Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Nishati. Kwanza nipende kusema kwamba naunga mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani. Pia nitaanzia pale Mheshimiwa Mwijage alipoachia alipojaribu kulinganisha barabara na bomba la gesi hili ya kutoka Songas na kuja Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba kwanza ukiangalia mradi wowote unaotakiwa kuanzishwa lazima uangalie cost effectiveness yake. Kwa maana yake lazima unaangalia return to capital, sasa anachotaka kututumainisha Mheshimiwa Mwijage ni kwamba haijalishi kama mtambo huu wa gesi unazalisha full capacity ama unazalisha under capacity.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa gesi kutokana na ripoti ya CAG ambayo imetoka Machi, 2018, unakuta kwamba matumizi ya mtambo huu ni asilimia 24 tu ukilinganisha na installed capacity. Kwa maana yake ni kwamba kwa asilimia 76 matambo huu una-run under capacity, maana yake ni nini, maana yake ni kwamba huu mtambo unaleta hasara maana TPDC lazima iendelee ku- service mradi ule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ukiangalia kama TPDC itandelea ku-service mtambo ambao hauzalishi maana yake nini, hapo hapo unganisha na TANESCO. TANESCO wanashindwa kulipa ankara za TPDC ambayo TPDC inaiuzia TANESCO gesi asilia kwa kuzalisha umeme wa Kinyerezi, Ubongo II, Symbion Power Plus. Ni wazi kwamba TPDC itashindwa kulipa mkopo wa Exim Bank ya China. Tumejua madhara ambayo wenzetu walioshindwa kulipa mikopo hii imekuwa ni nini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia mkataba ule Kifungu Na.2 ni wazi kwamba TPDC watakaposhindwa kulipa mkopo ule, Exim Bank ya China itachukua huu mradi na ui- run na ukijua kwamba wenzetu wa China wana fedha za kumwaga ni kwamba wataufanya u-run kwenye full capacity, gesi yetu yote itakuwa inachukuliwa kwa Wachina na sisi tutakuwa tunabaki tukishangaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kusema tu kwamba, TANESCO wanajitahidi sana, lakini pamoja na jitihada hizo wanakumbwa na matatizo mawili. Kwanza TANESCO wanakuwa controlled na EWURA, EWURA ndiyo wanaopanga bei. Waheshimiwa Wabunge, wewe angalia una product yako unauza, lakini ni mtu mwingine anakupangia bei unategemea hiyo biashara iende kwa namna gani. Kwa mfano, TANESCO wananunua umeme kwa shilingi 544.65 kwa unit na kuuza kwa shilingi 279.35, haihitaji kwenda Chuo Kikuu kuchukua economics kujua kwamba kwa njia hii tunaiua TANESCO. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili Mashirika ya Umma hawalipi madeni kwa TANESCO, TANESCO inadai fedha nyingi sana kwa mashirika mbalimbali ya umma. Pamoja na Mheshimiwa Rais kusema kwamba wakatie


umeme yale mashirika ambayo hayalipi umeme, napenda nikuulize wewe ambaye unailaumu TANESCO. Kama ingekuwa wewe uambiwe ukatie umeme Muhimbili, kwa ubinadamu ungeweza kuikatia Muhimbili umeme? Kama huwezi ina maana gani, kwa nini Serikali isichukue jukumu la kulipia mashirika yale ambayo wanajua hayatengenezi faida na hayawezi kulipia umeme. Ni wazi kwamba Shirika la TANESCO, kama halitaweza kusaidiwa na Serikali ni wazi kwamba litakufa katika muda mfupi ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kusema pamoja na Waziri amesema kwamba TANESCO hawahitaji ruzuku, lakini tujue kwamba kama Mashirika ya Umma hayalipi na sina hakika kama Wizara yenyewe ya Nishati wameshalipa deni lake kwa TANESCO. Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kuipa ruzuku au kulipia yale mashirika ambayo yameshindwa kulipa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye REA namba tatu, kwanza niseme namshukuru Waziri amefanya jitihada sana kumpigia Meneja kwenye Jimbo langu kwamba waweke umeme kwenye vile vijiji alivyoahidi. Tulifanya ufunguzi wa mbwembwe wa Mkoa wa Kilimanjaro pale Mwanga, lakini unakuta sasa hivi kinachotokea REA wanapeleka nguzo wanaweka hapa halafu wanatoweka. Sasa wananchi wanaona hiki ni kiini macho au maana yake ni nini? Pia nipende kuuliza, kule kwangu Jimbo la Same Mashariki kuna mito mikubwa ambayo ina maporomoko ambayo tungeweza kutumia maji kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati yangu ya PAC ilipotembelea Arusha Technical College tuliona wanafunzi wale wanavyojaribu kuzalisha umeme lakini kwa kutumia laboratory na kutumia ndoo za maji. Kwa nini Serikali isisaidie vyuo kama hivi vikaenda kufanya majaribio au practical kwenye mito kama hii ambayo ina maporomoko na kwa ajili hiyo nisingemsumbua Waziri kwamba vijiji vyangu na vitongoji vyangu havina umeme. Kwa hiyo naomba kwanza akija kuhitimisha anieleze kwamba mpaka sasa hivi ule mkopo Exim Bank wa China umelipwa kwa asilimia ngapi. Pili, napenda anieleze kwamba kama hawataweza kushinikiza mashirika ya umma yakalipa yale madeni, wanategemeaje TANESCO iendelee ku-survive? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho napenda nizungumzie tu kwamba katika ajira, katika Sekta ya Mafuta na Gesi inasikitisha kuona kwamba kampuni za ndani ziliweza kupata sehemu ya manunuzi au ya ku-supply vitu kwa asilimia tisa tu. Makampuni yote ya nje ndiyo yamefaidi miradi inayoletwa Tanzania. Ukiangalia mafunzo katika sekta hii yamefanywa kwa asilimia 20 tu kwa maana hiyo ina maana kwamba hatuna personnel ya kuweza ku-run gesi zetu au mitambo hii ya gesi. Ukiangalia katika wataalam waliofundishwa au walioelimishwa mpaka sasa labda wawe wameongezwa wengine kutokana na ripoti ya CAG, ni asilimia sita tu ambayo katika Sekta ya Gesi na Mafuta wameweza kupata masomo ambayo ndiyo relevant kwenye hii sekta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunachotaka kusema, hivi Tanzania kwa nini sisi tunakumbatia mashirika ya nje hata kama mradi ume-provide kwamba mafunzo yafanyike, hayafanyiki. Matokeo yake watu wetu hawapati ajira, watu wetu hawafaidiki na fedha hizi ambayo ni mikopo kutoka nje ambayo italipwa na jasho la wananchi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)