gharama za kutanua Mradi wa Kinyerezi.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba Bunge litambue kwamba kuna wengine wanajua bomba lililopo ni moja tu ambalo linasafirisha gesi kutoka Mtwara, hapana, yapo mabomba mawili. Kwanza tuna bomba dogo na Serikali iliona kwamba hili bomba ni dogo ndiyo maana tulivyokuja kuongeza bomba lingine ikawa ni kwamba limetengenezwa bomba kubwa ili kuweza kuchukua ujazo mkubwa kutokana na ambavyo uwekezaji utakuwa unafanyika.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kutumika kwa asilimia sita tuna-save future investment kama tungekuwa labda tayari tuna bomba lingine ambalo ni dogo. Na pindi kwamba uzalishaji na visima vingine vya gesi vitaongezwa basi tayari tutakuwa na means ambayo ipo inayotosheleza kusafirisha hiyo gesi.

Mheshimiwa Spika, na uwekezaji ambao unafanyika wa kuongeza hapo Kinyerezi hizo bilioni 60 ambazo amezisema ikiwa ni moja wapo ni kuendana na Sera ya Nishati katika kuwa na energy mix kama ambavyo wengine wameweza kuchangia. Na kimsingi, masuala ya ku-quantify investment cost, kwamba unalinganisha mpaka zinafika trilioni sita, ni masuala ya kitaalam na wataalam wamekwishakaa wakaangalia kwamba uwekezaji wa kwenye Rufiji Hydropower wa more than six trillion ni kwamba utakuwa na manufaa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, na manufaa hayo, kwanza umeme wa maji ndiyo umeme ambao ni wa gharama nafuu sana duniani kote. Uniti moja gharama yake ni shilingi 36 wakati umeme unaotokana na gesi ni shilingi 547. Angalia tofauti ya zaidi ya shilingi 500 kama na 11...

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. RICHARD P. MBOGO: …sasa kama tuna-save…

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Mbogo; Mheshimiwa Silinde.

T A A R I F A

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa kutokana na kwamba anakwenda kwenye ule mchango ambao nilichangia. Na wakati nachangia nilisema tunachotaka sisi ni kufikiri kibiashara, na mantiki yangu ni nini; nilikuwa nachukua kwamba think beyond the box, kwamba ukichukua 1.4 trillion ukaenda uka-expand Kinyerezi leo hii ndani ya miezi sita utapata megawati 4,440, ndani ya miezi sita. Hii 1.4 trillion haileti ile megawati 2,000 leo wala kesho.

Mheshimiwa Spika, sasa nikasema leo ukipata six trillion ukaingiza ukafanya expansion utapata megawati 18,500 ambazo umeme wake tutazalisha nchi mbalimbali, tukiuza kule nikasema ndiyo tunakwenda kuweza kwenye Stiegler’s Gorge. Sasa hii ni sawa na mtu ana nyumba pagala halafu ana kiwanja amepata milioni 10 anafukuzwa na mwenye nyumba, unaambiwa sasa nenda kamalizie pagala lako…

SPIKA: Ahsante, dakika yako imeisha.

MHE. DAVID E. SILINDE: …haya, ahsante, ameelewa lakini.

SPIKA: Utazipata hizo kwa gesi ipi wakati inayokuja ni 6% only? Endelea Mheshimiwa Mbogo.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ninaomba ulinde muda wangu. Nafikiri akafanye cost benefit analysis tena kuangalia uwekezaji kwenye Hydropower kwa miaka ijayo na lifespan ya gesi ni by 2047 inakuwa haipo.

Mheshimiwa Spika, suala la kutumia umeme wa maji pia ni suala la msingi kwa uchumi wa nchi yetu. Hii Rufiji Hydropower itakuwa na faida mojawapo, itapunguza gharama, kwa hiyo Watanzania zaidi ya milioni 50 watafaidika na unafuu wa gharama kwa sababu watatumia umeme ambao una bei nafuu. Production cost kwenye viwanda zitapungua upande wa utility kwa sababu umeme utakuwa una bei nafuu. Kwa hiyo, ile economic benefit itakuwa kwenye sekta karibu zote, mpaka kwenye kilimo, kwenye sekta zote economic benefit ya umeme wa bei nafuu itakuwepo.

Mheshimiwa Spika, jana wakati inawasilishwa hii taarifa ya Kambi Rasmi ya Upinzani, walizungumzia kwamba ujenzi wa hii Rufiji Hydropower, kwamba utaongezeka kwa asilimia 30 na msemaji akasema itafikia bilioni 9 US Dollars, takribani trilioni 22. Lakini ukichukua kimahesabu ongezeko la asilimia 30 toka kwenye bilioni 3.7 unafika bilioni 4.8 – sijui hesabu zake alizifanyaje – na tunajua katika ujenzi siku zote variation huwa zinakuwa ni ndogo sana. Kwa hiyo, nafikiri sentensi zingine za gharama zinakuwa zinapotosha Umma, kwamba huu mradi utakuwa ni wa gharama sana. Ingekuwa ni vyema sasa na Waziri uje uwaeleze vizuri gharama za mradi zitakuaje.

Mheshimiwa Spika, ilizungumziwa kuhusu matumizi ya fedha nje ya ukomo wa bajeti. Naomba niwakumbushe; Sheria ya Bajeti kuna kifungu kinaruhusu kutumia nje ya ukomo ambao tumeidhinisha na taarifa inaletwa Bungeni. Na tena kuna asilimia, ikiwa inafika asilimia 9 ndiyo iko chini ya idhini ya Waziri.

Mheshimiwa Spika, pia katika ile taarifa waliitisha mikataba kwamba iletwe Bungeni, lakini naomba nikumbushe; uliunda Kamati Maalum ya kwako ya kuchunguza Serikali itafaidika vipi na gesi asilia na ilitoa mapendekezo, mojawapo pia ni kupitia mikataba yote. Kwa hiyo, kazi uliifanya kabla hata wao wanaokuja sasa kuiagiza Serikali kwamba ifanye.

Mheshimiwa Spika, niseme tu Sheria ya Uchimbaji Gesi, gharama ya gesi ni kubwa sana na Serikali tumejitoa kwenye ile gharama. Kwa sababu ukichimba na usipopata inakuwa ni hasara kwa aliyechimba, na nakumbuka katika hili Bunge lako Tukufu, Mheshimiwa Zitto Kabwe aliwahi kuisifu sana Serikali kwa kuweka utaratibu huu katika Sheria ya Uchimbaji wa Gesi. Kwa hiyo, niombe tu kwamba Serikali inafanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, na kuhusiana na mazingira, kwamba Stiegler’s inakwenda kuharibu mazingira yote; hapana. Angalia, tumejenga miundombinu mingi katika nchi yetu; barabara, reli, tulikata miti. Wangetoa ushauri kwamba hebu tutengeneze uoto maeneo mengine kama hii Dodoma pamoja na Singida.

Mheshimiwa Spika, la mwisho, niombe sasa Serikali kwenye suala la mafuta tuangalie namna gani Kampuni ile ya TIPER jinsi gani ambavyo sasa itakwenda kuhusishwa katika kutunza mafuta ili tu-control kodi inayotokana na mafuta na tuweze ku-control uhitaji wa mafuta katika nchi yetu. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)